Uimamu na Hotuba ya Ijumaa Safarini.
Question
Ni ipi hukumu ya Imamu ambaye ametoa hotuba ya Ijumaa na akaswalisha watu Swala ya Ijumaa hali ya kuwa yeye yupo safarini?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Swala ya Ijumaa ni Swala ya Faradhi kwa Muislamu mwanamume, aliye huru, mwenye umri wa kutakiwa kutekeleza maamrisho ya Mungu, mkazi mwenye afya. Kwani msafiri hana ulazima wa kuiswali Swala ya Ijumaa. Imepokelewa Hadithi na Ad-Darqatniy na Al-Baihaqiy, Hadithi kutoka kwa Jabir Ibn Abdallah amesema: Amesema Mtume S.A.W: “Mwenye kumwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, basi analazimika kuswali Swala ya Ijumaa siku ya Ijumaa, isipokuwa mgonjwa au msafiri au mwanamke au mtoto mdogo au mtumwa. Mwenye kujitenga na Swala ya Ijumaa kwa michezo au biashara, basi Mwenyezi Mungu Anajitenga naye, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mkwasi, si muhitaji, naye ni Msifiwa kwa sifa njema” akasema As-Sarkhasiy: “Kwa maana ya kuwa msafiri hukumbana na tabu kwa kuingia ndani ya mji anaokwenda, na wakati huo huo kuhudhuria Swala ya Ijumaa, huenda hatapata mtu wa kumlindia mizigo yake, na huenda akaachwa na wasafiri wenzake, kwa kuondoa uzito huu, ndipo sheria ilipoamua kumuondolea ulazima wa Swala ya Ijumaa msafiri” [Al-Mabsut cha As-Sarkhasy, 2/22, chapa ya Dar Al-Maarifa].
Kutokuwa lazima hakumaanishi kutofaa, kwani inafaa msafiri kuhudhuria Swala ya Ijumaa na inafaa kwake pia kuwaswalisha Waumini hata kama hilo si lazima kwake. Amesema At-Tamartashiy Al-Hanafiy katika kitabu cha: [Tanwir Al-Absar]: “Inafaa uimamu wa Swala ya Ijumaa kama inavyofaa kwa wengine, na kwa hivyo basi inafaa uimamu wa msafiri, mtumwa na mgonjwa” [Radd Al-Muhtar ala Al-Dur Al-Mukhtar sherehe ya kitabu cha Tanwir Al-Absar, 1/548 chapa ya Ihyaa At-Turath].
Na akasema Al-Marghaniy Al-Hanafiy: “Msafri, mwanamke au mgonjwa, mtumwa au kipofu, hawa hawalazimiki kuiswali Swala ya Ijumaa, na kwa hivyo basi, ikiwa watahudhuria Swala ya Ijumaa na wakasali pamoja na watu itawatosha kuwa ni lazima, kwa sababu wamejibebesha jukumu hilo na wakawa kama vile msafiri pale anapofunga, na inafaa kwa msafiri na kwa mtumwa, pia kwa mgonjwa kuongoza Swala ya Ijumaa, kwa sababu hii ni ruhusa. Na ikiwa watahudhuria swala ya Ijumaa basi inakuwa ni lazima kwao” [Al-Hidaya sherehe ya Bidayat Al-Mubtadi, 1/83 chapa ya Al-Maktaba Al-Islamiya].
Na akasema Ibn Qudamah: “Amesema Abu Hanifa, na Imamu Shafiy: inafaa kwa mtumwa na msafiri kuwa imamu kwenye Swala ya Ijumaa, na akalikubali jambo hilo Imamu Malik kwamba msafiri anaweza kuwa Imamu wa swala ya Ijumaa. Na Abii Hanifa akaeleza kuwa Swala ya Ijumaa inafaa kwa watumwa na wasafiri. Na kwa kuwa wao ni wanaume basi inafaa kwao Swala ya Ijumaa”. [Kitabu cha Al-Mughniy cha Ibn Qudama, 2/197, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Arabiy].
Kutokana na maelezo yaliyotangulia ni kuwa: inafaa kisheria msafiri kuongoza Swala ya Ijumaa na kutoa hotuba ya Swala ya Ijumaa kwa watu. Na mwisho, Swala yake na Swala za Waumini wengine wote zinakuwa ni sahihi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.