Kuachia Mikono Miwili baada ya Kuin...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuachia Mikono Miwili baada ya Kuinuka Kutoka katika Rukuu.

Question

 Ni ipi hukumu ya kufunga mikono kwa mwenye kuswali baada ya kuinuka kutoka katika rukuu na kuwa katika hali ambayo alikuwa nayo kwenye kisimamo cha kabla ya kurukuu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Hatua mbalimbali zinazofanyika kwenye Swala zinagawanyika sehemu ambazo ni za lazima, sehemu za Sunna na sehemu za vipambo vya Swala.
Hatua za lazima: Ni zile ambazo ikiwa zitaachwa kutekelezwa kwa makusudi au kwa kusahau, basi hazina mbadala wa kuleta sijida ya kusahau wala kitu kingine chochote miongoni mwa vitu vya Sunna za Swala.
Hatua za Sunna: Ni katika mambo yanayopendeza ambayo yanalazimisha kuleta sijida ya kusahau.
Ama hatua za Vipambo vya Swala: Ni katika mambo yanayopendeza ambayo hayalazimishi kuleta sijida ya kusahau. [Angalia kitabu cha Al-Iqnaa cha Sherbiny – pamoja na Hashiyat Al-Bujairamy – 2/102: 108, chapa ya Dar Al-Fikr].
Katika jumla ya hatua za Vipambo vya Swala: Ni pamoja na hali ya uwekaji mikono baada ya kuinuka kutoka katika rukuu. Wanachuoni wametofautiana kwenye namna ya hali hii ya mikono, kati ya wale wanaosema kuwa mikono miwili hufungwa juu ya kifua kama vile katika hali ya kisomo na kati yao ni wale wanaosema kuwa ni vizuri kuiachia.
Kilicho sahihi ni kuwa hali ya mikono miwili katika maudhui hii ni kuachiwa na sio kufungwa, na maelezo haya ni katika Madhehebu ya wanachuoni kuanzia Imamu Abu Hanifa, Imamu Malik, Imamu Shafi na wengineo.
Amesema Imamu Al-Kasaniy Al-Hanafiy katika kitabu cha: [Badai Al-Sanaai 1/201, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya]: “Wamekubaliana wanazuoni kuwa haijasuniwa kufunga mikono katika kusimama kutoka katika rukuu na sijida, kwa sababu hakuna makubaliano ya hilo wala hakuna kisomo chochote”.
Imekuja katika kitabu cha: [Multaqa Al-Abhar] na sharhu yake kitabu cha: [Majmaa Al-Anhar, cha mwanachuoni Damad Al-Hanafy 1/94, chapa ya Dar Ihayaa At-Turath Al-Araby]: “Huachiwa mikono katika kisimamo cha rukuu na kati ya takbira za Eid kwa makubaliano ya wanachuoni”, kwa sababu katika hali hizo hakuna utajo wowote ambao ni mwendelezo wa Sunna na kisomo”.
Na imekuja katika kitabu cha: [Al-Mudawana Al-Kubra” cha Sahnun 1/170, chapa ya Al-Saada]: “Na amesema imamu Malik katika kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika Sala: silifahamu hilo katika Swala ya Faradhi –na alikuwa akichukia– lakini katika Swala za Sunna ikiwa kisimamo ni kirefu hakuna ubaya kufanya hivyo, kwani huko kunamsaidia yeye mwenyewe”.
Na imekuja katika kitabu cha: [Mukhtasar Khalil, pamoja na sharhu yake ya mwanachuoni Al-Kharashy, katika vitabu vya imamu Malik 1/286, chapa ya Dar Al-Fikr]: kuachia mikono yake miwili usawa wa pembeni mwake wakati wa kuleta takbira ya kuhirimia Swala, katika Swala ya Faradhi na Sunna, inachukiza kufunga mikono katika Swala ya Faradhi”.
Amesema imamu An-Nawawiy katika kitabu cha: [Raudhat Al-Talibeen 1/252, chapa ya Al-Maktaba Al-Islamia]: “Inapendeza wakati wa kuinuka kutoka katika rukuu kuinua mikono miwili usawa wa mabega mawili, kama ilivyotangulia katika sifa za kuinuka, mwanzo wa kuinua kwake mikono kunaendana na kuanza kuinua kichwa, baada ya kusimama sawa sawa ataiachia”.
Na amesema Al-Shams Al-Ramliy katika kitabu cha: [Nihayat Al-Muhtaj 1/502, chapa ya Al-Halabiy]: “Baada ya kusimama – mwenye kusali – ataachia mikono yake”.
Hayo pia ni mapokezi ya imamu Ahmad. Amesema Al-Mardawy Al-Hanbaliy katika kitabu cha: [Al-Insaf 2/63, chapa ya Dar Ihayaa At-Turath Al-Arabiy]: “Kutoka kwa - imamu Ahmad - pindi mtu atakaposimama ataiinua mikono yake kisha ataiachia tu”.
Kutoka kwa imamu Ahmad kuna mapokezi mengine ya hiyari, na akasema: “pindi mtu atakapoinua kichwa chake kutoka katika rukuu, basi akitaka ataachia mikono yake, na akitaka atauweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto” [Kitab Al-Inswaaf, 2/63].
Na dalili ya hilo: Ni kuwa asili katika mikono miwili ni kuiachia, hilo linakubaliana na kukosekana kwa asili -ni kutofunga mikono - hukumu haipishani na hivyo isipokuwa kwa dalili, na yaliyopokelewa kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto ni katika hali ya kusoma.
Mtazamo huu upo wazi katika mitazamo ya baadhi ya wanachuoni katika hiyari ya kuachia mikono moja kwa moja hata katika hali ya kusoma, limeelezewa hilo na baadhi ya wanachuoni waliotangulia: Amefasiri Ibn Abi Shaiba katika kitabu chake [1/429, chapa ya Dar Al-Fikr]: Mwenye kuachia mikono yake miwili katika Sala: kisha akaiegemeza dalili yake hii kwa Ibrahim An-Nakhaiy kuwa alikuwa akiachia mikono yake akiwa ndani ya Swala. Na kutoka kwa Amr Ibn Dinar amesema: Alikuwa Ibn Zubeir pindi akisali huachia mikono yake.
Na kutoka pia kwa Muhammad Ibn Syreen, aliulizwa kuhusu mtu ambaye hufunga mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto na akasema: Hakika anafanya hivyo kwa sababu ya damu.
Kutoka kwa Abdullah Ibn Yazid amesema: Sijamwona Ibn Musayab akifunga mkono wake wa kulia katika Swala, alikuwa akiiachia.
Na kutoka kwa Abdullah Ibn Al-Ayzar amesema: Nilikuwa ninafanya ibada ya kutufu pamoja na Said Ibn Jubeir akamwona mtu anasali akiwa ameweka mmoja wa mikono yake juu ya mkono mwengine, mkono huu juu ya huu, akamwendea na kumwachanisha kisha akarudi.
Hayo ni Madhehebu ya Imamu Malik kama ilivyotangulia, bali imepokelewa mapokezi kutoka kwa Imamu Ahmad kuhusu hilo yanayofanana na mapokezi ya Imamu Malik, amesema Al-Mardawy katika kitabu cha: [Al-Inswaaf” 2/473]: “Na huwekwa mikono hiyo miwili chini ya kitovu chake” katika madhehebu haya kuna jopo kubwa la watetezi wake, na pia jopo lingine linasema kuwa mikono huwekwa chini ya kifua, na wengine wanahiyarisha, na wengine huwachia kabisa mikono yao, na wengine huachia mikono yao kwenye Swala za Sunna hufunga mikono yao kwenye Swala za Faradhi”.
Na hupewa nguvu pia kwa sababu baadhi ya wanachuoni hufunga mikono na wengine huachia kwa kutoa sababu mbalimbali, pindi sababu inapomalizika jambo hili hurudi kwenye asili yake ikiwa ni kuachia mikono.
Amesema mwanachuoni Damad katika kitabu cha: [Majmaa Al-Anhar 1/94]: “Kwa upande wa Muhammad” anakizingatia kila kisimamo cha sharia ambacho kina kisomo, kwa sababu hali ya kuachia kufunga mikono imewekewa sharia kwa kuhofia mkusanyiko wa damu kwenye ncha za vidole, kutokana na hofu ya kisomo kwa sababu Sunna ni kurefusha kisomo (ataachia kwenye kunuti na Swala ya Jeneza).
