Maneno ya Mwanamke Redioni na Kutaja Jina Lake.
Question
Je, inaruhusiwa kwa wanawake kuzungumza Redioni kwa sauti laini ambapo husikilizwa na wanaume wasio ndugu zao na wakayajua majina yao?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Inaruhusiwa kusikia sauti ya mwanamke kwa mujibu wa hukumu ya Sheria, lakini hairuhusiwi kwa mwanaume kuisikia sauti ya mwanamke ikiwa mwanamke huyo atachelea fitina kwa nafsi yake. Basi ni haramu kwa mwanamke kuregeza sauti yake kwa ajili ya kuchochea fitina.
Hivyo, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema} [AL AHZAB: 32]
Ibn Katheir katika tafsiri yake [6/409, Dar Taibah] alisema kuwa: “Maana ya hayo ni kwamba: Mwanamke atazungumza na watu wasio ndugu zake kwa sauti isiyo laini, kwa maana kuwa hairuhusiwi kwa mwanamke kuzungumza na wanaume wasio kuwa ndugu zake kama anavyomzungumza na mumewe”.
Kwa hivyo, maneno mazuri yameruhusiwa, na maneno yaliyoregezwa hayaruhusiwi. Kwa hivyo, Masahaba walikuwa wakisikiliza Hadithi kutoka kwa Mama wa Waumini na wengine wakisikiliza kutoka kwa Masahaba, na watu waliokuja baada yao walifuata mtazamo huo.
Wanavyuoni walisema kama tulivyosema hapo juu:
Ibn Abdein katika kitabu chake [1/271, Ihyaa Al-Turath] amesema: “Kauli yake” Sauti ya mwanamke … yaani sauti yake siyo uchi”.
Al-Dusuqi Al-Malki katika kitabu chake Al-Sharhul Kabiir [1/195, Darul Fikr] alisema: “Pengine inasemekana kuwa sauti ya mwanamke siyo uchi kwa kweli kufuatana na Hadithi ya wanawake wa Masahaba, lakini ni kama uchi katika uharamu wa kuifurahia”.
Imam Abu Abbas Al-Qurtubi Al-Malki katika kitabu chake amesema: “Tuliposema kuwa sauti ya mwanamke ni uchi asiyefahamu vizuri anaweza kufikiri kuwa tunakusudia maneno yake, na hivyo sivyo, tunawaruhusu wanawake kuzungumza na wanaume wasio zao kama kuna haja ya kuafanya hivyo, na hatuwaruhu kuzungumza kwa kuregeza sauti zao, kwani hali hii huchochea matamanio ya wanaume, kwa ajili hii, wanawake hawaruhusiwi kuadhini” [Ibn Abdein 1/271].
Al-Khatib Al-Sherbini Al-Shafi katika kitabu cha Mughni Al-Muhtaaj [3/129, Darul Fikr] alisema: “Sauti ya mwanamke siyo uchi na inaruhusiwa kuisikiliza kama hatuchelei fitina”.
Muhtasari: Sauti ya mwanamke siyo uchi, na kama mwanamke anazungumza bila kuregeza sauti yake, basi anaruhusiwa kuzungumza na kusikilizwa na wanaume wasio ndugu zake, ama kuhusu kujua jina lake hakuna ubaya wowote kwa mujibu wa Sheria. Na hawa ni wake zake Mtume S.A.W. walitupokelea Sunna ya Mtume S.A.W, watu wote waliyajua majina yao, na kama pangekuwa na ubaya wowote, basi wasingeyatoa majina yao moja kwa moja.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.