Kuomba Dua kwa Pamoja Kwenye Kaburi...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuomba Dua kwa Pamoja Kwenye Kaburi Wakati wa Mazishi

Question

Ni nini hukumu ya kumsomea maiti Dua kwa pamoja kwa wale wanaomsindikiza maiti huyo wakati wa kumzika na baada ya kumzika? Na je mwombaji anaelekea Kibla wakati wa kuomba dua au hapana?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Maana ya Dua katika lugha ni maombi, inasemwa: "Nimemuomba Mwenyezi Mungu ninamuomba dua na nyiradi nyingine", kwa maana ya: "nimeisoma dua kwa kumuomba na nikayataka ya kheri kutoka kwake", na neno hili pia lina maana ya wito; inasemwa: " dua ina maana ya kumwita mtu". Na nimeomba dua kwa kusema: nimemwomba au nimefanya maombi, na nimemwita Zaid: kwa maana ya kumwita na kumtaka aje, na Muadhini amewaita watu wakaswali naye ni mtoaji wito kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Wito: kwa maana ya utashi juu ya kitu, na amemwita Zaid: ametaka msaada wake. Na amelilingania jambo: kwa maana ya kulipigania jambo hilo.maana zote hizi zinatuama katika neno "Dua" lenye asili ya kiarabu. [Lisaanu Al Arab 261/14, Ch. Dar Swader. Na AL Mswbaah Al Muneer 194/1, Ch. Al Maktabah Al Elmiyah. Na Taaju Al Aruos 46/38, Ch. Dar Al Hedaya]
Dua katika istilahi ni: maneno yaliyoandaliwa yenye maana ya ombi na kwa unyenyekevu. Na huitwa pia uombaji au kuomba. [Tazama Kawaid Al Fiqh kwa Al Barkatiy Uk. 292, Ch. Dar Al Hadaf]
Al Khatwabiy amesema katika kitabu cha [Sha'n Al Duaa, Uk. 4, Ch. Dar Al Thaqafah Al Diniyah]: Ukweli wa dua ni mja kumwomba Mola wake ulinzi na kumpa msaada anaouomba, na ukweli wake ni kudhihirisha unyenyekevu kwa Mola na utakasifu wa Uwezo na Nguvu alizonazo Mwenyezi Mungu, na hii ni alama ya uja na udhihirishaji wa udhalili wa kibinadamu, na ndani yake kuna maana ya kumsifu Mwenyezi Mungu na kuongeza utoaji wa Mwenyezi Mungu na ukarimu wake.
Na Dua ni katika ibada zilizo bora mno, na kutoka kwa Al Nu'maan Bin Basheer (R.A) alisema: Mtume S.A.W. anasema: "Dua ni Ibada" Halafu akasoma tamko la Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na Mola wenu Mlezi anasema: Niombeni nitakuitikieni. Kwa hakika wale ambao wanajivuna kuniabudu Mimi wataingia Jahannamu wadhalilike.} [GHAAFIR 60]. [Imetolewa na Ahmad, Ab Dawud na Atarmeziy, na akasema hadithi hii ni njema na sahihi, na Ibn majah na Al Haakem akaisahihishia na Adhahabiy akaafikiana naye]
Na katika Sunna wakati wa kulisindikiza jeneza, wasimame pembezoni mwa kaburi hao wasindikizaji wa jeneza kwa muda wa saa moja baada ya mazishi wakimwombea maiti ndani ya muda huo. Na kutoka kwa bwana wetu Othmaan Bin Affaan (R.A) alisema: Mtume S.A.W. alikuwa akimaliza kumzika aliyekufa atamsimamia na kusema: "Mwombeeni msamaha ndugu yenu huyu na mwuombeeni uimara kwani yeye hivi sasa anaulizwa". [Hadithi hii Imetolewa na Abu Dawud katika Sunna zake, na Al Haakem katika kitabu cha Al Mustadrak na akasema Hadithi hii ni sahihi]
Muslim amepokea Hadithi kutoka kwa Amru Ibn Al Aas R.A.kwamba alisema: "Mtakaponizika na mkanifukia kwa udongo juu yangu basi simameni pembezoni mwa kaburi langu kiasi cha kumchinja mnyaka na kuigawa nyama yake ili mimi niweze kuliwazika kutokana nanyi na nikaangalia ni nini nitakachokirejea kwacho kwa ajili ya wajumbe wa Mola wangu" [Kitabu cha Sahih Muslim] Na haya yanakuwa baada ya mazishi.
Na sio vibaya dua kuyatangulia mawaidha mafupi yanayokumbusha umauti na nyumba ya Akhera, kutokana na faida yake ya kuzilainisha nyoyo na kuziandaa na unyenyekevu kwa ajili ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kukusanya juhudi katika dua. Basi kutoka kwa Aliy R.A na Mwenyezi Mungu autukuze uso wake, alisema: "Tulikuwa katika jeneza katika mtaa wa Baqi'i Al Gharqad, basi Mtume S.A.W. akaja, na akakaa na sisi tukakaa nae tukimzunguka huku yeye akiwa na fimbo ndogo, akanyanyua fimbo yake ardhini kisha akasema: "Hakuna yeyote kati yenu, alieumbwa kutokana na nafsi iliyoumbwa isipokuwa atakuwa ameandikiwa sehemu yake peponi au motoni, ima atakuwa ameandikiwa kuwa mtu mwovu au mtu mwema" basi mtu mmoja akasema: ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu kwanini tusitegemee kile tulichoandikiwa na Mwenyezi Mungu? Mtume S.A.W. akasema: "fanyezi kazi; kila mtu amerahisishiwa kwa kile alichoumbiwa". Wanazuoni wamekubaliana juu ya Hadithi hii.
Imamu Bukhari aliyataja hayo katika kitabu chake cha: [Sahihu Al Bukhariy] (Mlango wa Mawaidha ya mzungumzaji pembezoni mwa kaburi na kukaa kwa wenzake kando kando yake).
Na imetajwa katika kitabu cha: [Fatwa za Kihindi] "Na inapendeza watu wakimzika maiti wakae kaburini kwa muda wa saa moja baada ya kumaliza, kiasi cha kuchinja mnyama na kuigawa nyama yake, wasome Quraani na kumuombea dua maiti". [166/1, Ch. Dar Al Fikr]
Imamu Anawawiy amesema: "Na inapendeza wakae kaburini kwa muda wa saa moja, kiasi cha kuchinja mnyama na kuigawa nyama yake, na walioketi wawe wanajishughulisha na usomaji wa Quraani, na kumwombea dua maiti na pia mawaidha, na simulizi za watu wema, na hali za watenda mema … Ashafiy na wenziwe wamesema: Na inapendeza wasome kiasi fulani cha Quraani, wakasema: wakihitimu Quraani yote basi itakuwa bora zaidi". [Al Idhkaar 161/1, Ch. Dar Al Fikr]
Na suala la kuelekea Kibla wakati wa kumwombea maiti kaburini kwake au kutofanya hivyo ndani yake kuna maelezo mengi, na wanazuoni ndani ya jambo hili wana njia mbili: Wapo wanaoona kushikamana na ujumla wa dalili zinazothibitisha kuwa inapendeza kuelekea Kibla wakati wa kumwombea maiti dua, na miongoni mwao wanaona inapendeza katika dua kwamba uso wa mwombaji uuelekee uso wa mwombewa ambaye ni maiti, na wanategemea hadithi ya Ibn Abaas (R.A) aliyosema: Mtume S.A.W. Alipita katika makaburi ya Madina akawaelekea kwa uso wake kisha akasema: "Amani iwe juu yenu enyi watu wa makaburi haya, Mwenyezi Mungu atatusaidia sisi nanyi, nanyi mmetutangulia na sisi twawafuata nyumba yenu". [Atarmidhiyu ameipokea Hadithi hii na akasema ni hadithi yenye hukumu ya Hassan na ni ngeni, na Al Dhiyaa Al Maqdisi ameeleza katika kitabu cha Al Ahadith Al Mukhtara]
Al Allamah Al Qaari' amesema: "Ndani yake kuna maana ya kwamba kinachopendeza wakati wa kutoa salamu juu ya maiti ni kwamba uso wake auelekee uso wa maiti, na aendelee kuwa hivyo katika dua pia, na waislamu wote wanapaswa kufanya hivyo, kinyume na yale aliyoyasema Ibnu Hajari kuwa Sunna kwetu sisi wakati wa dua ni kuelekea kibla kama ilivyojulikana kutokana na Hadithi nyingi za Mtume kutokana na upana wa kuomba dua. Na kuna kauli kuwa sehemu nyingi za dua Mtume S.A.W. hakuelekea Kibla kama vile sisi tunavyofuata, na miongoni mwa sehemu hizo ni kama katika Twawafu, katika Saayu, Kuingia na kutoka msikitini, na wakati wa kula na kunywa, kumtembelea mgonjwa na mfano wa hayo. Inategemea mtu akaelekea au kuacha kuelekea Kibla kwa mujibu wa mapokezi yakiwapo, kama sio hivyo basi vikao vilivyo bora ni vile vya kuelekea Kibla kama ilivyopokelewa katika Hadithi. [Merqat Al Mafateeh Sharhu Meshkat Al Maswabeeh 30-31/6].
Na kwa kuwa jambo hili laendelea kuwa na hitilafu basi hapana haja ya kuwa na misimamo mikali ndani yake, na msingi wa Kisheria ni kuwa: "Jambo wanalohitilafiana watu halikatazwi" na usahihi wa jambo hili ni watu kuyaacha ya ndani yao, na anaetaka kuelekea Kilba na afanye hivyo. Na anaetaka basi na aelekeze uso wake Kibla cha uso wa maiti kwa kuchukua uwazi wa Hadithi ya Mtume S.A.W. na kwa ajili ya kuwa na adabu wakati wa kuwa na maiti na haswa akiwa ni katika mawalii wa Mwenyezi Mungu Mtukufu basi anapata heshima hiyo, bali ni vizuri zaidi wakati huo kufanya hivyo, na wala haizuiliwi kufanya hivyo, na wala sio hili wala sio lile, hakika ya zingatio hapo katika dua ni lile mwislamu analolipata moyoni mwake, na ugomvi katika jambo kama hili hudhoofisha moyo wa kusoma dua na uzuri wa kumwelekea Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Ama kwa upande wa dua: je huwa kwa siri au kwa sauti? Na je mtu anasoma dua hiyo peke yake au kwa pamoja na watu wengine? Basi tunasema: Jambo hili lina mapana yake, na kugombana kwa ajili yake hakumridhishi Mwenyezi Mungu wala Mtume wake S.A.W. bali ni katika uzushi uliosemwa vibaya; kwani katika uzushi kuna kubana kile alichokipanua Mwenyezi Mungu na Mtume wake rehma na amani zimwendee yeye na jamaa zake. Na pindi Mwenyezi Mungu anapoweka jambo kwa sifa ya uwazi na pakawepo uwezekano wa utendaji wa jambo hilo na jinsi ya kulitekeleza kwake kwa zaidi ya njia moja miongoni mwa njia zake, basi huchukuliwa uwazi na upana wake, na wala haiswihi kulibana jambo hilo kwa njia moja na kuzuia nyingine isipokuwa kwa dalili.
Na dua inayosomwa kwa pamoja ina matarajio zaidi ya kukubalika na huuamsha moyo na huwakusanya watu wakawa na ari ya pamoja, na dua hiyo pia hupelekea unyenyevu zaidi na kujidhalilisha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na hasa ikiwa kuna mawaidha ndani yake. Na Mtume S.A.W. amesema: "Mkono wa Mwenyezi Mungu uko pamoja na jamaa". [Atarmidhi amepokea Hadithi hii na akaisahihisha kwa kusema ni hadithi Hassan].
Na kwa mujibu wa yaliyotangulia ni kwamba inajuzu kwa wasindikizaji wa jeneza kumwombea dua maiti na pia wakati wa mazishi, kwa pamoja, kwa kuelekea Kibla au kutoelekea Kibla. Inajuzu pia dua hii kuyatangulia mawaidha yanayowakumbusha wasindikizaji siku ya Akhera na kuwahimiza utiifu na unyenyekevu katika dua, na wala hakuna uzushi katika jambo hili, na wala haijuzu kuhitilafiana na kutengana kutokana na mambo kama haya, kwani ndani ya jambo hili kuna mengi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas