Kuuziana kwa Sharti la Kurejesheana...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuuziana kwa Sharti la Kurejesheana Amana.

Question

Nilikuwa ninahitaji mali lakini sijapata mtu wa kunikopesha kwa mkopo usio na riba. Baadhi ya marafiki zangu wakaniashiria kunipa mali ambayo ninaihitaji lakini kwa kumwuzia mkopeshaji gari langu ili apate kulitumia, ili nimlipe mali yake baada ya mwaka mmoja na yeye atanirudishia gari langu. Je kitendo hiki ni sahihi kisharia au hapana? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya hayo:
Sharia takatifu inapendelea kutoa msaada kwa mwenye matatizo na kumwondolea mazito aliyonayo. Katika Hadithi sahihi ya Imamu Muslim kutoka kwa Abu Huraira: “Mwenye kumwondolea tatizo Muumini katika matatizo ya dunia Mwenyezi Mungu Atamwondolea matatizo miongoni mwa matatizo ya Siku ya Kiyama, mwenye kumwepesishia mwenye mazito Mwenyezi Mungu Atamwondolea mazito yake duniani na Akhera, na mwenye kumsitiri Mwislamu Mwenyezi Mungu Atamsitiri duniani na Akhera, Mwenyezi Mungu humsaidia mja mwenye tabia ya kumsaidia ndugu yake…”. kuondoa matatizo ni katika mambo ambayo hujifaharisha nayo wasio kuwa Waislamu ikiwa ni kuonesha utu wao mpaka Sharia takatifu ikafanya malipo yake ni kumwondolea muhusika matatizo miongoni mwa matatizo ya Siku ya Kiyama.
Makubaliano yaliyofanyika kati ya muulizaji na rafiki yake yanaitwa “Uuzaji wa Amana” pia uuzaji huu una majina mengine mengi, kwa mfano wafuasi wa Imamu Malik wameuita “Mauziano ya wawili”. Na wafuasi wa Imamu Shafi wameita “Uuzaji wa makubaliano” na wafuasi wa Imamu Hanbal wameyaita kuwa ni “Uuzaji wa kuaminiana”, lakini pia huitwa “Uuzaji wa utiifu” na “Uuzaji unaofaa”. Na yakaitwa katika baadhi ya vitabu vya wafuasi wa Imamu Abu Hanifa “Uuzaji wa ushirikiano” na namna zake ni kama ilivyo kuja katika swali, ni kuuza bidhaa kwa sharti muuzaji wakati wowote atakaporejesha fedha mnunuzi anapaswa kurudisha kile kilichouzwa, makubaliano haya yameitwa “Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana” kwa sababu mnunuzi analazimika kununua kwa sharti, uuzaji huu umekuwa maarufu kwenye tafiti za kifiqhi na kisheria kwa jina la “Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana”, katika mtazamo wetu sababu ya kuwepo kwa uuzaji wa aina hii ni kuwa tatizo la uuzaji huu lilianza ndani ya karne ya tano katika nchi za Bukhara, lakini sababu yoyote itakayokuwa, uuzaji huu watu wameukimbilia kama mbadala wa mikopo ya riba. Jambo linakufahamika ni kuwa kila mkopo wenye faida ni haramu, pamoja shida kubwa ya watu kuhitaji mtu atakayewakopesha, na dhamira ya watu wenye mitaji ya kutoa mikopo isiyokuwa na riba hupelekea kwenye aina hii ya kuuziana ambapo kunakidhi utashi wa kila upande, mwenye kuhitaji anamaliza tatizo lake kwa kutokuuza chombo chake au bidhaa yake ambayo anaichunga kwa uangalifu mkubwa, na mwenye mali ananufaika na hicho chombo au hiyo bidhaa pamoja na kuwa na dhamana ya kutopata hasara ya mali pasi na kuwepo kitu mbadala. Pande zote mbili zinakuwa mbali na kuingia kwenye dhambi inayotokana na uharamu wa kushirikiana kiriba kwa maana ya riba ya deni.
Muamala huu unafanana na makubaliano ya rehani, isipokuwa unatofautiana na rehani kwa baadhi ya sifa, ambapo makubaliano ya rehani yanaondoa uhalali kwa mwenye kuwekewa rehani kutumia kitu kilichowekwa rehani, hata wale waliopitisha uhalali wa kunufaika na rehani kwa sharti la kutokua hiyo rehani ni deni la mkopo, wakati ambapo Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana inakuwa ni halali kwa mwenye kununua kunufaika au kutumia kile kilichouzwa kwa sababu ni miliki yake.
