Upimaji na Kutoa Hukumu
Question
Katika baadhi ya wakati tunasoma katika tafiti za kisasa za kifiqhi kwamba hukumu ya suala fulani kwa mujibu wa upimaji na suala lengine ni hivi au ni kadha, na kwamba hukumu ya suala lile kwa mujibu wa utoaji wa hukumu kufuatana na Madhehebu ya Al-Shafi kwa mfano ni hivi au kadha, basi tofauti gani kati ya utoaji wa hukumu na upimaji?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu:
Al-Qiyas maana yake katika lugha ni upimaji, ambayo inaashiria kupima kitu kwa kitu kingine. [Rejea: Mu’jam Maqayiis Al-Lugha kwa Ibn Fares 5/40, Darul Fikr].
Na katika istilahi imesemekana kuwa: Ni usawa wa suala fulani na suala lengine katika sababu ya hukumu au kuongeza katika maana inayozingatiwa katika hukumu. Imesemekana pia: Ni kupima suala linalojulikana kwa suala lengine katika kuthibitisha au kukataa hukumu au maelezo ya hukumu.
Wanavyuoni wametofautiana katika maana ya upimaji, hata Imam wa Al-Haramain alisema, kipimo hakiwezi kuwa na kikomo halisi; kwa sababu inahusisha mambo mbalimbali, kama vile; hukumu, sababu, suala linalopimwa na uhusiano. [(Al-Bahru Al-Muhiit kwa Al-Zrkashi 5/7, Dar Al-Kutbi, na Nihayatul Suul kwa Al-Isnawi 3/3, Alam Al-Kutub].
Upimaji umehitajika wakati yalipozidi masuala mapya ambayo matini za Kisheria hazikubainisha hukumu za masuala haya. Mara nyingi suala lililo jipya halina hukumu wazi. Kwa hivyo, ilikuwa muhimu kupata hukumu kwa njia ya matini zisizo za moja kwa moja, kwa njia ya upimaji ambao ni chanzo cha dalili za hukumu ya nne zilizokubaliwa na wanavyuoni wa Madhehebu manne yanayofuatwa na wengi wa Maulamaa wa Uislamu, ambayo ni: “Qurani, Sunnah, makubaliano ya Wanavyuoni na upimaji”, Hakuna mgogoro miongoni mwa wanavyuoni kwamba upimaji ni hoja katika mambo ya kidunia kama vile chakula na dawa. Lakini upimaji katika hukumu za kisheria wakati hakuna matini wala hakuna makubaliano, katika hali hii wengi wa Masahaba, wafuasi, idadi kubwa ya wanavyuoni na wanafiqhi wanasema kwamba upimaji wa kisheria ni chanzo miongoni mwa vyanzo vya sheria, kinachothibitishwa na hukumu ambayo haikusikika. Imepokelewa kutoka kwa Imam Ahmed kwamba alisema: “Hakuna yeyote anayeweza kuishi pasipo na kutumia upimaji”. [Rejea: Al-Bahr Al-Muhiit 5/16, na Al-Tahsiil mina Al-Mahsuul kwa Siraaji Diin Al-Rmoy 2/159, Muasastur Resalah, na Irshaadul Fuhuul uk. 185, Mustafa Al-Halabi].
Nguzo za upimaji ni nne, nazo ni: Suala linalopimiwa, suala linalopimwa, hukumu na sababu. Asili ni hukumu inayopimiwa kwa ajili ya kuwepo kwa matini za kisheria zinazohusiana nayo. Suala linalopimwa: Ni jambo au suala linalohitajika kujua hukumu yake na hakuna matini za kisheria kwake. Hukumu: hiyo inathibitishwa na sheria mwanzo kama uharimisho wa mvinyo. Na Sababu: ni maelezo kamili kati ya suala linalopimiwa na suala linalopimwa [Irshaadul Fuhuul kwa Al-Shawkani uk.204, na Al-Bahr Al-Muhiit 5/83].
Kwa mfano, uharimisho kabisa kila kinachoharibu akili -kama bia - kwa ulinganisho na mvinyo, asili hapa ni mvinyo inayotajwa hukumu yake katika matini za Sharia; Qur'ani na Sunna, na suala linalopimwa ni bia ambayo haikutajwa na matini wazi, ama hukumu ni uharimisho kwa mujibu wa upimaji wa uharimisho wa mvinyo uliotajwa katika matini za Sheria, na sababu ni ulevi na uharibifu uliosababisha kukataliwa mvinyo, sababu ni hii hii iliyotokea pia katika bia. Huo ni mfano unaoeleza haja ya kupima kwa dharura ya kujua hukumu ya Kisheria kuhusu kila linalojitokeza miongoni mwa masuala mapya, kwa sababu hakuna suala jipya halina hukumu ya Mwenyezi Mungu. Mwenyezi amesema: {Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu,na rehema, na bishara kwa Waislamu} [AN-NAHL: 89].
Imam Al-Haramain anasema katika kitabu chake: [Ghaithul Umam, Uk. 310, Daru Al-Dawah]: “Inaaminiwa kwamba hakuna tukio lolote linalotokea ila lina hukumu yake katika sheria”.
Upimaji unategemea kufahamu fiqhi, kujua siri za sheria, makusudi yake, na sababu za hukumu zake vizuri sana, kwa hiyo, siyo kila mmoja anaweza kutoa dalili kupitia upimaji wa hukumu za Kisheria, bali ni kazi ya wanavyuoni ambao tayari wameshafikia cheo cha jitihada tu, kama vile Maimamu wanaofuatiwa, kama vile; Abu Hanifa, Malik, Shafiy, na Ahmad R.A.
Na kwa sababu ya uhaba wa wenye jitihada, inahitajika kinachojulikana utoaji hukumu kwa mujibu wa madhehebu ya mwenye jitihada, au jitihada katika madhehebu maalumu, hali hii inafanana na upimaji ambapo inapimiwa suala linalotajwa katika matini za Kisheria na suala lengine lisilotajwa, na tofauti kati ya upimaji na utoaji hukumu ni kwamba suala hili limetajwa kwenye matini za Imam huyu mwenye jitihada, na halikutajwa katika matini za Kisheria; Qur`ani na Sunna, kama katika upimaji. Ambapo mwenye kutoa hukumu hafiki cheo cha mwenye jitihada ili aweze kupima masuala yanayotajwa katika Sheria, lakini inafahamika hukumu za masuala mapya kupitia misingi iliyothibitishwa na Maimamu wenye jitihada kwa ajili ya kufahamu hukumu za Sheria, sababu zake, na makusudi yake.
Ibn Badran kutoka madhehebu ya Hanbali ametaja katika kitabu chake: [Al-Madkhal Ila Madhehabul Imam Ahmad, Uk. 35, 140 Muasastur Resalah]: “Usemi wa “Utoaji hukumu” uko katika maneno ya wanavyuoni na wanafiqhi, nao ni aina ya utoaji maana: yaani kutoa hukumu kutegemea matini zilizotajwa na Imam mwenye jitihada, au kutegmea misingi ya Imam wa madhehebu maalumu kama vile misingi iliyochukuliwa au Sheria au akili pasipo na hukumu iliyotajwa na Imam huyo. Mifano ni pamoja na: kupima kwa msingi wa “Kutoamuru kwa kazi isiyowezekana kufanywa”.
Kutokana na yaliyotangulia hapo juu, inaonesha kuwa kuna tofauti kati ya upimaji na utoaji wa hukumu, ambapo upimaji katika istilahi ni chanzo kimoja miongoni mwa vyanzo vinne vinavyokubaliwa na Wanavyuoni wengi ambacho hategemewa kwake isipokuwa mwenye jitihada katika fatwa zake, na jitihada zake za Kifiqhi, wakati ambapo utoaji wa hukumu ni kama upimaji katika sura yake tu, na unahusiana na mwenye jitihada katika madhehebu moja miongoni mwa madhehebu ya Maimamu kwa ajili ya kufikia hukumu ya Kisheria inayohusu masuala mapya yasiyotajwa kwa njia ya moja kwa moja katika Qur`ani na Sunna kupitia misingi ya Imam mwenye jitihada na misingi ya kufahamu Sheria na makusudi yake katika madhehebu haya.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.