Jamaa ya Wanawake Katika Swala

Egypt's Dar Al-Ifta

Jamaa ya Wanawake Katika Swala

Question

Swala ni nguzo ya Dini. Mwenye kuisimamisha amesimamisha Dini, na mwenye kuiharibu ameiharibu Dini. Kuswali jamaa ni miongoni mwa alama za Uislamu, na miongoni mwa sifa za watu wema na waongofu. Sharia Tukufu imehimiza kwa kiwango kikubwa, na kuhimiza ifanywe; na akasema Mola Mlezi: {Na inameni pamoja na wanao inama}

Answer

Swala ni nguzo ya Dini. Mwenye kuisimamisha amesimamisha Dini, na mwenye kuiharibu ameiharibu Dini. Kuswali jamaa ni miongoni mwa alama za Uislamu, na miongoni mwa sifa za watu wema na waongofu. Sharia Tukufu imehimiza kwa kiwango kikubwa, na kuhimiza ifanywe; na akasema Mola Mlezi: {Na inameni pamoja na wanao inama}. [AL BAQAR.A.H: 43], yaani: katika jamaa yao, na Mtume S.A.W., alisema: "Swala ya jamaa ni bora. mara ishirini na saba kuliko kuswali mtu pekee".[1] Na akasema: “Hawawi watatu katika kijiji au Bedui ambao hawasimamishi ndani yake Swala isipokuwa Shetani amewahodhi, basi lazima mjiunge na Jamaa, kwani mbwa mwitu anakula mbuzi aliye mbali”.[2] Na As-saib Ibn Hubaish -mmoja wa wapokezi wa Hadithi- alisema kuwa: maana ya jamaa ni  katika Swala.

Matini hii na nyingine inaonesha kuwa hakuna tofauti katika kuhitajika kwa Swala ya jamaa baina ya mwanamke na mwanamume, Swala ya mwanamke katika jamaa pamoja na wanawake wengine na kuwaongoza katika Swala imehalalishwa na ni yenye kuhitajika.

Na usemi wa (kuliko) katika kauli yake Mtume S.A.W.: "Swala ya jamaa ni bora mara ishirini na saba kuliko kusali mtu pekee" unaonesha ni wa kuhitajika.

Na Hadithi iko wazi haikuweka kikomo, na Mtume S.A.W., hakuiweka kwa mwanamume wala mwanamke tu, na hii inaashiria kuwa wanawake wako sawa na wanaume katika kupata fadhila ya jamaa, na kusimamisha Swala peke yao, kama vile wanaume wanavyofanya peke yao.

Na kutoka kwa Ummu Waraqah R.A, kwamba Mtume S.A.W., alikuwa akimzuru nyumbani kwake, na akamwekea muadhini ili kuadhini kwa ajili yake, na akamuamuru kuwaongoza watu wa nyumba yake katika Swala.[3] Kwa hivyo Mtume S.A.W., alipomuamuru kuwaongoza katika Swala inaashiria uhalali wa mwanamke kuwaongoza wengine nyumbani; kwa sababu lau mwanamke asingeruhusiwa kumuongoza mtu mwingine, Mtume S.A.W., asingemuamuru kuwaongoza wanawake wengine.

Hayo yametajwa katika matendo ya mama wa Waumini; kutoka kwa Raitah Al-Hanafiyah alisema: “Aisha alituongoza, na akasimama miongoni mwao katika Swala ya faradhi. [4]

Na kutoka kwa Hujairah, alisema: “Ummu Salamah alituongoza katika Swala ya Alasiri, na akasimama baina yetu”.[5] Na lau kuwa Swala yao kwa jamaa haikuwa halali, hayo yasingelitokea kwa mama wa Waumini R.A., kutokana na ukaribu wao na Mtume na ujuzi wao wa Sunna zake  S.A.W..

Hayo ndiyo yaliyopokewa kutoka kwa Ibn Abbas R.A., ambapo alisema: "Mwanamke anawaongoza wanawake wengine katika Swala, akiwa amesimama katikati yao".[6]

Na imepokewa kutoka kwa Ibn Umar kwamba alikuwa akimuamuru kijakazi wake kuwaongoza Wanawake katika Swala za usiku wa Ramadhani.[7] Nayo ni Madhehebu ya A’ataa, Ath-Thawriy, Al-Awazaiy, Is-haaq, na Abu Thawr.[8]

Na hayo pia yametajwa na Wanachuoni wa Fiqhi wa Madhehebu ya Shafi na ya Hanbal:

Sheikh wa UIslamu Zakariya Al-Ansariy amesema katika kitabu cha: Asna Al-Mataalib, moja ya vitabu vya Madhehebu ya Shafi: “(Na hakuna wajibu ndani yake) yaani: Swala ya Jamaa (juu ya wanawake, bali ni jambo linalopendwa) kwao, na wala si yakini kuwa ni jambo la kupendwa kwao kama inavyopendwa kwa wanaume, kwa sababu ya ile daraja ya wanaume juu ya wanawake, na Mwenyezi Mungu amesema: {Na wanaume wana daraja zaidi kuliko wao}. [AL BAQAR.A.H: 228]”.[9]

Sheikh Al-Bahutiy, Mwanachuoni wa Fiqhi wa Wadhehebu ya Hanbal amesema katika Sharh Muntahaa Al-Iraadaat: “(na) Swala ya Jamaa imetungwa kama Sunna (kwa wanawake peke yao) mbali na wanaume, S.A.W. mwanamume au mwanamke akiwaongoza”.[10]

Wafuasi wa Madhehebu ya Hanafi walishikilia kwamba Swala ya jamaa ya wanawake ni Makuruhi iliyo karibu na haramu ”. Imamu Ibn Abidiin alisema katika Hashiya yake kwa mujibu wa maneno ya mtunzi wa Ad-Durr ul-Mukhtaar: “(Na) inachukiwa kukaribia uharamu (jamaa ya wanawake); hata katika Swala ya Tarawiyh, isipokuwa Swala ya Janaza”. Yaani: “Kauli yake (Inachukiwa kukaribia uharamu) Ameibainisha katika Al-Fath na Al-Bahr, na kauli yake (hata katika Swala ya Tarawiyh) imeeleza kuwa uchukuzi ni katika kila kitu ambacho jamaa ya  wanaume ni sheria kwao, iwe ni faradhi au Sunna”.[11]

Na wakatoa dalili kutokana na yaliyopokewa kwamba Mtume S.A.W., amesema: “Hakuna heri katika Swala ya jamaa ya wanawake isipokuwa msikitini au kwenye mazishi ya aliyeuawa”.[12]

Ushahidi ni kwamba yeye S.A.W., alikanusha ubora wa Swala ya jamaa ya  wanawake nje ya msikiti wa jamaa, na haifichiki kuwa jamaa yao katika msikiti wa jamaa iko pamoja na wanaume. Kwa sababu hakuna aliyesema kwamba inajuzu kwao kuswali Swala ya jamaa katika msikiti wa jamaa peke yao mbali na wanaume, kwa hivyo inajulikana kuwa Swala yao ya jamaa peke yao ndiyo ni makuruhi”.[13]

Ama katika dalili ya akili, ikiwa mwanamke atawaongoza wanawake wengine katika kuswali, basi jamaa yao haiko mbali na kufanya jambo lililoharamishwa, kwa sababu wao wamefungwa na moja ya mambo yaliyokatazwa.

Ama mwanamke akisimama mbele yao, yaani: akawatangulia, kwa mbele kuna ongezeko la kudhihirisha sehemu za siri, na kuzidhihirisha ni haramu.

Au mwanamke asimame katikati yao, na katika kusimama katikati yao huachiwa utangulizi wa Imamu, nao ni wajibu; Kwa sababu Mtume S.A.W., amedumu katika kuuendeleza uongozi bila kuuacha.

Na katika hali hii, Swala yao inalingana na Swala ya walio uchi, na Swala ya jamaa ya walio uchi ni makuruhi yenye uharamu.[14]

Ama yale yaliyopokewa kuhusu kitendo cha Bibi Aisha R.A., kuhusu uongozi wa wanawake, walisema - kwa kujibu yanayosemwa: Ikiwa uongozi wao ni makuruhi, basi vipi Aisha alifanya hivyo?- Inachukuliwa kuwa  ilikuwa mwanzoni mwa Uislamu, kisha ikafutwa.

Ikiwa wakapinga na kuswali jamaa, basi mwanamke husimama katikati yao. Kwa sababu kuacha kutangulia ni rahisi zaidi kuliko kuzidisha kufichua uchi, na ni lazima kiwepo kimojawapo, na pia walitoa dalili kwa kitendo cha Bibi Aisha R.A., pale alipowaongoza wanawake katika Swala, kwa sababu yeye hakuacha wajibu wa kuwa mbele isipokuwa kwa jambo ambalo lilikuwa ni wajibu zaidi kuliko hilo.[15]

Ushahidi wao unajadiliwa kama ifuatavyo:

Ama Hadithi isemayo: “Hakuna heri katika Swala ya Jamaa ya wanawake isipokuwa Msikitini au kwenye mazishi ya aliyeuawa”,  Ibn Lahia’ah ni mmoja wa wapokezi wake, ambapo kuna maneno yanayomhusu, kama alivyotaja Al-Haithamiy katika Majmaa Az-Zawaaid[16], na Imamu Al-Dhahabiy amesema katika Al-Kaashif: “Maoni ni  kuidhoofisha Hadithi yake”[17] , Na Hadithi hiyo ina kasoro mbili kwa mujibu wa rai ya Imamu Ibn Al-Jawziy: udhaifu wa Ibn Lahia’ah, na kutoelewa kwa Al-Waliid Ibn Abil-Waliid - mmoja wa wapokezi wa Hadithi hiyo.[18]

Na ikiwa Hadithi ni sahihi, hakuna dalili ndani yake kuhusu kinachotakiwa; Kwa sababu kukanusha ubora. hakuhitaji kuharamishwa na mfano wake ni yale aliyoyapokea Ahmad, kutoka kwa Anas R.A., kwamba Mtume S.A.W., amesema: “Na nguo ndefu ni nusu ya mguu hadi ya vifundoni, hakuna jema katika hilo”[19]. Na kupita vifundoni siyo haramu.

Ikisemwa: Inaweza kuafikiwa kuwa pokezi linaashiria kuwa jamaa ya wanawake ni makuruhu, na kazi yake ni kujuzu , na kuchukia kitu hakupingani na kuruhusiwa kwake[20].

Tunasema: Karaha isiyopingana na kuruhusiwa ni ile iliyopendeza, na kumetambulishwa katika madhehebu ya Hanafi kuwa ni karaha iliyoharamishwa, na ni kinyume na kuruhusiwa inavyojulikana; Kwa sababu iko karibu zaidi na haramu, bali ni haramu, na uharamu wake umethibitishwa kwa ushahidi wa dhana.[21]

Ama walivyotaja kuwa: mwanamke akiwaongoza wanawake wengine, basi kuna moja ya makatazo mawili: Ama kudhihirisha zaidi sehemu za siri kwa sababu ya kuwa mbele, au kuacha kuwa mbele akisimama katikati yao, na kuwa mbele ni wajibu wa Imamu.

Katazo la kwanza ni marufuku; Kwa sababu ikiwa mwanamke atafunika sehemu zake za siri wakati wa Swala kwa namna ambayo wanawake wengine wanaweza kumuona hali yake, basi inathibitika kusitiri sehemu zake za siri, na usemi wa kuwaongoza wanawake wengine unapelekea kufichuka sehemu zake za siri unamtaka mwenye kupinga aseme hivyo: ni haramu kabisa kwa mwanamke kuwa mbele na wanawake wengine, si kwa kuwekea vikwazo Swala tu, na lazima hii ni mbaya.

Ama katazo kwa kuacha kutangulia katika hali ya kuwa ni Imamu, haikubaliwi kuwa ni katazo; Kwa sababu sisi tunazuia kuwa Imamu awe mbele, lakini katazo ndiyo maamuma kuwa ni mbele, na hali kadhalika kusimama kwa Imamu mwanamke katikati ya wanawake wanaoongzwa naye hakumlazimu kuacha kuwa mbele, bali badala yake anaweza kuwa mbele hata lau hatua ndogo, na kisha yale makatazo mawili ambayo Mahanafi walizingatia yanaondolewa.

Kulinganisha Sala yao na Sala ya walio uchi, na jamaa ya walio uchi ni mfano mbaya, kwa sababu unapingana na matini yaliyopokewa  kwamba Mtume S.A.W., alimuamuru Ummu Waraqah aongoze watu wa nyumba yake, na kuzingatia mlinganisho pamoja na kuwepo matini ni mazingatio kwake pamoja na ushahidi wenye nguvu zaidi kuliko, kwa hivyo si sahihi.[22]

Ama jibu lao kuhusu kitendo cha Bibi Aisha R.A., kwamba kilikuwa mwanzoni mwa Uislamu na kilifutwa, jawabu yake ni kwamba yeye S.A.W., aliishi Makkah baada ya kupata Unabii muda wa miaka kumi na mitatu, kisha akamwoa Aisha R.A., na akafunga naye ndoa huko Madina alipokuwa msichana wa miaka tisa, na akakaa naye kwa muda wa miaka tisa, na hakuongoza Swala ila baada ya kuvunja ungo, basi iko wapi huko tangu mwanzo wa Uislamu?

Ikisemwa: Inajuzu kwa yale yaliyokusudiwa na mwanzo wa Uislamu kuwa kabla ya kufutwa, basi ni mwanzo kuhusiana na yanayokuja baada yake.

Tulisema: Madai ya kufutwa lazima yabainishe mwenye kufuta, na hakuna mwenye kufuta wa kitendo chake, kwa hivyo madai yao si sahihi.

Ama yale waliyoyataja baadhi yao juu ya uwezekano kuwa kauli inayofuta ni ile iliyoyapokelewa na Abu Dawud na Ibn Khuzaimah, kutoka kwa Mtume S.A.W.,: “Swala ya mwanamke chumbani kwake ni bora kuliko Swala yake katika nyumba yake, na Swala yake ndani ya mahali pa kulala ni bora kuliko Swala yake ndani ya chumba chake”.[23] Na Ibn Khuzaimah amepokea kutoka kwake S.A.W.,: “Swala ya mwanamke ambayo kupendwa sana kwa Mwenyezi Mungu kuliko zote ni ile anayoiswali katika mahali penye giza zaidi nyumbani kwake”.[24] Na katika Hadithi yake na Ibn Hibban: “Naye si karibu mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko ilivyo ndani kabisa ya chumba chake.[25]

Na maana ya chumba hapa ni: chumba kilicho ndani ya nyumba, na inajulikana kuwa chumbani hakuwezi kukusanya jamaa, kadhalika ndani kabisa ya nyumba yake na giza zaidi.

Jibu lake ni kuwa Hadithi zote zinaonesha kuwa imependekezwa kwa mwanamke kuswali katika sehemu zinazomfunika zaidi. Ili kumkinga na madhara. na ubaya anaoweza kupata, na kuepusha kile ambacho kinasababisha fitna na ufisadi kwake, na hakuna kutajwa katika Hadithi kwamba anaswali kwa jamaa au kibinafsi.

Na chumba cha kulala: kinaitwa chumbani ndani ya nyumba ambayo vitu vya thamani huwekwa, au nyumba ndogo katika nyumba kubwa kama chumba,[26] na chumba kidogo kinaweza kutosha kwa jamaa ya watu wawili, na wawili ni wachache zaidi wa jamaa. Na ndani kabisa ya kitu ni mwisho wa chini yake, na kukaa chini ya nyumba ni sitiara ya kukaa daima,[27] na ndani kabisa ya nyumba yake yaani: ndani ya nyumba yake, kwa hivyo hakuna ushahidi wa kufutwa ndani ya Hadithi.

Na ikiwa tutakubali kufutwa, basi ni kwa maana ya kupendelea, na si kwa maana ya uthibitisho wa karaha inayokaribia uharamu katika kitendo, bali ni karaha iliyopendekezwa, au kinyume cha lililotakiwa kwa jumla.[28]

Wafuasi wa Madhehebu ya Malik walielekea ubatili wa uongozi wa mwanamke kwa wengine, na ubatili wa Swala ya wanaomfuata. Sheikh Al-Kharshiy amesema katika maelezo yake ya kauli ya Khalil katika Mukhtasar wake: “Na inabatilika kwa kufuata mfano wa kafiri au mwanamke.” Yaani: Haisihi uongozi wa mwanamke katika Swala, awe anawaongoza wanaume au wanawake katika Swala za faradhi au Sunna.[29]

Na dalili ya madai yao ni Hadithi: “Watu wanaomteua mwanamke kuwa mtawala wao hawatafanikiwa”.[30]  Al-Qarafiy pia alitoa dalili kuwa mwanamke ni mbaya zaidi kuliko mtumwa, kwa hivyo Swala ya mtumwa ni halali siku ya Ijumaa, tofauti na mwanamke ambaye pia ni mbaya zaidi kuliko mvulana; Kwa amri ya achelewe safuni, tofauti na mvulana.[31]

Kwa yaliyopokewa kutoka kwa Mtume S.A.W.,: "Wachelewesheni pale ambapo Mwenyezi Mungu amewachelewesha"[32], hii ni amri ya kuwachelewesha wanawake, na ikiwa mmoja wao amewongoza, angekuwa amepinga agizo hilo la kinabii, kwa sababu jukumu la imamu ni kumtangulia mwingine, na Mtume S.A.W., aliamuru wacheleweshwe, hivyo haijuzu uongozi wa wanawake, kwa sababu matokeo ya mbele ni kinyume cha amri yake S.A.W..

Na wakatoa dalili iliyopokewa kutoka kwa Ali bin Abi Talib R.A., kwamba alisema: “Mwanamke asiongoze Swala”.[33]

Ama Hadithi: “Watu hawatafaulu” ni ya jumla, na dalili zetu ni ya hasa, kwa hivyo zina umbele. Kwa sababu kanuni ni kwamba dalili hasa ina nafasi ya kwanza juu ya jumla kwenye mgogoro.

Ama mwanamke ni mbaya zaidi kuliko mtumwa, kwa sababu Swala ya Ijumaa si sahihi kutoka kwake tofauti na yeye, inafaa kutajwa kama dalili ikiwa masuala mawili ni sahihi, ya kwanza: kuthibitisha kuwa ni sahihi mtumwa asiongoze, ya pili: ili kuthibitisha kuwa Swala  ya Ijumaa ya mwanamke si sahihi.

Kwa hivyo mfumo ni: Iwapo mtumwa si sahihi kwake kuongoza Swala, basi mwanamke anastahiki zaidi kuliko yeye kuhusu kutosihi uongozi wake, kwa sababu kuhusu mtumwa Ijumaa yake ni sahihi, kinyume cha mwanamke. Lakini masuala haya mawili ni marufuku; kwa sababu uongozi wa mtumwa ni sahihi, na rai hii imenukuliwa na Ibn Qudamah, kutoka kwa Ijmaa ya Masahaba.[34]

Na wafuasi wenyewe wa madhehebu ya Maaliki walinukulu usahihi wa uongozi wake katika Swala za Sunna zilizothibitishwa na Swala za faradhi zisizokuwa Ijumaa.[35]

Ama kuhusu kauli ya kuwa mwanamke si sahihi kwake Swala ya Ijumaa, kauli hii si kweli; Al-Muwaffaq amesema katika Al-Mughniy: “Ibn Al-Mundhir amesema: Watu wote wenye elimu tuliojifunza kutoka kwao wameafikiana kwa kauli moja kwamba hakuna Swala ya Ijumaa kwa wanawake.

Walikubaliana kwa kauli moja kwamba ikiwa wanawake watahudhuria Swala ya Ijumaa, hiyo itatosha kwao, kwa sababu kuangusha Swala ya Ijumaa ni kwa ajili ya kuwapunguzia mizigo yao, na wakibeba uzito na wakaswali itawatosheleza kama mfano wa mgonjwa.[36]

Na Sheikh Al-Kharshiy, mfuasi wa madhehebu ya Malik amesema katika maelezo yake ya ufupisho wa Khaliil: “Ama mwanamke, pia inakubaliwa kwake kwa mapatano – yaani Ijumaa – na Swala yake nyumbani kwake ni bora zaidi kwake”[37].

Ama kusema kwao: Ni mbaya zaidi kuliko kijana; kutokana na amri ya kucheleweshwa safu, tofauti na yule kijana, kwa sababu Mtume S.A.W., amesema: "Wacheleweshe kama Mwenyezi Mungu alivyowachelewesha".[38]

Maana yake ni kuwa wanabaki nyuma ya safu za wanaume katika Swala, kwa ajili ya kuwasitiri, na kuepusha yale yanayoweza kutokea kutokana na ufisadi wa wanaume na wanawake kuchanganyika katika Swala.

Na Hadithi iliyotajwa hapo juu haikunasibishwa ipasavyo kwa Mtume S.A.W., na Al-Hafidh Ibn Hajar amesema: “Sikuona kuwa ni Marfuu’, nayo ni katika Abdurrazzaq na At-Tabara nayo ni kutoka Hadithi ya Ibn Masuud”,[39] na Az-Zailai'iy ameashiria hiyo katika (Nasbur-rayah).[40]

Ibn Al-Humam amesema: “Haikuthibitika kuwa Marfuu’, pamoja na kuwa Mashuhuri, bali ni katika Musnad ya Abdul-razzaq, ambayo ni Mawquuf juu ya Ibn Masuud”.[41]

Ama mapokezi yaliyotajwa hapo juu ni kutoka kwa Ali R.A., si sahihi kwa njia ya Isnaad; kwa sababu kuna mpokezi asiyejulikana ambaye hakutajwa jina, naye ni (Mawla Bani Hashim), na tukikubali usahihi wake kama dalili, basi linapingana na zile zilizo na nguvu zaidi miongoni mwa dalili tulizozitaja.

(Ombi kuhusu nafasi ya mwanamke anapoongoza wanawake wengine katika Swala)

Wanachuoni - wale waliokuwa na rai ya wanawake wanaowaongoza wengine, au wale walioisahihisha jamaa zao ikiwa walifanya hivyo, licha ya kuwa Makuruhi kwa rai ya wafuasi wa madhehebu ya Hanafi - wamekubali kwamba mwanamke anayewaongoza wanawake wengine katika Swala asimame katikati yao, na wala asimame mbele yao kama cheo cha Imamu wa wanaume.

Imamu Ibn Qudamah amesema: “Akiwaongoza katika Swala anasimama katikati yao, na hatujui hitilafu yoyote baina ya wale walioona kuwa akiwaongoza katika Swala, Na kwa sababu inapendwa kwa mwanamke kujisitiri, kwa hiyo haipendwi kwake kuwa mbali na wenziwe, na akiwa katikati ya safu kumjaalia kujisitiri zaidi; Kwa sababu amejisitiri mbavuni mwake kwa wenziwe, na hali hii inapewa kwake mfano wa aliye uchi”.[42]

Wametoa dalili ya hayo kutokana na matendo ya Bibi Aisha na Bibi Umm Salamah R.A., wanapowaongoza wengine kwa kusimama katikati ya safu, na kwa kauli ya Ibn Abbas R.A.: "Mwanamke huongoza wanawake, husimama katikati yao".[43]

Na mwanamke akimwongoza mwanamke mmoja katika Swala, basi mwanamke husimama kuliani kwake, mfano wa hali ya maamuma wa wanaume.

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

[1] Muttafaq, ameipokea Bukhariy katika kitabu cha (Al-Adhaan), Mlango wa (Salatul Jamaa), Hadithi: (645); na Muslim katika kitabu cha (Al-Masaajid Wa Mawadhii’ As-Salah), Mlango wa (Fadhlu Salaat Al-jamaa Wa Bayaan At-Tashdiid Fil Jamaa), Hadithi:(650), na tamko lake ni la Muslim.

[2] Wameipokea Abu Dawuud (460); An nasaiy (838); na An-Nawawiy aliisahihisha katika kitabu cha Al-Majmuu: 4/84.

[3] Wameipokea Abu Dawuud katika Kitabu cha (Sala), Mlango wa (Imamatun Nisaa) Hadithi: 591, na hakuiweka katika Dhaifu; Ad Daar Qutniy katika (As-Sunan): 1/279; Al-Haakim katika (Al-Mustdrak): 1/320, Hadithi: 730; Al Baihaqiy katika (As-Sunan Al-Kubraa) Mlango wa (Ithbaat imamat Al-marah Lil Marah): 3/130, Hadithi; 5136, na Hadithi hii imesahihishwa na Ibn Khuzaimah, kama ilivyotajwa katika: Nailul Awtaar: 3/196.

[4] Ad-Dar Qutniy ameipokea katika As-Sunan; 1/404; Al-Baihaqiy katika As-Sunan Al-Kubraa: Mlango wa: Al-Marah Taummu An Nisaa Fa Taquum Wasatahunna: 3/131, Hadithi: 5138, na An-Nawawiy aliisahihisha katika Al-Majmuu: 4/95.

[5] Ad-Dar Qutniy ameipokea katika As-Sunan; 1/405; Al-Baihaqiy katika As-Sunan Al-Kubraa: Mlango wa: Al-Marah Taummu An Nisaa Fa Taquum Wasatahunna: 3/131, Hadithi: 5140, na An-Nawawiy aliisahihisha katika Al-Majmuu: 4/95.

[6] Abdur-Razzak ameipokea: 3/140, Hadithi: 5083; Al-Baihaqiy katika As-Sunan Al-Kubraa, Mlango wa: Al-Marah Taummu An Nisaa Fa Taquumu Wasatahunna: 3/131, Hadithi: 5141.

[7] Ibn Hazm aliitaja katika Al-Muhallaa: 3/128.

[8] Al-majmuu: 4/94; Al-Mughniy: 2/ 17.

[9] Asnaa Al-Mataalib; 1/209.

[10] Sharh Muntahaa Al-Iraadaat: 1/260.

[11] Hashiyat Ibn Abidiin: 1/565.

[12] Ameipokea Ahmad katika Al-Munad: 6/66, Hadithi: 244221; At-Tabaraniy Katika Al-Muujam Al-Awsat: 9/142, Hadithi: 9359.

[13] Iilaa As-Sunan: 4/242.

[14] Taz. Hashiyat Ibn Aabidiin Alaa Al-Bahr Ar-Raaiq: 1/372; Fat-h Al-Qadiir: 1/352- 354.

[15] Taz. Fat-hul Qadiir: 1/352-354; Al-Inayah Sharh Al-Hidayah: 1/353.

[16] Majmaa Az-Zawaaid: 2/33.

[17] Al-Kaashif Fi Maarifat Man Lahu Riwayah Fil Kutub As-Sittah: 1/590.

[18] Al-Ilal Al-Mutanayiyah: 2/898.

[19] Musnad Ahmad: 3/140.

[20] Ii’laa As-Sunan: 4/242.

[21] Taz. At-Talwiih Sharh At-Tawdhiih: 2/243.

[22] Taz. Qawaadih Al-Illah Fil Qiyaas, katika Sharh Al-Kawkab Al-Muniir, na Ibn An-Najjar: Uk. 542.

[23] Ameipokea Abu Dawuud katika Kitabu cha (Sala), Mlango wa (At-Tashdiid Fi Dhalika), Hadithi: 570.

[24] Ameipokea Ibn Khuzaimah katika (Sahih) yake, Mlango wa (Ikhtiyaar Salaat Al-Marah Fi Makhdaiihaa Alaa Salatihaa Fi Baitihaa): 3/95, Hadithi: 1691.

[25] Ameipokea Ibn Khuzaimah katika (Sahih) yake, Mlango wa (Ikhtiyaar Salaat Al-Marah Fi Baitihaa Alaa Salaatihaa Fi Hujratihaa): 3/94, Hadithi: 1686; Ibn Hibban katika (Sahih) yake; 12/ 412, Hadithi: 5598.

[26] Al-Mu’jam Al-Wasiit: 1/461; An-Nihayah Fi Ghariib Al-Athar: 2/250; Al-Misbaah Al-Muniir: 1/165.

[27] Al-Misbaah Al-Muniir: 2/510.

[28] Fat-hul Qadiir: 1/354.

[29] Sharh Al-Kharshiy Alaa Mukhtasar Khaliil: 2/22.

[30] Al-Fawakih Ad-Dawaniy: 1/205, na Hadithi hii ameipokea Bukhariy: 4073.

[31] Adh-Dhakhiirah: 2/242.

[32] Ameipokea Abdur-Razzaq katika (Al-Musannaf): 3/149, Hadithi; 5115; At-Tabaraniy kwa njia ya Abdur-Razzaq katika Al-Mu’jam Al-Kabiir: 9/295, Hadithi: 9484, kuwa ni Mauquuf kwa Ibn masuud RA.

[33] Ameipokea Ibn Abi Shaibah katika Al-Musannaf; 1/537.

[34] Al-Mughniy: 2/13

[35] Hashiyat Ad-Disuuqiy Alaa Ash-Sharh Al-Kabiir: 1/330-331.

[36] Al-Mughniy: 2/96.

[37] Sharh Al-Khrshiy Alaa Mukhtasar Khaliil: 1/376.

[38] Upokeaji wake ni hapo juu.

[39] Ad-Dirayah Fii Takhriij Ahadiith Al-Hidayah: 1/171.

[40] Nasbur-Rayah: 2/44-45.

[41] Fat-hul Qadiir: 1/360.

[42] Al-Mughniy: 2/18

[43] Upokeaji wake ni hapo juu.

Share this:

Related Fatwas