Amesema Al-Kasaniy katika kitabu cha: [Al-Badai 1/202]: na akasema Malik: Sunna ni kuachia mikono. Sura ya kauli yake: Ni kuwa kuachia mikono ni ugumu zaidi kwenye mwili, na hali halisi inahitaji utulivu, amechukua dalili katika yale yaliyopokewa na Ibrahim Al-Nakhaiy aliposema: “Hakika wao walikuwa wanafanya hivyo kwa kuhofia kukusanyika damu kwenye ncha za vidole, kwa sababu walikuwa wakirefusha Sala zao”.
Na kwa kauli za baadhi ya watu wa Shafi ni kufanya hivyo katika hali ya kisomo: Ni kuwa ikiwa mtu ataachia mikono yake pasi na sababu yoyote basi hakuna ubaya, kwa sababu makusudio yaliyotajwa ya kufunga mikono: Ni kutoleta mchezo kwa kutumia mikono miwili. Yamekuja haya kwenye kitabu cha: [Hashiyat Al-Shihab Al-Qalyubiy kwenye sharhu ya kitabu cha Al-Minhaj, 1/173, chapa ya Al-Halabiy].
Kama ambavyo kauli ya kuachia mikono hali ya kuinuka kutoka katika rukuu ni kauli yenye kufanyiwa kazi na wanachuoni wengi wa Kiislamu.
Mtazamo katika kauli za wanachuoni ni kuwa, kilichonukuliwa kwa vitendo ni kuachia mikono baada ya kuinuka toka katika rukuu, na hili linapaswa kutosahaulika. Amelijengea hoja hili imamu Ahmad katika baadhi ya masuala, akasema pia imamu Hanbal: “Nimemsikia imamu Ahmad anasema katika kukamilisha Qurani kuwa: Pindi unapomaliza kusoma: {Sema: Ninajikinga kwa Bwana Mwenye kuwalea}, basi inua mikono yako kwa dua hii kabla ya kurukuu: Nikasema: Ni kwa dalili gani unaileta katika hili? Akasema: Nimewaona watu wa Makkah wanafanya hivyo. Na alikuwa Sufiyani akifanya hivyo pamoja nao huko Makkah”. Amesema Abbas Ibn Abduladhim: “Vile vile tumewakuta watu wakifanya hivyo huko Basra na Makkah. Na kupokelewa na watu wa Madina katika hili na imetajwa pia kutoka kwa Othman Ibn Affan”. [Kitabu Al-Mughniy 1/459, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Amesema Abu Dawud: “Ahmad alikuwa anaswali na watu na kuswali nao pia Swala ya Witri… aliulizwa Ahmad: Je wewe huwa unachelewesha kuswali yaani Swala ya Tarawehe mpaka usiku sana? Akasema: hapana, ni Sunna ya Waislamu ninayoipenda sana” [kitabu Al-Mughniy, 1/458].
Ama dalili ya Hadithi zilizopokewa katika kueleza kuwa Sunna ni kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika kisimamo, sisi tunapitisha Hadithi hizo usahihi wake, lakini hata hivyo tunasema kufunga hiyo mikono ni kwenye kusimama hali ya kusoma, na wala sio kisimamo tu kama inavyofahamika na baadhi ya wanachuoni.
Na kauli kuwa maneno ya wanachuoni katika kufunga mikono wakati wa kusoma inachukuliwa ni katika hali ya kusimama kutoka katika rukuu, sio sahihi. Maelezo ya wanachuoni yametangulia yanayoeleza kinyume na hivyo, na haya maelezo ya Ibn Qayyim Al-Juziy - pamoja na kufahamika kuchukua maana ya wazi ya andiko hasa katika mambo ya ibada -anatoa maelezo kwa kuainisha, ambapo anasema kwenye kitabu cha: [Madarij Al-Salikin, 2/364, chapa ya Dar Al-Katab Al-Arabiy): “Miongoni mwa mambo ya adabu za kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu ukiwa ndani ya Swala: Ni kuweka mkono wa kulia juu ya mkono wa kushoto katika kusimama hali ya kusoma, katika kitabu cha Al-Muwatwau cha Imamu Malik, Sahli Ibn Saad amesema: Hilo ni katika Sunna, na watu walikuwa wanaamrishwa kufanya hivyo. Hakuna shaka ni katika adabu za kusimama mbele ya Wafalme na watu wakubwa na kwa hivyo basi kusimama hivyo mbele ya Mkubwa wa wakubwa kwake ni haki zaidi”.
Maelezo ya wanachuoni katika suala hili hata kama yametangulia lakini umuhimu wa kuhusisha kuna mambo ya kuchunga, kuna mitazamo katika kauli zao nje ya mlango huu, miongoni mwa kauli hizo:
Yale yaliyonukuliwa na Al-Hafidh Ibn Hajar katika kitabu cha: [Fat-h Al-Bari 2/310, chapa ya Aalam Al-Maarifa] amesema: Amesema Ibn Rushd: "Ikiwa pataelezwa ndani ya Hadithi suala la kukaa katika Swala pasi na kuainisha kikazi hicho, basi kusudio lake linakuwa ni: Kikazi cha Attahiyyat".
Na akasema Ibn Muflih katika kitabu cha: [Al-Furuu, 1/412, chapa ya Aalam Al-Kutub]: “Amesema Abu Hafs: Huweka mikono yake miwili usawa wa mabega yake, na matumbo ya vidole vyake gumba usawa wa masikio yake. Na akasema katika maelezo kuwa: Mkono unapotajwa pasi na kuainishwa huwa inakusudiwa kiganja cha mkono”.
Ama Hadithi ya Abi Humaid Al-Saaidy na wengine, ambayo imechukuliwa kama ni hoja ya baadhi ya wanachuoni wenye kufuata hoja ya kufunga mikono wakati wa kusimama kutoka kwenye rukuu, hawana cha kuthibitishia hoja yao, isipokuwa kusudio lake ni kuonesha hali ya utulivu katika nguzo hii.
Imepokelewa na imamu Bukhari kutoka kwa Muhammad Ibn Amr bin Atwaau kuwa siku moja alikuwa amekaa na Masahaba wa Mtume S.A.W, wakawa wanazungumzia Sala ya Mtume S.A.W, basi akasema Abu Humaid Al-Saaidy: Mimi nimekuwa ni mwenye kuhifadhi zaidi Sala ya Mtume S.A.W, na nimemwona pindi anapotoa takbira huinua mikono yake usawa wa mabega yake, pindi anaporukuu huweka mikono yake kwenye magoti yake, kisha hunyoosha mgongo wake, anapoinua kichwa chake husimama kwa kunyooka mpaka uti wa mgongo wake unaporehea sehemu yake, anaposujudu huweka mikono yake pasi na kuifunga, na huelekeza ncha za vidole vyake vya miguu kibla, anapokaa baada ya rakaa mbili hukalia mguu wake wa kushoto na kuunyoosha wa kulia, na anapokaa baada ya rakaa ya mwisho hutanguliza mguu wake wa kushoto na kuunyoosha mwengine na kuukalia kwa makalio yake.
Amesema Hafidh Ibn Hajar katika kitabu cha: [Al-Fat-h 2/308]: kauli yake: “Mpaka uti wake wa mgongo utakaporejea pahala pake….. kusudio ya kauli hiyo ni: Ukamilifu wa kusimama”.
Hadithi hii imepokewa pia kwa tamko: “Kila mfupa unaporejea kwenye sehemu yake” kama ilivyopokelewa na Tirmidhiy na wengine: “Alirukuu kisha akawa sawa pasi na kunyoosha shingo ya kichwa chake, na akaweka mikono yake juu ya magoti yake kisha akasema: Samia llahu liman hamidah. Akainua mikono yake na kuwa sawa mpaka kila mfupa ukarudi sehemu yake akiwa amesimama sawa sawa, kisha akaelekea kwenye ardhi hali ya kusujudu kisha akasema: Allahu Akbar. Kisha akakunjua mikono yake mbali na kwapa zake na kukunjua vidole vyake vya miguuni kisha akakunja mguu wake wa kushoto na kuukalia. Kisha akawa sawa sawa mpaka kila mfupa ukarudi sehemu yake, kisha akasujudu tena”. Tamko hili linachukuliwa kutoka katika tamko la mapokezi ya kwanza na makusudio yake, na wala hatujakuta mwenye kuleta hoja kwenye mfumo huu. Mwenye kuzingatia Hadithi atakuta kuwa imetumika ibara ile ile katika kuinuka kutoka katika sijida ya kwanza, kwa maana mfupa kurudi sehemu yake wakati huo isipokuwa mfupa wa uti wa mgongo kama mapokezi ya kwanza yanavyoelezea.
Maelezo yaliyotangulia yanaonesha hukumu ya masuala haya, na linalochukuliwa na mwenye kuswali baada ya kuinuka kutoka rukuu na kabla ya kuelekea chini kusujudu ni kuwa mikono yake katika hali ya kuachiwa pasi na kufungwa.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas