Athari ya Maasi Inaweza Ikawa Bora ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Athari ya Maasi Inaweza Ikawa Bora Zaidi Kuliko Athari ya Utiifu.

Question

Ni nini maana ya kauli ya Ibn Atwaa-a Allah katika kitabu chake cha: [Al Hekima]: "Maasi yaliyomrithisha mtu udhalili na ufukara ni bora kuliko utiifu uliomrithisha mtu majivuno na kiburi". Na je, hayo yanaafikiana na Misingi ya Sheria na Dini, au ndani yake kuna kujisifu kwa ajili ya kufanya maasi na Mwenyezi Mungu Mtukufu atukinge nako? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Hekima za Ibn Atwaa-a Allahi Asakandariy R.A., ni miongoni mwa mambo yenye faida zaidi kuliko yaliyoandikwa vizuri katika mambo ya hakika ya Tauhid, na kuisifu njia ya mja ya kwenda kwa Mola wake. Mmoja miongoni mwa wanaozieleza; Bwana wetu Sheikh Ahmad Azab Asharnubiy anasema: "Hekima za Ibnu Atwaa-a ni manufaa ya kweli ya juu anayoweza kuyafikia Muridi katika kuijua njia ya wajuzi ipelekeayo kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu Mmiliki wa Arshi Tukufu; kwa kujumuisha kwake mambo nyeti ya Upwekeshaji ulio Mtakatifu, pamoja na kufupisha maelezo yake mazuri na mepesi" [Hekam Ibn Atwaa-a Allah Asakandariy, Sharhu wa Tahkik Sheikh Abdulmajed Asharnubiy, Uk.3 Ch. Maktabatu Al Qahirah].
Ama kuhusu suala la Utiifu na Maasi Mwenyezi Mungu Mtukufu ameamrisha atiiwe, na akaufanya utiifu kuwa sababu ya kufuzu radhi pamoja na pepo yake, na sababu ya kusuhubiana na Mitume amani iwe juu yao, na Wasema kweli na Mashahidi.
Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na anaye mt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, Yeye atamtia katika Pepo zipitazo mito kati yake, wadumu humo. Na huko ndiko kufuzu kukubwa} [AN NISAA 13]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume, hao wapamoja na wale aliowaneemesha Mwenyezi Mungu miongoni mwa Manabii, na Wasemakweli, na Mashahidi, na Watu wema. Na uzuri ulioje kuwa pamoja na watu hao!} [AN NISAA 69]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Na wenye kumt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na wakamwogopa Mwenyezi Mungu na wakamcha, basi hao ndio wenye kufuzu} [AN NUUR 52]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Na anayemt'ii Mwenyezi Mungu na Mtume wake, bila ya shaka amefanikiwa mafanikio makubwa} [AL AHZAAB 71]
Na Mola wetu akataza Maasi, na kuyafanya kuwa ni sababu ya kutumbukia katika ghadhabu na hasira zake, na kukumbwa na adhabu yake ya Akhera, na akafanya maasi kuwa ni alama ya upotevu wa wazi. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na anaye muasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake, na akaipindukia mipaka yake, (Mwenyezi Mungu) atamtia Motoni adumu humo, na atapata adhabu ya kudhalilisha} [AN NISAA 14]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Na mwenye kumuasi Mwenyezi Mungu na Mtume wake basi hakika amepotea upotofu ulio wazi} [AL AHZAAB 36]
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Akajaalia moyo kuwa ndio msingi, na kwa moyo huo kunategemewa kupelekea ukaribu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu; Basi Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Kwani hakika si macho yanayo pofuka, lakini zinazopofuka ni nyoyo ziliomo vifuani} [AL HAJ 46]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Ndio hivyo! Na anayetukuza ibada za Mwenyezi Mungu, basi hayo ni katika unyenyekevu wa nyoyo} [AL HAJ 32], Na Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Ili Mwenyezi Mungu ayajaribu yaliyomo vifuani mwenu, na asafishe yaliyomo nyoyoni mwenu. Na Mwenyezi Mungu anayajua yaliyomo vifuani} [AAL IMRAAN 154]
Na Mtume S.A.W. anasema: "Hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu hatazami nyuso na mali zenu lakini anatazama nyoyo na kazi zenu", [Imetolewa na Imamu Muslim katika kitabu chake Sahihi].
Na Mtume S.A.W., anasema: "Tambueni kuwa katika mwili kuna pande la nyama iwapo litasalimika basi mwili mzima utasalimika, na likifasidika basi mwili mzima utafisidika, tambueni kuwa pande hilo la damu ni Moyo". [Mutafaqu alaihi].
Na Maasi yaliyowajibisha udhalili ni bora kuliko utiifu uliowajibisha majivuno na kiburi. Kwani kusudio la utiifu ni unyenyekevu na hushui ni kujinyenyekeza na kujidogesha kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu. Na katika Hadithi: "Mimi ni pamoja na wale wenye miyoyo inayonyenyekea", [Imepokelewa na Abu Nuaim katika kitabu cha Al Heliah, Ina hukumu ya Mauquufu].
Basi tunda la utiifu ni kujinyenyekeza na kujidogesha, na tunda la maasi ni ukali na kiburi. Kwa hivyo basi matunda yakigeuka, uhalisia hugeuka pia na utiifu ukawa maasi na maasia yakawa utiifu.
Na utiifu unapoepukana na maana hizi husifika kinyume chake. Kwa hiyo maasi yanayowajibisha maana hizi ni bora zaidi yake; kwani hakuna Zingatio kwa sura ya utiifu au ya maasi, isipokuwa katika kinachozalikana kutokana navyo moyoni. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Siku ambayo kwamba mali hayatofaa kitu wala wana. Isipokuwa mwenye kumjia Mwenyezi Mungu na moyo safi} [AS SHURAA 88-89].
Kwa hiyo maasi ya moyo ni hatari zaidi kuliko maasi ya viungo vya mwili, kama ambavyo maasi ya viungo hudhihirisha magonjwa ya moyo yanayopaswa kutibiwa; kwa hivyo, viungo husalimika pale moyo unapokuwa salama. Na utiifu wa dhahiri wa viungo unaweza kuzua maasi ya hatari mno moyoni kama mtu hajazindukana na akawa mkweli kwa utiifu wake, wakati ambapo maasi yanaweza kufuatiwa na aina za utiifu zenye manufaa iwapo mtu atazinduka na akamtegemea Mola wake.
Basi katika hadithi tukufu kutoka kwa Abu Hurairah R.A. anasema: Mtume S.A.W anasema: "Naapa kwa yule ambaye nafsi yangu iko mikononi mwake hata kama msingelifanya makosa basi Mwenyezi Mungu Mtukufu angelikuondosheni akawaleta wengine wenye kufanya makosa wakamwomba msamaha na akawasamehe". [Imepokelewa na Muslim].
Na kauli ya Ibn Atwaa-a Allahi AS Sakandariy: "Maasi yaliyomrithisha mtu udhalili na ufukara ni bora kuliko utiifu uliomrithisha mtu majivuno na kiburi" yana hekima na faida kubwa, haifahamiki kwa maana yake sahihi iliyo kamili zaidi isipokuwa kuiunga kwa hekima inayoitangulia, ambapo Bwana wetu Ibn Atwaa-a Allaahi As Sakandariy alisema katika hekima iliyotangulia: "Mola wetu amekufungulia mlango wa utiifu na hajakufungulia mlango wa kukubaliwa, huwenda amekuamulia dhambi ikawa ndio sababu ya kufikia huko".
Sheikh Ibn Abaad An Nafaziy Ar Randiy katika maelezo hekima hiyo: "Na Hiyo ni kwa kuwa utiifu unaweza kufanana na maafa makubwa kwenye unyenyekevu ndani yake, na kuutegemea, pamoja na kumchukia asie utekeleza. Na dhambi inaweza kufananishwa na kumrejea Mwenyezi Mungu Mtukufu na kumwomba radhi na kujidhalilisha yeye mwenyewe, na kumtukuza yule ambaye hajafanya, hivyo huja ikawa sababu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kumsamehe na yeye kumfikia; na mja anapaswa kutoangalia sura za vitu, bali aangalie uhalisia wake". [Sharhu Sheikh Mohamad Bin Ibrahim anayejulikana kwa Ibn Abad An Nafaziy Ar Randiy Ala Kitab Al Hekam 74/1, Ch. Muswtafa Al Babiy Al Halabiy]
Kisha Ibn Atwaa-a Allah R.A. alitilia mkazo juu ya maana hiyo katika hekima hiyo ambayo ni mahali iko mahala pake: "Maasi yaliyomrithisha mtu udhalili na ufukara ni bora kuliko utiifu uliomrithisha mtu majivuno na kiburi",
As Sharhu Arendiy – Mwenyezi Mungu Mtukufu Alimrehemu – anasema: "Hapana shaka kwamba udhalili na ukata ni katika sifa za utumwa, na kupatikana kwake kunapelekea kufikia uwepo wa Mwenyezi Mungu, wakati ambapo Utukufu na kiburi ni katika sifa za Uungu, na upatikanaji wake unategemea kuvunjika nguvu na kutokukubali. Abu Madian – isafike siri yake – anasema: "Kujidogesha kwa asi ni bora zaidi ya kujivuna kwa mtiifu". [Sharhu Ibn Ibad Ala Hekam 74/1]
Na Kutokana na hayo, hakika hekima ya Imamu Bi Atwaa Allahu Sakandariy R.A, inaafikiana na Misingi ya Dini, na Malengo Makuu ya Sheria Tukufu, na mambo nyeti ya Maadili yaliyonyooka; hiyo ni hekima ambayo maana yake haipingani na haya yote, bali inaungana nayo na kuyathibitisha. Na ndani yake hakuna kuyasifia maasi na kukemea utiifu kwa mbali au kwa karibu au kwa mbali, isipokuwa hutanabahisha juu ya kuuchunga moyo, na kujiepusha na kujiona baada ya utiifu, pia hutanabahisha juu ya kujisogeza kwa Mola na kutubu baada ya kutumbukia makosani.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas