Kuua wanawake vitani

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuua wanawake vitani

Question

Je, inajuzu kuwaua wanawake vitani?

Answer

 

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

     Makusudio ya swali hili ni pale Waislamu wanapopigana na wengine wasio waislamu, je inajuzu kuwaua wapiganaji wanaobeba silaha au hata wasiobeba silaha wakati wa kuifungua nchi yao kwa nguvu, na je hujumuisha wote wakiwemo wanawake?

     Hukumu: Haijuzu kwa Waislamu kuwaua wanawake wapiganaji, ikiwa Waislamu wapo katika hali ya kujilinda au kuvamia. Hata kama Waislamu wataingia nchi ya wapiganaji maadui ikajuzu kuwaua, basi haijuzu kuwaua wanawake. Lakini mwanamke akiwa ni mpiganaji dhidi ya waislamu basi inajuzu kumuua.

     Na dalili ya hayo ni kwamba asili katika tabia ya mwanamke hapigani wala habebi silaha kwa tabia na maumbile yake, na kuna matini nyingi zilizo wazi ambazo zinaharamisha kuwaua wanawake.

     Miongoni mwa matini hizo ni hadithi ya Ibn Omar R.A. iliyotajwa katika Sahihi mbili, alisema: “Mwanamke alikutwa ameuliwa katika baadhi ya vita alivyopigana Mtume S.A.W., basi Mtume S.A.W. akakemea kuwaua wanawake na watoto”.

     Aidha Mtume S.A.W. katika baadhi ya vita aliwaona watu wamekusanyika juu ya jambo, basi akamtuma mtu na akamwambia: "Angalia ni kwa lipi wamekusanyika?" Basi aliporudi yule mtu akasema: "Mwanamke ameuawa!" Mtume S.A.W. akasema: "Hakustahiki kuuawa." Na Khalid Bin Al Waleed wakati huo alikuwa katika mstari wa mbele wa jeshi, basi Mtume S.A.W. alimtuma mtu: "Mwambie Khalid asimuue mwanamke wala mzee mkongwe"

     Na katika Sunan Abu Dawud kutoka kwa Anas Bin Malik R.A. kuwa Mtume S.A.W. alisema: “Nendeni kwa jina la Mwenyezi Mungu, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu na juu ya Mila ya Mtume S.A.W. na msimuue mzee mkongwe, mtoto mchanga, mtoto mdogo wala mwanamke, na msipindukie mipaka katika dini yenu, kusanyeni ngawira zenu, tendeni mema na fanyeni wema, hakika Allah S.W. anawapenda wafanyao wema”.

     Na katika Musnad kutoka Hadithi ya Ibn Kaab Bin Malik kutoka kwa ami yake: “Mtume S.A.W. alipotuma risala kwa Ibn Abu Al Haqiq huko Khaibar alikataza jambo la kuwaua wanawake na watoto”.

     Naye Assiddiyq R.A aliusia kutowagusa, aliposema katika wasia wake kwa Yazid Bin Abu Sufiyan alipomtuma Sham: “Usimuue mtoto, mwanamke wala mzee mkongwe”. Ameitoa Malik katika Muatwa.

     Wanachuoni wanasema hadithi hizo zenye makatazo zinamaanisha kuharamisha, Al Baghawiy alisema baada ya kutaja hadithi ya Ibn Omar R.A. iliyopita: “Hadithi hii usahihi wake umekubaliwa, na kwa wanachuoni kuifanyia kazi ni wajibu, kwamba hawauliwi wanawake wa vita na watoto wao mpaka waanze kupigana na hapo wanastahiki kuuliwa” [Al Baghawiy, Sharh Sunna, 11/47, Ch. Al Maktabu Al Islamiy).

     Na Ibn Al Qayim Al Hanbaliy amesema: “Mtume S.A.W. hakuhalalisha katu kuwaua wanawake na watoto katika vita vyake” [Ahkaam Ahlu Dhimma, 1/152, Ch. Ramadiy].

     Na Al Nawawiy Al Shaafiy amesema: “Inaharamishwa kuwaua wanawake wa makafiri, watoto wao, wendawazimu na makhuntha, wakianza wao kupigana vita basi inajuzu kuwaua” [Al Nawawiy, Rawdhat Al Talebeen, 10/244].

Shihaabuddin Al Ramliy alisema: “(Inaharamishwa kuua mtoto, mwendawazimu na mwanamke) hata kama hana ahadi, tofauti na rai iliyoshurutisha awe na ahadi” [Nihayatu Al Muhtaaj, 8/64, Ch. Mustafa Al Halabiy].

     Al Kassaniy Al Hanafiy amesema: “Hali hii inakuwa wakati wa kupigana au baada ya kumalizika kupigana yaani baada ya kuchukua ngawira na mateka. Ama katika hali ya kupigana basi inaharamishwa kumuua mwanamke, mtoto, mzee mkongwe na asiyeweza kutembea kwa miguu, ama katika hali ya baada ya kumalizika kupigana; baada ya kupata mateka na ngawira basi kila asiyehalali kumuua wakati wa kupigana, inaharamishwa kumuua wakati wa baada ya kumalizika kupigana” [Badaiu Sanai, 7/101, Ch. Al Maktabatu Al-Elmiya).

     Al Dosuqiy Al Malikiy amesema: “Jua kwamba mwanamke ana hali nane. Mwanamke ima aue mtu au asiue, na katika hali mbili ima apigane kwa silaha au kwa kitu chengine, na katika hali hizi mbili inawezekana kutekwa au la. Basi akiua mtu inajuzu kumuua, sawa kapigana kwa silaha au kwa kitu chengine kama mawe, na sawa ametekwa au ameuawa moja kwa moja. Na kama hajamuua mtu basi akipigana kwa silaha kama wanaume inajuzu kumuua akiwa ametekwa au la, na kama akipigana kwa kurusha mawe basi hauliwi baada ya kutekwa kama walivyoafikiana wanachuoni.” [Hashiyat Al Dosuqiy ala Sharh Al Kabreer 2/176, Ch. Dar Al Fikr).

     Na Ibn Qudama Al Hanbaliy amesema: “Usiue mwanamke wala mzee mkongwe. Hii ni rai ya Malik na watu wa maoni. Na imepokewa hivyo kutoka kwa Abu Bakar Assiddiyq na Mujahid. Imepokewa kutoka kwa Ibn Abass akifasiri maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wala msipindukie mipaka}[AL BAQARAH, 190], yaani “msiwaue wanawake, watoto na mzee mkongwe, na yeyote miongoni mwao akipigana basi inajuzu kumuua.” [Al Mughniy, 9/311, Maktabat Al Qahira Al kKubra).

     Ibn Hazm Dhaahiriy alisema: “Haifai kuwaua wanawake wao au kuwaua wasio baleghe isipokuwa wakipigana basi ikiwa hapana budi inajuzu kuwaua. Imepokelewa na Al Bukhari kutoka kwa Ibn Omar R.A. “Mwanamke alikutwa ameuliwa katika baadhi ya vita alivyopigana Mtume S.A.W., basi Mtume S.A.W. akakemea kuwaua wanawake na watoto.” [Al Mahaliy, 5/346, Ch. Dar Al Fikr].

     Al Kamal Bin Al Humam Al Hanafiy amesema: “Inaaminika kwamba kuwaua wanawake na watoto ni haramu kwa makubaliano ya maulamaa” (Fat-h Al Qadeer, 5/452, Ch. Dar Al Fikr).

     Ibn Batal alisema: “Katika makubaliano ya maulamaa haifai kukusudia kuwaua wanawake wanaopigana au watoto wao; kwani aghalabu wanakuwa hawapigani” [Sharh Al Bukhari, 5/170, Ch. Maktabat Al Rushd].

     Yaliyopita yote yanahusiana na mwanamke ambaye hajaingia vitani, ama yule mwanamke ambaye kaingia vitani akapigana, basi inajuzu kumuua kwa mujibu wa maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi atakayekufanyieni uadui, nanyi mfanyieni uadui kwa kadiri alivyokufanyieni uadui. Na mcheni Allah, na jueni kwamba Allah Yu Pamoja na wachamungu.} [AL BAQARAH, 194]. Na katika Al Mujam Al Kabeer (Al Tabaraniy) kutoka hadithi ya Ibn Abbas R.A. ya kwamba: “Mtume S.A.W. alikuwa anapita siku ya Handaki akamkuta mwanamke ameuliwa, Mtume S.A.W. akasema: Nani aliyemuua huyu?. Mtu mmoja akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mimi ndiye niliyemuua. Mtume S.A.W. akasema: kwa nini umefanya hivyo? Yule mtu akasema: alipigana nami kwa upanga, basi Mtume S.A.W. akanyamza”.

     Na maneno ya wanachuoni yametangulia katika kuruhusu haya, kwamba: Mwanamke akipigana vita, basi inajuzu kumuua. Na tunahitimisha kwa kubainisha vipi sheria inawahurumia wanawake wakati wa vita, Ibn Al Qayim alisema: “Waislamu wakizingira ngome ambayo haina watu isipokuwa wanawake, basi wakikubali kutoa jizya wakawa watu wa dhima basi itakuwa haramu (kwa Waislamu) kuwafanya watumwa” [Ahkam Ahl Dhimma, 1/156].

     Kutokana na yaliyopita: haijuzu kwa Waislamu kuwaua wanawake wapiganaji, sawa Waislamu wapo katika hali ya kujilinda au kuvamia. Lakini mwanamke akipigana vita , basi inajuzu kumuua kwa kuwa wakati huo anakuwa sawa na mwanamme madamu kuna uwezekano waislamu kuuliwa na mwanamke huyo. 

Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas