Kununua gari kwa malipo ya awamu (mkopo) kutoka Benki
Question
Je, inajuzu kununua gari kwa malipo ya awamu, ikijulikana kuwa malipo hayo yanafanyika kupitia Benki?
Answer
Imethibitishwa kisharia kujuzu kuuza kwa malipo ya awamu mkabala wa nyongeza katika bei ya bidhaa; kwa sharti kwamba awamu hizo ziwe kwa muda maalumu na ulioainishwa. Muamala huu unaofanyika kwa kuridhiana kati ya muuzaji na mnunuzi unaitwa "Murabahah", na ni aina miongoni mwa aina za mauzo yanayojuzu kisharia. Hakuna ubaya pia kwa muamala huu kufanyika kati ya mtu (mnunuzi) na Benki (kama muuzaji wa bidhaa kwa awamu). Kununua kutoka benki kwa aina hii haihesabiki kuwa ni mkopo uliovuta manufaa, ikawa ni katika mlango wa riba iliyoharamishwa; kwa sababu kanuni ya kisharia imehukumu kwamba: "Bidhaa ikizunguka (ikiwa ndiyo kiungo), basi hakuna riba". Hivyo, mtu kununua gari kwa malipo ya awamu kutoka Benki mkabala wa nyongeza katika bei yake ni jambo linalojuzu kisharia na halina ubaya.
Maelezo
Imethibitishwa kisharia kujuzu kuuza na kununua, iwe thamani atakayolipa mnunuzi kwa muuzaji ni ya papo hapo kwa ukamilifu, au thamani atakayolipa mnunuzi kwa muuzaji ni ya baadaye kwa mfumo wa awamu maalumu kwa muda unaojulikana, na hiyo ikiwa ni mkabala wa nyongeza katika bei ya bidhaa, jambo ambalo linaitwa «Kuuza kwa awamu»; Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Lakini Mwenyezi Mungu ameihalalisha biashara na ameiharimisha riba.} [Al-Baqarah: 275].
Kuuza kwa awamu kunajuzu kisharia kwa mafakihi wote na hakuna ubaya ndani yake; ikiwa hilo ni kwa kuridhiana kati ya muuzaji na mnunuzi; ndio maana Sharia tukufu imelihalalisha kutokana na hitaji kubwa la watu kwalo, wawe ni wauzaji au wanunuzi.
Lakini kuna wanaosema: «Hakika kushirikiana na Benki katika kununua gari kwa awamu ni jambo la haramu kisharia»; kwa sababu benki humpa mnunuzi kiasi cha fedha ili anunue gari, kisha mteja (mnunuzi) hurudisha kiasi hicho kwa nyongeza kupitia awamu kadhaa, na hii ni aina ya riba aliyoiharamisha Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kanuni ya kisharia inasema: «Kila mkopo unaovuta manufaa basi huo ni riba».
kujibu rai hii tunasema: Hakika kununua gari na mengineyo kwa awamu kupitia Benki ni jambo linalojuzu kisharia na halina ubaya, na hiyo ni kwa sababu zifuatazo:
Malipo ya awamu kupitia Benki hufanyika kupitia mikataba miwili:
Wa kwanza: Mkataba kati ya benki na muuzaji anayemiliki bidhaa; ambapo benki hununua gari lile analolitaka mnunuzi kutoka kwa muuzaji.
Wa pili: Mkataba kati ya benki na mnunuzi; ambapo Benki humuuzia mnunuzi gari lile kwa bei ya juu mkabala wa kulipa thamani yake kwa awamu kwa muda maalumu. Aina hii inayoundwa na mikataba miwili inaitwa kwa mafakihi wa sasa "Murabahah"[1], na ni miongoni mwa miamala inayojuzu kisheria.
Muamala huo hauhesabiki kuwa ni miongoni mwa riba iliyoharamishwa; kwa sababu kanuni ya kisharia imepitisha kwamba «Bidhaa ikizunguka, basi hakuna riba», na gari limekuwa kiungo katika muamala kati ya Benki na mnunuzi; hivyo ni muamala sahihi kisharia, na haipasi wakati huo kuuita muamala huo kuwa ni mkopo wa gari kutoka Benki.
Aina ya riba iliyoharamishwa ni mteja kuchukua fedha kutoka Benki ili azirudishe kwa nyongeza ya kile alichochukua, na aina hii ni haramu; kwa sababu inaingia chini ya kanuni «Kila mkopo unaovuta manufaa basi huo ni riba», na jambo hili halipo katika muamala huu.
Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:
Baada ya ufafanuzi huu; rai sahihi zaidi na ambayo imetolewa Fatwa na Ofisi ya Mufti wa Misri ni kama ifuatavyo:
Kujuzu kwa kuuza kwa bei ya papo hapo, au ya baadaye kwa awamu pamoja na nyongeza ya bei kwa kuridhiana kati ya muuzaji na mnunuzi, kwa ajili ya hitaji la watu kwa jambo hilo.
Kununua gari kupitia Benki ni jambo linalojuzu kisharia na halina ubaya, kwani ni katika aina ya Murabahah inayojuzu, na kanuni ya kisharia zimepitisha: «Kwamba bidhaa ikizunguka, basi hakuna riba».
Riba iliyoharamishwa ni mtu kuchukua kiasi cha fedha kisha akakirudisha kwa nyongeza; kwa sababu inaingia wakati huo chini ya kanuni «Kila mkopo unaovuta manufaa basi huo ni riba». Na sura hii haipo katika ununuzi kutoka Benki kwa awamu.
[1] "Bay'ul-Murabahah"; maana yake ni kuuza bidhaa kwa ongezeko la bei zaidi ya bei yake ya kwanza.
Arabic
Englsh
French
Deutsch
Urdu
Pashto
Hausa
