Ni Upi Usahihi wa Hadithi hii: “Si...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ni Upi Usahihi wa Hadithi hii: “Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu ambaye kila kitu kinamnyenyekea kwa utukufu wake”? Na ipi hukumu ya kuitekeleza?

Question

Ni upi usahihi wa Hadithi ya: “Anayesema: Alhamdulillahi ambaye kila kitu kinamnyenyekea kwa utukufu wake, na Alhamdulillahi ambaye kila kitu kimedhalilika kwa enzi yake, na Alhamdulillahi ambaye kila kitu kimeinama kwa milki yake, na Alhamdulillahi ambaye kila kitu kimejisalimisha kwa uwezo wake, akisema hivi kwa ajili ya kuomba lililoko kwa Mwenyezi Mungu, basi Mwenyezi Mungu atamwandikia mema elfu moja, na kumpandishia ngazi elfu, na kuwaamuru Malaika elfu sabini wamwombee msamaha mpaka siku ya Kiyama”? Na nini hukumu ya kuitekeleza?

Answer

 Sifa njema ni za Mwenyezi Mungu na rehema na amani zimshukie Mtume wa Mwenyezi Mungu na Aali zake na Masahaba zake na waliomfuata, na baada ya hayo:
At-Tabaranit amepokea katika (Al-Mu’jam Al-Kabiir), kutoka kwa Abdillahi Ibn Umar RA, alisema: “Nilisikia Mtume S.A.W, akisema: Anayesema: Alhamdulillahi ambaye kila kitu kimenyenyekea kwa utukufu wake, na Alhamdulillahi ambaye kila kitu kimedhalilika kwa enzi yake, na Alhamdulillahi ambaye kila kitu kimeinama kwa milki yake, na Alhamdulillahi ambaye kimejisalimisha kwa uwezo wake, akisema hivi kwa ajili ya kuomba lililoko kwa Allah, basi Mwenyezi Mungu atamwandikia mema elfu, na kumpandishia ngazi elfu, na kuwaamuru Malaika elfu sabini wamwombee msamaha mpaka siku ya Kiyama”.
Hadithi hii Isnad yake ni dhaifu, kwa sababu miongoni mwa wapokeaji wake Ayyub Ibn Nuhaik, naye Hadithi yake huachwa, na Al-Baihaqiy vile vile aliitaja Hadithi kwa Isnad ndani yake Ayyub ibn Nuhaik, lakini kwa mabadiliko kidogo ya “Malaika elfu nne wamwombee msamaha mpaka siku ya Kiyama”, kisha akasema: Abu-Bakr Ibn Is-haq As-Sibghiy ameipokea kutoka kwa Ab-Shua’ib akisema katika Hadithi: “Mwenyezi Mungu atamwandikia mema elfu, na kumpandishia ngazi elfu”, ameipokea Yahya Ibn Abdillahi peke yake, naye si yenye nguvu, na Hadithi ina mashahidi mawili wenye ngazi ya (Muwquuf). [Al_Asmaa’ Was-Sifaat: 1/322, Ch. Ya Maktabat As-sawadiy].
Na shahidi Mauquuf, kutoka kwa Ibn Masu’ud, ameipokea Al-Baihaqiy kwa Isnad ndani yake Bakr Ibn Khunais, naye ni dhaifu, na lafudhi yake ni: “Mwenyezi Mungu atamwandikia mema elfu themanini, na kumfutia maovu elfu themanini, na kumpandishia ngazi elfu themanini”, vile vile ina shahidi mwingine Isnad yake ni dhaifu pia ameipokea At-Tabaraniy katika (Ad-Dua’a), kutoka kwa Umm-salamah RA, alisema: Mtume SAW, alisema kwa lafudhi ya: “Anayeisema itaandikwa kwake mema laki, na akifa roho yake itakuwa katika vibofu vya ndege kijani ambao huenda na kurudi katika Pepo kama wapendavyo”, na Isnad yake ni dhaifu pia, na katika (Al-Mu’jam Al-Kabiir) kwa lafudhi ya: “Itaandikwa kwake mema kumi’.
Al-Haithamiy aliitaja Hadithi hii katika [Majma’ Az-Zawaid], akasema: At-Tabaraniy aliipokea, na miongomi mwa wapokeaji ni Yahya Ibn Abdillahi Al-Babiltiy, naye ni dhaifu, na Al-Muttaqiy Al-Hindiy katika [kanz Al-U’mmaal], akasema: miongoni mwa wapokeaji ni Ayyub ibn Nuhaik, ambaye Hadithi yake ni Munkari, kama aliitaja Abu-Hamid Al-Ghazaliy katika [Al-Ihiyaa], na Al-hafidh Al-Iraaqiy katika upokeaji wake katika [Al-Ihiyaa] anasema: At-Tabaraniy aliipokea kutoka Hadithi ya Ibn Umar kwa Isnad Dhaifu, vile vile At-tabaraniy aliipokea katika [Ad-Dua’a], kutoka kwa Hadithi ya Umm Salamah, na Isnad yake pia ni Dhaifu”. [Al-Mughniy An Haml Al-Asfaar; Uk. 380, Ch. Ya Ibn Hazm].
Ibn Asakir aliitaja katika Tariikh yake [5/202, Ch. Ya Dar Al-Fikr], na Ibn Hajar katika [Lisaan Al-Mizaan], kutoka kwa Ibn Asakir, pamoja na Isnad yake, miongoni mwa wapokeaji wake ni Ayyub Ibn Nuhaik. [lisaan Al-Mizaan, na Ibn Hajar: 1/490, Ch. ya Muassasat Al-Aa’la, Bayruit].
Ingawa Hadithi hii ni Dhaifu, lakini inaingia katika msingi wa Sheria kuhusu matakwa ya kumtaja Mwenyezi Mungu kwa ujumla, na Mwenyezi Mungu alisema: {Na mumkumbuke Mwenyezi Mungu kwa wingi ili mpate kufaulu}. [Al Anfal: 45], na Hadithi za kuhimiza kumtaja Mwenyezi Mungu ni nyingi; Katika Hadithi ya Bukhariy na Muslim, kutoka kwa Abi-Hurairah RA, alisema: Mtume SAW, alisema: “Mwenyezi Mungu anasema: Mimi nipo katika dhana ya mja wangu, na Mimi ni pamoja naye wakati akinitaja, kama akinitaja nafsini mwake, nitamtaja nafsini mwangu, na akinitaja mbele ya kaumu ya watu, nitamtaja mbele ya kaumu ya watu bora kuliko wao”.
At-Tirmidhiy amepokea kutoka kwa Abid-Dardaa RA, kwa Isnad Marfuu’ alisema: Mtume S.A.W, alisema: “Je, nikuambieni kazi zenu ni bora sana, na zenye kutakasa kwa Mfalme wenu, na zenye kupanda kwa ngazi zenu, na bora sana kwenu kuliko kutumia dhahabu na fedha, na bora sana kwenu kuliko mnawalaki adui zenu, na hali mkizipiga shingo zao, na wao wakizipiga shingo zenu? Wakasema: ndiyo, akasema: kumkumbuka Mwenyezi Mungu”. Na Muslim amepokea Hadthi kutoka kwa Abi-Hurairah RA, alisema: Mtume SAW, alisema: “Al-Mufaridun wameshinda, wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, Al-Mufaridun ni nani? Akasema: wanaomkumbuka Mwenyezi Mungu kwa wingi, wanaume na wanawake”.
Hadithi dhaifu inaitekelezwa katika matendo mazuri, kama walivyosema hivi jamaa kubwa ya wanachuoni, miongoni mwao; Imamu Ahmad, Abdur-Rahman Ibn Mahdiy, Ibn As-Salaah, Ibn Taymiyah, Az-Zarkashiy, An-Nawawiy, Al-A’llaniy, na Ibn Daqiq Al-Iid, na waliwafuata jumla nyingine ya wanachuoni, kama vile: As-Sayutiy, Al-Haitamiy, na wengineo wengi.
Imamu Ibn As-Salaah anasema: “Inajuzu kwa mtazamo wa Wanachuoni wa Hadithi na wengineo kurahisisha katika Isnad na kupokea Hadithi zisizokuwa za aina za (Maudhui) miongoni mwa Hadithi Dhaifu, bila ya kujali kuonesha Udhaifu wake, isipokuwa Hadithi za Sifa za Mwenyezi Mungu, hukumu za Sharia za halali na haramu na nyinginezo; kama vile: mawaidha, visa, matendo mazuri, na maudhui zote za Targhibu na Tarhibu (kupendezesha na kuogopesha), na Hadithi zote zisizoambatana na Hukumu za Sharia na Imani. Miongoni mwa tuliopokea kwao urahisishi huu ni: Abdur-Rahman Ibn Mahdiy, Ahmad Ibn Hanbal, RA,”. [Muqadimat Ibn As-Salaah: 1/103, Ch. Ya Dar Al-Fikr].
Hivyo, Ofisi ya kutoa Fatwa ya Misri imechapisha Fatwa peke yake kuhusu suala la kuitekeleza Hadithi Dhaifu katika matendo mazuri, na Fatwa nyingine kuhusu kutekeleza katika Hukumu za Sharia.
Kwa mujibu wa hayo, Hadithi hii iliyopo katika swali, ingawa Isnad yake ni Dhaifu lakini inajuzu kutekelezwa kwayo, kutokana na maoni ya jumla kubwa ya Wanachuoni kuwa: inajuzu kuitekeleza Hadithi Dhaifu katika matendo mazuri.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi .

 

 

Share this:

Related Fatwas