Kuwaua Raia Vitani

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuwaua Raia Vitani

Question

Nini hukumu ya kisheria ya kuwaua raia wa maadui vitani?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Raia: ni istilahi ya kisasa inayomaanisha wasio wanajeshi; kila asiyekuwa mwanajeshi anaitwa raia, aidha mwanajeshi ni tofauti na mpiganaji kwani wapiganaji ni wasio Waislamu ambao hawajafunga mkataba wa dhima wala ahadi ya usalama na Waislamu, na vita vinaweza kuzuka muda wowote baina yao na Waislamu.

Ibn Al Qayim alisema katika kitabu cha [Ahkam Ahl Al dhima, 2/873:874, cha. Dar Al Ramadiy]: “Makafiri: wanaweza kuwa ni watu wa vita au wanaofunga mkataba wa amani na Waislamu, na watu wa aina ya pili wanakuwa katika makundi matatu: watu wa dhima, watu wa makubaliano ya amani na wenye mkataba wa usalama”.

Wanachuoni wengi wa fiqhi wanaafikiana juu ya kutojuzu kuwaua wasiopigana au wasiosaidia katika kupigana kama; mwanamke, mtoto, huntha, mzee mkongwe, asiyeweza kutembea, kipofu, akatwaye mkono na mguu wake kwa mabadilisho, akatwaye mkono wa kulia, mwendawazimu, mtawa anayekuwa katika hekalu, mtalii anayekuwepo katika mlima ambaye hachanganyiki na watu, yoyote anayekuwepo katika nyumba au kanisa na wafanyabiashara, wakulima, mafundi na watumwa. Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msipindukie mipaka (mkawapiga wasiokupigeni). Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka. Na waueni (hao wanaokupigeni bure) popote muwakutapo, na muwatowe popote walipokutoweni; kwani kuwaharibu watu na dini yao ni kubaya zaidi kuliko kuua. Wala msipigane nao karibu na Msikiti Mtakatifu (wa Makka) mpaka wakupigeni huko. Wakikupigeni (huko) basi nanyi pia wapigeni. Namna hivi ndivyo yalivyo malipo ya makafiri . Lakini kama wakikoma, (basi); na Mwenyezi Mungu ni Mwingi wa kusamehe (na) Mwingi wa kurehemu. Na piganeni nao mpaka kusiwe na mateso (wao kuwatesa Waislamu bure), na dini iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu tu. Na kama wakiacha basi usiweko uadilifu ila kwa madhalimu. Mwezi mtakatifu kwa mwezi mtakatifu. Na vitu vitakatifu vimeekewa kisasi (vikiondolewa heshima yake). Na wanaokushambulieni, nanyi pia washambulieni, kwa kadiri waliyokushambulieni. Na mwogopeni Mwenyezi Mungu (msiongeze kuliko walivyokufanyieni). Na jueni kwamba Mwenyezi Mungu yu pamoja na wanaomwogopa}[AL BAQARAH, 190, 191, 192, 193, 194].

Yaani: piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni lakini msichupe mipaka, msije kuwaua wale ambao hawastahiki kuuawa; wanawake wao, watoto wao, watawa wao, wazee wakongwe pamoja na wagonjwa, wasioweza kutembea, vipofu na wendawazimu.

Makatazo ya kuwaua yalitajwa katika Hadithi ya Mtume S.A.W. pamoja na wasia wa Makhalifa Waongofu kwa viongozi wa majeshi yao, maana watu wa namna hiyo haijuzu kuwaua isipokuwa katika hali ya kuwepo dalili ya kushiriki kwao katika kupigana au kuchochea kwao katika vita.

Miongoni mwa Hadithi hizo ni ile iliyotajwa katika Sahihi ya Muslim kutoka kwa Barida ya kwamba S.A.W. alikuwa anasema: “Piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaomkufuru Mwenyezi Mungu wala msipindukie mipaka wala msiwaue watoto au wanaokuwepo katika mahekalu" [Rejea: Al Tafseer Al Waseet, 1/408, Dar Nah-dhat Misr & Tafseer Ibn Kathir, 1/524, Dar Tiba].

Ilipokelewa na Ibn Omar R.A. ya kwamba: “Mwanamke fulani alikutwa ameuliwa katika baadhi ya vita alivyopigana Mtume S.A.W. Mtume S.A.W. akakemea kuwaua wanawake na watoto”. [Bukhari na Muslim].

Na katika lafdhi ya masheikh wawili: “alikataza kitendo cha kuwaua wanawake na watoto”.
Imamu Malik alitaja katika kitabu chake Almuwatwa pamoja na maelezo ya Al Zarqaniy [3/16, Mak-tabat Al Thaqafa Al Diniya] kutoka kwa Abdulrahman Bin Kaab ya kwamba: “Mtume S.A.W. alikataza wale waliomwua Ibn Abu Alhaqiq wasiwaue wanawake wala watoto …”. Hadithi hiyo ilipokelewa na Shafii katika kitabu chake [Al Umm,4/252, cha. Dar Al Maarifa].

Na katika Musnad Imamu Ahmad na Sunan Abu Dawoud kutoka kwa Rabah bin Rabii ya kwamba: “Mtume S.A.W. katika vita aliwaona watu wamekusanyika juu ya jambo fulani, akamtuma mtu na akamwambia: angalia kwaninini wamekusanyika wale, basi aliporudi yule mtu akasema: mwanamke ameuawa, Mtume S.A.W. akasema: hakustahiki kuuliwa. Naye Khalid Bin Al Waleed wakati huo alikuwepo katika mstari wa mbele wa jeshi basi Mtume S.A.W. alimtuma mtu kwake: mwambie Khalid asiue mwanamke wala mtumwa”.

Hadithi hiyo ilipokelewa na Ibn Majah, na Ibn Haban alihakikisha usahihi wake, naye Al Hakim alisema: "Hadithi hiyo ni sahihi kwa mujibu wa maneno ya masheikh wawili ingawa walitaja kwa neno “dhuria” (kizazi) badala ya “imraa” (mwanamke)".

Na katika Sunan Abu Dawoud kutoka kwa Anas Bin Malik R.A ya kwamba: Mtume S.A.W. alisema: “Nendeni kwa Jina la Mwenyezi Mungu na kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na juu ya Mila ya Mtume S.A.W. na msiuue mzee mkongwe, mtoto mchanga, mtoto mdogo wala mwanamke na msipindukie mipaka katika dini yenu, tendeni mema na fanyeni wema, hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema”.

Na katika Al Muwatwa kitabu cha Imamu Malik kutoka kwa Yahya Bin Said ya kwamba: Abu Bakar R.A alimwambia Yazid Bin Abu Sufiyan: usiue mwanamke, mzee mkongwe, na usikate miti yenye kutoa matunda, usiharibu mji ulioimarika, usichinje mbuzi wala ngamia ila kwa ajili ya kula, usichome moto mitende wala usipindukie mipaka.

Na katika Sunan Al Bayhaqiy kutoka kwa Omar Bin Khattab R.A alisema: Mcheni Mwenyezi Mungu katika wakulima msije kuwaua ila wakijiandaa kupigana nanyi.

Na katika Musnad Imamu Ahmad na Al Ttabaraniy kutoka kwa Ibn Abass R.A alisema: Mtume S.A.W. alipokuwa akituma jeshi lake husema: “Nendeni kwa Jina la mwenyezi Mungu, mpigane katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokufuru Mwenyezi Mungu wala msipindukie mipaka wala msiwaue watoto au wanaokuwepo katika mahekalu”.

Aidha Hadithi hiyo ilipokelewa na Abu Yaliy kutoka kwa Ibn Abass ya kwamba: Mtume S.A.W. alisema: “Msiwaue wanaokuwepo katika mahekalu”.

Na katika Al Muwatwa kitabu cha Imamu Malik kutoka kwa Yahya Bin Said ya kwamba Abu Bakar alimwambia Yazid Bin Abu Sufiyan: utawakuta huko kundi la watu wanaodai kuwa wanajizuia kwa Allah, basi uwaache na dhana zao wanazoziamini.

Na katika riwaya iliyopokelewa na Abdulrazaq na Al Baihaqiy: wanaojizuia katika mahekalu.
Al Kassaniy Al Hanafiy alisema: “Basi inaharamishwa katika hali ya kupigana kuua mwanamke, mtoto, mzee mkongwe na asiyeweza kutembea kwa miguu, kipofu, akatwaye mkono na mguu wake kwa mabadilisho, akatwaye mkono wa kulia, mwendawazimu, mtawa anayekuwa katika hekalu, mtalii anayekuwepo katika mlima ambaye hachanganyiki na watu, na anayekuwepo katika nyumba au kanisa … kwani watu hao hawaingii katika kundi la watu wa kupigana, basi hawastahiki kuuawa” [Badai’ AL Sanai’, 6/63, Al Mak-taba Al Elmiya].

Alhadadiy alisema katika [Al Jawhara Alnayira, 2/259, Al Mat-ba’ Al Khayira]: “(Haijuzu kuua mwanamke, mtoto, mwendawazimu, mzee mkongwe, kipofu, asiyeweza kutembea) kwani hao hawakuwa miongoni mwa watu wa vita; wapiganaji isipokuwa wakianza kupigana au kuchochea mapigano na wakawa ni wenye kutiiwa, basi inajuzu kuwaua. Kauli yake: mzee mkongwe; inamaanisha asiyekuwa na uwezo wa kutoa rai katika mambo ya kivita, lakini watu wakiwa wanachukua rai yake, basi inajuzu kumuua”.

Ibn Al-Arabiy alizungumzia katika tafsiri yake [1/148, Dar Alkutub Al-Elmiya] makundi ya watu ambao hawatakiwi kuuawa: watu hao wako katika aina sita:

Kwanza: Wanawake: Wanachuoni wetu walisema: msiwaue wanawake mpaka wapigane, kwani Mtume S.A.W. alikataza kitendo cha kuwaua kama ilivyopokelewa na Imamu Bukhary na Muslim wakiwa hawapigani, ama wakipigana basi inajuzu kuwaua. Sahnun alisema: wanauawa katika hali ya kupigana, na sahihi kuwaua wakishiriki kupigana wakiwa katika hali ya kupigana au ikiwa baada ya hayo kukimalizika kupigana; kwa mujibu wa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msipindukie mipaka (mkawapiga wasiokupigeni). Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka. Na waueni (hao wanaokupigeni bure) popote muwakutapo}[AL BAQARAH, 190, 191]. Mwanamke ana athari zake kubwa katika hali ya kupigana; kutoa mali, na kuchochea; kwani wakati wa kupigana wanawake walikuwa wanatoka bila ya kufunika vichwa kudhihirisha ghadhabu na hasira, na hayo ni miongoni mwa sababu zinazosababisha kuwaua.

Pili: Watoto: haijuzu kuwaua watoto, kwani Mtume s.a.w. alikataza kuua kizazi, kama ilivyopokelewa na Maimamu wote, na mtoto angepigana angeuawa katika hali ya kupigana na kukimalizika kupigana, basi anauawa kwa mujibu wa maneno ya Yahya, aidha mwanamke aliyeshiriki kupigana. Lakini iliyosahihi haijuzu mtoto kuuawa kwani hajafikia umri wa kulazimika kisheria ... rai iliyo bora zaidi kwangu kuuawa kwa mwanamke aliyeshiriki kupigana na kumsamehe mtoto kwani Mwenyezi Mungu anamsamehe katika masuala ya madhambi.

Tatu: Watawa: Wanachuoni wetu walisema: hawauawi wala hawachukuliwi mateka, bali wanachukua mali inayowasaidia kuishi wakiwa mbali na watu wa kupigana kwa mujibu wa kauli ya Abu Bakar R.A kwa Yazid bin Abu Sufiyan: utawakuta huko kundi la watu wanaodai kuwa wanajizuia kwa Allah, basi uwaache na dhana zao wanazoziamini.

Nne: Wenye maradhi yasiyotibika. Sahnun alisema: wanauawa, naye ibn Habib alisema: hawauawi. Ama rai iliyo sahihi zaidi kwangu ni kuangalia hali zao; wakiwa miongoni mwa wanaoweza kuleta madhara, basi inajuzu kuwaua, ama wakiwa hawawezi kuleta madhara basi wanaachiwa na hali zao zisizotibika.

Tano: Wazee wakongwe. Imamu Malik alisema katika kitabu cha Muhammad: hawauawi ingawa rai yangu wauawe kwa mujibu wa yaliyopokelewa na Nisaaiy kutoka kwa Samrat bin Jundub ya kwamba Mtume S.A.W. alisema: “Waueni wazee wakongwe wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na wacheni watoto wao”, na hiyo ndiyo matini ya kisheria yenye kushikiliwa.

Sita: Waajiriwa; nao ni wafanyakazi na wakulima. Maulamaa walitofautiana katika suala lao; Malik alisema (katika Kitabu cha Muhammad): haijuzu kuuawa, na katika wasia wa Abu Bakar R.A. kwa Yazid Bin Abu Sufiyan: Usimwue mwajiriwa. Na rai iliyo sahihi zaidi kwangu ni kwamba inajuzu kuwaua wakiwa hawapigani, kwani watawasaidia wapiganaji.

Imamu Shafiy alisema katika kitabu cha [Al Umm, 4/152]: “Haijuzu kwa mwislamu yoyote kuua wanawake na watoto kwa makusudi, kwani Mtume S.A.W. alikataza kitendo cha kuwaua”.

Al Shirbiniy alisema katika [Mughniy Al Muhtajm, 4/220]: “(Ni haramu juu ya Mwislamu kuuua mtoto na mwendawazimu) pamoja na mtumwa, mwanamke, huntha kama ilivyotajwa katika Sahihi mbili. Na hapa mwendawazimu aliwekwa katika kundi la mtoto, na huntha aliwekwa katika kundi la wanawake kwa ujanajike wake unaoweza kutokea”.

Ibn Qudama alisema katika [Al Mughniy, 9/310, Ch. Mak-tabat Al Qahira]: “Kiongozi akiwateka makafiri, haijuzu kumwua mtoto ambaye hajafikia umri wa kubaleghe kwa mujibu wa Hadithi ya Mtume S.A.W.: "Alikataza kitendo cha kuwaua wanawake na watoto"; kwani kumwua mtoto aliyetekwa ni sawa na kuiharibu mali bure hata akiwa mtoto mmoja tu kwani anaweza kuwa Mwislamu baadaye, hivyo kitendo cha kumwua kinakuwa ni jambo la uharibifu kwani inawezekana akasilimu … aidha haijuzu kumwua mwanamke wala mzee mkongwe kama alivyosema Malik na watu wa rai. Na hiyo ndiyo iliyopokelewa na Abu Bakar R.A. na Mujahid. Aidha ilipokelewa na Ibn Abass R.A. katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {wala msipindukie mipaka} [AL BAQARAH, 190] akisema: msiwaue wanawake, watoto, mzee mkongwe … : wala haijuzu kuwaua wenye maradhi yasiyotibika, kipofu na mtawa. Na maoni ya hitilafu kuhusu makundi hayo ni sawa na yale yanayomhusu mzee mkongwe; kwani wenye maradhi yasiyotibika, kipofu hawawi miongoni mwa watu wa vita kama ile hali ya mwanamke. Ama mtawa basi imepokelewa na Abu Bakar R.A. akisema “mtawapitia watu wa mahekalu wanaojizuia, basi waacheni kwa Mwenyezi Mungu atawafisha katika hali yao ya upotofu”, aidha watawa hawapigani kwa ibada zao ndio maana wamefananishwa na asiyeweza kupigana. Halikadhalika mtumwa haijuzu kumwua kama alivyobainisha Imamu Shafiy kwa mujibu wa kauli ya Mtume S.A.W.: “Jitahidini kumwahi Khalid, mwambie asiue mwanamke wala mtumwa”, hapa hukumu ya watumwa inakuwa sawa na hukumu ya wanawake na watoto”.

Baadhi ya wafuasi wa Shafii walihitalifiana hapa, wakawa na maoni tofauti ambapo ilitajwa katika [Al Mughniy Al Muhtaj, 6/30]: “Inajuzu kuua mtawa, mwajiriwa, mzee mkongwe (hata akiwa mnyonge), kipofu, mwenye maradhi yasiyotibika, akatwaye mkono na mguu wake hata wakiwa hawakushiriki kupigana. Hayo ni kwa mujibu wa maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {basi waueni (piganeni na) washirikina} [AT TAWBA, 5]; kwani watu wa aina hizi ni waungwana, wenye jukumu kisheria basi inajuzu kuwaua kama wengineo. Hiyo ndiyo rai ya kwanza, na rai ya pili inasema: marufuku: kwani wanakuwa hawapigani, basi wakafananishwa na wanawake na watoto (katika hali zao). Tanbihi: kiini cha hitilafu kinakuwa kinahusiana na kushiriki katika kupigana; maana wakipigana wanastahiki kuuawa, aidha mtawa hapa ni anayefanya ibada ya kinasara akiwa mzee, kijana, mwanamume au mwanamke”.

Na katika [Al Ahkam Al Sultaniya, 69, Dar Al Hadith]: “Inajuzu kwa Mwislamu aue mateka mshirikina akiwa mpiganaji au raia, na suala la hitilafu liko katika kuwaua wazee na watawa wanaokaa katika hekalu, hitilafu za kifiqhi ziko katika kauli mbili; ya kwanza: hawastahiki kuuawa mpaka wapigane.

Ya pili: wanastahiki kuuawa hata wakiwa hawakupigana kwani labda walishiriki katika kupigana kwa maoni yao ambayo yanaweza kuwa na athari mbaya zaidi juu ya Waislamu kuliko kushiriki kwao katika kupigana, na kwa sababu hiyo Durid bin Al Sama aliuawa katika vita vya Hawazin”.

Hapa walipata dalili za kisheria kutokana na maneno ya Imamu Shafiy yaliyotajwa katika Kitabu cha [Al Umm, 4/254]: “Yeyote akiulizia ni ipi dalili ya kuwaua wasiopigana miongoni mwa washirikina? jibu: masahaba wa Mtume S.A.W. walimwua Durid Bin Al Sama katika siku ya Hunain hali ya kuwa umri wake ni miaka mia moja na hamsini, naye Mtume S.A.W. hakukosoa kitendo hicho, nami sijamwona anayeaibisha kuwaua washirikina wasiokuwa watawa”.

Aidha walipata dalili za kisheria kutokana na Hadithi ya Mtume S.A.W.: “Waueni wazee wakongwe miongoni mwa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na wacheni watoto wao”.

Ibn Rushd alibainisha sababu ya hitilafu katika kitabu cha [Bidayat Al Mujtahidm 2/148, Dar Al Hadith]: “Walihitalifiana katika suala la kuwaua; kwani walihitalifiana katika sababu inayolazimisha kuwaua; maana anayeona kuwa sababu ya kuwaua ni ukafiri wao, basi hukumu hapa ni ya kiujumla inayojumuisha washirikina wote, na anayeona kuwa sababu inayolazimisha inahusiana na uwezo wa kupigana basi huvuliwa yule asiyeweza kama mkulima, mtoto mdogo … n.k.”.

Lakini maoni hayo yamepingwa; maana Hadithi iliyopokelewa na Samra kutoka kwa Abu Daoud iliyotajwa katika Musnad Imamu Ahmad inasema: “waueni wazee wakongwe miongoni mwa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na wacheni watoto wao” ni Hadithi yenye udhaifu kama alivyosema Al Baihaqiy: Al Hajaj Bin Artaa alipinga kupata dalili ya kisheria kutokana na hadithi hiyo”.

Aidha jibu linaweza kuwa: Durid Bin Sama alikuwa mtu mwenye rai yenye kutekelezwa katika vita, hupigwa hata akiwa hashiriki, na imekatazwa kuwaua wanawake, watoto na wazee wakongwe wasiopigana au asiyekuwa na rai yenye kutekelezwa katika kupigana.

Tukiafikiana na hayo, tutamkuta Ibn Qudama aliijibu ile hitilafu ya kifiqhi katika kitabu cha [Al Mughniy, 9/312] aliposema: “Haijuzu kuua mwanamke wala mzee mkongwe kama alivyosema Malik na watu wa rai. Na hiyo ndiyo iliyopokelewa na Abu Bakar R.A. na Mujahid. Aidha ilipokelewa na Ibn Abass R.A. katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {wala msipindukie mipaka} [AL BAQARAH, 190] akisema: Msiwaue wanawake, watoto na mzee mkongwe. Naye Shafiy katika moja ya rai zake mbili kuhusu suala hilo aliafikiana naye Ibn Al Mundhir akisema: “Waueni wazee wakongwe miongoni mwa wanaomshirikisha Mwenyezi Mungu na wacheni watoto wao” (Hadithi hiyo ilipokelewa na Abu Dawoud, na Al Tirmiziy alisema Hadithi hiyo ni hasan sahihi), hivyo kwa mujibu wa maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {basi waueni (piganeni na) washirikina}[AT TAWBA, 5] na hukumu hapa ni ya kiujumla inayojumuisha wazee wote. Ibn Al Mundhir alisema: sioni hoja nzito katika maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {basi waueni (piganeni na) washirikina} ya kuzuia kuwaua wazee kwani mzee anayekusudiwa hapa ni kafiri haitatokea faida kutokana na maisha yake na kwa hivyo inajuzu kumwua kama kijana. Jambo ambalo halipingani na kauli ya Mtume S.A.W. Imepokelewa na Abu Daowd katika Sunan yake: (msimwue mwanamke, mtoto mchanga wala mzee mkongwe). Aidha ilipokelewa na Abu Bakar R.A alimwambia Yazid bin Abu Sufiyan alipomtuma eneo la Sham: (usimwue mwanamke, mzee mkongwe). Naye Omar Bin Khatab alimwusia Salma Bin Qayis akisema: (msimwue mwanamke, mtoto mchanga wala mzee mkongwe) kwani mzee si mtu wa vita, basi hastahiki kuuawa kama hali ya mwanamke. Naye Mtume S.A.W. alidokeza sababu hiyo inayomhusu (hukumu ya) mwanamke asiyepigana akisema: “Kwa nini aliuawa hali ya kuwa hakupigana”. Hali kadhalika Aya iliyotajwa ina hukumu maalumu kama tulivyobainisha hapo juu ambayo haijumuishi mwanamke wala mzee mkongwe. Ama rai yao kuhusu mzee, basi tunaona kwamba wanakusudia wazee wakongwe ambao hawana uwezo wa kupigana au hawana rai inayotekelezwa ambayo inakuwa msaada kwa wapiganaji. Aidha wenye maradhi yasiyotibika, vipofu na watawa hawastahiki kuuawa, na hitilafu inayohusiana na hukumu yao ni sawa na ile hitilafu juu ya mzee; hukumu hizi mbili zina hoja moja. Na ikiwa mwenye maradhi yasiyotibika na kipofu hawawi miongoni mwa watu wa vita, basi hali yao itakuwa sawa na hali ya mwanamke, ama mtawa basi tutapata hukumu yake ya kisheria kutokana na Hadithi iliyopokelewa na Abu Bakar E.A. “Mtawapitia watu wa mahekalu wanaojizuia, basi waacheni Mwenyezi Mungu Atawafisha katika hali yao ya Upotofu”, aidha watawa hawapigani kwa ibada zao mpaka wakafananishwa na asiyeweza kupigana”.

Naye Ibn Taimiya katika kitabu cha [Al Siasa Al Sharia,uk. 99] alisema: “Ikiwa asili katika upiganaji ni jihadi katika njia ya Allah ili dini iwe kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, na neno la Mwenyezi Mungu liwe juu, basi anayezuia watu na dini ya Mwenyezi Mungu malipo yake auawe kwa makubaliano ya Waislamu wote. Ama asiyezuia watu na dini ya mwenyezi Mungu wala hakupigana kama mwanamke, mtoto, mtawa, mzee mkongwe, kipofu, mwenye maradhi yasiyotibika, basi hukumu yake aachiwe bila ya kuuawa kwa mujibu wa maoni ya maulamaa wengi isipokuwa akianza kupigana kwa kitendo au maneno yake, ingawa baadhi ya maulamaa wanaona kujuzu kisheria kuwaua wote kwa ajili ya ukafiri wao isipokuwa wanawake na watoto kwani kwa kuwateka watakuwa ni mali kwa Waislamu … lakini rai ya kwanza ndiyo sahihi zaidi kwani tunalazimishwa kuwapiga wale wanaotupiga, ikiwa tunataka kutetea dini ya Mwenyezi Mungu kama Alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na piganeni katika njia ya Mwenyezi Mungu na wale wanaokupigeni, wala msipindukie mipaka (mkawapiga wasiokupigeni). Kwani Mwenyezi Mungu hawapendi warukao mipaka} [AL BAQARAH, 190], na katika Sunan: “Mtume S.A.W. katika baadhi ya vita aliona kundi la watu wamekusanyika pamoja, akamtuma mtu na akamwambia: angalia wamekusanyika kwa lipi, basi aliporudi yule mtu akasema: mwanamke ameuawa, Mtume S.A.W. akasema: alikuwa hana haja ya kupigana. Naye Khalid bin Al Walid wakati huo alikuwepo katika mstari wa mbele wa jeshi basi Mtume S.A.W. alimtuma mtu kwake akisema: mwambie Khalid asimwue mwanamke wala mtumwa”. Kwa hiyo Mwenyezi Mungu Ameruhusu kuwaua watu kwa ajili ya kuirekebisha jamii kama Alivyobainisha katika Kitabu Chake: {Na kuwazuia watu na dini yao ni mbaya zaidi kuliko kuua} [AL BAQARAH, 217]. Maana kitendo cha kuwaua watu hata kikiwa na shari na uovu kitakuwa bora zaidi kuliko fitna za makafiri, basi yoyote asiyezuia watu na dini ya Mwenyezi Mungu, mabaya ya ukafiri wake yataambatana naye tu ndiyo anaweza kuachwa. Kwa hivyo, wanachuoni walisema: Mwenye kulingania bidaa inayokwenda kinyume na Qurani na Sunna anastahiki adhabu kali zaidi kuliko anayeizuia nafsi yake. Kwa hiyo, sheria imelazimisha kuwaua makafiri. Ama waliotekwa basi hukumu yao ni kutouliwa; maana mtu akitekwa katika vita au katika hali nyingine kama kwamba amepotea njia ya bahari au ya jangwani tukampata au akitekwa kwa hila, basi Imamu ana uhuru wa kuchagua hukumu inayomfaa; anaweza kutoa hukumu ya kumwua, kumfukuza mbali, kumwacha kwa ihsani au kumbadilisha kwa mali au Mwislamu mwingine aliyetekwa na makafiri kama walivyoona wanachuoni wengi kwa mujibu wa Quraani na Sunna”.

Kutokana na yaliyopita: mtazamo ulio sahihi zaidi ni ule ulioshikiliwa na maulamaa wengi kuhusu kutojuzu kumwua asiyepigana au asiyesaidia wapiganaji katika vita, miongoni mwao wazee wakongwe na watawa kwani sababu ya kupigana na makafiri ni kwa ajili ya uadui wao siyo ukafiri ulio nao.

Kwa hiyo, haijuzu kuwaua raia vitani au kupigana nao wakiwa hawakupigana nasi au hawakusaidia wenzao katika kutupiga kwani sababu ya kuwaua haitatokea kwa hoja zilizotajwa na wanachuoni hapo juu, na kila asiye kuwa na madhara kwetu hastahiki kuuawa.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

 

 

Share this:

Related Fatwas