Mikataba Mipya.

Egypt's Dar Al-Ifta

Mikataba Mipya.

Question

Je, inafaa kuboresha mikataba na miamala mipya? Au lazima kutosheka na mikataba iliyopo? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Ndani ya zama hizi biashara zimeenea kwa kiasi kikubwa, na kuwepo mikataba ya aina mbalimbali, kwa hivyo basi, ni vipi tunaifanyia kazi mikataba hii mipya ambayo haina mfano wake ndani ya urithi wa Fiqhi?
Masuala haya ni muhimu sana kwenye mlango huu lakini na swali lenyewe pia nani aliyeyataja kwa jina la mikataba mipya? Na jibu ni kuwa: Wanazuoni wa Fiqhi ndio waliolitaja lile jina.
Hukumu ya masuala haya kisheria ni kuwa inafaa kuingiza mikataba mipya katika aina mbalimbali za biashara, hata kama mikataba hiyo haitakuwa ikiitwa hivyo ndani ya vitabu vya urithi wa Fiqhi.
Miongoni mwa dalili ya hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu pale aliposema: {Lakini Mwenyezi Mungu Ameihalalisha biashara} [AL BAQARAH 275].
Dalili hapa ni ule ujumla unaotokana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {biashara} hivyo ni biashara kwa ujumla wake na wala hakuna kinachovuliwa isipokuwa kile kinachovuliwa na Sharia.
Amesema Imamu Qurtubiy kwenye kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu pale aliposema: {Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba} hii ni katika ujumla wa Qur`ani, ambapo neno Biashara lililotajwa linarejea kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu, kama Alivyosema pia: {Naapa kwa Zama! Hakika binadamu bila ya shaka yumo katika khasara} kisha Mwenyezi Mungu Mtukufu akavua juu ya hasara hii na Akasema {Ila wale walioamini, na wakatenda mema} hao ndio hawamo kwenye hasara hii, hivyo ikiwa imethibiti kuwa biashara inachukua sifa ya jumla basi yenyewe imehusishwa kwa yale tuliyoyataja miongoni mwa riba na mengineyo katika yale yaliyokatazwa na kuzuiliwa kuingia nayo makubaliano, kama vile mikataba ya vitu vyenye kulewesha, mizoga, kwa maana ya vilivyokufa na vinavyotokana na hivyo na vyinginevyo katika vile vilivyothibiti kwenye Sunna na kauli ya umma wa wanachuoni katika yaliyokatazwa, na mfano mwingine pia kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu {basi wauweni washirikina} na matukio mengine ambayo yanapelekea hukumu ya jumla na kuingia ndani yake umaalumu, na kauli hizi ni za wanachuoni wengi. Na baadhi yao wakasema: huo ni ujumla wa Qur`ani ambayo imetafsiri uhalali wa biashara na uharamu wa riba, hivyo haiwezekani kutumika uhalali wa biashara na uharamu wake isipokuwa pale zinapokutana dalili kutoka katika Sunna za Mtume S.A.W, ikiwa zinaonesha uhalali wa biashara kwa ujumla wake pasina ufafanuzi. Na hii ndiyo tofauti kati ya ukusanyaji na ujumla.
Ukusanyaji unauonesha uhalali wa biashara kwa ujumla wake na kwa maelezo ikiwa hakujahusishwa dalili.
Na ujumla hauoneshi uhalali wake katika maelezo ila pale kunapofungamana na dalili. Hivyo hukumu ya kwanza ndiyo sahihi zaidi. Mwenyezi Mungu Mtukufu Ndiye Anayejua zaidi. [Al-Jamii li Ahkam Al-Qur`ani, 3/365].
Na haya yaliyotangulia yanakubaliana na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Enyi mlioamini! timizeni ahadi} [AL MAIDAH 01], hii ni hukumu inayokusanya mikataba yote isiyopingana na Sharia Takatatifu.
Na katika dalili za Sunna ni Hadithi iliyotokana na Imamu Muslim kutoka kwa Ubada Ibn As-Samit, amesema: Amesema Mtume S.A.W.: “Madini ya dhahabu kwa madini ya dhahabu, madini ya fedha kwa madini ya fedha, nafaka ya ngano nzima kwa ngano nzima, ngano iliyokobolewa kwa ngano iliyokobolewa, tende kwa tende, chunvi kwa chunvi, mfano kwa mfano, sawa kwa sawa, mkono kwa mkono, ikiwa aina hizi zimetofautiana basi uzeni vile mtakavyo ikiwa mkono kwa mkono”.
Dalili hapa ni kauli yake Mtume pale aliposema: “Uzeni vile mtakavyo”, imeonesha kuwa Sharia imefanya asili ya biashara ni halali, lakini Sharia ikabainisha yale yanayotaka kuyavua.
Na hayo ndiyo yaliyofahamika na Masahaba R.A. kwani walikuwa wanauziana yale ambayo hayajafika katika ujuzi wao kuwa yamekatazwa katika yale waliyonayo, kama ilivyopokelewa katika Sahihi mbili za Imamu Muslim na Bukhari kutoka kwa Abi Said Al-Khudriy R.A. amesema: Bilal alikuja kwa Mtume S.A.W, na Tende barniy kisha akaulizwa na Mtume S.A.W.: “Umezipata wapi hizi?” Bilal akasema: tulikuwa na tende ambazo hazikuwa nzuri nikaziuza pishi mbili kwa pishi moja lengo tumlishe Mtume S.A.W, Mtume akasema: “Hapana hapana, ni aina ya riba aina ya riba, usifanye, lakini ikiwa utataka kununua basi uza tende kwa kitu kingine, kisha ununue”.
Hapa unatuwekea wazi kabisa uamuzi wa Mtume S.A.W. kwao juu ya kuuziana pasi na kurejea kwake, na pindi walipofahamu kosa lao hakutumia nguvu isipokuwa aliwabainishia kilicho sahihi, pamoja na kukiri kwake kwao kwa juhudi waliyoifanya katika kuuza na kununua ijapokuwa hawakuwa na andiko maalumu katika jambo hilo.
Na katika dalili pia ni pamoja na Hadithi iliyosahihishwa na Tirmidhiy kutoka kwa Amr Ibn Aauf Al-Mazniy kuwa Mtume S.A.W. amesema: “Usuluhisho ni jambo lenye kufaa kwa Waislamu, isipokuwa usuluhisho unaoharamisha halali, au kuhalalisha haramu, na Waislamu wana desturi zao, isipokuwa desturi iliyoharamisha halali, au kuhalalisha haramu”.
Dalili katika Hadithi hii ni kufaa kuleta usuluhisho, na kufaa kwa desturi za watu, isipokuwa tu ikiwa hivi vitu vitaenda kinyume na Sharia.
Na hili linakubaliana na mikataba yote iwe ile ya zamani au mipya, inachukuliwa hukumu ya kufaa kwake pindipo sharti zilizopo hazitakuwa ni haramu, hivyo Sharia hizi zinafahamika uhalali wake na kufanya kazi kwake ndani ya nyakati zote na zama zote.
Na katika mlango huu ni pamoja na kufanyia kazi desturi, Imamu Bukhari amefasiri katika Sahihi yake: (mlango wa mwenye kufanya mambo yanayowapelekea watu kufahamiana kwao katika kazi za biashara, upangishaji, ujazo, uzito, mwenendo wao na madhehebu yao yanayofahamika).
Amesema Badr Ad-Din akifafanua yale yaliyoelezwa na Imamu Bukhari: kwa maana: mlango huu unataja ndani yake mwenye kufanya mambo yake kwa watu wa miji mbalimbali katika yale yanayofahamika kati yao, kwa maana: desturi zao na kawaida zao katika mambo ya biashara, kukodisha na ujazo, na katika baadhi ya vitabu: ujazo na uzito mfano kwa mfano, kila kitu ambacho hakina andiko la kisharia kikiwa cha ujazo au uzito kinafanyiwa kazi katika utaratibu unaofahamika na wenyeji wa eneo hilo, kwa mfano mpunga hakuna tamko la Sharia kuwa ni ujazo au uzito, basi huzingatiwa katika hali ya kawaida ya wenyeji wa eneo husika wao kwa wao vile inavyofahamika, kwani ndani ya nchi ya Misri wao wanazingatia ni kipimo cha ujazo, katika nchi za Sham ni kipimo cha uzito, na mfano wa hayo katika vitu vingine mbalimbali, kwa sababu kurejea kwenye mazoea ni katika jumla ya kanuni ya kifiqhi. [Angalia: kitabu Umdat Al-Qaari, 12/16, chapa ya Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Na kutokana na haya baadhi ya wanachuoni wamehalalisha kile kinachofahamika kwa jina la kupeana.
Amesema Ibn Qudama: “Kupeana ni kama mfano wa kusema: nipatie kwa hiki kipande cha mkate, basi anampa kile kinachomridhisha, au anasema: chukua nguo hii kwa dinari moja, basi anaichukua na inakuwa ni sahihi, kwa sababu Sharia imeelezea biashara na kuweka hukumu nyingi na wala haikuainisha tamko maalumu, na kufahamika kuwa ndilo jibu lao kwa yale waliyozoeana katika mambo ya biashara, watu na mifumo yao ya masoko na mauziano yao ndiyo wapo hivyo”. [kitabu Al-Kafi katika Fiqhi ya Imamu Ahmad, 2/3, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Na kundi lingine limeangalia kuwa uitaji wa jina hakubadilishi ukweli wa kitu, wakaingiza miamala mbalimbali katika jumla ya kazi za biashara ijapokuwa wametumia majina maalumu.
Amesema Al-Bahutiy: "Uuzaji wa bei ya manunuzi, ushirika, uuzaji wa faida na wa kupatana (ni aina za biashara) zimehusishwa kwa majina haya, kama vile ilivyohusishwa biashara ya Salamu". [kitabu cha: Kashaf Al-Qanai, 3/229, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Misingi asili ya uhalali imeendelea kuwepo kwenye makubalino na mikataba kwa wanachuoni, yanaonekana haya katika vitabu vyao vya Fiqhi, amesema Sheikh Taqiy Ad-Din Ibn Taimiya: "Kauli ya pili: ni kuwa asili katika makubaliano, mikataba na desturi ni kufaa kwake bila ya kuharamisha, lakini hubatilika baadhi yake kwa kuingi ndani yake mambo haramu na batili, na asili kwa Imamu Ahmad R.A. kwenye matamko yake mengi yanazingatiwa kwenye kauli hii, na Imamu Malik yupo karibu na kauli hii pia, lakini Imamu Ahmad amejuzisha sana desturi, hakuna katika Maimamu wanne aliyejuzisha zaidi desturi kuliko Imamu Ahmad.
Na mara zote anachopitisha Imamu Ahmad katika mambo ya mikataba makubaliano na desturi ndani yake kuna kuwa na dalili maalumu kutoka katika maandiko au hukumu ya ulinganishi, lakini hata hivyo hoja ya wale waliotangulia haiwi kizuizi cha kutokufaa, wala kupingana kwake na sharti lililotofauti na makubaliano au kutokuwepo andiko, na kumekuwa na athari katika mikataba na desturi kutoka kwa Mtume S.A.W. na Masahaba, ikiwa Imamu hajapata kwa Maimamu wenzake tamko na kulisemea jambo hilo katika maana ya ulinganisho, na kile kilichotegemewa na wengine katika kubatilisha desturi miongoni mwa andiko, huenda ikadhoofisha dalili yake, na vile vile huenda ikadhoofisha kile kilichotegemewa miongoni mwa ulinganishaji, wafuasi wa Imamu Ahmad wametegemea maana jumla ya maandiko ya Qur`ani na Hadithi ambayo tutayataja katika kujuzisha desturi". [Kitabu: Al-Fatawa Al-Kubra, 4/79, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na kutokana na maelezo hayo yaliyotangulia ni kuwa: Kisharia inafaa kutumia makubaliano na mikataba mipya, kwa sharti kuwa mikataba hiyo isiwe na mambo yanayopingana na Sharia kama vile udanganyifu na kughushi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas