Ushahidi wa Kimaada wa Usahihi wa Q...

Egypt's Dar Al-Ifta

Ushahidi wa Kimaada wa Usahihi wa Qur`ani

Question

 Je, ni ushahidi gani wa kiakili na kimaada unaothibitisha kwamba Qur`ani Tukufu haikuwa na aina yoyote ya mabadiliko kwa kuongeza, kupunguza au kuondosha?
Mweyezi Mungu akujaalieni fahamu, swali hili liliulizwa na mwanafunzi wangu mmoja pale shuleni, na kila nikimpinga kwa hoja anajibu huku akisisitiza maneno yangu hayana majibu ya uhakika, basi tufahamisheni, na Mwenyezi Mungu akujaalieni fahamu.

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Mwenyezi Mungu Mtukufu ameupambanua umma huu kwa sifa, na akaubainisha kwa sifa ambayo haipatikani katika taifa miongoni mwa walimwengu, na sifa hii inawakilishwa na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakao ulinda} [AL HIJR 9]
Ama mataifa mengine Mwenyezi Mungu hakuahidi kuhifadhi vitabu vyao, lakini Mwenyezi Mungu Mtukufu aliwajaalia wahifadhi vitabu vyao, akasema: {Hakika Sisi tuliteremsha Taurati} [AL MAIDAH 44]
Na Mwenyezi Mungu akitaka kitu, atatayarisha sababu zake; Mwenyezi Mungu alipotaka kuhifadhi kitabu hiki, katika kutimiza ahadi yake tukufu isiyovunjika, awatayarishe watakaohifadhi ambao wanakihifadhi kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, na wanakiandika vile vile kinapoteremka kutoka kinywani mwake S.A.W. Na hao wanapokea kutoka kwa waliokihifadhi kama wao, mpaka Qur`ani Tukufu inatufikia imehifadhiwa vifuani, na imeandikwa kwa mistari kama alivyoteremshiwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, na kama ilivyoandikwa mbele yake, hapakuwa na mabadiliko ya herufi wala sura ya herufi, kama vile Fatha, Kasra, Alifu na maumbo mengine.
Nitaeleza historia fupi ya Qur`ani Tukufu kuanzia wakati wa kuteremshwa kwake hadi kuwepo kwake katika vifua na katika mistari.
Kwanza: Kukusanywa kwa Qur`ani Tukufu vifuani:
Zamani Waarabu walikuwa taifa lisilojua kusoma na kuandika isipokuwa wachache tu kati yao. Na Mwenyezi Mungu anasema: {Yeye ndiye aliye mpeleka Mtume kwenye watu wasio jua kusoma, awasomee Aya zake na awatakase, na awafunze Kitabu na hikima, ijapo kuwa kabla ya haya walikuwa katika upotofu ulio dhaahiri}. [AJ JUMU'AH 2]
Mtu asiyejua kusoma na kuandika ana uwezekano mkubwa wa kuitegemea kumbukumbu yake katika mambo yanayomhusu, hasa iwapo atakumbuka kwa nguvu.
Na Mtume S.A.W, alikuwa na shime ya kuikariri Qurani na kuihifadhi, mpaka Mwenyezi Mungu akamteremshia kauli yake: {Usiutikisie huu wahyi ulimi wako kwa kuufanyia haraka. Hakika ni juu yetu kuukusanya na kuusomesha. Tunapo usoma, basi nawe fuatiliza kusoma kwake. Kisha ni juu yetu kuubainisha} [AL QIYAMAH 61-19]
Hapo Mtume S.A.W, alikuwa mbora zaidi katika kuikusanya Qur`ani ndani ya moyo wake Mtukufu, na alikuwa marejeo kwa Waislamu katika kila jambo linalohusu Qur`ani Tukufu na Elimu za Qur`ani, na alikuwa akiwasomea Masahaba watukufu katika kipindi chote kama alivyoamrishwa na Mwenyezi Mungu, na alikuwa akiisherehekea usiku na kuipambia Swala.
Na Mwaminifu wa wahyi Jibril AS, alikuwa akimsomesha Mtume Qur`ani mara moja kila mwaka, na akamsomesha mara mbili ndani ya mwaka wa mwisho kabla ya kufariki kwake. Na Bibi Aisha RA, na Bibi Fatima A.S, wamesema: tumemsikia Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, akisema kuwa: “Jibril alikuwa akinisomesha Qur`ani mara moja kila mwaka, na akanisomesha mara mbili ndani ya mwaka huu, na sioni chochote isipokuwa wakati wangu (wa kuiaga Dunia) unakaribia kufika”.
Masahaba R.A, walishindana katika kuikariri Qur`ani Tukufu na kuhifadhi, na wakashindana katika kuisoma na kuifahamu, na wakahitilifiana baina yao kwa kiasi cha walichokihifadhi, mpaka ikawa yeyote anayepita katika nyumba za Masahaba - wakati wowote wa mchana au usiku - anasikia sauti inayofanana na ya nyuki ndani yake kutokana na kuisoma Qur`ani kwa wingi.
Na Mtume S.A.W, alikuwa akiwatakasa kwa uangalifu huo, na awajulishe yale yaliyoteremshwa kwake kutoka kwa Mola wake Mlezi, na akawatuma Yeye S.A.W, kwa watu wa nchi zilizo karibu naye ili wawasomee Qur`ani, pia yeye S.A.W, aliwatuma akina Musa’ab Ibn Umair na Ibn Umm Maktuum kwa watu wa Madina kabla ya yeye kuhamia huko, akiwafundisha Uislamu na kuwasomesha Qur`ani, na vilevile alimtuma Mua’adh Ibin Jabal Kuelekea Makkah baada ya kuhama kwake kuhifadhisha Qur`ani.
Ubada Ibn As-Samit R.A., amesema: “Wakati mtu anapohama, Mtume S.A.W, alikuwa akimpelekea mtu miongoni mwetu wa kumfundisha Qur`ani, na kulikuwa kukisikika kelele kwenye Msikiti wa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, kutokana na usomaji wa Qur`ani, mpaka Mtume S.A.W, akawaamrisha kupunguza sauti zao ili wasikoseshane”.
Hivyo, waliohifadhi Qur`ani Tukufu katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, walikuwa wengi, wakiwemo Makhalifa wanne, Tariq, Saad, Ibn Masuud, Hudhaifah, Salem Mawla Abu Hudhaifah, Abu Huraira, Ibn Umar, Ibn Abbas, Amr Ibn Al-A’as, mwanawe Abdullah, Mua’awiyah, Ibn Az-Zubair, Abdullah Ibn As-Saaib, Aisha, Hafsa, Umm Salamah na wote hawa Miongoni mwa Muhajirina. Na miongoni mwa Al-Ansaar walikuwa ni: Abay Ibn Kaab, Mua’adh Ibn Jabal, Zaid Ibn Thabit, Abu Ad-Dardaa, Majma’ Ibin Harithah, Anas Ibn Malik, na Abu Zaid, Mungu awe radhi nao wote. Na hao walikuwa wakifikisha imehifadhiwa kwa waliowafuata.
Hizi ni zama za Masahaba, na zama za Taabiin hazikuwa chini ya hapo kuhusu kuhifadhi Qur`ani Tukufu, na kutoka kwa Masahaba, Qur`ani ilihifadhiwa kwa maelfu ya Taabiin. Na kuendelea, Qur`ani Tukufu ikapokelewa na tabaka kwa tabaka kwa kuihifadhi, kuitunza na kuiangalia mpaka Qur`ani Tukufu ikatufikia bila ya kuongezwa wala kufutwa, au kupotoshwa au kubadilishwa, na ilikuwa ni uthibitisho wa kauli yake Mola Mtukufu: {Hakika Sisi ndio tulio teremsha Ukumbusho huu, na hakika Sisi ndio tutakao ulinda}.
Ndiyo hiki ni kitabu cha Ghayat An-Nihayah na Ibn Al-Jazariy, ndani yake wasifu wa wasomaji umefikia karibu watu elfu nne, Ikiwa hii ni idadi ya wasomaji waliosomesha, kama hivyo ndivyo ilivyo, inakuwaje idadi ya wanafunzi waliohifadhi.
Zaidi ya hayo, kutegemea katika upokeaji wa Qur`ani ni kuhifadhi nyoyoni na vifuani, na sio kuandika kwa mkono katika misahafu na maandiko, na hii ndiyo sifa mahsusi ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa umma huu.
Katika Hadithi Sahihi ni kuwa; Mtume S.A.W amesema: “Mola wangu mlezi ameniambia: Simama katika Makoreshi, uwaonye. Nikamwambia: Mola wangu mlezi basi watakipasua kichwa changu mpaka kiwe kama mkate, akaseama: Hakika Mimi nitakutahini na kukujaalia mtihani kwa wengine, na kukiteremsha kwako kitabu kisichoweza kuoshwa kwa maji, unaweza kukisoma wakati wa kulala na wa kuwa macho, basi tuma majeshi, nitatuma mfano wake, na pigana pamoja na wale waliokufuata dhidi ya wale waliokuasi, na tumia mali kwao. Hapo Mwenyezi Mungu akasema kuwa: Qur`ani haihitaji sahifa isiyoweza kuoshwa kwa maji, bali inasomwa kila wakati. Hivyo hivyo ilitajwa katika sifa ya umma wake S.A.W, kuwa: “Injili zao ni ndani vifuani mwao”.
Mwenye kuzingatia zama na hali za watu ataona kuwa kuhesabu idadi nyingi zinazoifikisha Qur`ani Tukufu haiwezekani, na atapata usahihi, ukamilifu na upana wa elimu kuwa ni jambo madhubuti ambalo ni ushahidi tosha kuhusu ukamilifu wa kitabu cha Mwenyezi Mungu na usahihi wake. Zaidi ya hayo atakuta idadi zaidi na zaidi kuliko wanavyotaka kwa ajili ya ukamilifu. Huyu ni Abud-Dardaa RA, alikuwa na wasomaji ambao idadi yao ni zaidi ya elfu moja na mia sita, na kila kundi moja la wasomaji lilikuwa na mwenye kuwasomesha, na Abud Dardaa alikuwa msimamizi wao, na mmoja wao alipokamilisha usomaji basi alielekea kwa Abud-Dardaa R.A.
Pili: Kukusanya Qur`ani kimaandishi katika zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W:
Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, aliwachagua Waandishi wa Wahyi. Kila kilipoteremshwa kitu katika Qur`ani, aliwaamrisha wakiandike, akitia maboresho katika usajili na uandikaji wake, na ziada katika hati na udhibiti na tahadhari katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu; mpaka kuandika huko kukasaidia kuhifadhi Qur`ani.
Waandishi hawa walikuwa miongoni mwa Masahaba bora; miongoni mwao ni Abu Bakr, Umar, Uthman, Muawiyah, Abban Ibn Said, Khalid Ibn Al-Waliid, Ubay Ibn Kaab, Zaid Ibn Thabit, Thabit Ibn Qais, Abu Ayyub Al-Ansariy, Said Ibn Al-A’as, Said Ibn Said Ibn Al-A’as, na Saad Ibn Abi Waqqas.
Profesa wetu Dkt. Abdul-Hay Al-Farmawiy amewahesabu miongoni mwao katika kitabu chake waandishi arobaini na sita, na hakutaka kuwahesabu wote, na wote walikuwa wakimwandikia Mtume S.A.W, Qur`ani. Lakini baadhi yao walibobea katika mambo mengine, kama vile kuandika mali za sadaka, kuandika mali za ngawira, kuandika ahadi na mapatano, kuandika barua na mengineyo. Na baadhi yao walikuwa wakiandika Qur`ani Tukufu zaidi kuliko ya wengine.
Dkt. Muhammad Mustafa Al-A’dhamiy ametaja katika kitabu chake (Waandishi wa Mtume S.A.W) Masahaba sitini na mmoja walioandika wahyi na mengineyo mbele yake S.A.W, na ishirini miongoni mwao walikuwa ni Masahaba waliomwandikia huko Makkah kabla ya kuhama. Na baada ya Dola la Waislamu kutulia huko Madinah, Mtume S.A.W., alichagua Waandishi maalumu kwa ajili ya kuiandika Qur`ani, kuziandika na kuzipanga Aya zake na Sura zake, hasa kwa vile Sura themanini na sita ziliteremshwa huko Makkah, kati ya zile mia moja kumi na nne, ambayo ni idadi ya Sura zote za Qur`ani Tukufu.
Ilikuwa ni mazoeo ya Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, baada ya kuteremka Aya ya Qur`ani Tukufu, kumwita mwandishi miongoni mwa Waandishi na kusema: “Ziwekeni Aya hizi katika sura ambayo imetajwa hivi na vile”.
Bali hakuna Aya yoyote iliyoteremshwa isipokuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W., alimuamrisha yeyote miongoni mwa waandishi wake aiweke mahali fulani katika sura fulani na fulani, na kuitaja kwa kuisoma yeye mwenyewe.
Al-Bukhari, Muslim, na wengineo wamepokea kutoka katika Hadithi ya Al-Baraa Ibn A’azib RA, akisema: Nilikuwa na Mtume S.A.W, wakati ilipoteremshwa: “Hawawi sawa Waumini wanaokaa tu”, na Mtume S.A.W, akasema: “Niitieni Zaid aje, au alete bega na wino au ubao na wino.” Basi akamjia na wino na ubao au bega, na Mtume S.A.W, akasema: “Andika: {Hawawi sawa Waumini wanao kaa tu, na wale wanao pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu}”, Na nyuma ya Mtume S.A.W, yuko Ibn Umm Maktuum aliyesema: “Ewe Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, mimi ni kipofu, hapo imeteremshwa mahali pake : {Hawawi sawa Waumini wanao kaa tu wala hawanadharura, na wale wanao pigana katika Njia ya Mwenyezi Mungu}.
Na walikuwa wakiandika Aya juu matawi ya mitende, ubao wa mawe, karatasi, ngozi za wanyama, mifupa ya mabega na mbavu, kisha maandishi yanawekwa ndani ya nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.
Ni muhimu kwamba Aya moja au Aya nyingi, ikibidi, ziandikwe upya mara moja au zaidi, kama vile kuandika upya ili kupanga Aya hii au Aya hizi katika Sura yake, na kuongeza sehemu kutoka katika sehemu zote za Qur`ani, ilipoteremshwa, ili kushikamana nazo.
Al-Hakim amepokea kwa Isnadi yake kutoka kwa Zaid Ibn Thabit, amesema: Tulikuwa na Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW, tukiiandika Qur`ani kwenye karatasi za ngozi. Hadithi.
Al-Bayhaqi amesema, “Ni sawa na ukweli kwamba kinachokusudiwa humo ni mkusanyiko wa Aya zilizotawanyika Sura zake na kuzikusanya humo kwa ishara kutoka kwa Mtume S.A.W.
Masahaba walikuwa wakimuandikia Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, na wao wenyewe Qur`ani Tukufu mbele yake S.A.W, na Yeye S.A.W, alikuwa akionesha mahali palipoandikwa katika Sura yake.
Haiwezekani kuwepo kosa katika Qur`ani kwa maandishi, na hali Mtume S.A.W, ndiye aliyeteremshiwa Wahyi, na Mwenyezi Mungu Mtukufu anamsimamishia hoja yake, anahifadhi Mawaidha, na yaliyoandikwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, anawatamkia yeye mwenyewe, na Masahaba wakayakagua, wakayaandika na wakayasoma.
Tatu: Ukusanyaji wa Qur`ani katika Msahafu mmoja katika zama za Abu Bakr RA:
Kama ulivyoona hapo juu, jambo hili liliishia zama za Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, kuikusanya Qu`rani vifuani ambayo ndiyo njia yenye kutegemewa, na pia kuikusanya katika maandiko ambayo ni nyaraka za ziada.
Ukhalifa Ulioongoka ulikuja kuwa Ukhalifa wa Abu Bakr R.A, wa kwanza katika Makhalifa Waongofu. Wakati wa utawala wake, vita vya Al-Yamamah vilitokea katika mwaka wa kumi na mbili wa Hijrah, ambapo Masahaba wengi, Wasomaji na waliohifadhi Qur`ani waliuawa vitani mashahidi. Basi ikawaje kuhusu jambo hili kwa Waislamu, hasa Umar Ibn Al-Khattab R.A, huyu mwenye ilhamu na mwenye kujaaliwa ufahamu wa aina yake, naye alitoa pendekezo kwa Abu Bakr RA, la kukusanya Qu`rani Tukufu katika Msahafu mmoja; ili iwe Maandiko yaliyo sambamba na ile iliyohifadhiwa vifuani. Na Abu Bakr alilikubali pendekezo hilo baada ya kuridhika kwamba “kuiandika Qur`ani si jambo la uzushi, kwani Yeye S.A.W, alikuwa akiamuru iandikwe, lakini iligawanywa katika karatasi, mabega na matawi ya mitende.
As-Siddiq aliamrisha zinakiliwe kutoka sehemu moja hadi nyingine kwa pamoja, na hiyo ilikuwa ni kama karatasi zilizopatikana katika nyumba ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, ambamo Qur`ani ilisambazwa. Basi akakusanya pamoja na kufungwa kwa uzi ili kitu chochote kisipotee”.
Sahifa hizi za Abu Bakr hazikuandikwa isipokuwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.
Kwa hiyo Abu Bakr aliamwamuru Zaid bin Thabit R.A, aliyekuwa aliyeihifadhi Qur`ani, na mwandishi wa Wahyi, na kushuhudia usomaji wa mwisho wa Qur`ani mwishoni mwa maisha yake S.A.W.
Imamu Bukhari amepokea katika Sahihi yake kwamba Zayd ibn Thabit R.A, amesema: Abu Bakr alinitumia habari ya kuuawa kwa watu wa Al-Yamamah, na Umar Ibn Al-Khattab RA, alikuwa pamoja naye. Abu Bakr R.A., akasema: “Umar alinijia na kusema kuwa: mauaji yalizidi sana Siku ya Vita vya Al-Yamamah kwa wasomaji wa Qur`ani, na ninachelea kuwa mauaji yakazidi kwa wasomaji kutokana na vita hivi, ambapo vinasababisha kupotea kwa sehemu kubwa ya Qur`ani. Kwa hiyo ninaona ni bora utoe amri ya kuikusanya Qur`ani...”. Hadi mwisho wa Hadithi.
Zaid hakutosheka na ile Qur`ani aliyoihifadhi yeye mwenyewe na Masahaba wengine, bali alijilazimisha jukumu la kutoandika chochote alichokihifadhi na kile kilichohifadhiwa na maswahaba wengine isipokuwa kwa kutimiza masharti mawili yafuatayo:
Kwanza: Baada ya mmiliki wake kuileta Qur`ani kwa maandishi kwamba imeandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, na mashahidi wawili wanashuhudia kwamba imeandikwa mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu SAW.
Pili: Iwe Qur`ani hiyo imehifadhiwa katika vifua vya watu.
Haya yanathibitishwa na yale yaliyopokelewa na Ibn Abi Dawuud kwa njia ya Yahya Ibn Abdir-Rahman Ibn Hatib, amesema: “Umar alikuja na kusema, yeyote aliyepokea kitu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W., akilete, na walikuwa wakiyaandika hayo kwenye sahifa, ubao, na matawi ya mitende. Na haikubaliki kitu kutoka kwa yeyote mpaka mashahidi wawili wawe wanashuhudia”.
Vile vile ushahidi wa yale aliyoyapokea Abu Dawud pia kwa njia ya Hisham Ibn Urwah, kutoka kwa baba yake kuwa: Abu Bakr R.A, aliwaambia Umar na Zaid: “Ketini mlangoni mwa Msikiti, na yeyote yule aliyeleta mashahidi wawili kwa kitu chochote kutoka katika Kitabu cha Mwenyezi Mungu, basi kiandikeni".
Na Sahifa hizi zilijumuisha Visomo ambavyo viliunganishwa katika yale waliyoyaandika Masahaba, na visomo hivi vimethibitishwa katika Sahifa za Kisiddiqiyah, na Sahifa za Kisiddiqi pamoja na maandishi mengine zimebaki kuhifadhiwa na wamiliki wake, nazo ni vitu vinavyopendwa zaidi kwao kwa sababu vimeandikwa mbele ya Mtume S.A.W, na hizi zilikaa mpaka Misahafu iliyoandikwa kwa hati ya Kiuthmani ikanukuliwa kutoka kwake.
Sahifa hizi ambazo ndani yake Qur`ani Tukufu yote iliandikwa zilihifadhiwa na Abu Bakr, kisha zikapitishwa kwa Umar wakati wa Ukhalifa wake, kisha kwa Bibi Hafsa, Mama wa Waumini baada ya kifo cha baba yake Umar R.A, kisha Uthman R.A, akaziomba kutoka kwake wakati wa Ukhalifa wake, ambapo alizitegemea katika uandishi wa Misahafu, kama itakavyokuja kuelezwa baadae.
Nne: Misahafu ya kiuthmani:
Mzozo ulizuka ambao ulipelekea Qur`ani iandikwe, ikanukuliwa kutoka kwa Sahifa za Kisiddiqiya, na wao walichukua maandishi yaliyokuwa ya Masahaba, na haya yaliyoandikwa mbele ya Mtume S.A.W.
Masahaba wakuu wanne walihudhuria kwa ajili ya ujumbe huu, ambao ni: Zaid Ibn Thabit, Mwandishi wa Sahifa za Kisiddiqiya , Abdullahi ibn Az-Zubair, Said Ibn Al-A’as, na Abdur-Rahman Ibn Al-Harith Ibn Hisham.
Na ikaja katika baadhi ya mapokezi kwamba waliopewa amri ya kunakili Misahafu walikuwa watu kumi na wawili, na hawakuandika chochote isipokuwa baada ya kuwasilishwa kwa Masahaba, na hao wakakiri kuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, alikuwa akiisoma Qur`ani namna hii ambayo tunaipata sasa hivi katika Misahafu.
Misahafu ya Uthmani inafanana sana na Misahafu ya Abu bakr, na hilo lilithibitishwa na Bukhari, Abu Dawuud, na Noeldeke katika kitabu chake (Historia ya Qur`ani).
Misahafu hii iliandikwa kama Sahifa za Abu Bakr zilivyoandikwa, ikikusanya Herufi Saba na Visomo Sahihi vya Qur`ani. Neno ambalo lina tofauti za Visomo hivi hutofautiana ndani yake, kama haliwezi kuandikwa katika hati inayowezekana kwa tofauti zote hizi, basi wanaliandika kwa hati inayolingana na baadhi ya tofauti ndani ya Msahafu Mmoja, kisha wanaliandika kwa hati nyingine inayolingana na baadhi ya tofauti nyingine ndani ya Msahafu mwingine.
Ama neno ambalo Visomo vinatafautiana nalo na linaoneshwa kwa njia moja ya kuandika, na sura moja inayobeba tofauti hii, basi wanaliandika kama lilivyo.
Na kinachowasaidia hivyo ni kutoweka nukta na alama za Irabu katika kuandika Misahafu ya zamani, kwa mfano: (Fatabayyanu) inaweza kusomwa (Fatathabbatu), na (Nanshuruha) inaweza kusomwa (Nunshizuha), na kwa mfano pia: (Tajry Tahtahal Anhaar) , katika Misahafu mingine: (Tajry Min tahtihal Anhaar), kwa kuongeza ( Min).
Kwa hivyo, tunakuta kwamba Visomo na Herufi Saba zilikuwa zikiandikwa kwa amri ya Mtume S.A.W, zikiwa zimegawiwa vipande vipande au kuambatanishwa kwa vingine, kama alivyoambatanisha Zaidi: {wala hawanadharura}. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Masahaba, na Abu Bakr akaziweka kwenye Sahifa alizozikusanya, kisha Uthman akazisambaza kwenye Misahafu, na hakuziambatanisha na Msahafu Mmoja; Kwa sababu alitaka kupunguza tofauti hizi katika sehemu nyingi ili kuepusha mizozo, na hakutaka kuzifuta, basi akazigawanya katika Misahafu.
Na Misahafu ya Kiuthmani ilikuwa mingi; Ili kukusanya Visomo, husambazwa kama tulivyotaja, na kupelekwa mijini, kila mji usome Msahafu wake kwa kuafikiana nao na kukubaliana nao, na kila Msahafu ulikuwa na Mwongozi, kwa sababu uandishi peke yake haukidhi vipengele vyote vya Visomo, na haudhibiti hukumu za usomaji, kama vile: Ishmam, Ikhtilaas, na daraja zote za Fatha.Kasra Alifu na nyinginezo.
Miongoni mwao ulikuwa ni Msahafu aliouweka Khalifa huko Madina na uliitwa: Msahafu wa Imamu, Na Msahafu wa Madina ndio uliwekwa kwa ajili ya watu, na Khalifa akaamrisha Zayd kusomesha kwa mujibu wake; na Msahafu wa Makka alimtuma Abdullah Ibn As-Saib kuusomesha, na Mushaf wa Kufa pamoja na Abu Abdir-Rahman As-Sulami, na Msahafu wa Basra pamoja na Aamir Ibn Qais, na Msahafu wa Sham Mwongozi wake Al-Mughirah Ibn Shihab.
Na anayetaka ziada, basi asome yale aliyoyaandika marehemu Profesa wetu, Prof. Dr. Abdel Ghafuur Mahmuud Mustafa katika kitabu chake kilichotajwa.
Tano: Kukusanywa kwa Qur`ani kwa mpangilio wa Sura na Aya mbele ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W:
Nitataja hapa dalili zaidi za kuthibitisha kwamba Qur`ani Tukufu ilizipanga Sura na Aya kwa wahyi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kwa idhini ya Mtume S.A.W, kama ilivyo katika Msahafu uliopo leo katika mikono ya watu.
Imam As-Sayuti, Mwenyezi Mungu amrehemu, anasema: “Na kinachoashiria kuwa ni idhini ya Mtume S.A.W, kuwa: Sura za Hawamim zimepangiliwa kwa mfuatano, vile vile sura za At-Tawasiin, lakini sura za Al-Musabbihaat hazikupangiliwa kwa mfuatano bali zimegawanywa kati ya Sura zake, kwa Sura za Ta Sin Mim Al-qasas zimegawanywa kati yake kwa Ta Sin, ingawa Sura hizi ni fupi kuliko zile za mwanzo, na lau mpangilio ungekuwa kijitihada basi Sura za Al-Musabbihaat zingetajwa kwa mfuatano, na Sura za Ta Sin zingeahirishwa na Al-Qasas”.
Na unaona kuwa: Msahafu uko mbele yetu unazipangilia Sura za: Yunus, Huud, na Yusuf kwa mpangilio wa nambari: 10-11-12, na hakika zimeteremshwa kwa mpangilio wa: 51-52-53. Vile vile Sura za: As-Shu’araa, An-Naml, na Al-Qasas mpangilio wake wa kuteremshwa ni: 47-48-49, na mpangilio wake katika msahafu ni: 26-27-28.
Na Sura za: Az-Zumar, Ghafir, Fussilat, As-Shuraa, Az-Zukhruf, Ad-Dukhan, Al-Jathiyah, Al-Ahqaaf zimeteremshwa kiufuatano, kwa nambari za: 61-60-59-62-64-63-65-66, na nambari zake katika mpangilio wa Msahafu ni: 39-40-41-42-43-44-45-46. Na Sura mbili za: Adh-Dhuhaa, Ash-Sharh zimeteremshwa kiufuatano: 11-12, kama vile nambari zake katika msahafu ni: 93-94. Vile vile sura za: Al-Falaq, na An-Nas.
Hili pia linathibitisha kuambatana kati ya maneno na kulingana kati ya maana, na uwiano kati ya Sura zilizo karibu katika Msahafu, na zile zinazotofautiana katika mpangilio wa Kuteremshwa. Chukua kwa mfano Surat Qaaf, mpangilio wake katika Msahafu ni 50 na katika kuteremshwa ni 34, na ndani yake kuna hadithi kuhusu kukanusha washirikina kwa ufufuo: {Ati tukifa na tukawa udongo? Kurejea huko huko mbali!} [QAAF 3] Na maelezo kwa baadhi ya matukio ya Siku ya Kiyama, na malipo ya kila mmoja kutoka katika aya 19-35, na hitimisho la hayo ni kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na sikiliza siku atapo nadi mwenye kunadi kutoka pahala pa karibu. Siku watakapo sikia ukelele wa haki. Hiyo ndiyo siku ya kufufuka. Hakika Sisi tunahuisha na tunafisha, na kwetu Sisi ndio marejeo. Siku itapo wapasukia ardhi mbio mbio! Mkusanyo huo kwetu ni mwepesi}. [QAAF 41-44]
Kwa kuongeza yale yaliyotajwa katika mafungu ya sura kuhusu udhihirishaji wa uwezo wa Mwenyezi Mungu aliye juu mbinguni na ardhini, na yale ambayo Mwenyezi Mungu ameyajaalia kuwa riziki kwa njia na sababu za maisha ya viumbe vyake, na kukadhibisha baadhi ya mataifa, na walivyopata na vitisho, na hayo yamo katika Aya za 6-14.
Kisha ikaja Surat Adh-Dhaariyaat, nayo ikaliapia hilo na kulithibitisha: {Hakika mnayo ahidiwa bila ya shaka ni kweli. Na kwa hakika malipo bila shaka yatatokea. Naapa kwa mbingu zenye njia. Hakika nyinyi bila ya shaka mmo katika kauli inayo khitilafiana. Anageuzwa kutokana na haki mwenye kugeuzwa. Wazushi wameangamizwa. Ambao wameghafilika katika ujinga. Wanauliza: Ni lini hiyo siku ya malipo? Hiyo ni siku watakayo adhibiwa Motoni. Onjeni adhabu yenu! Haya ndiyo mliyo kuwa mkiyahimiza}.[AD DHARIYAAT 5-14]
Kisha inamaliza kwa kitisho hili: {Hakika walio dhulumu wana fungu lao la adhabu kama fungu la wenzao. Basi wasinihimize. Ole wao walio ikanusha siku yao waliyo ahidiwa}. [AD DHARIYAAT 59-60]
Vile vile imetaja kwa ufupi katika mafungu yake adhabu ya wale wanaowakadhibisha Mitume wao miongoni mwa mataifa, vile vile imebainisha kuwa yale yaliyotajwa katika udhihirishaji wa uwezo wa Mwenyezi Mungu mbinguni na ardhini, na ishara na maajabu yanayotangazwa katika ulimwengu, ni kwa uumbaji wa Mwenyeezi Mungu na kipimo kitokacho kwake. Licha ya utangamano huu na mshikamano, Surat Adh-Dhaariyaat iliteremka baada ya Surat Qaaf kwa idadi ya Sura thelathini na tatu. Ametakasika aliyedhibiti zaidi kauli hii na akaiteremsha.
Kisha inakuja Surat At-Tuur, ikafuata njia hiyo hiyo, ikatoa lawama kali kwa wakanushaji, na kauli inayowasumbua, kutia sana vitisho na maonyo, na kwamba wataishukia adhabu chungu katika dunia na wakaipata katika Akhera: {Hakika adhabu ya Mola wako Mlezi hapana shaka itatokea. Hapana wa kuizuia.
Siku zitakapo tikisika mbingu kwa mtikiso. Na milima iwe inakwenda kwa mwendo mkubwa. Basi ole wao siku hiyo hao wanao kadhibisha}. [AT TWOR 7-11]
Na kauli yake Mwenyezi Mungu: {Basi waache mpaka wakutane na siku yao watakapo hilikishwa. Siku ambayo hila zao hazitawafaa hata kidogo, wala wao hawatanusuriwa. Na hakika walio dhulumu watapata adhabu nyingine isiyo kuwa hii, lakini wengi wao hawajui}.
Ni yale yale ambayo Surat Adh-Dhaariyaat ilihitimishwa, iliyo kabla yake kwa mpangilio wa Msahafu, na Surat At-Tuur ilicheleweshwa kutoka kwayo katika kuteremka kwa idadi ya Sura tisa. Kwa kuongeza mfanano uliopo baina ya Sura mbili katika ukumbusho wa Siku ya Kiyama na mazungumzo kuhusu watu wa Motoni na watu wa Peponi.
Kisha tazama kuambatana na matamshi, na kuuwiana na maana, baina ya mwisho wa Surat At-Tuur na mwanzo wa Surat An-Najm katika mazungumzo juu ya Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, ingawa umbali uliopo baina ya Sura mbili kuhusu kuteremka, ambapo Surat At-Tuur iliteremka baada ya Surat An-Najm kwa idadi ya Sura hamsini na tatu.
Mwenyezi Mungu alisema katika mwisho wa Surat At-Tuur: {Na ingojee hukumu ya Mola wako Mlezi, kwani wewe hakika uko mbele ya macho yetu, na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi unapo simama. Na usiku pia mtakase, na zinapo kuchwa nyota}. [AT TWUR 48-49]
Kisha Surat An-Najm ilifunguliwa kwa kauli yake mwenyezi Mungu: {Naapa kwa nyota inapo tua. Mwenzenu huyu hakupotea wala hakukosea. Wala hatamki kwa matamanio. Hayakuwa haya ila ni ufunuo ulio funuliwa. Amemfundisha aliye mwingi wa nguvu. Mwenye kutua, akatulia. Naye yuko juu kabisa upeo wa macho. Kisha akakaribia na akateremka. Akawa ni kama baina ya mipinde miwili, au karibu zaidi. Akamfunulia mja wake (Mwenyezi Mungu) alicho mfunulia. Moyo haukusema uwongo uliyo yaona. Je! Mnabishana naye kwa aliyo yaona? Na akamwona mara yingine. Penye Mkunazi wa mwisho. Karibu yake ndiyo ipo Bustani inayo kaliwa. Kilipo ufunika huo Mkunazi hicho kilicho ufunuika. Jicho halikuhangaika wala halikuruka mpaka. Kwa yakini aliona katika Ishara kubwa kabisa za Mola wake Mlezi}. [AN NAJM 1-18]
Vilevile uhusiano uliopo baina ya Surat An-Najm na Surat Al-Qamar uliocheleweshwa katika kuteremshwa kwa idadi ya Sura kumi na nne, ambapo Surat Al-Qamar ilieleza hali za wakanushaji wa Mitume wao, na kuwaweka sawa kulingana na kuwepo kwao. Kwa sababu Surat An-Najm iliwataja kwa ujumla, bila utaratibu, katika kauli yake Mwenyezi Mungu: {Au hakuambiwa yaliyomo katika Vitabu vya Musa?}, [AN NAJM 36]
na kauli yake Mwenyezi Mungu: {Na kwamba Yeye ndiye aliye waangamiza A'di wa kwanza. Na Thamudi hakuwabakisha. Na kabla yao kaumu ya Nuhu, na hao hakika walikuwa ni madhaalimu zaidi, na waovu zaidi. Na miji iliyo pinduliwa, ni Yeye aliye ipindua. Vikaifunika vilivyo funika}. [AN NAJM 50-54]
Kisha utangamano baina ya kauli yake Mwenyezi Mungu: {Kiyama kimekaribia!}, [AN NAJM 57]
na kauli yake: {Saa imekaribia, na mwezi umepasuka!} [AL QAMAR 1]
Na maelezo ya hali za mataifa yaliyotangulia ndani yake katika Aya 9-43, kisha mwisho wake unaafikiana na mwanzo wa Surat Ar-Rahman iliyocheleweshwa nayo kwa idadi ya Sura sitini katika kuteremshwa, na mwishoni mwa Surat Al- Qamar:
{Hakika wachamngu watakuwa katika Mabustani na mito. Katika makalio ya haki kwa Mfalme Mwenye uweza}. [AL QAMAR 54-55]
Kisha ikaja Sura iliyofuata, na ikaonesha kwamba Mfalme Mwenye uweza ni: (Ar-Rahman) ambaye: “alifundisha Qur`ani” kama alivyoifanya kuwa nyepesi, kabla ya hapo, katika Surat Al-Qamar.
Hivyo basi, mwenye kuiangalia Qur`ani, mwenye kuzingatia maneno na maana zake, mwenye kutafakari mifumo na miundo yake, atapata zaidi ya ushahidi kwamba mpangilio huu wa Sura za Qur`ani unatokana na idhini ya Mtume S.A.W, kutoka kwa Jibril A.S, na hakuna yeyote mwenye rai wala jitihada.
Na huu ni mfano mmoja, na sitaki kurefusha kwa kutaja mifano mingine, basi na airejelee anayetaka kufanya hivyo. Na katika Sunna ya Mtume S.A.W, kuna mifano mingi, na Al-Qurtubiy, Mwenyezi Mungu amrehemu, alinikulu mapokezi kutoka kwa Ibn Abbas R.A, na ndani yake ni: “Mwisho wa kuteremshwa kutoka Qur`ani: {Na iogopeni Siku ambayo mtarudishwa kwa Mwenyezi Mungu, kisha kila nafsi italipwa ilicho chuma. Nao hawatadhulumiwa}. , na Jibril akamwambia Mtume: Ewe Muhammad iweke mwishoni mwa Aya mia mbili na themanini kutoka kwa Al-Baqarah”.
Na wewe ukiurejea Msahafu utaikuta Aya hii ya 281, basi kuna dalili gani baada ya hii.
Imaam Ahmad amepokea kutoka kwa Hadithi ya Uthman Ibn Abi Al-A’as amesema: “Nilikuwa nimekaa na Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, alipotazama, akalenga kwa macho yake, mpaka akakaribia ardhini, kisha akatazama tena, akisema: Jibril, amani iwe juu yake, amenijia, na akaniamrisha niiweke Aya hii mahali hapa pa Sura hii: {Hakika Mwenyezi Mungu anaamrisha kufanya uadilifu, na hisani, na kuwapa jamaa; na anakataza uchafu, na uovu, na dhulma. Anakuwaidhini ili mpate kukumbuka}.
Na katika Al-Musnad na As-Sunan na mengineyo, na At-Tirmidhiy ameifanya iwe na Hukumu ya Hasan, na Al-Hakim ameifanya Sahihi, kutoka kwa Hadith ya Uthman Ibn A’affan RA, amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, kila wakati, alikuwa akiteremshiwa Sura nyingi, na alipoteremshiwa kitu chochote aliwaita baadhi ya Maswahaba waliokuwa wakimwandika Qur`ani, na kusema: “kiwekeni kitu hiki katika Sura inayotajwa ndani yake hivi na hivi”, na alipoteremshiwa Aya nyingi, alisema: “Ziwekeni Aya hizi katika sura inayotajwa ndani yake hivi na hivi”, na alipoteremshiwa Aya moja, alisema: “iwekeni Aya hii katika Sura ambayo inatajwa ndani yake hivi na hivi”.
Na katika Al-musnad, na As-Sunan, kutoka kwa njia ya Abdullahi Ibn Abdur-Rahman Ibn Ya’laa, kutoka kwa Uthman Ibn Abdullahi Ibn Aws, kutoka kwa babu yake: Aws Ibn Aws, naye ni: Aws Ibn Hudhaifa Ath-Thaqafiy, alisema:
Tulikuja kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, pamoja na wajumbe wa Thaqif, basi washirika walishuka na Al-Mughirah bin Shu’bah, na Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, aliwashikisha Bani Malik katika kuba lake. Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W, alikuwa akitujia kila usiku baada ya chakula cha jioni, na alikuwa akizungumza nasi akiwa amesimama kwa miguu yake, mpaka akategemea mguu huu mara moja na mguu ule mara nyingine kwa sababu ya urefu wa muda wa kusimama, na mengi ya yale anayotuambia ni yale yaliyomkuta yeye na watu wake kutoka kwa Maquraishi, na akasema: “ Hakuna usawa, tulikuwa wanyonge, tulidhalilishwa huko Makkah, na tulipokwenda Madinah vita kati yetu vilikuwa tofauti; (Sisi tunashinda mara, na wao wanshinda mara nyingine).
Usiku mmoja alichelewa kuliko muda aliokuwa akitujia. Basi tukasema: umetuchelewesha usiku huu. Akasema: “Imetokea sehemu yangu ya Qur`ani, nikachukia kutoka mpaka nikamaliza”.
Aus akasema: Niliwauliza Masahaba wa Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W: Vipi mnaigawanya Qur`ani (iwe Hizb)? Wakasema: Sura tatu, surah tano, surah saba, surah tisa, surah kumi na moja, surah kumi na tatu, na Hizb ya Al-Mufassal kutoka kwa Qaaf mpaka mwisho.
Imamu Ahmad na Abu dawuud At-tayalisiy wamepokea kutoka kwa Wathilah Ibn Al-Asqaa’ R.A, alisema: Mtume S.A.W, alisema: “Nimepewa Assaba’ At-Tiwaal (Sura ndefu saba) mahali pa Tawrati, na Al-Miin (Sura zenye Aya mia) mahali pa Zaburi, na Al-Mathaniy (Sura zenye chini ya Aya mia) mahali pa Injili, na nimependelewa kwa Al-Mufassal”.
Hii inaashiria kuwa Qur`ani Tukufu yote ilikuwa ni mkusanyiko uliopangwa kwa mujibu wa sifa hii katika zama zake S.A.W, na Masahaba pia walikuwa wakiihifadhi kwa utaratibu huu, na kuisoma katika Swala zao na katika nyakati zao zote, kila walipofika mwishoni mwake, walianza kuisoma kuanzia mwanzoni. Na mmoja wao anamuuliza Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W: Ni muda kiasi gani ninatakiwa kuisoma Qu`ani? Na Mtume S.A.W, anamjibu kila mmoja wao kwa kile anachokiona kinafaa zaidi kwa hali yake, na miongoni mwao walikuwa wakigawanya usomaji wao katika Sura nzima, na baadhi yao wakawa wanachagua baadhi ya sehemu zinazojulikana katika Msahafu, na kuzisoma.... Na kadhalika.

 

 

Share this:

Related Fatwas