Wametofautiana wanachuoni katika muamala huu, je uhalisia wake ni uuzaji au ni kuweka kitu rehani? Kama vile ambavyo wametofautiana katika uhalali wake kwa mitazamo tofauti:
Mtazamo wa kwanza: Ni kuwa Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana si sahihi, miongoni mwao wapo walioona kuwa uuzaji huu ni batili, nayo ni kauli ya Jamhuri ya wanachuoni wa Madhehebu ya Imamu Malik na Hanbal, na Jamhuri ya wanachuoni wa Madhehebu ya Imamu Abu Hanifa na Shafi, na wakatoa sababu ya hilo kuwa sharti la kurudisha kilichouzwa kwa kurudisha thamani ni sharti lenye kugongana na kusigana na makubaliano ya kuuza kunakopelekea kumiliki moja kwa moja kilichouzwa kwa mnunuzi, kama ambavyo hakuna dalili ya kufaa sharti kwa hiki kigezo, na Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana haikusudiwi uuzaji wa kweli, pamoja na kuwa sura yake ni ya uuzaji, kinachopatikana ndani ya mkopo wenye faida hakifai. [Angalia kitabu: Tabyiin Al-Haqaiq, Sharh Kanz Al-Daqaiq cha Zailaiy, 5/183 – 184, Ch. Dar Al-Kitab Al-Islamiy, na kitabu cha Al-Inaaya cha Babartiy na Fath Al-Qadir cha Ibn Al-Hamam, 9/236 – 237, Ch. Dar Al-Fikr, na kitabu cha Radd Al-Muhtar cha Ibn A’abideen, 5/276, Ch. Dar Al-Fikr, na kitabu Al-Muntaqa cha Al-Bajiy, 4/210 Ch. Dar Al-Kitab Al-Islamiy, na Menah Al-Jalil cha Sheikh Aliish, 5/52, Ch. Dar Al-Fikr, na kitabu cha Tahrir Al-Kalam cha Al-Hatwab, 232, Ch. Dar Al-Gharb Al-Islamiy, na kitabu cha Tuhfat Al-Muhtaj cha Ibn Hajar Al-Haitamiy, 4/297 Ch. Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy, na Kashaf Al-Qinaa cha Bahutiy, 3/149 – 150, Ch. Dar Al-Fikr).
Na kwa maelezo hayo thamani itarejeshwa kwa mnunuzi na kitu kilichouzwa (kilichowekwa kama dhamana) kitarejeshwa kwa muuzaji. Mtazamo huu unaendana na madhehebu ya Abu Hanifa na Shafi katika masharti ya makubaliano, ambapo wao hawapitishi masharti isipokuwa masharti ambayo yanakubaliana na makubaliano au kuendana na makubaliano, au yale masharti ambayo yalikuwa yanatambulika kwenye jamii kama ilivyo kauli ya Abu Hanifa, tofauti na wafuasi wa Imamu Maliki na Hambali wao wanakunjua zaidi masharti na kurekebisha masharti yote isipokuwa sharti lolote linalopingana na makubaliano au Sharia.
Na miongoni mwa watu wenye mtazamo huu ni pamoja na wale walioufanya Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana kuwa ni rehani batili, nao ni baadhi ya wafuasi wa Imamu Malik, [rejea: Kitabu Tahrir Al-Kalam cha Al-Hatwab, uk. 236].
Miongoni mwao ni wale waliozingatia kuwa ni uuzaji wa uovu na kuushusha nafasi ya uuzaji wenye kuchukiza, ni kauli ya baadhi ya wafuasi wa Abu Hanafi, huthibiti umiliki wa kilichouzwa kwa muuzaji ikiwa atapokea malipo na kuthibiti haki kwa muuzaji ya kufuta makubaliano. [Rejea: Kitabu Tabyin Al-Haqaiq cha Zeylaiy 5/183).
Mtazamo wa pili: Ni kuwa Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana ni makubaliano sahihi, na kuzingatiwa sawa na uwekaji rehani, mtazamo huu umeegemewa na baadhi ya watu wa Abu Hanifa, na kutoa sababu kuwa muuzaji ameweka sharti kwa mnunuzi kuchukua kitu kilichouzwa mpaka pale atakapolipa deni. Jambo hilo linachukua maana sawa na uwekaji kitu rehani, na mazingatio katika makubaliano ni maana zake na wala sio muundo wake. Na katika hilo huchukuliwa kwenye makubaliano haya hukumu za uwekaji rehani ambapo hakuna umiliki kwa mnunuzi wala kunufaika na alichokinunua, na kuzingatiwa kile kinacho haribika ni uadui au matumizi yaliyopindukia. [Al-Enaya Sharh Al-Hidaya, 9/236].
Na kauli hii imechunga zaidi usahihi wa mkataba kadri inavyowezekana na kulindwa kwake na kutokuwa batili, lakini hayo huchukuliwa baada ya kufanyika makubaliano na wala si katika mwanzo wake, hasa mwenendo wa makubaliano kuzingatiwa ni rehani kutokidhi utashi wa moja ya pande mbili na wala hakupelekei lengo la kweli ambalo kwa ajili ya lengo hilo kumepelekea kuwepo kwa makubaliano hayo, kwa sababu ya hali hii kuwa si halali kwa mnunuzi (mwenye mali) kutumia na kunufaika na kilichouzwa ndani ya kipindi cha rehani.
Mtazamo wa tatu: Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana ni uuzaji sahihi wenye kuzalisha baadhi ya hukumu, na dalili ya usahihi wake ni haja ya watu kufanya miamala hii. Wamesema baadhi ya watu wa Abu Hanifah: maana yake ni kuwa halali kwa mnunuzi kunufaika na kilichouzwa pasi na kuwa na haki ya kukiuza au kutoa zawadi na mfano wa hayo. [Kitabu: Al-Enaya Sharh Al-Hidaya, kwa Al Babartiy 9/236, 237].
Na kwa kuangalia Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana tunakuta kuwa hukumu yake kifiqhi inayavuta mambo mengi, kwa upande wa umbo lake na muundo wa makubaliano ya kuuza, na kwa upande wa madhumuni ya makubaliano ya rehani. Wala haifai katika makubaliano ya rehani kwa kauli ya Jamhuri ya wanachuoni kunufaika au kutumia kile kilichowekwa rehani, hata wale waliopitisha uhalali wa kutumia wameweka sharti zisizokubali kufaa kwa sura ya Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana, na kuleta kanuni kuwa je mazingatio katika makubaliano ni tamko au maana? Inafaa kwa mwenye kuzingatia tamko bila ya kuwa na nia na makusudio iwapo uuzaji huo utakuwa sahihi au si sahihi, na pia inafaa kwa yule mwenye kuzingatia kinyume chake - kwa maana ya kuzingatia nia na makusudio - kuifanya kuwa ni rehani sahihi au si sahihi. Kuongezea na maelezo hayo ni kuwa msukumo wa kuanzishwa kwa uuzaji huu unatokana na kuhitaji mkopo bila mkopeshaji kuamua kujitolea mkopo huo. Na kwa maana hii mkopo wa aina hii unakuwa na faida. Na faida hiyo ni haramu kwa kauli za wanachuoni wote. Na kwa maana hii wanachuoni hawajatoa kauli ya kuipa nguvu kauli ya kuzuia, ambapo Jamhuri ya Wanazuoni wa Kimataifa wa Fiqih katika mkutano wao wa saba uliofanyika Jidda Saudi Arabia kuanzia mwezi 7 – 12 mfungo pili mwaka 1412 sawa na tarehe 14/ Mei / 1992 waliichukua kauli hiyo kwa maamzi nambari (66). Na katika kuzuia uuzaji huu ujulikanao kama Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana, kanuni ya Misri imechukua katika kipengele chake cha (465 cha sheria ya kiraia), ambacho kinasema: “Ikiwa muuzaji ataitunza haki ya kukirejesha kilichouzwa ndani ya muda maalumu, basi kuuziana huko kunakuwa ni batili”.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia na sura ya swali: Ni kuwa haifai kwa muulizaji kuuza gari lake kwa mtu yeyote kwa sharti la kurudishiwa gari hilo baada ya mwaka mmoja pindi atakapokuwa na uwezo wa kurudisha pesa alizouzia. Huku ndiko Kuuziana kwa Sharti la kurejesheana Amana au uuzaji wa makubaliano. pamoja na majina mengine, ambapo kisharia haijuzu kwa kauli yenye nguvu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas