Ndoa ya Walionyonya Ziwa Moja
Question
Ni ipi hukumu ya mtoto wa kiume na msichana ambao wote wawili walikuwa katika malezi ya pamoja na walinyonya ziwa moja la mke wa mlezi wao, au kwa mmoja wa dada wa mke huyu, au kutoka kwa mwanamke mwengine? Na katika hali hiyo inajuzu kwa mtoto wa kiume huyo mwenye malezi hayo kumwoa msichana aliyelelewa pamoja naye, au wawili hawa ni ndugu kwa kunyonya ziwa moja?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Kunyonya ziwa moja kukiwa ndani ya miaka miwili ya kwanza ya umri wa kichanga, na kukawa mara tano katika nyakati tofauti, basi ndoa haitajuzu katika hali iliyotajwa katika swali. Kwani kwa kunyonya mtoto wa kiume na mtoto wa kike ziwa moja la mwanamke, awe mwanamke huyo ni mlezi au mwanamke mwingine yoyote, hakika mambo yalivyo, watoto hao wawili watakuwa ndugu kwa kunyonya ziwa moja, na kwa hivyo haijuzu kuoana kwa wawili hao, sawa na kutokujuzu ndoa ya ndugu wa tumbo moja.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.