Uharamu wa Kuyashambulia Makanisa.
Question
Nini hukumu ya kushambulia makanisa na mahali pa ibada au kuyaharibu maeneo haya? Nini hukumu kama kuna watu ndani ya maeneo haya wanaabudu? Baadhi ya Watu wanadai kwamba hakuna agano kati yao na Waislamu, je, kauli yake ni kweli?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wafuasi, na baada ya hayo:
Uislamu ni dini ya kuishi pamoja, na kanuni zake hazina kulazimisha, na hazikiri kwa dhuluma, kwa hivyo Uislamu haukuwalazimisha wenye dini zingine kusilimu, lakini ilifanya jambo hili kwa hiari ya mwanadamu mwenyewe, katika Aya nyingi sheria inatoa uhuru wa dini; kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hapana kulazimisha katika Dini. Kwani Uwongofu umekwisha pambanuka na upotofu) [AL BAQARAH: 256], na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na sema: Hii ni kweli itokayo kwa Mola wako Mlezi. Basi atakaye, aamini. Na atakaye, akatae} [AL KAHF: 29], na kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pia {Nyinyi mna dini yenu, nami nina Dini yangu} [AL KAFRUN: 6].
Uislamu ulipoacha watu kwenye dini zao, uliwaruhusu kuabudu katika mahala pao pa ibada, na uliwahakikishia usalama wa mahali pa ibada, na uliangalia maeneo haya; tena ulizuia aina zote za kuyashambulia. Hakika Qur`ani imefanya kushinda kwa Waislamu na jihadi yao ili kuondosha dhulumu na kuzui uadui na kuwawezesha kwao katika ardhi ni sababu ya kuhifadhi mahali pa ibada kutokana na uharibifu na kuhakikisha usalama wake na usalama kwa wamiliki wake, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu alivyosema: {Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu, basi hapana shaka zingelivunjwa nyumba za watawa, na Makanisa, na masinagogi, na Misikiti, ambamo ndani yake jina la Mwenyezi Mungu linatajwa kwa wingi. Na bila ya shaka Mwenyezi Mungu humsaidia yule anaye msaidia Yeye. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye nguvu Mtukufu. (41). Wale ambao tukiwapa madaraka katika nchi husimamisha Sala, na wakatoa Zaka, na wakaamrisha mema, na wakakataza mabaya. Na kwa Mwenyezi Mungu ndio marejeo ya mambo yote} [AL HAAJJ: 40-41].
Ibn Abbas R.A. amesema: “Nyumba za watawa: ni mahekalu ya Mayahudi, na Makanisa: ni ya Wakristo, na Misikiti: ni ya Waislamu” [Imepokelewa kutoka kwa Abd Ibn Hamid na Ibn Abi Hatim katika tafsiri].
Muqatil Ibn Suleiman amesema katika [Tafsiri] yake [2/385, Ch. Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]: "Wenye dini hizi wote humtaja Mwenyezi Mungu sana katika Misikiti yao, basi Mwenyezi Mungu aliwakinga Waislamu kwa hili”
Imam Al-Qurtwubiy alisema katika (Tafsiri} yake [12/70, Ch. Dar Al-Kutub]: “Lau kuwa Mwenyezi Mungu hakuwaruhusu Mitume kupigana kwa ajili ya kujikinga na maadui zao basi washirikina wangelitawala na kuondosha majengo yote ya ibada ya dini nyingine, lakini ameweka ulinzi kwa kuwajibisha kujikinga na maadui ili wenye dini wapate kufanya ibada zao. Jihadi ni suala la kale ulimwenguni, na kutokana nayo mambo ya sheria yalikuwa sawa, kana kwamba Mwenyezi Mungu alisema: iliidhinishwa katika mapigano, waumini wapigane. Hapo akaimarisha jambo hili katika mapigano kwa kusema kuwa: (Na lau kuwa Mwenyezi Mungu hawakingi watu kwa watu) yaani lau hakukuwepo kupigania jihadi, basi haki ingeshindwa katika kila taifa”.
Kwa mujibu wa Sunna, Mtume S.A.W. aliandika kwa Askofu wa Bani Al-Harith Ibn Ka'b na Maaskofu wa Najran na Mapadri wao na wale waliowafuata na Watawa wao: (amemwandikia Askofu wa Bani Harith Bin Kaab na Askofu wa Najraan na makasisi wengine: “Wanayo yale wanayoyamiliki mikononi mwao iwe kidogo na kikubwa katika nyumba za ibada, na swala zao, na Utawa wao, na ujirani na Mtume wa Mwenyezi Mungu (Rehma na amani zimshukie), na mimi simbadilishi Askofu na uaskofu wake, na wala Kasisi na ukasisi wake, na wala sibadilishi haki miongoni mwa haki, na wala sibadilishi chochote katika vile walivyokuwa navyo, kusuluhisha na kutengeneza ni kwao wenyewe, bila ya kufanya dhuluma na wala kudhulumiwa).
Imepokelewa kutoka kwa Abu Obeid Al-Qasim Ibn Salam kwenye kitabu cha [Al-Amwa Uk. 244, Ch. Dar Al-Fikr], Abu Omar Ibn Al-Numayriy katika kitabu cha: [Tarikh Al-Madina Al-Munawara 2 / 584-586, Ch. Dar Al-Fikr], na Ibn Zangwai katika kitabu cha: [Al-Amwal 2/449, Ch. Markaz Faisal Lilbuhuuth], Ibn Saad katika kitabu cha: [Al-Twabaqaat Al-Kubra 1/266, Ch. Dar Sader], na Al-Hafiz na Al-Baiyhaqi katika kitabu cha: [Dalaail Al-Nubuwah 5/389, Ch. Dar Al-Kutub Al-Elmiyah], na ilitajwa na Imamu Muhammad ibn Hassan Al-Shaibani kwenye kitabu cha [Al-Sir 1/266, Al-Dar Al-Mutahida Lilnashr].
Mwenyezi Mungu amewaamrisha waislamu kuonesha wema na upendo na usawa wanaposhirikiana na wafuasi wa itikadi nyingine, akasema {Mwenyezi Mungu hakukatazini kuwafanyia wema na uadilifu wale ambao hawakukupigeni vita, wala hawakukutoeni makwenu. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao uadilifu} [AL MUMTAHINAH: 8].
Kwa ajili hiyo, Waislamu waliotangulia wakati wa historia yao nzuri na tabia zao njema ambazo zilipenya na kuingia katika nyoyo za watu ambao waliingia katika miji yao, tangu zama za makhalifa walioongoka mpaka sasa.
Maneno ya Omar Bin Al Khatab “Haya ndio aliyoyatoa mja wa Mwenyezi Mungu Omar kiongozi wa waislamu kwa watu wa Ilyaai, kuwapa ulinzi na amani wa nafsi zao na mali zao na Makanisa yao na sala zao na mila zao nyingine. Msikae katika Makanisa yao wala msiyabomoe wala musipunguze kitu hata kama ni kidogo, hata msalaba wake, na chochote katika mali zao, wala msiwalazimishe juu ya dini yao na wala asidhuriwe yeyote katika hao”
Na kwa haya yaliyomo katika waraka ni ahadi ya Mwenyezi Mungu na dhima ya Mtume wake (Rehma na amani zimshukie) na dhima ya viongozi na dhima ya waumini pindi wakipewa wale wenye kutakiwa kulipa kodi. Na hili wameshuhudia Khalid Bin Walid, Amru Bin Aas, Abdulrahman Bin Auf, Muawiyah Bin Abi Sufyan.
Na akaandika waraka kwa watu wa Ludda wenye kufanana na huu, “kwa jina la Mwenyezi Mungu Mwingi wa rehema Mwenye kurehemu, huu aliotoa mja wa Mwenyezi Mungu Omar kiongozi wa waumini kwa watu wa Ludda na walioingia pamoja nao katika watu wa Palestina, wapeni usalama wa nafsi zao, mali zao, Makanisa yao, misalaba yao, visima vyao na mila zao nyingine: Makanisa yao yasikaliwe wala kubomolewa wala pasipunguzwe ndani yake kitu chochote hata kama ni kidogo, wala msalaba wake wala mali zake, wala musiwalazimishe katika dini yao na wala asidhuriwe yeyote. [2/449, Ch. Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]
Na alipoingia Omar R.A. Nyumba Tukufu ya Qudsi ukakaribia wakati wa swala naye yumo ndani ya Kanisa, akasema kumwaambia Askofu: “Ninataka kuswali” akaambiwa: “Swali hapo ulipo, hakuswali pale alipo na akaswali peke yake katika ngazi iliyopo nje ya mlango wa Kanisa. Alipomaliza swala akamwambia Askofu: “Ningeliswali ndani ya Kanisa waislamu baada yangu wangelilichukua na kusema Omar aliswali sehemu hii”. Ibn Khaldun ametaja hivyo katika “Historia yake” [2/225, Ch. Dar At-Turath Al-Arabi]
Na wamagharibi wamelichukua tukio hili kwa mshangao mkubwa sana kama alivyofanya Darmunghim katika kitabu chake “Maisha ya Muhammad (Rehma na amani zimshukie). Na Qur`ani na Hadithi za Mtume zina mifano mingi sana yenye kuonesha usamehevu. Na wafunguzi wa kiislamu walifuata nyayo za waliowatangulia kwa umakini zaidi. Wakati Omar alipoingia Qudsi alitoa maagizo kwa waislamu kuwa wasiwasababishie Wakiristo au Makanisa yao matatizo yoyote. Na alipoitwa na kiongozi wa Kikiristo kufanya ibada ndani ya kanisa alijizuia na kutoa sababu ya kuwa, pindi angeliingia na kuswali ndani ya kanisa basi waislamu wangeliwashinda wakiristo na kufanya kuwa ni sehemu yao, "na mfano wake ni B. Smith katika kitabu chake: [Muhammad na Muhammadiyah, At-Tasamuh Wal-Adawaniya, Salih Al-Husein,[Uk 120-121].
Na mfano kama huu Khalid bin Waliyd aliwapa usalama na amani watu wa Damascus kwenye makanisa yao na akawaandikia pia, kama ilivyotajwa na Al-Balathriy katika kitabu cha: [Futouh Al-Bildaan Uk. 120, Lajnatul Bayan Al-Arabi].
Na mfano mwingine unaofanana na huu, Sharhabiyl Bin Hassan R.A. amewaandikia watu wa Twabariya, akawapa usalama wa nafsi zao na Makanisa yao. Al-Balathriy katika kitabu cha: [Futouh Al-Bildaan Uk. 115, Ch. Lajnatul Bayan Al-Arabi].
Watu wa Baalbek walimuulizia Abu 'Ubaydah' Aamir Ibn Al-Jarrah, R.A., akawapa usalama wa Makanisa yao, kwa hivyo akawapa kitabu, kama ilivyosemwa katika kitabu Cha: [Futouh Al-Bildaan Uk. 129], Vilevile wamefanyiwa watu wa Hums na watu wa Halab, kama ilivyooneshwa katika kitabu cha: [Futouh Al-Bildaan Uk. 130-146] .
Iyaadh Bin Ghannam (Radhi za Mwenyezi Mungu zimshukie) kawaandikia watu wa Riqa kupewa usalama wa nafsi zao na usalama wa Makanisa yao na akawaandikia mkataba uliotajwa na Al-Balathri katika kitabu cha: [Futouh Al-Bildaan Uk. 172].
Namna hiyo hiyo amefanya Habib Ibn Muslima R.A. kwa watu wa Dabiyl, ni mji uliopo Urminia, akawapa amani wa nafsi zao, mali zao, Makanisa yao na nyumba za Watawa wao wa Kiyahudi na Kinasara na waabudiao moto, waliokuwepo na wasiokuwepo, akawaandikia mkataba, na hayo yalikuwa katika zama za uongozi wa Othman Bin Affan R.A.. Kama ilivyotajwa katika kitabu cha: [Futouh Al-Bildaan Uk. 199].
Imepokewa kutoka kwa Abi Ibn Abdallah Anaghaiy amesema: “Omar Bin Abdul Aziz R.A. alituletea barua kuwa “msibomoe nyumba za Watawa, wala Kanisa, wala nyumba za waabudiao moto”. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abi Shaiba katika kitabu cha: [Al-Musanaf na Abu Ubaid Alqasim Ibn Salaam katika kitabu cha: [Al-Amwal Uk. 123, Ch. Dar Al – Fikr].
Kutoka kwa Atwaa R.A. aliulizwa: “je Makanisa hubomolewa? Akasema “Hapana” isipokuwa yaliyomo ndani ya Haram” [Imepokewa kutoka kwa Ibn Abi Shaiba katika “Al-Musanaf”].
Na ilipotokezea matatizo katika mikataba hii ikarudishwa kwa kiongozi na kuifanyia marekebisho kisha ikarudishwa tena kwa wenyewe: imepokewa kutoka kwa Ali bin Abi Himlah amesema; tuliwashitaki wageni wa Damascus kwa Omar Bin Abdul Aziz R.A. kuhusu Kanisa ambalo mtu fulani alilifanya kuwa ni la bani Nasri nchini Damascus, Omar akatutoa ndani ya kanisa hilo na kuwarudishia (wenyewe) Manasara.
Kwa hivyo, ni wazi kwamba kuyabomoa au kuyaharibu Makanisa, kuwaua au kuwatisha watu wao ni miongoni mwa mambo ambayo hayaruhusiwi katika sheria ya Kiislamu, bali jambo hili ni ukiukwaji wa Dhima ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W. Na mwenye kufanya hivyo amefanya Mtume S.A.W. ni hasimu wake siku ya kiyama; imepokewa kutoka kwa Abu Dawud katika kitabu cha: [Sunan], na kutoka kwa Ibn Zanjawih katika kitabu cha: [Al-Amwal], na kutoka kwa Al-Baihaqiy katika kitabu cha: [Al-Sunan Al-Kubra] kutoka kwa Swafwan Ibn Sulaim, kutoka kwa Maswahaba wengi – kutoka kwa Ibn Zanjawih na Al-Baihaqiy: kutoka kwa karibu Masahaba thelathini wa Mtume wa Mwenyezi Mungu kutoka watoto wa masahaba wa Mtume S.A.W. Kutoka kwa baba zao - ambao ni karibu na ukoo - kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.W.A. akasema: “Mwenye kumdhulumu mtu wa dhima au kumkalifisha zaidi ya uwezo wake basi mimi nitakuwa kinyume naye (hasimu yake) siku ya kiyama.”, Ibn Zanjawih na Al-Baihaqiy waliongeza:
Na Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. ameashiria kidole chake kwa kifua chake akisema: “Atakaemuua aliefungamana ahadi na Waislamu (au dola ya kiislamu), hatosikia harufu ya pepo (yaani hatoingia peponi), na harufu ya pepo inasikika mwendo wa miaka sabini”. Al-Haafiz Al-Iraqiy alisema katika kitabu cha: [Sharul tabsirah wal tadhkirah kuwa Uk. 191]: “Hadithi hii mapokezi yake ni hasan, hata ikiwa haikutaja majina ya Maswahaba wengi walioipokea”.
Kuhusu yale yanayopatikana katika vitabu vya Fiqhi ya Kiislamu miongoni mwa baadhi ya maoni kuhusu ubomoaji wa Makanisa: ni maoni ambayo yana muktadha wake wa kihistoria na yanahusiana na hali ya kijamii katika wakati maalum, na hairuhusiwi kamwe kufanya maoni haya yatawale Sheria; kwani dalili za kisheria na ambazo ni wazi, historia nzima ya Kiislamu na ustaarabu wa Waislamu, vile vile kukaa kwa Makanisa na mahekalu yenyewe katika nchi yote ya Uislamu, katika Mashariki na Magharibi, katika nyakati za zamani na za kisasa - yote haya yanathibitisha kwa uwazi jinsi Uislamu ulivyoheshimu mahali pa ibada na kuipatia utunzaji na ulinzi hali isiyopatikana katika dini yoyote au ustaarabu mwingine.
Kama kwamba hukumu ya mwenye mamlaka inaondoa tofauti; basi kama mwenye mamlaka akichagua madhehebu maalumu ya kifiqhi akiona kuwa madhehebu hii ina masilahi na usalama wa kijamii, imekuwa ni lazima kufuatwa na wote ambao walikuwa chini ya mamlaka yake, na hairuhusiwi uhalifu wa madhehebu hii, vinginevyo akihesabiwa uhalifu wa amri ya mwenye mamlaka na uhalifu kwa waislamu wote na maoni yao, jambo ambalo linasababisha ufisadi unaopotea masilahi ya nchi na raia pia.
Hapana shaka kuwa kuyafanyia uadui Makanisa na wakristo nchi Misri na kokote kule duniani ni kuvunja ahadi ya utaifa (uzalendo), kwani wao ni wananchi na wana haki, na wamewekeana ahadi na waislamu ya kuishi kwa pamoja na kwa salama. Kuwafanyia uadui au kuwabughudhi na kumwaga damu zao au kubomoa na kuvunja Makanisa yao kuna utenguaji wa ahadi na kupoteza dhima ya waislamu kitu ambacho kimekatazwa na Aya za Qur`ani pia mienendo ya Masahaba. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: [Enyi mlio amini! Timizeni ahadi] [AL MAIDAH: 1].
Imepokewa na Imam Al-Bukhariy katika kitabu chake kutoka kwa Abdalla Ibn Amru R.A. kuwa Mtume S.A.W. anasema: “Mambo manne mwenye kuwa nayo huwa ni mnafiki wa kweli, na mwenye kuwa na chembe yake basi huwa na chembe ya unafiki mpaka aliache; akiaminiwa hatimizi, akizungumza hudanganya, akiahidiwa huvunja ahadi na akigombana basi huvuka mipaka.
Na katika mapokezi ya Ibn Maja kutoka kwa Amru Ibn Al-Hamaq Al-Khuzaiy kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: “Pindi mtu atakuwa yupo katika amani ya nafsi yake kasha akamuua hubebeshwa bendera ya kuvunja ahadi katika siku ya Kiyama”
Katika mapokezi ya Al-Baihaqiy na Al-Twailasi kwamba “Pindi mtu atakuwa yupo katika amani ya nafsi yake kasha akamuua (mwingine) basi mimi niko mbali na muuaji na hata kama aliyeuliwa ni kafiri.”
Na imepokewa kutoka kwa Al-Bukhariy kutoka kwa Ali R.A. kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: “Dhima (ahadi) ya waislamu ni moja wanakuwa nayo hadi mdogo wao basi mwenye kuikengeuka laana za Mwenyezi Mungu na Malaika na watu wote ni juu yake, na hatakubaliwa matendo wala amali 49.(hatokubaliwa matendo yake yoyote, ya faradhi au ya Sunna”.
Pia haifichikani kuwa, kutoyalinda Makanisa na kinyume chake kuwatishia watu wake, ni katika kuvunja ahadi na kuwakera wananchi. Imepokewa kutoka kwa Abu Dawud, na Al-Hakim kutoka kwa Abi Hurayra R.A. amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. amesema: “Muumini haiwezikani kusambaratika imani yake hata kidogo”. Ibn Al-Athiir alisema katika Al-Nihaya kuwa: “kusambaratika hutokea kwa mwingine wakati ambapo mwenzake alipoghafilika akamshambulia na kumwuua”.
Na maana ya Hadithi hii ni kuwa; imani inazuia mtu kusambaratika kama inavyozuia pingu mtu kutoweza kufanya atakalo.”
Mtume S.A.W. amewausia watu wa Misri wasia maalumu, akasema kutoka kwa mama wa waumini Ummu Salama R.A. kuwa Mtume S.A.W. ameusia wakati wa kufariki kwake, akasema; “Tahadharini tahadharini na Waqibti wa Misri, nyinyi mtakwenda kwao na watakupokeeni na ni wasaidizi katika njia ya Mwenyezi Mungu”, Al-Hafidh Al-Haythamiy alisema: “Wapokezi wake ni wa Sahihi”
Imepokewa kutoka kwa Abu Yala katika "Musnad yake" na kutoka kwa Ibn Hibban katika "Sahihi yake" kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akasema: “Wausieni (Waqibti) kheri,; kwani wao ni nguvu kwenu na watakuwa wasaidizi wenu katika kushinda adui yenu, kwa amri ya Mwenyezi Mungu”. Al-Hafidh Al-Haythamiy alisema: “Wapokezi wake ni wa Sahihi”.
Imepokewa kutoka kwa Ibn Saad katika kitabu cha: [Al-Twabaqat Al-Kubra] - kama ilivyo katika kitabu cha: [Kanzul Umaal kwa Al-Mutaqiy Al-Hindiy 5/760, Muasastur Resalah] – kutoka kwa Musa ibn Jubayr, kutoka kwa mashehe wa watu wa Madina: kuwa Omar Bin Al-khatwab R.A. amemwandikia kiongozi wa Misri Amru Ibn Al-Aas R.A.: “Elewa ewe Amru kuwa Mwenyezi Mungu anakuona na anaona matendo yako Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema {Na tukawafanya wacha Mungu kuwa ndio viongozi} akikusudia; kuwa ndio afuatwe. Na unao watu wa dhima na wa ahadi na Mtume S.A.W. amewausia Maqibti akasema: “Wausieni Waqibti kheri, kwani wana dhima na nasaba” yaani mama wa Mtume Ismail alikuwa miongoni mwao. Na Mtume S.A.W. amesema: “Mwenye kumdhulumu mtu wa dhima au kumkalifisha zaidi ya uwezo wake basi mimi nitakuwa kinyume naye (hasimu yake) siku ya kiyama.” Jihadhari ewe Amru kuwa Mtume yuko kinyume nawe (hasimu yake), kwani mwenye kuwa kinyume naye basi atakuwa mbali mno.
Na mwenye kuangalia historia ataona ukweli wa maneno ya Mtume S.A.W. kwa namna alivyowakaribisha Maqibti wa Misri kwa waislamu waliofungua na wao wakawafungulia nyoyo zao. Na wakaishi nao kwa amani na usalama. Na kuifanya Misri kuwa ni jaribio kubwa la historia iliyojaa mafanikio ya kuishi kwa pamoja na kushirikiana ndani ya nchi moja baina ya raia zake kama sheria inavyosema.
Na kwa kuwa kuna ulazima wa kuhifadhi mambo matano ambayo mila zote zimekiri kuyahifadhi nayo ni;- dini, nafsi, akili, heshima na mali kwa kuwa haya ndio mambo ya msingi wa kila sheria.
Na baadhi ya waovu wanapinga haya makusudio matano ya kisheria ambayo ni lazima yalindwe na kuhifadhiwa, mfano kuhifadhi nafsi, anayeuliwa huwa ni raia asiyejua hili wala lile na ana nafsi ambayo ni lazima ilindwe isiyohitaji kufanyiwa uadui. Mwenyezi Mungu ameipa nafsi ya mwanadamu nafasi ya juu kabisa akasema: {Aliyemuuwa mtu bila ya yeye kuuwa, au kufanya uchafuzi katika nchi, basi ni kama amewauwa watu wote. Na mwenye kumuokoa mtu na mauti ni kama amewaokoa watu wote.} [AL MAIDAH: 32.].
Kwa ajili hii, uharibifu wa nafsi ni katika ufisadi mkubwa, kwani kuna sura mbaya inajengeka katika akili za watu wa Mashariki na Magharibi kwa kuwapa picha isiyo sahihi ambayo maadui wa Uislamu wanaidhihirisha ulimwenguni kuwa Uislamu una kiu ya damu nalo ni neno lisilo na ukweli ndani yake. Kwa njia hii maadui wengi wamepitia njia hii kwa ajili ya kusema mambo ya ndani ya Uislamu bila ya haki.
Mwenyezi Mungu ameamrisha kuacha sababu za kupelekea kuwatusi wengine ili wasije kumtusi Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema {Wala msiwatukane hao wanao waomba badala ya Mwenyezi Mungu, wasije na wao wakamtukana Mwenyezi Mungu kwa jeuri bila ya kujua. Namna hivyo, tumewapambia kila umma vitendo vyao. Kisha marejeo yao yatakuwa kwa Mola wao Mlezi, naye atawaambia waliyokuwa wakiyatenda.} [AL ANAAM:108].
Imamu Ar-Raziy amesema katika kitabu cha: [Tafsiri yake 13/115, Ch. Dar Al-Kutub Al-Elmiyah] kuwa: “Aya hii inaonesha kuwa makafiri hawatakiwi kutendewa kile ambacho kitazidi kuwaweka mbali na ukweli na kuwazidishia inadi, na kama itafaa basi ingefaa kuamrishwa, na Mwenyezi Mungu anaamrisha upole wakati wa ulinganio kama mfano wa Mtume Mussa na Harouna A.S. {Mukamwambie maneno laini huenda akakumbuka au akaogopa}
Hali hii ikiwa tendo lenyewe linaruhusiwa, vipi ikiwa tendo hilo hapo awali lilikuwa haramu?
Mauaji na vitisho katika vitendo hivi vya ubaya huitwa (Al-Harabah). Nayo ni ufisadi katika ardhi na ufisadi, na mwenye kufanya tendo hilo anastahili adhabu kali kuliko ya muuaji, ya mwizi na ya mzinzi, kwa sababu mwenye uhalifu huu anafanya hivyo dhidi ya jamii. Mwenyezi Mungu amesema: {Basi malipo ya wale wanao mpiga vita Mwenyezi Mungu na Mtume wake na wakawania kufanya uchafuzi katika nchi, ni kuuwawa, au kusalibiwa, au kukatwa mikono yao na miguu yao kwa mabadilisho, au kutolewa nchi. Hii ndiyo hizaya yao katika dunia; na katika Akhera watapata adhabu kubwa} [AL MAIDAH: 33].
Kuhusu mitazamo ya baadhi yao: kwamba ahadi ambayo ilikuwa kati yetu na wao ni ahadi ya dhima, na ahadi hii imeondolewa, na kwa hivyo hakuna ahadi kati yetu na wao: mtazamo huu ni wa uwongo na kuna upungufu mkubwa wa ufahamu na Fiqhi; uraia ni msingi wa Kiislamu uliopitishwa na sheria ya Kiislamu, ambao kwa njia yao imekubaliwa kutumika katika katiba za nchi zote za Kiislamu, pamoja na Katiba ya Misri, ambayo imetajwa katika Kifungu cha pili kwamba sheria ya Uislamu ni rejeleo la msingi. Uislamu umeweka msingi wa uraia tangu karne kumi na nne; msingi ambao Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. ameutekeleza katika hati ya Madina, ambayo huthibitisha kuishi pamoja, ushirikiano, na usawa katika haki na majukumu kati ya wananchi wa nchi moja bila kujali mazingatio ya kidini, kikabila, madhehebu au mambo yoyote mengine, na kisha mkataba huu ni miongoni mwa mikataba ambayo ni halali na ambayo lazima itimizwe.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.