Hadithi ya Kuiweka Rehani Ngao ya M...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hadithi ya Kuiweka Rehani Ngao ya Mtume S.A.W kwa Myahudi.

Question

Nilisikia kutoka kwa baadhi ya watu kuwa: Hadithi ya kuiweka rehani ngao ya Mtume S.A.W, kwa Myahudi, ni Hadithi Munkari (Ina hukumu ya kukanushwa) na haikubaliki kiakili, lakini nilipouliza baadhi ya wanafunzi wa elimu waliniambia kuwa Hadithi hii ni miongoni mwa Hadithi zilizoko katika kitabu cha Imamu Bukhari. Je, Hadithi hii ni ya Imamu Bukhari, na Je Imamu Bukhari anapokea Hadithi Munkari? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Baadhi ya watu wanafaikiri kuwa wanaweza kuzitathmini Hadithi Tukufu za Mtume kwa mawazo yao wenyewe tu, na bila ya kuwa na elimu ya akili au ya matini inayowawezesha kufanya hivyo, na hii inasababishwa kwa baadhi ya mashaka ambayo wanayasikia au kuyasoma, na bila ya kuwa na elimu ya kutosha inayowawezesha kutofautisha kati ya mabaya na mazuri.
Kuhusu tathmini ya Hadithi za Mtume, haiwezekani isipokuwa kwa wanachuoni ambao walijifunza Elimu za Hadithi Tukufu, wakazoea kuzitumia, na kujaribu elimu zingine za Sharia, ambazo huwawezesha kufanya hivyo, kama vile elimu ya (Uhakiki wa Matini za Hadithi).
Hukumu ya Sharia kuhusu jambo hili ni kuharamisha kuizungumzia Hadithi kwa maoni binafsi tu, au kwa wasio wanachuoni, bali wajibu katika jambo hili ni kuomba Fatwa kutoka kwa wanachuoni wa Hadithi za Mtume, ambao walitumia maisha yao kuihudumusha elimu hii.
Dalili ya hayo kuwa Hadithi Tukufu asili yake ni Wahyi, na kama ikisemwa kuwa haya si maneno ya Mtume S.A.W. mwenyewe, basi jibu ni kuwa: matendo yake S.A.W., ni hoja, ikiwa njia yake ni Wahyi au yametegemezwa kwa Wahyi, kwa hiyo Mwenyezi Mungu anasema: {Bila shaka mnao mfano mwema (ruwaza nzuri) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana}. [AL AHZAAB: 21], hapo angalifanya yasiyojuzu kisheria asingalikuwa ruwaza nzuri.
Na mtu ambaye hakufahamu Hadithi basi ni wajibu awaulize wanachuoni, kwa kauli yake Mwenyezi Mungu: {Basi waulizeni wenye kumbukumbu (ya mambo ya zamani) ikiwa nyinyi hamjui.} [AL ANBIYAA: 7].
Kuhusu upokeaji: Hadithi ambayo waliipokea Imamu Bukhari, Muslim, na wengineo miongoni mwa wanachuoni wa Hadithi kutokana na njia za Al-Aa’mash, kutoka kwa Al-Aswad, kutoka kwa Aisha R.A, kuwa: Mtume S.A.W, alikinunua chakula kutoka kwa Myahudi kwa mkopo, na kumuwekea rehani ngao yake ya chuma. Isnadi hii ni sahihi, na wapokeaji wake wote ni waaminifu na wahusika mashuhuri.
Na Hadithi hii pia imepokewa kwa njia nyingine, kutoka kwa Anas Ibn Malik R.A., na ameipokea Imamu Bukhari na wengineo.
Kuhusu maana yake, hakuna kitu katika matini ya Hadithi kinachoweza kukanushwa, kwa sababu kuweka rehani kwa Myahudi na kwa mtu mwingine miongoni mwa wasio waislamu kunajuzu, na Mtume S.A.W., yeye mwenyewe aliamiliana nao katika miamala mingi, na dalili aliyemkodisha siku ya Hijrah alikuwa mshirikina.
Kama ambavyo kuacha kwake rehani kwa baadhi ya Masahaba zake hakukanushwi, kwa sababu uwekaji wa rehani kwa Mayahudi kulikuwa kwa ajili ya chakula ambacho ni shairi, na huwenda Sahaba aliona haya kuchukua rehani yake kutoka kwa Mtume S.A.W., kama vile Jabir aliyeona haya katika Hadithi ya ngamia, wakati Mtume S.A.W., alipomwomba kuwa anataka kumnunua ngamia wa Jabir, na jabir akaona haya, basi akakubali, na hali ya kuwa ngamia anafanya kazi ya kuchota maji ya kunywa, na kama ambavyo Mtume S.A.W., aliacha kuwaoa wanawake wa Madinah kwa sababu wana wivu mwingi, na hali ya kuwa yeye aliwasifu sana wanawake hao, na Aisha anasema: “Wanawake wa madinah ni wazuri sana”, na Hadithi imo katika Sahihi ya Imamu Bukhari.
Ni bora kwa mweye kuuliza aangalie kuwa: kuna baadhi ya watu wanataka kuitusi Sunna kwa njia ya kuitukana sehemu ya Sunna hiyo kwa ajili ya kuziangusha Sunna zote, na mbinu hii sio mpya, ni ya zamani sana, na kwa hiyo, wanaitazama historia ili waone kasoro yoyote ndani yake, iliyosemwa na waliotangulia na inayowasaidia hivyo. Abu Muhammad ibn Qutaibah, Mungu amrehemu, ametaja mfano wa kuipinga Hadithi hii ambapo baadhi ya watu wanasema: “Inakuwaje apate njaa, ambaye anamiliki mabustani saba yaliyo pamoja huko Al-Aliyah, na kisha akawa haoni wa kumkopa pishi za shairi, mpaka akaamua kuiweka ngao yake rehani? Abu Muhammad anasema: maoni yetu kuwa: hakuna ajabu katika hili, kwa sababu Mtume S.A.W., alikuwa akiwapendelea wengine sana kwa mali zake kuliko nafsi yake, na kuzigawanya kwa wahitaji miongoni mwa Masahaba, mafakiri na maskini, hasa wakati wa majanga yaliyowapata waislamu, wala hamnyimi mwenye kuhitaji, na katika hali ya utajiri alikuwa akitumia mengi, na alikuwa halimbikizi dirhamu”. Aliendelea kuzungumzia kujinyima kwa Mtume S.A.W, na anasa ya dunia, kisha akasema: “Bahili mwenye utajiri huenda akapata wakati wa dhiki, na hali ya kuwa ana mashamba, vyombo, na mikopo kwa wengine, kwa hiyo anahitajia kukopa, na kuweka rehani, basi inakuwaje mtu asiye na dirham kwa sababu ya kuwaliwaza watu na kutumia fedha katika majanga ya watu wengine ?!!
Na vipi waislamu na matajiri miongoni mwa Masahaba zake wanajua kuwa ana haja ya chakula, wakati yeye hajawajulisha kisa hicho na hajawaambia jambo hili? Na tunajionea hivi sisi wenyewe au kupitia wenzetu, kama tunavyomwona mtu anayehitaji kitu, kisha hamwambii hata mtoto wake wala jamaa zake wala jirani yake, na anaamua kuuza kitu cha thamani na kukopa kwa watu wa karibu na wa mbali.
Hakika Mtume S.A.W, aliiweka rehani ngao yake kwa Myahudi, kwa sababu Wayahudi wakati huo walikuwa wakiuza chakula, lakini Waislamu hawakuwa wanafanya biashara hiyo, kutokana na katazo la Mtume kwao la kuwazuia kuhodhi soko la chakula.
Ni lipi walilolipinga? Mpaka likawastaajabisha, na hata baadhi ya wajinga walimnasibisha Ala’mash kwa uongo kwa ajili yake?!”. [Taawiil Mukhtalif Al-Hadiith: Uk. 216-220, Ch. Ya Al-maktab Al-Islamiy, Muassasat Al-Ishraaq].
Na Ibn Hibban alipoipokea Hadithi hii katika kitabu chake [3/19, Ch. Ya Muassasat Ar-Risalah], aliiwekea anwani akisema: “kutaja habari ya Hadithi ambayo baadhi ya wapingaji waliwakashifu wanachuoni wa Hadithi, kutokana na kutofahamu maana yake’.
Hapo kwa kuwa Imamu Bukhari, Mungu amrehemu, alipewa elimu ya Fiqhi na Mwenyezi Mungu pamoja na elimu ya Hadithi, aliweka anwani nyingi ambazo zilidhihirisha faida nyingi za Fiqhi zinazofahamika kwa Hadithi hii, kwa hiyo aliipokea katika sehemu kadhaa za kitabu chake kilicho sahihi, miongoni mwake kauli yake: Mua’lla Ibn Asad, Abdulwahid, na Al-Aa’mash walituhadithia kuwa: tulitaja Rehani na Salam mbele ya Ibrahimu, akasema: Al-Aswad alinihadithia, kutoka kwa Aisha R.A., kuwa: “Mtume S.A.W, alinunua chakula kutoka kwa Myahudi kwa mkopo, na kumwekea rehani ngao yake ya chuma”.
Miongoni mwa anwani nzuri za Hadithi hii ni:
(Mlango wa Mtume S.A.W, kununua chakula kwa mkopo), na
(Mlango wa kununua chakula kwa mkopo)
Na tofauti kati yake ni kuepusha maana ya kutokea na hasa kwa Mtume tu, au kununua kwa mkopo kunapunguza uungwana, na (Mlango wa aliyenunua kwa mkopo hali ya kuwa hana malipo yake, au haikuwa mikononi mwake), na hii ni wazi.
Na An-Nasaiy aliweka anwani ya: Mtu kununua chakula kwa mkopo, na kumwekea muuzaji rehani ya malipo iwe mikononi mwake, na (mlango wa kuweka rehani mijini (sio mashambani).
Suala hili linahitajia Mwanazuoni wa Fiqhi; kwa sababu Aya iliyoitaja Rehani hakika iliambatana safari, kama alivyosema Mwenyezi Mungu: {Na kama mkiwa safarini na hamkupata mwandishi, basi (mdai) apewe (kitu kiwe) rahani mikononi mwake}. [AL BAQARAH: 283].
Kuhusu Hadithi hii ni dalili ya kujuzisha rehani mijini pia, na hii ni kutokana na kurahisisha katika hukumu za Sharia, ambapo, kwa kawaida, miamala mingi huwa inafanyika mijini.
Imamu An-Nawawiy aliweka anwani ya Hadithi hii kwenye Sharhu Sahihi Muslim, akisema: Mlango wa Rehani na kujuzu kwake mijini na safarini, na (Mlango wa aliyeweka rehani ngao yake).
Anwani hii inabainisha kuwa inajuzu kuweka rehani vitu vya aina ya silaha, na hii si haramu, na (Mlango wa kuweka rehani kwa Mayahudi na wengineo).
Anwani hii inabainisha kujuzu kwa muamala na asiye mwislamu, na Imamu An-Nasaiy aliiweka anwani ya: Kuahidiana na Watu wa Kitabu.
Hizi ni baadhi ya anwani za Imamu Bukhari na kanuni zake za kifiqhi, pia kuna suala la kujinyima kwa Mtume S.A.W, na kuziepuka anasa za dunia, kwa hiyo Imamu Ahmad ameipokea Hadithi hii mwanzoni mwa Mlango wa kujiepusha na anasa ya dunia. Na Abusheikh Al-Asbahaniy aliweka anwani ya: “Mlango wa kutaja kujizuia kwake Mtume S.A.W, na anasa za dunia, na kuwapendelea wengine zaidi kwa mali yake kuliko nafsi yake, na kuzigawanya mali hizo kwa wenye kuhitaji miongoni mwa Masahaba zake, kwa kuwa ukarimu ni tabia yake, usaidizi ni shani yake, ridhaa ni sifa yake, na kukipendelea zaidi kinachobaki kuliko kinachotoka, na mazoea yake yalikuwa ni kutomrejesha mtu mwenye kuhitaji, au kumnyima mwombaji. Rehema na amani za Mwenyezi Mungu ziwe juu yake na wakeze”. [Akhlaq An-Nabii wa Adaabih: 4/138, Ch. Ya Dar Al-muslim Lin-Nashr wat-Tawzii’].
Wanachuoni walitaja faida nyingi muhimu zilizomo katika Hadithi hii, miongoni mwake ni kauli ya Al-Hafidh Ibn Hajar: “Kauli yake: katika miji, ni ishara kuwa kuainisha safari katika Aya huonesha aghalabu, basi haitegemezwi hali zote, na Hadithi inaonesha kujuzu kwake mijini, kama nitakavyotaja, na hii ni kauli ya wengi wa wanachuoni, nao walitoa dalili yake kuhusu maana yake kuwa: Rehani imewekwa kwa ajili ya kuweka ushahidi wa deni, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na kama mmoja wenu amewekewa amana na mwingine}, kwa kuashiria kuwa rehani imekusudiwa kuwepo uthibitisho, na kutaja safari hapo kwa sababu ya kutokuwepo mwandishi wakati wa safari, kwa hiyo ilitolewa kwa aghalabu. Mujahid na Adhahaak katika Hadithi ilivyopokelewa na At-Tabariy kutoka kwao, waliyapinga haya maelezo huku wakisema: hakuna rehani isipokuwa katika hali ya safari, ambapo mwandishi hayupo, na huu ni mfano wa kauli ya Dawud na wanachuoni wa Madhehebi ya Dhaahiriyah. Ibn Hazmi anasema: kama mwekewa rehani akiishurutisha ifanyike mijini haitasihi, lakini ikitolewa na mwekaji rehani kwa hiari yake basi inajuzu, na kwa maoni yake, hii ndiyo maana ya Hadithi ya mlango huu. Imamu Bukhari, kwa uzoefu wake aliashiria mapokezi mengine ya Hadithi, na Hadithi hii imewahi kutajwa katika mlango wa Mtume S.A.W, kununua kwa mkopo, mwanzoni mwa mauziano kwa njia hii isemayo: “Hakika aliiweka rehani ngao yake huko Madinah kwa Myahudi”, na kwa maana hii inatujulisha jibu la aliyepinga kuwa: hakuna ishara katika Aya na Hadithi ya uwekaji wa rehani katika miji.” [Fathul-Bariy: 5/140, Ch. Dar Al-Maarifah]
Anasema pia: “Hadithi hii inaonesha uhalali wa kuamiliana na makafiri katika vitu ambavyo havina dalili ya kuharamishwa kwake, bila ya kujali ubaya wa imani yao, na kuamiliana kati yao wenyewe kwa wenyewe, na pia inajuzu kuamiliana na yule mwenye mali na wingi wa mali hiyo ni haramu, na inajuzu kuiuza silaha, kuiweka rehani, na kuikodisha n.k, kutoka kwa kafiri, kwa sharti la kwamba asiwe miongoni mwa maadui. Ndani yake pia kunathibitisha miliki za Watu wa Dhima ziwe mikononi mwao, kujuzu kununua kwa mkopo, kupata ngao na zana za kivita, na kufanya hivyo hakupingani hata kidogo na kumtegemea Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kupata vyombo vya vita hakuoneshi kuwa kufanya hivyo ni kuzihodhi, na hii ni kauli ya Ibn Al-Muniir.
Katika zama hizi chakula kinachopatikana sana ni Shairi, kama alivyosema Ad-Dawudiy, na kuhusu bei ya kitu inachowekewa rehani kauli ya mwekewa rehani inakubalika pamoja na kiapo chake, kama alivysema Ibn At-Tiin, na ndani yake pia alivyokuwa Mtume S.A.W, unyenyekevu na kujinyima na anasa ya dunia, kupunguza mahitaji yake pamoja na uwezo, ukarimu wake uliompelekea kutoweka akiba mpaka akahitaji kuiwekea rehani ngao yake, kuivumilia dhiki ya maisha, kuridhika na uhaba, na fadhila ya wake zake kwa kuyavumilia maisha na undani wake pia kwa kuyavumilia mengi na mengi.
Wanachuoni wanasema: hekima ya kuamiliana kwa Mtume S.A.W, na Mayahudi badala ya kufanya hivyo na Masahaba walio matajiri ni kuwa: ima kwa ajili ya kubainisha kuwa jambo hili linajuzu au huenda masahaba wakawa hawana chakula zaidi ya mahitaji yao, au kwa kuochelea kwamba wao wasingechukua malipo au fidia, na kwa hivyo basi, Mtume hakutaka kuwalazimisha, na bila shaka miongoni mwao alikuwapo anayeweza kufanya hivyo na zaidi pia, lakini Mtume hakutaka kuwajulisha, isipokuwa wale wasio matajiri ambao walipokea kwa mfumo huo, na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi wa kila kitu”. [Fathul-Bariy: 5/141].
Nyongeza kwa maelezo yaliyotangulia ni kuwa: kuna haja ya waislamu wa sasa kuifanyia kazi Hadithi hii, kwa sababu mtu atakaeitazama Hadithi hii anaweza kuzifahamu faida mpya, ambapo miongoni mwake ni: silaha ya uchumi huenda ikawa na nguvu kubwa kuliko silaha ya vita, na silaha ya Mayahudi hivi sasa ni mali, kwa hiyo asiye kuwa na chakula chake cha kutosha huwa ni sawa na mtu ambaye hana silaha ya kumuhami. Na kuna mifano mingine mingi ambayo waislamu wangaliitafakari wasingalikuwa na unyonge na umaskini.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia: Hadithi hii sio ya kukanushwa, bali ni sahihi na imeipokewa na Imamu Bukhari. Na kukanushwa au kupingwa kwa Hadithi kunafanyika kielimu na wala sio kwa uzushi wa akili dhaifu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 


 

Share this:

Related Fatwas