Kumwita Mtoto Asiyeujua Ukoo wake, ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kumwita Mtoto Asiyeujua Ukoo wake, kwa Jina la Mlezi wake.

Question

Je, inajuzu kisharia Kumuita mtoto asiyeujua ukoo wake, kwa jina la Mlezi wake na kudai kuwa ni mwanae, kwa hoja ya kuyalinda masilahi yake? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Haijuzu kisharia kwa Mlezi au Mdhamini kumwita mtoto kwa jina lake, ambapo mtoto huyo atakuwa na ubini wake kikamilifu, kwa sababu hii ni aina ya kujiasilishia mtoto, ambayo imeharamishwa kisharia. Na Mwenyezi Mungu amesema: {Waiteni kwa (ubini wa) baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu}. [AL AHZAAB: 5], na inajulikana kuwa Sahaba Mtukufu Zaid Ibn Harithah alikuwa akiitwa (Zaid bin Muhammad) wakati Mtume S.A.W. alipomuasilisha yeye kama mwanae, na ilioposhuka hukumu hiyo ya kuharamisha uasilishaji, jina lake lilirejeshewa ubini wake kama lilivyokuwa awali (Zaid Bin Harithah).
Na kinachojuzu ni kumpa mtoto aliyeasiliwa, jila la familia ya mdhamini wake, ambapo itakuwa wazi kumnasibishia na familia hiyo, na kuepusha udanganyifu wa kuwa mtoto huyo ni wake kweli; ili isije kuingia katika Uasilishaji ulio haramu Kisheria, lakini ubini wa mtoto yatima au asiyeujua ukoo wake utakuwa mfano wa uhusiano wa muungano uliokuwa kati ya Makabila ya Waarabu zamani.
Na hii sio miongoni mwa Uasilishaji haramu kisharia; maana Uasilishaji ni kumuunga mtoto wa mwingine ili awe mtoto wake mwenyewe na kumuweka mahali pa mtoto wake mwenyewe katika mirathi, nasaba, na upweke wa wanawake wa familia kama kwamba mtoto huyo ni sehemu ya jamaa zake, na mengineyo yaliyo maarufu zama za Ujahili na mwanzoni mwa Uislamu, kisha Uislamu uliyaharamisha kwa ajili ya kutozichanganya nasaba.
Na uhusiano huu uliotajwa unajuzu kisharia, na maneno ya Wanachuoni wa Tafsiri ya Qur`ani Tukufu huashiria hivyo. Na Mtaalamu At-Tahir Ibn A’ashur kwenye tafsiri yake katika kauli ya Mwenyezi Mungu: {Waiteni kwa (ubini wa) baba zao, maana huo ndio uadilifu zaidi mbele ya Mwenyezi Mungu. Na ikiwa hamwajui baba zao, basi ni ndugu zenu katika Dini, na rafiki zenu. Wala si lawama juu yenu kwa mlivyokosea. Lakini ipo lawama katika yale ziliyofanya nyoyo zenu kwa makusudi. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu}. [AL AHZAAB: 5].
Alitaja kuwa: maana ya urafiki katika kauli yake (rafiki zenu) ni uhusiano wa muungano. [Taz. At-Tahrir Wat-Tanwir: 21/263, Ch. ya AD-Dar At-Tunusiyah Linnashr].
Na Mtaalamu Al-Alusiy anasema: “Kauli yake (rafiki zenu) yaani wasaidizi wenu katika dini, kwa hiyo waiteni ndugu na wasaidizi, yaani katika dini. Na maana hiyo hiyo, baada ya kuteremshwa Aya hii, kuambiwa Salim: Rafiki ya Hudhifah, maana Hudhifah alimuasili kabla ya hapo. Na imesemwa (rafiki zenu) yaani watoto wa ndugu za baba zenu, na huitwa hivyo kwa njia ya kufurahisha nyoyo zao, na kwa hiyo hawakuitwa kwa majina yao tu”.
Akasema pia: “Ni wazi Aya hiyo inaonesha uharamu wa kumuita mtu kwa ubini usio wa baba yake, na huenda hilo likawa katika njia iliyokuwa wakati wa Ujahili, lakini ikiwa kinyume cha hilo kama mkubwa kumwambia mdogo: Mwanangu, kwa njia ya upole na huruma – kama invyotokea siku zote – basi kwa uwazi wake huo, hakuna uharamu wowote”.
Na katika Hashiyat Al-Khafaji Ala Tafsiir Al-Baidahwiy: uana unalingana na udugu, lakini umekatazwa kwa sababu ya milingano wa makafiri, na katazo hapa ni aina ya ubora. [Mwisho].
Na huenda hakutaka katazo lililotajwa katika Aya, maana Aya huonesha uharamisho wa kuita kwa njia iliyokuwa wakati wa Ujahili”. [Mwisho, kutokana na: Ruhul Maaniy: 21/148-149, Ch. ya Dar Ihiyaa At-Turath Al-Arabiy, Bairut].
Na Imamu Ibn Kathiir katika Tafsiiri yake anasema: “Kuhusu kumuita mtoto kwa njia ya kumhishimu na kumpendezesha, hayo hayakatazwi katika Aya, na akatoa dalili, miongoni mwake: ilivyopokelewa na Imamu Muslim katika Sahihi yake, kutoka kwa Anas Ibn Malik R.A, alisema: Mtume S.A.W., aliniita “Ewe mwanangu”. [Tafsiir Ibn Kathiir: 6/377-378, Ch. ya Dar Tiibah, 1420 H.].
Na katika Sunna ya Mtume, dalili ya hayo ni; katika Hadithi ya Sahihi Mbili, kutoka kwa Anas R.A, alisema: Mtume S.A.W., aliwaita watu wa Madinah (Al-Ansaar) akawaambia: Je, kuna mtu kati yenu anayenasibishwa na ukoo mwingine? Wakasema: hapana, isipokuwa mtoto wa dada yetu, na Mtume S.A.W., akasema: Mtoto wa dada katika watu ni miongoni mwao”.
Al-Munawiy anasema: “Kauli yake: (Mtoto wa dada ya watu ni miongoni mwao) kwa sababu ananasibishwa na jamaa yao, naye ni mama yake, na anahusiana na jamaa zake katika kila linalopaswa kuhusiana, kama vile: kunusuru, kushauri, kupenda, kufichua siri, kusaidia, kufanya wema, huruma, kufanya ukarimu, na mengineyo”. [Taz. Faidhul Qadir: 1/87-88, Ch. 2, Dar Al-Ma’rifah, Bairut, 1391 H.].
Katika Hadithi hii Mtume S.A.W., alibainisha kuwa mtoto alinasibishwa na kabila la mama yake, ingawa kiuhalisia yeye si miongoni mwao.
Na katika Sahihi Bukhari: Hatib Ibn Baltaa’ah R.A., alimwambia Mtume S.A.W: “Hakika mimi nilikuwa Mkureshi, lakini sikuwa miongoni mwa nasaba zao.
Ibn Hajar katika Sharhu yake anasema: “Kauli yake: (nilikuwa mtu Mkureshi), yaani kwa muungano, maana alisema baadaya: (sikuwa miongoni mwa nasaba yao) hapa hakuna ukinzani wowote, lakini amekusudia kuwa yeye ni msaidizi wao. Na imethibiti katika Hadithi ya: “Rafiki wa watu ni miongoniu mwao”. [Mwisho, Taz. Fat-h Al-Bariy: 8/634, Ch. ya dar Al-Ma’arifah, Bairut]
Na katika Hadithi hii Hatib R.A, alitaja kuwa alinasibishwa na Kabila la Kureshi kwa njia ya muungano, lakini kiuhalisia hana nasaba nao. Na suala letu hili la kumwepusha asiyeujua ukoo wake na Ubini wa mdhamini wake linafahamika kutokana na sura hizi zilizotajwa katika Aya na Hadithi.
Na kwa njia hii kazi za Wema waliotutangulia na Wanazuoni wa Hadithi zimekubalika bila ya kukanushwa; ambapo kati yao kumnasibisha mtu kwa sababu ndogo zaidi au uhusiano wowote kulikuwa maarufu sana, na kama kufanya hivyo kungekuwa haramu au kunalazimisha Uasilishaji uliokatazwa, basi hapana shaka, wao wangezuia haraka kufanya hivyo.
Al-Hafidh As-Sakhawiy katika Sharh yake ya Al-Hafidh Al-I’iraqiy katika Kasida yake ya Elfu anasema:

Walinasibisha awe Badriy kwa sababu maalumu
Aliyeshuka Badr mfano wa U’uqbqh Ibn Amr.

“(Walinasibisha) yaani Wanazuoni wa Hadithi waliwanasibisha baadhi ya Wapokeaji wa Hadithi kwa mahali pa vita, mji, kabila, ufundi, sifa, muungano, au mengineyo na hayo yote hayafahamiki udhahiri wake, lakini kwa (sababu) maalumu, na kuna mifano mingi ya hayo”. [Taz. Fat-hul Mughith Bisharh Alifiyat Al-Hadith: 3/297, Ch. 1, Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah, Lebanon, Mwaka 1403 H.]
Al-Hafidh As-Seyutiy katika kitabu cha: [Tadribu Ar-Rawiy] anasema: “Huenda Mpokeaji wa Hadithi akanasibishwa na mahali, vita, kabila, au ufundi, na udhahiri huu haufahamiki hasa muradi wake ni nini, lakini ni kwa sababu maalumu ya kumshukia mahali hapa au kabila hilo, n.k,” [Taz. Tadribu Ar-Rawiy: 2/340, Maktabat Ar-riyadh Al-Hadithah]
Unasibishaji na mdhamini hauna athari yoyote ya Uasilishaji ulio haramu kisharia, lakini ni mfano wa kuwanasibisha Wanazuoni na Wapokeaji wa Hadithi wawe wa makabila yasiyo yao, na unasibishaji huu umeitwa kwao hata iko dhana ya kuwa wamenasibishwa kizazi, yaani wawe ni watoto wa kiuhalisia.
Kwa hiyo unasibishaji huu usipokuwa na mtu mwenyewe, basi utakuwa kwa sababu zifuatazo:
1- Kumwacha huru, na hali hii ni ya kawaida, kwa mfano: Abul Bukhtariy At-Taaiy, naye ni Tabiina, na jina lake; Saidi Ibn Fayruz, naye ni huru wa Kabila la Taii’, na Bwana wake alikuwa mtu wa Taii’, akamwacha huru.
2- Urafiki wa uhusiano: asili yake ni mkataba na ahadi kwa ajili ya ushirikiano, usaidizi, na makubaliano, kwa mfano: Imamu Malik Ibn Anas Al-Asbahiy At-Taimiy; alinasibishwa na kizazi cha kabila la Asbah, kwa njia ya uhusiano wa kirafiki lakini yeye kiasili ni wa Taim, kwa sababu watu wake (Asbah) ni marafiki wa (Taim Quraish) kwa mkataba wa muungano.
Na Uislamu ulitengua urafiki wa muungano wa Ujahili ulioundwa kwa ajili ya kuzuka fitina, vita kati ya makabila, na mashambulio, bila ya kumnusuru mdhulumiwa, wala kufanya wema kwa jamaa.
3- Urafiki wa kusaidiana kama ujira au kujifunza, kwa mfano: Miqsam, aliitwa Rafiki ya Ibn Abbas kwa sababu ya kumuunga kwa ajili ya elimu, au mfano wa Malik Ibn Anas, ambapo imesemwa kuwa: alinasibishwa na (Taim) kwa sababu babu yake Malik Ibn Abi Amir alikuwa muajiriwa wa Talhah Ibn Ubaidillahi, wakati Talhah alikuwa mfanya biashara.
4- Kupata kunyonya: kwa mfano Abdullahi Ibn As-Saadiy, naye ni Sahaba, na Ibn Abdul Bar katika kitabu chake Al-Istia’ab anasema kuwa: Baba ya huyu Abudullahi ameitwa As-Saadiy kwa sababu aliwahi kunyonyeshwa na Kabila la Ukoo wa Saad Ibn Bakr.
5- Urafiki wa Dini na Uislamu: kwa mfano Muhammad Ibn Ismail Al-Bukhariy Al-Juu’fiy; na Babu yake AlMughirah Alikuwa Mwajemi (Majusiy), na akasilimu mikononi mwa Al-Yaman Ibn Akhnas Al-Juu’fiy, kwa hiyo akanasibishwa naye.
6- Diwani: maana jina lake limeandikwa katika daftari ya wazaliwa wa ukoo wa Diwani hiyo, kwa mfano; Al-Laith Ibn Saad Ibn Abdur-Rahman Al-Fahmiy, akanasibishwa na (Fahm); na jina lake limeandikwa katika Diwani ya Misri miongoni mwa marafiki wa Kinanah Ibn Fahm, na jamaa zake wanasema kuwa: wao ni miongoni mwa Waajemi, Wakazi wa Aspahan, yaani asili yake ni kutoka katika Uhispania, lakini akanasibishwa na (Fahm), maana jina lake liko katika Diwani ya Fahm. [Taz. Tarikh Dimashq: 50/347, Ch. 1, Dar Al-Fikr, Bairut, Mwaka 1419 H.].
Na kumnasibisha Mtu na kabila lisilolo lake ni jambo linaloenezwa na lipo, na kutajwa katika vitabu. Na Ibn As-Salah katika Kitabu chake cha Muqadimat, alitaja kuwa kuna watu walionasibishwa na wasio baba zao; miongoni mwao walionasibishwa na mama, kwa mfano; ShurahbilI bin Hasanah, naye ni mamake, na aliyenasibishwa na nyanya yake, kama vile: Yalaa Ibn Munyah, naye ni Sahaba, na aliyenasibishwa na babu yake, kama vile: Abu U’baidah Ibn Al-jarrah, na aliyenasibishwa na mtu asiye babake kutokana na uhusiano maalumu, kama vile: Al-Miqdad Ibn Al-Aswad, naye ni Al-Miqdad Ibn Amr ibn Tha’labah Al-Kindiy, naye alikuwa mtoto wa kambo wa Al-Aswad Ibn Abdi Yaghuth, kwa hiyo alinasibishwa naye.
Na kuna walionasibishwa na namna ilivyo ndani yake ni kinyume na inavyofahamika kwa nje, kwa mfano: Abu Masu’ud Al-Badriy U’uqbqh Ibn Amr, naye hakushuhudia Vita vya Badri, kwa rai ya wengi, lakini siku moja alifika mahali hapo, kwa hiyo akanasibishwa napo. [Muqadimat Ibn As-Salah, Uk. 629 na zifuatazo, Ch. ya Dar Al-Ma’arif].
Na hii ni mifano ya kweli ambayo inaonesha kuwa: mtu anaweza kujinasibisha na asiye baba yake au kabila lake, kwa kuwa tu hali hiyo haiingii chini ya katazo la kisharia la kuasiliana, nalo ni Kuasili na athari zake, na zaidi ya hayo, ni kama ilivyotajwa kuwa mtu hunasibishwa na mahali alipo tu, kama ilivyotajwa katika mfano wa Abu Masu’ud Al-Badriy.
Na huenda uhusishaji huu unachukua sura pana zaidi, ambapo mtu ananasibishwa na kabila, kwa sababu alikuwa ni rafiki ya rafiki ya kabila, kwa mfano: Said Ibn Yasar Abul Hubab Al-Hashimiy, naye ni rafiki ya Shuqran Mtumwa wa Mtume S.A.W., kwa hiyo alinasibishwa na Bani Hashim. [Taz. Fat-hul Mughith: 3/393].
Na Uhusishaji wa asiye mzazi kama ilivyotajwa katika mifano ya hapo juu, hauna makatazo ya kisharia yaliyopo katika upangaji. Na hali hiyo ndivyo ilivyo hivyo hivyo, katika Kumuasili mtoto na mdhamini wake; kwa sababu kusudio la Uhusishaji huo huambatana na jina tu, na siyo halisi.
Na kwa mujibu wa maelezo hayo:
Kumuita mtoto asiyeujua ukoo wake jina la mdhamini wake hakujuzu kisharia; kwa sababu sura yake ni ya Kuasilisha ambako ni haramu kisheria. Na kuhusu mdhamini au mlezi kumpa mtoto jina la familia, kwa njia ya kumuunga tu kunajuzu kisharia; kwa dalili zilizotajwa hapo juu, ambapo uwazi wa kazi hiyo ni kumuunganisha na familia hiyo bila udanganyifu wa kumfanya awe kama Mtoto wa kumzaa.
Na Uhusishaji huu huleta masilahi ya mtoto – hasa akiwa haelewi ukoo wake – katika vipindi mbali mbali vya umri wake; pamoja na kuwa kazi hiyo itayaongezea maisha yake usalama zaidi, utulivu, na matumaini kwa wingi. Pia mtoto katika hali hii atakuwa na Mlezi mbele ya watu kupitia vipindi mbali mbali vya umri, pamoja na kuihifadhi hukumu ya kisharia kuwa: Uharamu wa Kumuasili mtoto, unatokana na athari zake mbaya. Kwa kufanya hivyo tutakuwa tunalinda makusudio ya Sharia na kutoingia katika jambo ambalo tumetahadharishwa nalo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas