Hukumu ya kuainisha kiwango maalumu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kuainisha kiwango maalumu cha faida katika Biashara

Question

Je, Uislamu umeweka ukomo maalumu wa faida katika biashara? Na ni ipi hukumu ya kupandisha bei kwa watu na kutumia vibaya uhitaji wa mafukara na masikini?

Answer

Sharia tukufu haikuweka ukomo maalumu kwa kiasi cha faida katika biashara, hivyo inajuzu kwa mfanyabiashara kupata faida atakavyo mradi tu kuwepo na kuridhiana kati yake na mnunuzi, na muamala huo uwe katika yale Aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.

Wala haijuzu kisharia kufanya udanganyifu au kuhodhi katika biashara, bali inampasa mfanyabiashara wa Kiislamu kuwa mwaminifu na mkweli katika muamala.

Kadhalika, inajuzu kwa kiongozi na mamlaka husika zinazosimamia masoko kupanga kiwango cha faida katika baadhi ya nyakati za kero (nyakati ngumu), na hiyo ni kwa baadhi ya bidhaa kama dawa na mahitaji ya msingi ambayo watu wote wanayahitaji kwa dharura; jambo hilo hufanyika kwa msingi wa kutanguliza maslahi ya wengi mbele ya maslahi ya mtu binafsi.

Maelezo

Uislamu umeweka sheria mahususi za miamala ya kifedha na mingineyo ili kutimiza manufaa ya watu na kukidhi mahitaji yao, kwa namna ambayo haileti madhara yoyote au mzozo kati ya watu katika miamala hiyo[1].

Miongoni mwa miamala hiyo ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu Ameihalalisha ni biashara kati ya watu kwa kuuza na kununua; Anasema Aliyetukuka: {Na Mwenyezi Mungu amehalalisha biashara na akaharamisha riba} [Al-Baqarah: 275]. Hivyo, biashara imewekwa ili kutimiza maslahi kati ya muuzaji na mnunuzi; muuzaji anatoa bidhaa na mnunuzi anatoa thamani (pesa), na hapo hutokea mabadilishano kati yao ili kupata faida kwa kila mmoja wao. Muuzaji ananufaika na thamani na kupata faida ya mali, na mnunuzi ananufaika na bidhaa. Hivyo, kutafuta faida kupitia kuuza na kununua ni jambo linalojuzu kisharia kwa makubaliano ya Wanazuoni[2].

Ama kuhusu suala la kupanga faida maalumu katika biashara, hukumu yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Sharia tukufu haikuweka ukomo maalumu wa kiasi cha faida katika biashara, bali imeacha jambo hili lifanyike kwa kuridhiana kati ya muuzaji na mnunuzi[3]; kwa kauli yake Aliyetukuka: {Enyi mlioamini! Msiliane mali zenu baina yenu kwa batili, isipokuwa iwe biashara kwa kuridhiana baina yenu. Wala msijiuwe. Hakika Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwarehemuni} [An-Nisa: 29].

Na kutoka kwa Urwa Al-Bariqi (R.A.) kwamba Mtume (S.A.W.): “Alimpa dinari ili amnunulie mbuzi mmoja, naye akamnunulia mbuzi wawili kwa dinari hiyo, kisha akamuuza mmoja wao kwa dinari moja, akamrejea Mtume na dinari pamoja na mbuzi mmoja. Mtume akamuombea baraka katika biashara yake, na ingekuwa ameinunua hata mchanga basi angepata faida ndani yake” [Imepokelewa na Al-Bukhari].

Matini hizi za kisharia hazikubainisha kiasi maalumu cha faida.

Pili: Ingawa Sharia haikuweka asilimia maalumu ya faida, imeharamisha faida inayotokana na muamala wa haramu kama riba na udanganyifu. Kutoka kwa Abu Huraira (R.A.): “Kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) alipita karibu na rundo la chakula[4], akaingiza mkono wake ndani yake, vidole vyake vikahisi unyevu. Akasema: Ni nini hiki ewe mwenye chakula? Akasema: Kimepatwa na mbingu[5] ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Akasema: Kwa nini usikiweke juu ya chakula ili watu wakione? Anayefanya udanganyifu hayuko pamoja nami” [Imepokelewa na Muslim].

Tatu: Kadhalika, Sharia imeharamisha dhuluma katika biashara[6] kwa kupandisha bei ya faida kupita kiasi na kutumia vibaya ujinga wa mnunuzi kuhusu bei sahihi ya bidhaa. Inampasa mfanyabiashara awe mkweli katika mauzo yake, na apate faida katika biashara yake kama ilivyo desturi ya wafanyabiashara wanaojulikana kwa ukweli wao sokoni[7]. Kutoka kwa Abu Said Al-Khudri (R.A.), kutoka kwa Mtume (S.A.W.) amesema: “Mfanyabiashara mkweli na mwaminifu atakuwa pamoja na Manabii, Masiddiki (wakweli), na Mashahidi” [Imepokelewa na At-Tirmidhi].

Na kutoka kwa Hakim bin Hizam (R.A.), kutoka kwa Mtume (S.A.W.) amesema: “Wafanyabiashara wawili wana hiyari (ya kuvunja mkataba) mradi tu hawajatengana; wakiwa wakweli na wakabainisha (kasoro), watabarikiwa katika biashara yao. Lakini wakidanganya na kuficha, baraka ya biashara yao itafutwa” [Imepokelewa na Al-Bukhari].

Nne: Haijuzu kisharia kwa mfanyabiashara kutumia vibaya uhitaji wa watu kwa bidhaa fulani na kupandisha thamani yake; jambo hili linahesabika kuwa ni miongoni mwa uhodhi (Ihtikar) ambao Sharia ya Kiislamu imeuharamisha. Kutoka kwa Umar bin al-Khattab (R.A.) amesema: Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: “Mleta bidhaa (sokoni) huruzukiwa, na mwenye kuhodhi amelaaniwa” [Imepokelewa na Ibn Majah]. Hivyo, inampasa mfanyabiashara aridhike na kiasi cha faida cha wastani ili kuwafanyia wepesi mafukara na masikini. Kutoka kwa Jabir bin Abdullah (R.A.) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu (S.A.W.) amesema: "Mwenyezi Mungu amrehemu mtu ambaye ni mkarimu na mwenye upole[8] anapouza, anaponunua, na anapodai haki yake[9]" [Imepokewa na Al-Bukhari].

Tano: Inajuzu kwa kiongozi na mamlaka husika zinazosimamia na kuratibu masoko kupanga kiwango cha faida kwa wafanyabiashara katika baadhi ya nyakati kwa baadhi ya bidhaa za lazima, kama vile dawa na mahitaji ya msingi ambayo watu hawawezi kuyaacha. Hii ni kwa ajili ya kuzuia aina yoyote ya uroho na ongezeko la bei lililopitiliza; hivyo basi, kupanga bei za baadhi ya bidhaa katika wakati huo ni jambo linalojuzu kisheria ili kuzuia madhara yasitokee, na kutanguliza maslahi ya wengi mbele ya maslahi ya mtu binafsi[10].

Na katika hali hii, inapaswa kuzingatia maelekezo yanayotolewa na mamlaka pamoja na vyombo husika vinavyohusika na uratibu wa udhibiti wa bei masokoni[11].

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

1- Sharia tukufu haikuweka ukomo maalumu wa kiasi cha faida katika biashara.

2- Inajuzu kwa mfanyabiashara kupata faida atakavyo mradi tu kuwepo na kuridhiana kati yake na mnunuzi, na muamala huo uwe katika yale Aliyoyahalalisha Mwenyezi Mungu Aliyetukuka.

3- Haijuzu kisharia kufanya udanganyifu au uhodhi katika biashara, bali inampasa mfanyabiashara wa Kiislamu kuwa mwaminifu na mkweli katika miamala yake.

4- Inajuzu kwa kiongozi na mamlaka husika zinazosimamia masoko kupanga kiwango cha faida katika baadhi ya nyakati za kero (nyakati ngumu), na hiyo ni kwa baadhi ya bidhaa kama dawa na mahitaji ya msingi ambayo watu wote wanayahitaji kwa dharura; jambo hilo hufanyika kwa msingi wa kutanguliza maslahi ya wengi mbele ya maslahi ya mtu binafsi.

 

[1] "Badai al-Sanai" cha Al-Kasani (5/143), na "Al-Furuq" cha Al-Qarafi (3/290).

[2] "Fath al-Qadir" cha Kamal al-Din bin al-Humam (6/247-248).

[3] "Al-Tashil li-Ulum al-Tanzil" cha Ibn Juzay (1/188).

[4] "Rundo la chakula": Mkusanyiko wa chakula kilichowekwa juu ya kingine.

[5] "Kimepatwa na mbingu": Kimepatwa na mvua.

[6] "Ghabn": Udanganyifu unaopelekea hasara kwa mmoja wa washiriki wa mkataba.

[7] "Mawahib al-Jalil" cha Al-Hattab al-Maliki (4/468), "Al-Ashbah wa al-Nazair" cha Al-Suyuti (uk. 7, uk. 89), na "Ahkam al-Quran" cha Ibn al-Arabi al-Maliki (4/1804).

[8] "سمحًا": Mkarimu, mwenye upole na anayekubali yanayotakiwa kwake bila kero.

[9] "اقتضى": Kudai haki yake aliyonayo kwa mwingine.

[10] "Al-Ashbah wa Al-Nazair" cha Ibn Nujaym (uk. 74), "Al-Ashbah wa Al-Nazair" cha Al-Suyuti (uk. 87), na "Al-Muwafaqat" cha Al-Shatibi (3/89).

[11] "Sharh Sahih Muslim" cha Al-Nawawi (12/222), na "Al-Fatawa Al-Fiqhiyya Al-Kubra" cha Ibn Hajar Al-Haytami (1/278).

Share this:

Related Fatwas