Je! Mitume Walikuwa kwa Waisrael tu au Mwenyezi Mungu Alipeleka kwa Kila Umma?
Question
Je! Mitume Walikuwa kwa Waisrael tu au Mwenyezi Mungu Alipeleka kwa Kila Umma?
Answer
Asili ya shaka
Ndani ya Qur`ani imekuja: {Na kila umma una Mtume. Alipo wajia Mtume wao walihukumiwa baina yao kwa uadilifu, wala hawakudhulumiwa} [YUNUS: 47]. Na Qur`ani ikasema tena: {Na kwa hakika kwa kila umma tuliutumia Mtume kwamba: Muabuduni Mwenyezi Mungu, na muepukeni shetani. Basi kati yao wapo aliowaongoa Mwenyezi Mungu. Na kati yao wapo ambao uliowathibitikia upotovu. Basi tembeeni katika ardhi, muangalie ulikuwaje mwisho wa wanao kanusha} [AN-NAHL: 36].
Na Qur`ani ikasema pia: {Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika kila umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao. Na tumekuteremshia Kitabu hiki kinacho bainisha kila kitu, na ni uwongofu, na rehema, na bishara kwa Waislamu} [AN-NAHL: 89]. Qur`ani inasema kuwa Mwenyezi Mungu Ametuma katika kila umma Nabii anayetokana na umma huo na kuelekea kwa umma huo, na Kitabu Kitakatifu kinasema: Manabii na Mitume ni Waisrael na wamepelekwa kwao na kwa walimwengu wote, ikiwa tutakubaliana na kauli za Qur`ani basi ni vipi katika umma za Kiafrika Ulaya Marekani Australia na Asia hawakutoka Manabii kwao na kupelekwa kwao? Lau ikiwa kwa umma huu kuna Manabii wanaotokana na umma huu na kupelekwa kwenye umma huu basi ingefaa kwa Waarabu kuwa na Mtume kutoka kwao.
Kuondoa shaka: Kituo cha tafiti za Kisharia Ofisi ya Mufti wa Misri.
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Mwenyezi Mungu Alihukumu kwa umma kupeleka Mtume ili awe hoja kwao siku ya Kiyama, na neno Umma ndani ya Qur`ani linakuja na maana nyingi – kama ilivyotajwa na Wanachuoni – na kusudio katika Aya hizi: Ni kundi kubwa la watu wanaokutanishwa na jambo la dini au zama au sehemu moja, ni sawa sawa mkusanyiko huo wa hiyari au wa lazima, haufungamani na idadi maalumu au miaka maalumu kama vile Umma wa Aad ambao Mwenyezi Mungu Alimpeleka kwao Nabii wake Huud, na Umma wa Thamud ambao Mwenyezi Mungu alimpeleka kwao Nabii Saleh, na Umma wa Madian ambao Mwenyezi Mungu Alimpeleka kwao Nabii wake Shuaib, na Umma wa Mayahudi ambao Mwenyezi Mungu Alimpeleka kwao Nabii wake Musa Amani ya Mungu iwe kwake na kwa Manabii na Mitume wote.
Ama maelezo yao kuwa Kitabu Kitakatifu kinasema: Manabii na Mitume ni kutoka kwa Wana wa Israel tu na wamepelekwa kwao na kwa ulimwengu wote, maneno haya si sahihi yanapingwa na uhalisia, na yanapingwa pia na Kitabu Kitakatifu, kwa sababu lau Manabii watakuwa ni kutoka kwa Waisrael tu na wamepelekwa kwao na kwa ulimwengu, basi wapo wapi Manabii na Mitume wa ulimwengu kabla ya uwepo wa Wana wa Israel? Na vipi husemwa kwa walimwengu wengine na Nabii Isa A.S. anasema kama ilivyokuja kwenye Injili: “Akajibu akasema, Sikutumwa ila kwa kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli”. Mathayo 15: 24, wala hakusema kutumwa kwake ni kwa umma wote.
Ama hoja ya kusema mbona katika Umma wa Afrika Ulaya Marekani Australia na Asia hakutokea Nabii kwao na kupelekwa pia kwao, tunasema: Hizi ni nchi na wala sio umma, pamoja na hayo nchi hizi ni zenye kutakiwa kuamini Mtume, kwani Mwenyezi Mungu Amemtuma pia na kwao na amemfanya ndio Mtume wa mwisho mpaka siku ya Kiyama, naye ni Mtume wetu Muhammad S.A.W.
Ni jambo la kushangaza muulizaji kutoa ushahidi kwa kauli ya Mola Mtukufu: {Na (waonye) siku tutakapo wainua mashahidi katika kila umma wakiwashuhudia kwa yanayo tokana na wao, na tutakuleta wewe uwe shahidi juu ya hao} kuwa kusudio la Aya ni Umma duniani, usahihi ni kuwa Aya inazungumia kuhusu siku ya Akhera nayo ni ushahidi wa kila Nabii kwa Umma wake, na wala hakuna uhusiano wa kutumwa Mitume kwa watu, vile vile kuhusu ushahidi wa Nabii Muhammad S.A.W. kwa Umma wake na kwa Umma zengine.