Biashara ya sarafu za zamani

Egypt's Dar Al-Ifta

Biashara ya sarafu za zamani

Question

Ni ipi hukumu ya kufanya biashara ya sarafu za zamani za Misri ambazo hazitumiki tena kwa sasa katika miamala?

Na ikiwa inajuzu, je, inajuzu kuziuza kwa mkopo au lazima kuwe na kukabidhiana papo hapo?

Answer

Kukusanya sarafu za zamani na kufanya biashara yake hakuna kizuizi kisheria; ikiwa sarafu hizi za zamani zikiuzwa na zikawa ni miongoni mwa dhahabu na fedha, basi sharti lake ni kukabidhiana katika kikao cha mauzo na malipo ya papo hapo. Ama ikiwa si katika dhahabu na fedha, basi sababu ya riba imeondoka, na zinakuwa bidhaa inayoruhusiwa kufanyiwa muamala wa kuuza na kununua kwa bei itakayokubaliwa na pande mbili muzaji na mnunuzi.

Maelezo

Kinachokusudiwa kwa “sarafu za zamani” ni zile sarafu ambazo serikali imezifuta na watu hawazitumii tena, kiasi kwamba baadhi yake zimegeuka kuwa mapambo au vitu vya thamani ambavyo watu wanapeana zawadi.

Asili ya kukusanya sarafu hizi za zamani, zisizotumika katika miamala, na kufanya biashara nazo ni kuwa ni jambo linaloruhusiwa, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na Mwenyezi Mungu ameharamisha riba na kuhalalisha biashara} [Al-Baqara: 275].

Ikiwa zitauzwa sarafu hizi za zamani ni za dhahabu au fedha, basi ni lazima zikabidhiwe kwa mkono katika kikao cha mauzo, kwa kuwa sharti katika kubadilishana mali zenye sifa ya kuzidi (riba) ni uwepo wa kukabidhiana kabla ya kutengana.

Na ni sawa katika hilo ikiwa badala mbili ni za aina moja, kama dhahabu kwa dhahabu, au fedha kwa fedha; au ni za aina mbili tofauti, kama dhahabu kwa fedha. Na dalili ya hilo ni Hadithi ya ‘Ubadah bin Ṣamit ambaye alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu ((S.A.W)) alisema: “Dhahabu kwa dhahabu, fedha kwa fedha, ngano kwa ngano, shahiri kwa shahiri, tende kwa tende, na chumvi kwa chumvi , kile kwa kile, sawa kwa sawa, mkabidhiane papo hapo. Lakini aina hizi zitakapokuwa tofauti, basi uzaeni mnavyotaka mradi tu mkabidhiane papo hapo.” Ama ikiwa sarafu hizi za zamani zikiuzwa na si miongoni mwa dhahabu na fedha , yaani sarafu za karatasi, basi sharia za malipo papo hapo na kukabidhiana hazitumiki, bali inaruhusiwa kuuzwa kwa malipo ya baadae (mkopo). Na maelezo ya maimamu wanne kwa dhahiri hayatumii riba katika sarafu za karatasi zinazotumika kwa kawaida na watu wanazikubali, isipokuwa moja ya mapokezi kutoka kwa Imamu Malik..

Kwa mujibu wa Abu Hanifa na Abu Yusuf: hakuna riba katika sarafu za kawaida  na wamejuzisha kubadilishana sarafu moja kwa mbili au zaidi ikiwa zote zinajulikana, hoja yake ikiwa, sarafu kiasili haina thamani katika umbile lake (la asili) kwa sababu thamani yake inatokana na makubaliano ya watu, na kile kinachoamuliwa kwa makubaliano kinaweza kufutwa kwa makubaliano.

Hili ndilo pia linaloaminika miongoni mwa Maliki, na pia miongoni mwa Hanbali: kuna riwaya mbili zilizotajwa za Imam Ahmad kuhusu kuuza sarafu moja kwa sarafu mbili, na riwaya sahihi ni ile inayoruhusu.[1]

Kwa kuwa hili linahusu sarafu za karatasi zinazotumika kwa kawaida, basi ni bora zaidi kwa  sarafu hizi za zamani ambazo hazitumiki sokoni kwa kiwa  zimeondokana na sababu ya riba, na inaruhusiwa kuifanya biashara yake kwa bei itakayokubaliwa na pande mbili zinazouziana.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kukusanya sarafu za zamani na kufanya biashara nazo inajuzu kisheria.

Kama sarafu hizo ni za dhahabu au fedha, lazima zikabidhiwe papo hapo katika kikao cha mauzo.

Ikiwa sarafu za zamani si miongoni mwa dhahabu na fedha, basi zinachukuliwa kuwa ni bidhaa, na inaruhusiwa kuuzwa na kununuliwa kwa bei itakayokubaliwa na pande mbili zinazofanya muamala.

 

[1] Sharḥ Fatḥ al-Qadīr” (juzuu 7, ukurasa 22, chapa ya Dār al-Fikr), “Ḥāshiyat ad-Dasuqī ʿalā ash-Sharḥ al-Kabīr” ya Aḥmad ad-Dardīr (juzuu 3, ukurasa 61, chapa ya Dār al-Fikr), “Al-Um” (juzuu 3, ukurasa 15, chapa ya Dār al-Maʿrifah), “Al-Furūʿ” ya al-‘Allāmah Ibn Mufliḥ na “Taṣḥīḥuh” ya al-‘Allāmah al-Mardāwī al-Hanbalī (juzuu 6, ukurasa 295, chapa ya Mu’assasat ar-Risālah)

Share this:

Related Fatwas