Swala ya Jamaa na Mgonjwa Mwenye Ma...

Egypt's Dar Al-Ifta

Swala ya Jamaa na Mgonjwa Mwenye Maradhi ya Kuambukiza.

Question

 Ni ipi hukumu ya Sala ya Jamaa (pamoja) kwa mgonjwa mwenye maradhi ya kuambukiza, na anaogopa kuwakera watu na kueneza ugonjwa?

Answer

 Namshukuru Mwenyezi Mungu, rehma na amani ziwe kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu na kwa watu wake Masahaba wake na wale wenye kumfuata, baada ya hayo…
Uislamu umekuwa na shime kubwa ya kuwakusanya Waumini katika mambo yao na nguvu zao wao kwa wao ili wawe kitu kimoja sifa moja na nguvu kubwa katika kazi za kheri na kupambana na mambo ya shari, kutokana na hilo imekuwa ni alama muhimu za Uislamu zenye kuonesha shime hiyo ni uwepo wa Swala ya Jamaa au ya Pamoja.
Mola Mtukufu Amesema: {Na shikamaneni kwa Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu iliyo juu yenu: vile mlivyo kuwa nyinyi kwa nyinyi maadui naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu} [AAL IMRAAN: 103]. Na Akasema Mola Mtukufu: {Na shikeni Swala, na toeni Zaka, na rukuuni pamoja na wanao rukuu} [AL BAQARAH: 43]. Na Akasema tena Mola Mtukufu: {Enyi mlio amini! Mcheni Mwenyezi Mungu, na kuweni pamoja na wakweli} [AT TAWBAH: 119]. Wala haipaswi kwa Muumini kujitosheleza kuwa mkweli isipokuwa lazima awe karibu na Waumini wa kweli na ndani ya Swala zao za pamoja kwenye nyumba za Mwenyezi Mungu na katika utiifu kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu, Muumini haishi peke yake na kujitenga isipokuwa anaishi pamoja na umma kwa mfungamano mkubwa wa mahusiano.
Kutoka Hadithi ya Abi Ad-dardaai R.A. amesema: nimemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. anasema: “Hawapatikani watu watatu kijijini wala majangwani hawasimamishi ibada ya Swala isipokuwa wanakuwa wametawaliwa na shetani, basi ni juu yako Swala ya Jamaa kwani mbwa mwitu anakula mbuzi aliyejitenga” imepokelewa na Abu Dawud, An-Nisaai na Al-Hakim.
Na kutoka kwa Abi Huraira R.A. amesema: “Mtume alijiwa na mtu kipofu na akasema: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa hakika mimi sina mtu wa kuniongoza kunipeleka msikitini, akamwomba Mtume S.A.W. ampe ruhusa ya kuwsali nyumbani kwake, basi Mtume akamruhusu, alipogeuka yule mtu kutaka kuondoka Mtume S.A.W. alimwita na kumwuliza: je unasikia sauti ya adhana ya Swala? Akasema ndiyo, Mtume akasema: basi unalazimika” imepokelewa na Imamu Muslim.
Aya hizi na Hadithi hizi zinaonesha juu ya ukubwa wa Swala ya Pamoja au Swala ya Jamaa na umuhimu wake katika maisha ya Mwislamu, mpaka amesema Sahaba mtukufu Abdillah Ibn Masuud R.A. “Hakika mwenye kuepukana na Swala huyo ni mnafiki na umefahamika unafiki wake, au ni mgonjwa, na kama atakuwa ni mgonjwa basi atatembea akiwa na watu wawili mpaka afike kuswali”, na akasema: “Hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. ametufundisha mwenendo wa uogofu, na hakika mwenendo wa uongofu ni kuswali kwenye msikiti ambao unatolewa adhana” amepokea Imamu Muslim. Inamaanisha kuwa maradhi yamekuwa ni katika jumla ya sababu ya kuepukana na Swala ya Jamaa au ya pamoja, ikiwa maradhi ni yenye kuleta kero na adha kwa wenye kuswali au kuwapelekea kuondoka au kuwasababishia madhara basi inatakiwa kwa mgonjwa kujizuia na Swala ya Jamaa msikitini mpaka pale Mwenyezi Mungu Atakapomwondoshea maradhi hayo, kwani kuwaletea kero na adha Waislamu au kuwasababishia kupatwa na madhara ni kinyume na makusudio ya sheria kuhusu Swala ya Pamoja, kutoka kwa Jaabir Ibn Abdillah, toka kwa Mtume S.A.W. amesema: “Mwenye kula hiki –kitunguu thaumu – na akasema tena: mwenye kula kitunguu na kitunguu saumu, basi wala asikaribie msikitini kwetu, kwani Malaika wanakereka na yale yanayo wakera wanadamu” imepokewa na Bukhariy na Muslimu.
Na kutoka kwa Abi Said Al-Khudriy kuwa kilitajwa mbele ya Mtume S.A.W: Kitunguu na kitunguu saumu, na pakaulizwa: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, na kilichokuwa zaidi ya kitunguu saumu, basi utakiharamisha? Mtume S.A.W. akasema: “Kuleni, na mwenye kula miongoni mwenu basi wala asikaribie msikiti huu mpaka aondoe harufu inayotokana na hicho” imepokelewa na Abu Daud.
Wanachuoni wamepima na kulinganisha kwa njia ya kwanza kuzuiliwa mgonjwa mwenye maradhi ya kuambukiza, kutokana na zuio linalopatikana kwenye Hadithi ya kero ya harufu ya kitunguu na kitunguu saumu, kwa sababu wenye kuswali wanakereka na kuudhika zaidi na mgonjwa aliyepata maradhi ya kuambukiza kuliko harufu mbaya inayotokana na kula kitunguu na kitunguu saumu, Mtume S.A.W. ameamrisha mwenye kula chochote katika hivyo basi asikaribie msikitini, na kutokana na Ibn Abbas R.A. amesema: amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu “Hakuna kudhuru wala kujidhuru” imepokelewa na Ibn Maja.
Na inasisitizwa kuzuiliwa kutokana na Hadithi ya Amru Ibn As-Sharid, kutoka kwa baba yake, amesema: katika ujumbe uliotoka Thaqiifu kulikuwa na mgonjwa wa mbaranga, alitumwa kwa Mtume S.A.W. “Hakika sisi tumekuridhia basi rudi” imepokelewa na Muslim. Pakasemwa ugonjwa wa mbaranga mara nyingi kwa kawaida ni wenye kuambukiza, na pakasemwa: ili asidhani yeyote kuwa ameambukizwa ikiwa amepatwa na ugonjwa wa mbaranga. (Hashiyat As-Sandy Ala Sunan Ibn Maja, 2/364, chapa ya Dar Al-Jil – Beirut).
Haya kumepatikana Hadithi mbili kwa nje kunaonekana kuwa zinapingana lakini ukweli kila moja inazungumza tofauti na nyingine, kutoka kwa Abi Huraira, pindi aliposema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.: “Hakuna kuambukiza wala imani mbaya ndani ya mwezi wa mfungo tano wala balaa litokanalo na ndege aina ya bundi” mtu mmoja mwarabu akauliza ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, basi inakuwaje kwa ngamia aliyekaa kwenye mchanga jangwani kisha akaja ngamia mwingine mwenye ugonjwa akaingia kwa wenzake na wakapatwa na ugonjwa? Akasema Mtume: “basi ni nani aliyemwambukiza yule wa kwanza?”
Na kutokana na Abi Huraira, kuwa hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: “Mgonjwa haambukizi maradhi kwa aliye mzima” imepokelewa na Muslim.
Amesema Imamu An-Nawawiy katika sharh sahih Muslim (14/213 – 214, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy): (wamesema jopo la wanachuoni kuwa, lazima kukusanya Hadithi hizi mbili ambazo zote ni sahihi, wakasema: njia ya kukusanya ni kuwa Hadithi inayosema hakuna kuambukiza kusudio lake ni kukanusha yale yaliyokuwepo zama za ujinga wakidhani na kuamini kuwa maradhi kwa asili ni yenye kuhama yenyewe na si kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, ama Hadithi inayosema Mgonjwa haambukizi maradhi mzima ikaelekeza kwenye ukaribu wa kutokea madhara kikawaida kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu na makadirio yake, kukanusha kwenye Hadithi ya kwanza kawaida ya kuhama na kuambukiza ugonjwa, na wala haijakanusha kupatikana kwa madhara wakati wa kuhama huko kwa makadirio ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kitendo chake, Hadithi ya pili ikaelekeza kwenye kuchukuwa tahadhari kutokana na madhara yanayopatikana kwa utendaji wa Mwenyezi Mungu na utashi wake pamoja na uwezo wake, basi haya ambayo tumeyataja katika kusahihisha Hadithi hizi mbili na kuzikusanya zote mbili ndio usahihi ambao umekubalika na Jamhuri ya wanachuoni na kuonesha mwelekeo”.
Hivyo basi maradhi au ugonjwa hauambukizi wala kuhama na kumpata mwanadamu isipokuwa ni kwa hukumu ya Mwenyezi Mungu na uwezo wake, kuna maradhi Mwenyezi Mungu Ameyafanya sababu ya kuambukiza ni kutokana na kuchanganyika au kwa maelezo ya kina zaidi ni kutokea ugonjwa kama huo kwa mtu mwingine lakini hilo ni kwa njia ya kawaida iliyopo kama vile athari ya moto ni kuunguza, maji ni kunywesheleza na chakula ni kushiba, hivyo kila athari na yanayofanana hakika yanatokea kwa kutaka kwake Mwenyezi Mungu, haya ndiyo yanayopaswa kuaminiwa, ama kwa mgonjwa mwenye ugonjwa wa kuambukiza anapaswa kuchukuwa tahadhari ya kutochanganyika na watu wazima ili asiwe sababu ya kupita kawaida kwao au sababu ya kutikisika kwa Imani zao kuwa hilo ni makadirio ya Mwenyezi Mungu na wala si kulipinga, ambapo mgonjwa wa kwanza kwa ukweli hausiki, lakini watu kawaida katika hali kama hii huondokana na maana hii na kuzidiwa na dhana mbaya na kutokea kati yao na mgonjwa ubaya na uovu.
Anasema Khatibu As-Sherbini katika kitabu cha: [Mughniy Al-Muhtaj Ala Maarifat Maani Alfadh Al-Minhaj, 1/476, chapa ya Dar Al-Kutub Al- Elmiya]: “Na huchukuliwa yale yaliyotajwa kuwa ni udhuru – kwa maana ya sababu ya kuacha Swala ya Jamaa – kwa harufu mbaya ya mdomo na harufu mbaya ya kikwapa hupewa hukumu kwa njia ile ya kwanza, na anasimamishwa na Swala ya Jamaa mwenye maradhi ya mbaranga na ukoma, kama alivyosema Az-Zarkashiy kwamba anapewa udhuru kwa maradhi hayo, kwa sababu kero na maudhi yanayotokana na maradhi ya ukoma na mbaranga ni makubwa zaidi kuliko ulaji wa kitunguu kitunguu saumu na mfano wake, amesema: Kadhi wa Iyaadh amenukuu toka kwa wanachuoni kuwa maradhi ya mbaranga na ukoma yanamzuia mgonjwa kwenda msikitini na kusali Swala ya Jamaa pamoja na kuchanganyika na watu”.
Na aliulizwa mwanachuoni Ibn Hajar Al-Haitimiy kuhusu maradhi hayo ya ukoma na mbaranga pamoja na mwenye kutoa harufu mbaya ya mdomo na kwapa je inaondoka kwao Swala ya Ijumaa na Swala ya Jamaa na kuzuiliwa kuziswali? Akajibu R.A. kwa kusema: “Ibn Al-Imad amenukuu toka kwa Masheikh wake kuwa, harufu mbaya ya mdomo na kwapa zinahukumiwa kama mwenye kula kitunguu saumu tena zaidi yake, akasema: na hata katika harufu ya nguo zake pia inachukiza, na kutokana na Malik amesema, yeyote mwenye kupatwa na mtihani wa maradhi ya mbaranga na ukoma naye akiwa ni mkazi wa kwenye madarasa ya kielimu, basi ataondolewa, kutokana na Hadithi inayosema: “Kimbia maradhi ya mbaranga kama vile unavyomkimbia simba” na Mtume S.A.W. alijiwa na mtu mwenye maradhi hayo ili kuja kumwunga mkono akasema: “Ninashika mkono wako hakika nimejikubalisha kwako” na imepokelewa kuwa Mtume alikula naye chakula, huenda ni uthibitihsho wa kufaa, ikiwa itafahamika, basi huzuiliwa mwenye maradhi haya kuswali Swala ya Ijumaa na Swala ya Jamaa na kunywa maji ya wapita njia mitaani, lakini hazuiliwi kuswali Swala ya Jamaa akiwa amesimama peke yake nyuma ya safu, na mtu mwingine anazuiliwa kusimama pamoja naye” [Al-Fatawa Al-Fiqhiya Al-Kubra, 1/240, chapa ya Maktabat Al-Islamiya].
Na kutokana na maelezo yaliyo tangulia ni kuwa: ikiwa itawezekana kwa mgonjwa mwenye maradhi ya kuambukiza kuhudhuria Swala ya Jamaa na kuchukuwa sehemu inayomwezesha kumfuata Imamu na akawa na uhakika kutowadhuru watu wengine, basi inafaa kwake kuswali jamaa, na kama ni tofauti na hivyo basi haifai kwake kuwaudhi Waislamu kupitia maradhi yake wala kuwasababishia madhara, hata ikiwa madhara ni yenye kusababishwa na hali ya kawaida, ambapo watu wengi ikaondoka akilini mwao kuwa kutokea kwa maradhi haya ni kutokana na kadari ya Mungu na wala sio uambukizaji na kuhama kwa maradhi kutoka kwa mgonjwa wa kwanza, na kutokea uadui au chuki tofauti na makusudio ya sheria takatifu ya Swala ya Jamaa na kueneza hisia za undugu na upendo kati ya Waislamu.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

 

 

 

 

 

Share this:

Related Fatwas