Kuuza nyumba ambayo mke anakaa Edah...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuuza nyumba ambayo mke anakaa Edah

Question

Mwanamke anauliza: Mume wangu amefariki siku chache zilizopita, na hana watoto. Warithi wanataka nitoke nyumbani kwa sababu wanataka kuiuza. Je, kisharia nina haki ya kukaa edah katika nyumba hiyo, au nyumba imekuwa urithi na hivyo nikae edah sehemu nyingine?

Answer

Asili (Kaida) ni kwamba mke anapaswa kukaa edah yake yote katika nyumba ya ndoa aliyokuwemo wakati wa kifo. Warithi hawana haki ya kumlazimisha atoke kabla ya edah kuisha, kwa mujibu wa kauli ya Jamhuri (wanazuoni wengi) wa Fiqhi. Hata hivyo, wanaruhusiwa kuingia mkataba wa kuuza lakini kwa masharti ya kutoa (kutenga) muda wa edah (miezi minne na siku kumi).

Ikiwa haiwezekani kwake kuendelea kukaa nyumbani (kwa dharura), inajuzu kutumia Madhehebu ya Imamu Hanafi ambayo inaruhusu mwanamke aliyefiwa na mumewe kuhamia kutoka katika nyumba ya ndoa na kukaa popote apendapo kwa sababu ya dharura.

Maelezo

Imethibiti kisharia kwamba mwanamke aliyefiwa na mumewe lazima akae edah kwa muda wa miezi minne na siku kumi, isipokuwa kama ana mimba. Hili ni kwa makubaliano ya Wanazuoni wote (Ijmaa) kwa mujibu wa Kauli ya Mwenyezi Mungu:

{Na wale miongoni mwenu wanao kufa na wakaacha wake, hawa wake wangoje peke yao miezi mine na siku kumi.{ [Al-Baqarah: 234]

Na mahali ambapo inamlazimu mwanamke anayekaa edah kukaa katika siku za edah yake: ni nyumba ya ndoa aliyokuwemo wakati wa kutokea kwa utengano (kwa kifo, au talaka, au kufutwa kwa ndoa).

Na asili (uthibitisho) wa hili ni: yaliyopokelewa kutoka kwa Al-Furay’ah bint Malik, dada yake Abu Sa’id Al-Khudri (R.A), alisema: Mume wangu alifariki huko Al-Qadum, nikamjia Mtume (S.A.W) na kumwambia kwake kwamba nyumba yetu ni mbali, basi akaniruhusu, kisha akamwita na akamwambia: “Kaa nyumbani kwako miezi minne na siku kumi mpaka umalize eda .” (Imepokewa na Tirmidhi katika Sunan yake).

Na upande wa dalili (ushahidi) kutoka katika Hadithi hii: ni kwamba ilifahamisha ulazima kwa mwanamke anayekaa eda kubaki katika nyumba ambayo alipokea habari za kifo cha mumewe, na hili ni mpaka amalize eda yake.

Abu Isa Al-Tirmidhi alisema katika Sunan yake: “Hii ni Hadithi Hasan Sahihi, na matendo yanategemea Hadith hii kwa wanazuoni wengi (wa Ahl al-Ilm).”

Na maneno ya wanazuoni wa Fiqhi wa Madhehebu manne yanayofuatwa yametokana na maana hii. Na Wanazuoni wa Fiqhi wametofautiana kuhusu hukumu ya kumtoa mwanamke anayekaa edah ya kifo kutoka katika nyumba ambayo eda ilimlazimu, jambo ambalo linaweza kutokea katika sura mbili: uuzaji wa nyumba ya marehemu na wadai, na uuzaji wa nyumba na warithi, ambayo ndiyo sura inayoulizwa.

Basi Jamhuri (wanazuoni wengi) wa Fiqhi kutoka kwa Imamu Maliki, Shafi, na Hanmbal wameona kuwa: Mwanamke anayekaa eda ya kifo ana haki zaidi ya kukaa katika nyumba ya ndoa, hasa ikiwa nyumba ilikuwa inamilikiwa na mume, bali hata kama ilikuwa imekodishwa na mume alilipa kodi kwa mwenye nyumba. Basi haki ya kukaa kwa mwanamke aliyefiwa na mumewe ni imara zaidi kuliko haki ya warithi ya kufanya matumizi ya mali baada ya umiliki kuhamia kwao, kiasi kwamba anaruhusiwa kisheria kukaa katika nyumba mpaka eda yake iishe [1].

Ama ikiwa baadhi ya warithi wametaka kuuza nyumba hii - kama ilivyo katika suala letu - inajuzu kwao kufanya mkataba wa mauzo, lakini kwa sharti la kuandika katika mkataba kuweka kando muda wa kukaa kwa eda - nao ni miezi minne na siku kumi - au kwa sharti la kuweka wazi kwamba nyumba hiyo ina mwanamke anayekaa eda. Basi ikiwa mnunuzi ameridhika na hilo, vyema, na ikiwa sivyo, anathibitishiwa haki ya kuchagua mauzo kwa sababu ya hasara inayompata.

Hata hivyo, Wanazuoni wa Fiqhi wa Imamu Hanafi wameona kwamba: Mwanamke aliyefiwa na mumewe anaruhusiwa kuhamia kutoka nyumba ya ndoa na kukaa popote apendapo kwa sababu ya dharura. Na wamehesabu miongoni mwa dharura hizo: pale ambapo sehemu yake ya urithi katika nyumba haimtoshelezi, na warithi hawakuridhia yeye kukaa katika nyumba hiyo.

Tunapata faida kutokana na yaliyotangulia:

Kwamba mwanamke aliyefiwa na mumewe lazima akae eda kwa muda wa miezi minne na siku kumi isipokuwa kama ana mimba.

Mahali ambapo inamlazimu mwanamke anayekaa eda kukaa katika siku za eda yake: ni nyumba ya ndoa aliyokuwemo wakati wa kutokea kwa utengano (kwa kifo, au talaka, au kufutwa ndoa).

Haki ya kukaa kwa mwanamke aliyefiwa na mumewe ni imara zaidi kuliko haki ya warithi ya kufanya matumizi ya mali baada ya umiliki kuhamia kwao, kiasi kwamba anaruhusiwa kisheria kukaa katika nyumba mpaka eda yake iishe.

Ikiwa baadhi ya warithi wametamani kuuza nyumba hii, inajuzu kwao kufanya mkataba wa mauzo, lakini kwa sharti la kuandika katika mkataba kuweka kando muda wa kukaa kwa eda.

Inajuzu katika hali ya dharura kwa mwanamke anayekaa eda kuhamia kutoka nyumba ya ndoa, na kukaa popote apendapo, kama vile sehemu yake ya urithi katika nyumba haimtoshelezi, na warithi hawakuridhia yeye kukaa katika nyumba hiyo.

 

[1] “Al-Hidayah” (2/279, iliyochapishwa na Dar Ihya’ al-Turath al-Arabi), “Sharh Mukhtasar Khalil” (4/157, iliyochapishwa na Dar al-Fikr), “Nihayat al-Muhtaj” (7/155, iliyochapishwa na Dar al-Fikr), “Sharh Muntaha al-Idaha al-Idah 4, iliyochapishwa na Alaam Al-Kutub 32/2).

Share this:

Related Fatwas