Hukumu ya kutia udhuu bila kufanya ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya kutia udhuu bila kufanya istinjai (kunawa sehemu za siri)

Question

Je, kutia udhuu bila ya kufanya istinjai ni sahihi?

Answer

Utwahara kutokana na hadathi mbili—ndogo na kubwa—vilevile utwahara wa nguo na mwili ni sharti miongoni mwa sharti za usahihi wa baadhi ya ibada; kama vile Swala, kushika msahafu, na tawafu.

Utwahara kutokana na hadathi ndogo huwa kwa kutawadha (udhuu), ama utwahara kutokana na hadathi kubwa huwa kwa kuoga.

Ni wajibu kwa Muislamu kufanya istinjai baada ya haja ndogo au kubwa, na anatumia katika istinjai hiyo maji au karatasi za msalani (tishu), na si wajibu kufanya istinjai kwa sababu ya kutoa upepo ikiwa mtu anataka kutawadha.

Maelezo

Imeamuliwa kisharia kwamba miongoni mwa sharti za usahihi wa baadhi ya ibada—kama vile Swala, tawafu, na kushika Msahafu Mtukufu—ni utwahara kutokana na hadathi mbili: ndogo na kubwa.

Ushahidi wa kuwekwa sharti la utwahara kwa ajili ya Swala ni mwingi; miongoni mwake ni kauli yake Aliyetukuka: {Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya Swala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifumboni, na mpake vichwa vyenu, na (osheni) miguu yenu mpaka kifundo cha mguu. Na mkiwa na janaba, basi jitwahirisheni} [Al-Ma'idah: 6]. Na Mtume (S.A.W.) amesema: “Mwenyezi Mungu hakubali Swala ya mmoja wenu anapopatwa na hadathi[1] mpaka atie udhuu” [Imepokelewa na Al-Bukhari].

Kadhalika, hali ni hiyo hiyo kwa upande wa tawafu ya kuizunguka Kaaba; kutoka kwa Abdullah bin Abbas (R.A.), kwamba Mtume (S.A.W.) amesema: “Tawafu ya kuizunguka Nyumba (Kaaba) ni kama sala, isipokuwa ninyi mnazungumza humo; basi atakayezungumza humo, asizungumze ila kheri” [Imepokelewa na Al-Tirmidhiy]. Hadithi hii inaonesha kuwa tawafu inawekewa sharti lile lile linalowekwa kwa ajili ya usahihi wa Swala, kama vile utwahara kutokana na hadathi ndogo na kubwa.

Pia, hali ni hiyo hiyo wakati wa kushika Msahafu, kwa mujibu wa kauli yake Mwenyezi Mungu (S.W.): {Hakika hito ni Qur'ani Tukufu (77) Katika Kitabu kilichohifadhiwa (78) Hawakigusi isipokuwa waliotwahirishwa (79)} [Al-Waqi'ah: 77-79]. Aya hii tukufu inaonyesha kuwa inawekwa sharti la utwahara kutokana na hadathi ndogo na kubwa ili kuushika Msahafu.

Imeamuliwa kisharia kwa makubaliano ya Wanazuoni kwamba utwahara kutokana na hadathi mbili—ndogo na kubwa—wakati maji yanapopatikana, huwa kama ifuatavyo:

Kwanza: Utwahara kutokana na hadathi ndogo[2]: Huwa kwa kutawadha (kutia udhuu), nako ni kuosha baadhi ya viungo vya mwili kwa maji, kama ilivyo katika kauli yake Aliyetukuka: {Enyi mlioamini! Mnaposimama kwa ajili ya sala, basi osheni nyuso zenu na mikono yenu mpaka vifumboni, na mpake vichwa vyenu, na (osheni) miguu yenu mpaka kifundo cha mguu} [Al-Ma'idah: 6].

Imepokelewa kutoka kwa bwana wetu Uthman bin Affan (R.A.) namna ya kutawadha; imepokelewa kutoka kwake: “Kwamba aliitisha maji ya udhu, akatawadha kwa kunawa vitanga vyake mara tatu, kisha akasukutua na kupandisha maji puani na kuyatoa[3] kisha akaosha uso wake mara tatu, kisha akaosha mkono wake wa kulia mpaka kifumboni mara tatu, kisha akaosha mkono wake wa kushoto mfano wa hivyo, kisha akapaka kichwa chake, kisha akaosha mguu wake wa kulia mpaka kifundo cha mguu mara tatu, kisha akaosha wa kushoto mfano wa hivyo, kisha akasema: Nilimuona Mtume (S.A.W.) akitawadha mfano wa udhu wangu huu, kisha Mtume (S.A.W.) akasema: Atakayetawadha mfano wa udhu wangu huu, kisha akasimama akaswali rakaa mbili ambazo hazungumzi na nafsi yake (kwa mambo ya dunia) humo, atasamehewa madhambi yake yaliyotangulia” [Imepokelewa na Muslim].

Pili: Utwahara kutokana na hadathi kubwa[4]: Huwa kwa kuoga , nako ni kuosha viungo vyote vya mwili na kuyaeneza maji mwili mzima; Mwenyezi Mungu (S.W.) Amesema: {Enyi mlioamini! Msikaribie sala hali mkiwa mmelewa mpaka mjue mnayoyasema, wala hali mkiwa na janaba—isipokuwa mmo safarini—mpaka muoge} [Al-Nisaa: 43]. Na kutoka kwa Ummu Salama (R.A.) amesema: “Ummu Sulaym alikuja kwa Mtume (S.A.W.) akasema: Ewe Mtume! Hakika Mwenyezi Mungu haoni haya katika ukweli; je, mwanamke analazimika kuoga akiamka na hali ya kuota (amefikia kilele cha matamanio)? Mtume (S.A.W.) akasema: Ndiyo, akiona maji (manii)” [Imepokelewa na Muslim]. Yaani manii yakitoka, basi analazimika kuoga wakati huo.

Ama kuhusu suala la istinjai wakati wa kutawadha, hukumu yake ni kama ifuatavyo:

Kwanza: Ni wajibu kwa mtu kuondoa athari ya najisi baada ya haja ndogo au kubwa, na hilo ni kwa kutumia maji au karatasi za msalani (tishu) na mfano wake, na huku ndiko kunakoitwa istinjai. Kutoka kwa Abdullah bin Abbas (R.A.) amesema: “Mtume (S.A.W.) alipita katika ukuta miongoni mwa kuta za Makka au Madina, akasikia sauti ya watu wawili wakiazibiwa katika kaburi zao, Mtume (S.A.W.) akasema: Wanaazibiwa, na hawaazibiwi kwa jambo kubwa (lililo gumu kuliepuka), kisha akasema: Kwani, mmoja wao alikuwa hajifanyii istibrai[5] kutokana na mkojo wake, na mwingine alikuwa akitembea na kusambaza umbea” [Imepokelewa na Al-Nasa'i].

Pili: Si wajibu kwa mtu kufanya istinjai kabla ya udhu ikiwa ametoa upepo; bali baadhi ya wanazuoni wamejalia istinjai katika hali hii kuwa ni chukizo (Makruh), kwa sababu inaweza kumpelekea mtu kupatwa na wasiwasi.

Tatu: Kutoa upepo pekee hakunajisishi nguo alizovaa mtu, hivyo inajuzu kwa mtu kutawadha katika hali hii bila kubadilisha nguo zake.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

1- Utwahara kutokana na hadathi mbili—ndogo na kubwa—vilevile utwahara wa nguo na mwili ni sharti miongoni mwa sharti za usahihi wa baadhi ya ibada; kama vile Swala, kushika Msahafu, na tawafu.

2- Utwahara kutokana na hadathi ndogo huwa kwa kutawadha, ama utwahara kutokana na hadathi kubwa huwa kwa kuoga.

3- Ni wajibu kwa Muislamu kufanya istinjai baada ya haja ndogo au kubwa, na anatumia katika istinjai hiyo maji au karatasi za msalani.

4- Si wajibu kufanya istinjai kwa sababu ya kutoa upepo ikiwa mtu anataka kutawadha.

 

[1]

[2] «Kuondoa hadathi ndogo»: Ni kutawadha baada ya haja ndogo, kubwa, au kutoa upepo.

[3] «Kuyatoa (puani)»: Ni kutoa maji puani baada ya kuyavuta kwa pumzi.

[4] «Kuondoa hadathi kubwa»: Ni kuoga baada ya kujamiiana au kuota.

[5] «Hajifanyii istibrai kutokana na mkojo wake»: Yaani hajitwahirishi kutokana na athari ya najisi baada ya kukojoa.

Share this:

Related Fatwas