Kati ya Hekima na Kujiepusha na Ana...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kati ya Hekima na Kujiepusha na Anasa.

Question

Maneno mengi huzungumzwa kuhusu kujiepusha na anasa, ni nini hasa maana yake na kuna mfungamano gani kati yake na hekima? 

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Waislamu waliosafi (wenye kuufuata Uislamu itakiwavyo) wametoa mifano mingi katika suala hili na kuinukisha dunia manukato mazuri kwa yale matukio ya ucha Mungu yaliyopokewa kutoka kwao ambayo ndani yake ilizalika hekima. {Yeye humpa hekima amtakaye; na aliye pewa hekima bila ya shaka amepewa kheri nyingi. Na hawakumbuki ila wenye akili} [AL BAQARAH 269].
Wacha Mungu wakubwa wanaashiria kuwapo mfungamano mkubwa kati ya kujiepusha na anasa na hekima, kwa kutoa ushahidi wa Hadithi iliyopokelewa na Abu Khalad (Mwenyezi Mungu amwie radhi) kutoka kwa Mtume ( rehema na amani zimshukie) amesema: “Mnapomuona mtu amepewa uwezo wa kujiepusha na anasa za dunia na uchache wa maneno, basi mtu huyo huwa anatamka hekima.” [Imepokewa na Ibnu Majah, Hadithi ya 4101- mapokezi dhaifu].
Na kwa kupitia maelezo haya itafahamika kuwa maana ya hekima ni yale ambayo Mwenyezi Mungu humpa muumini katika mambo ya utulivu wa kimawazo, kiakili na kimatendo.
Na kujiepusha na anasa hakumaanishi maana moja ambayo itatumika kwa watu wote, kwani wapo wanaoamini kuwa kujiepusha na anasa ni kule kuacha yaliyoharamisha pekee, kwa kuwa mambo ya halali yanafaa kuyatenda kwa upande wa Mwenyezi Mungu. Mwenyezi Mungu anapomneemesha mja wake kwa mali ya halali na akawa (mja) anaemuabudu na kumshukuru kwa mali hiyo,na kisha akaiacha mali hiyo kwa hiari yake kwa ajili ya Mwenyezi Mungu basi huwa halazimishwi kwa kuwa ni hiari yake.
Wengine wanaona kuwa kujiepusha na anasa katika mambo ya haramu ni jambo la lazima (wajibu), ama katika mambo ya halali ni kitu (jambo) lililo bora. Mja kupungukiwa na mali na akawa na subira kwa hali aliyonayo na akaridhika kwa kile akitowacho na kukigawa, na akawa mja amepewa uwezo na Mwenyezi Mungu wa kujiepusha pia na anasa za kilimwengu atakuwa kweli amejiepusha na anasa za kidunia. Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema {Sema: Starehe ya dunia ni ndogo,na Akhera ni bora zaidi kwa mwenye kumcha Mungu. Wala hamtadhulumiwa hata uzi wa kokwa ya tende} [AN NISAA; 77]. Na aya nyingine zinazozungumzia juu ya uduni wa dunia na kujiepusha nayo.
Pia kujiepusha na anasa kumetafsiriwa kuwa ni: Pindi mja anapotoa sadaka katika mali yake kwa ajili ya kumcha Mungu na akawa anaivumilia hali aliyonayo na kujiepusha namambo yaliyokatazwa na sheria wakati ana uwezo wa kufanya hivyo, hapo ndipo ile sifa ya kuwa mja aliyejiepusha na anasa za kidunia inapokuwa imekamilika.
Wengine wakasema kuwa kujiepusha na anasa si kuviacha vitu vya halali kwa hiari yakemja, na wala si kutaka ziada kwa asichokihitajia, kwani hali ya kusubiri huwa ni bora kwa aliye fakiri na hali ya kushukuru huwa ni bora kwa mwenye mali.
Na hapa tutaona kuwa kuna tofauti ya maana ya kujiepusha na anasa nayo ni kwa sababu inaweza kutumika kwa maana nyingi sana zilizo tofauti.Kwa ajili hiyo, mitazamo ya maana yake ni mingi. Na kila mwanachuoni ameuelezea kwa mujibu wa zama zake, isipokuwa pamoja na kuwa na mitazamo tofauti ila lengo lake ni moja nalo ni kule mja kuwa na mema mengi yatakayomsaidia mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kwa mfano Imamu mkubwa Sufiyan Thaury anaona kuwa, kujiepusha na anasa ni kule kufupisha tamaa na sio kula chakula kikavu (bila ya kitoweo) na wala sio kuvaa nguo chakavu.
Wengine wanaona kuwa kujiepusha na anasa kuliko sahihi ni kama ilivyoelezwa katika Qur`ani tukufu: {Ili msihuzunike kwa kilicho kupoteeni, wala msijitape kwa alicho kupeni} [AL HADID; 23]. Asiyependa anasa huwa havifurahii vilivyomo duniani na wala hakati tamaa kwa alivyovikosa.
Imamu Abdallah BinMubarak anatuletea ufahamu mwingine juu ya kujiepusha na anasa kwa kusema; “kujiepusha na anasa ni kuwa na imani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kupenda umasikini, kwani mja hawezi kuwa mchamungu wa kweli mpaka awe na imani kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu.
Na kujiepusha na anasa kwa mtazamo wa kiislamu ni; “kupatikana utulivu wakati wa kuwa unamiliki na kuusahaulisha moyo kutokana na sababu za matamanio, ili mja apate wepesi wa kuacha vishawishi vya dunia na pia itamlazimu aiangalie dunia kwa jicho la dharau ili iwe ndogo (duni) katika upeo wa macho yake".
Na kwa namna hiyo ndio Yahya Bin Muadh anaona kuwa hakuna ambaye atafikia na kujua uhakika wa kujiepusha na anasa za dunia mpaka awe na mambo matatu; “Kutenda bila ya kuangalia masilahi, kusema bila ya kuwa na tamaa (ya kupata vitu) na kuwa na nguvu bila ya kuongoza.” Na kuna mtu aliuliza “Lini nitakuwa katika wanaomtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuvaa vazi la kujiepusha na anasa za ulimwengu na kukaa na wacha Mungu? Yahya BinMuadh akamjibu, “Pindi utakapoiwezesha nafsi yako kwa siri kiasi ambacho lau kama Mwenyezi Mungu Mtukufu atakukatiza riziki kwa siku tatu basi nafsi yako haitadhoofika, ama kwa asiyefikia kiwango hiki basi kukaa pamoja na wachamungu ni kama kupoteza muda wake, nakisha ingawa hakuna uhakika pengine muda wowote anaweza kufedheheka.”
Na kujiepusha na anasa kuna daraja:-
Daraja ya mwanzo ni kuacha ya kila kilichoharamishwa. Daraja ya kati ni kuacha mambo yaliyozidikatika mambo ya halali. Na daraja la juu kabisa ni kuacha yale yote ambayo yatamshawishi mja kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu.
Hivyo ni wajibu kwa muislamu kujiepusha katika kuyakaribia aliyoyaharamisha Mwenyezi Mungu, na ajaribu kuwa makini na mambo ya halali ili yasije kumchanganya na pia aiwezeshe nafsi yake katika jambo hili.
Aliyeamua kuacha anasa basi huwa muislamu aliyekamilika Uislamu wake natabia zake. Kuacha anasa pamoja na kuwa na subira ni silaha kubwa kwa muumini kwani huhifadhi heshima yake. Kwa maana hiyo, muislamu kwa kuacha kwake anasa na akawa na subira, atakuwa na uwezo wa kuvumilia yote yanayoweza kuharibu utu wake.
Na muislamu awapo na sifa hii ya kutopenda anasa basi atasifika kwa sifa nyingi nzuri ambazo zinapendwa kisheria. Na bila ya kuwa na tabia hii ya kuacha anasa muislamu hataweza kusifika kwa sifa zenye kuathirikwani mtu anapoandamana na sifa maalumu basi si lazima imuathiri.
Hakika wacha Mungu na waliojiepusha na anasa za dunia ambao baadae wakajulikana kama ni Masufi, hawakujiweka mbali na mafunzo ya kiislamu, ni sawa iwe kwa kiasi kidogo au kwa kiasi kikubwa, isipokuwa tumeona kutoka kwao mifano mizuri ya kufuata mafunzo ya dini ikiwemo kujikinga na kujiepusha na kuacha kuandamana kwa kupenda vitu ambavyo hupelekea kuvishikilia sana mpaka kuathiri au kama tuitavyo katika zama zetu hizi ugonjwa wa kupindukia.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.
Chanzo: Profesa; Abdullatif Abdu, Dirasaat fiy Alfikri Al Islaamiy, Kairo. Maktaba ya Anglo Misria 1977 A.D. (Uk. 39-43)

 

 

 

Share this:

Related Fatwas