Kutoa Sauti Wakati wa Tahlili na Kumtaja Mwenyezi Mungu Nyuma ya Jeneza
Question
Je, Inajuzu Kutoa sauti wakati wa Tahlili na kumtaja Mwenyezi Mungu nyuma ya jeneza?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Miongoni mwa Utamkaji wa Dhikri ni Tahlil na Tahlil ni kusema: Laailaaha illa llahu, na Tasbihi ni kusema: Subhaana llahu au Subhaana llahu wabihamdihi. Na kuhimidi ni kusema: Alhamdu lillah, na nyiradi nyingine nyingi.
Na kutoa sauti maana yake ni kunyanyua sauti ili kujisikiliza au kumsikiliza mtu anayemfuatia, na hakuna upeo (kiwango) maalumu cha kuiinua sauti hiyo, na siri ni kujisikiliza mtu yeye mwenyewe. [Hashiyat Aswawiy Ala Asharhu Aswagheer 318/1, Ch. Dar Al Maarif]
Utamkaji wa aina nyingi upo usiodhibitiwa na upo uliodhibitiwa, kwa siri au kwa sauti isipokuwa katika hali ambazo inapendeza kutoa sauti ndani yake na sehemu ambazo inapendeza kusoma kwa siri ndani yake. Na zimetajwa sehemu ambazo inapendeza kunyamaza kimya na kutonyanyua sauti kwa kumtaja Mwenyezi Mungu au kwa nyiradi zozote kama vile wakati wa kutembea nyuma ya jeneza, katika yaliyopokelewa na Abu Dawud kutoka Hadithi ya Abu Hurairah kutoka kwa Mtume (S.A.W) alisema: "Jeneza halisindikizwi kwa sauti wala kwa moto".
Na imepokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Ibrahim Al Nakhaiy amesema: alikuwa akichukia kwamba mtu analifuata jeneza na anasema: Mwombeni msamaha Mola wetu atakusameheni.
Na imepokewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Bakeer Bin Ateeq amesema: nilikuwa katika jeneza likihudhuriwa na Sayid Bin Jubeyr, basi mtu mmoja akasema Mwombeni msamaha Mola wetu atakusameheni. Basi Sayid Bin Jubeyr akasema: hatakusamehe Mwenyezi Mungu.
Na imepokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Atwaa kwamba alichukizwa kwa mtu kusema: Mwombeni msamaha Mola wetu atakusameheni.
Na imepokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Al Hassan kwamba alichukizwa na mtu kusema: Mwombeni msamaha Mola wetu atakusameheni.
Na imepokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Abdul-Rahman Bin Harmalah: kwamba alikuwa katika jeneza basi akasikia mtu mmoja akisema, basi Sayid Bin Al Musaib akasema: Ndugu yenu huyo anasema nini?
Na inapokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Mughirah amesema: Mtu mmoja alikuwa anatembea nyuma ya jeneza na akisoma Suratul Waaqiah, basi akamwuliza Ibrahim juu ya hayo naye akachukizwa na jambo hilo.
Na imepokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Ayub kutoka kwa Abi Qulabah amesema: Tulikuwa kwenye mazishi, watu wa Kisasi wakanyanyua sauti zao na Abuu Qalaba akasema: walikuwa wanamtukuza maiti kwa utulivu.
Na imepokelewa na Ibn Abi Shaibah kutoka kwa Qais Bin Abaad amesema: maswahaba wa Mtume (S.A.W) walikuwa wakipendelea kupunguza sauti kwenye mambo matatu; Vitani, katika kusoma Quraanina katika mazishi.
Ibn Nujaim Al Hanafiy amesema: "Mtu anaelifuata jeneza anapaswa akithirishe ukimya na inachukiza kunyanyua sauti kwa dhikri na kusoma Quraanina nyiradi nyinginezo katika jeneza, na chukizo linalokusudiwa hapa ni uharamu kwa mujibu wa fatuwa za kisasa na kwa maimamu wa Turkiman. Amesema Alaamu Diin Naaswiriy: kuacha ni bora zaidi, na katika Dhwahiiriyyah: na iwapo mtu atataka kumtaja Mwenyezi Mungu basi amtaje ndani ya nafsi yake, kwa tamko la Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Muombeni Mola wenu Mlezi kwa unyenyekevu na kwa siri. Hakika Yeye hawapendi warukao mipaka} [AL AARAF 55] maana yake ni wale wanaotoa sauti katika dua, [Al Bahr Araaiq Sharh Kanz Adqaaiq 207/2, Ch. Dar Al Maarif]
Na Asheikh Adardiriy Al Malikiy amesema: "Na inachukiza kupiga kelele nyuma ya jeneza kwa kusema 'muombeeni msamaha' na mfano wa maneno hayo, na Swaawiy anachangia juu ya jambo hili kwa kusema: kwani kufanya hivyo sio katika kitendo cha Salafi (waliotutangulia). [Hashiyat Aswawiy Ala Asharh Aswagheer 568/1, Ch. Dar Al Maarif]
Na Al Khatwib Asherbiniy Ashafiy amesema: "Na inachukiza pia kunyanyua sauti wakati wa kulisindikiza jeneza." Kwa yaliyopokelewa na Al Baihaqiy kwamba maswahaba walichukizwa na kunyanyua sauti kwenye mazishi, upiganaji (vita) na katika dhikri, akasema katika kitabu cha [Al Majmu'i]: Na kilichochaguliwa bali kilichosahihi na ambacho walikifanya Salafi ni kunyamaza wakati wa kulisindikiza jeneza, na wala mtu yeyote asinyanyue sauti yake kwa kisomo chochote wala uradi wowote, bali atajishughulisha na kufikiria mauti na yanayohusiana na umauti. Na yale yanayofanywa na watu wasiojua kwa kusoma nyiradi kwa sauti na kutoa maneno sehemu yake ni haramu ambayo ni lazima ikatazwe.
Na Al Hassan na wengine, walichukizwa na tamko hili la "mwombeeni ndugu yenu msamaha kwa Mwenyezi Mungu", na Ibn Omar alimsikia msemaji akisema: mwombeni msamaha Mola wetu atakusameheni. Basi akasema hatakusamehe Mwenyezi Mungu. Sayid Ibn Mansour ameyapokea hayo katika Sunna zake. [Mughniy Al Muhtaaj Sharh Minhaaj Atwalbeen 360/1, Ch. Dar Al Fikr]
Arahibaaniy Al Hanmbaliy amesema: "Na inachukiza kunyanyua sauti wakati wa kulinyanyua jeneza na pia wakati wa kuwa nalo, hata kwa kisomo au dhikri, kwani jambo hili ni uzushi. Na imesuniwa kwa wenye kulifuata jeneza kusoma Quraanina dhikri kwa siri.
Na tamko la msemaji anapokuwa na jeneza; "mwombeeni msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu" na maneno mengine ni uzushi kwa Ahmad, na Abu Hafswi alichukizwa na akaharamisha tamko hilo, Ibn Masour amenukulu: sipendezwi na tamko hili. Na Sayid alipokea kwamba Ibn Omar na Sayid Bin Jubeyr wamesema kwa mtu aliyeyasema maneno hayo: hatakusamehe Mwenyezi Mungu." [Matwalib Uliy Anuha katika Sharh Ghayat Al Muntaha 897/1, Ch. Al Maktab Al Islamiy]
Na kutokana na hayo yaliyotangulia: kusoma kwa sauti au kumtaja Mwenyezi Mungu kwa dhikiri nyuma ya jeneza ni jambo linalochukiza na inapendeza kufanya hivyo kwa siri au kimya kimya. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi ya wote.