Mashairi Ya Kumsifu Mtume S.A.W.
Question
Nini hukumu ya mashairi yaliyotungwa na kuimbwa kwa ajili ya kumsifu Mtume S.A.W? Na mashairi hayo yalitungwa lini? Je, mashairi hayo yanawahusu Masufi tu kama wanavyodai baadhi ya watu?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Shairi asili yake ni maneno yenye uzani, yaani yenye arudhi, na Imamu Nawawiy alizungumzia hukumu yake katika ufafanuzi wake wa (Sahihi Muslim 15/14, Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabiy): “Wanachuoni wote walisema: inaruhusiwa kama hamna ndani yake maneno machafu na mfano wake, wakasema: nayo ni maneno ambayo mazuri yake ni mazuri, na mabaya yake ni mabaya, mtazamo huo ni sawasawa; kwa sababu Mtume S.A.W aliyasikia mashairi na kumwomba Hassan kuyaimba kwa kuwafanyia tashtiti washirikina, na Masahaba wake wameyaimba katika safari, n.k. Makhalifa, maimamu wa Masahaba na watu wema waliotangulia wameyaimba, na hakuyakana hata mmoja wao kabisa, lakini waliyakataa mashairi yenye maneno machafu ambayo ndiyo ubaya wenyewe”. Maneno bora anayotamka mtu ni maneno ya kumsifu Mtume S.A.W, au kuyarudia au kuyasikiliza, nayo ndiyo yaliyojulikana hivi karibuni ni mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W. Imepokelewa na Bukhari kutoka kwa Abu Kaabu kutoka kwa Mtume: “Miongoni mwa mashairi ni hekima”. Pia Mtume S.A.W alisikiliza mashairi, na imepokelewa hivyo katika hadithi nyingi, kati ya hizo ni hadithi za Sahihi ya Imamu Muslim na Bukhari.
Mashairi ya kumsifu Mtume yalianza katika zama ya Mtume, ambapo mashairi yalikuwa miongoni mwa silaha za makala yaliyotumiwa na Waarabu kwa ajili ya tashtiti na kusifu, washairi wa washirikina walikuwa wakimfanyia tashtiti Mtume S.A.W, basi mashairi ya kumsifu Mtume yaliyajibu mashairi hayo yaliyotungwa kwa ajili ya tashtiti. Hassan bin Thaabit ni miongoni mwa washairi waliomtetea Mtume S.A.W na kumsifu, na Mtume alikubali hivyo. Imepokelewa na Imamu Muslim na Bukhari kutoka kwa Albaraa ibn Azib R.A kwamba Mtume S.A.W, alimwambia Hassan: “Wafanyie tashtiti, na Jibril yuko pamoja nawe”.
Na kumsifu Mtume S.A.W ni dalili ya upendo kwake, ambao ni msingi miongoni mwa misingi ya imani, Mwenyezi Mungu anasema: {Sema: Ikiwa baba zenu, na wanenu, na ndugu zenu, na wake zenu, na jamaa zenu, na mali mliyoichuma, na biashara mnazoogopa kuharibika, na majumba mnayoyapenda, ni vipenzi zaidi kwenu kuliko Mwenyezi Mungu na Mtume wake na Jihadi katika Njia yake, basi ngojeni mpaka Mwenyezi Mungu alete amri yake. Na Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wapotovu.} [AT-Tawba: 24], na Mtume S.A.W akasema: “Naapa kwa yule ambaye roho yangu iko mikononi mwake, haamini mmoja wenu mpaka anipende zaidi kuliko baba yake na mtoto wake”. Sahihi Bukhari.
Pia alisema: “Haamini mmoja wenu mpaka niwe ananipenda zaidi kuliko mtoto wake, baba yake na watu wote”. [Sahihi Muslim.]
Na kumpenda Mtume S.A.W ni dalili ya kumpenda Mwenyezi Mungu mwenyewe, kwani anayempenda Mfalme anampenda mjumbe wake, na Mtume wa Mwenyezi Mungu ni kipenzi cha Mwenyezi Mungu, Mtume S.A.W. ametujia na kheri zote, na amevumilia shida ili tuingie katika Uislamu na tuingie peponi, na Mwenyezi Mungu amemsifu katika aya nyingi za Quraani zinazoonyesha fadhila zake, kama vile kauli ya Mwenyezi Mungu aliposema: {Na hakika wewe una tabia tukufu.} [Al-Qalam: 4].
Wanachuoni wanasema kumsifu Mtume S.A.W ni mashairi yanayojikita katika kumsifu Mtume S.A.W kwa kuhesabu sifa zake za kimaumbile na kitabia, kuonyesha hamu ya kumwona, kulitembelea kaburi lake na maeneo matakatifu yanayohusiana na maisha ya Mtume S.A.W, pamoja na kutaja miujiza yake ya kimwili na kiroho, na kuyatunga mashairi yanayohusiana na sera yake, na kuvisifu vita vyake na sifa zake ambazo ni mfano mzuri, na kumwombea rehma kwa ajili ya heshima na kutukuka kwake, nayo ni mashairi ya ukweli, yanayojiepusha na uwongo na kupata riziki, na yakusudiwe kujikurubisha kwa Mwenyezi Mungu, na kila sifa anazozisifiwa Mtume S.A.W hazitoshi katika haki yake.
Sheikh AL-Bajuri R.A alisema katika [Utangulizi wa maelezo yake kuhusu AL-Burda uk. 5-6, Maktabat AL-Adaab.]: “Hakika sifa zake S.A.W za ukamilifu haiwezekani kuhesabiwa, na tabia zake nzuri haiwezekani kuchunguzwa, wanaomsifu hawawezi kumsifu kama anavyostahiki. Mwenyezi Mungu amemsifu katika Quraani Tukufu kwa sifa zinazoshangaza akili, na hatuwezi kuzifikia. Watu waliotangulia na wengine wakitaka kutia chumvi kuhusu hesabu ya tabia zake nzuri, hawataweza kuzitambua sifa hizo alizopewa na Mwenyezi Mungu.
Hakuna anayeeleza kikamilifu sifa zake njema katika haki yake, na wenye fasaha hawawezi kumsifu Mtume S.A.W kama anavyostahiki.
Mtume S.A.W hakusifiwa baada ya kuenea Uislamu tu, bali alisifiwa pia katika zama za ujinga, Umu Maabad amemsifu Mtume S.A.W kwa mume wake kuwa yeye ana tabia nzuri akisema: “Mwanamume mmoja ametupitia alikuwa na uso mzuri sana unga’ao, nyusi zake zina nywele nyingi sana, macho yake ni pana sana, sauti yake ya kiume, urefu wake ni wa katikati, huchukii urefu wake, wala hudharau ufupi wake, hana tumbo kubwa, hana upara, shingo yake ni kama jagi la fedha, kama akitamka, matamshi yake yana bashasha, na akinyamaza ana heshima, maneno yake ni mazuri sana kama shanga, umbo lake ni zuri sana kuliko wenzake wote, uso wake ni mzuri sana kuliko wote, ana watu wanaomzunguka, akiwaamuru wanashindana katika kutekeleza amri yake, na akiwakataza wanamtii katika makatazo yake, alisema: Sifa hii ni ya mtu mmoja kutoka Quraish (anakusudia Mtume S.A.W.), na nikimwona nitamfuatilia, na nitafanya bidii kwa ajili ya hivyo” AL-Muujam AL-Kabiir Li Tabaraani.
Baadhi ya watafiti akiwemo Busayri na Ibn Dakik AL-Idi walisema kwamba: mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W. ni sanaa mpya haikuwepo isipokuwa katika karne ya saba Hijriya, ni kweli kwamba mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W yalitungwa na Hassan bin Thaabit, Kaab Ibn Malik, Kaab Ibn Zuhair na Abdullah Ibn Rawahah kuhusu maisha ya Mtume S.A.W. Na Mtume aliyapitisha mashairi hayo, na dalili ya hivyo ni kwamba Mtume S.A.W aliuimba utenzi maarufu wa Kaab Ibn Zuhair Ibn Abi Salma katika msikiti ambapo utenzi huo unamsifu Mtume S.A.W.
Naye Mtume S.A.W akayapitisha mashairi hayo na hakumkataza Kaab Ibn Zuhair kumsifu, wala hakumkataza kuyaimba katika msikiti, bali alimvalisha vazi. Rejea: [AL-Isaba Fi Tamiizi AL-Sahaba Li Ibn Hajar 5/444, Dar Al-Kutub Al-Elmiya.].
Imepokelewa na Khuraim Ibn Aws Ibn Haritha Ibn Lam, alisema: “Tulikuwa pamoja na Mtume S.A.W, Abbas Bin Abdul Muttalib R.A akamwambia: “Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu nataka kukusifu, Mtume S.A.W. akamwambia, haya lete nakuombea Mwenyezi Mungu akubariki” Al-Mujam Al-Kabiir Li Tabarani.
Tunaona kwamba Mtume S.A.W. alimkubalia mjomba wake kumsifu na hakumkataza kufanya hivyo, na hiyo ni dalili ya uhalali wa kumsifu Mtume S.A.W.
Ama kuhusu kauli yake Mtume S.A.W: “Msinisifu kwa ubatili kama Wakristo walivyomsifu Ibn Mariamu kwa ubatili, lakini mimi ni mja wake Mwenyezi Mungu, basi mseme kwamba mimi ni mja wa Allah na Mtume wake.”. Katika Sahihi ya Bukhari, maana ya kusifu hapa ni kusifu kwa ubatili, kama ukisema: nilimsifiu mtu fulani kwa uwongo kama alivyosema: “Kama Wakristo walivyomsifu Ibn Mariamu kwa ubatili” yaani: katika madai yao kwamba yeye ni Mungu na kadhalika. [Fathu Al-Bari Li Ibn Hajar 6/490, Dar Al-Maarifa]. Mtume S.A.W alichowakataza ni kusifu kwa ubatili tu, na hakuwakataza kabisa kuhusu kusifu. Basi Mtume S.A.W amepiga marufuku kumsifu kwa kutia chumvi na kumsifu Mtume S.A.W kwa kumpachika sifa za Mwenyezi Mungu, kama vile kumpandisha katika cheo cha uungu au kupewa baadhi ya sifa za Mwenyezi Mungu. Kuna mwanamke katika zama yake, alikuwa akimsifu kwa kauli yake: “Na miongoni mwetu kuna Nabii anayejua yatakayotokea kesho”, Mtume S.A.W alimwambia: “Usiseme hivyo, lakini sema uliyokuwa ukisema”. Katika Sahihi Bukhari, tunaona kwamba Mtume S.A.W alimkataza, kwa sababu ujuaji wa mambo ya ghaibu (yasiyoonekana) ni sifa miongoni mwa sifa za Mwenyezi Mungu, na Mwenyezi Mungu amemwamuru Mtume wake kusema: {Na lau kuwa ninayajua ya ghaibu ningejizidishia mema mengi} [Al-Aaraaf: 188]. Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W hajui mambo ya ghaibu isipokuwa yale aliyofundishwa na Allah S.W.
Mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W hayatungwi na Masufi tu, kwani kuna washairi wengi walimsifu Mtume S.A.W, na hawakuwa miongoni mwa Masufi, kwa sababu kumpenda Mtume S.A.W na kumsifu hakuhusu baadhi ya watu tu, au madhehebu fulani, au kikundi cha Waislamu tu, kwa sababu Mtume amepelekwa kwa watu wote.
Hata hivyo, mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W. yamestawi sana na yamefanikiwa katika mazingira ya Masufi mwishoni mwa karne ya saba na mwanzoni mwa karne ya nane katika zama za madola, walikuwepo washairi wengi wa kumsifu Mtume S.A.W katika siku hizo, na mashairi yao yalikuwa mengi sana, na Busayri mwenyewe ni mkuu wa sanaa hii, siyo katika zama yake tu, bali katika zama zilizofuata baadaye pia, washairi wengi katika enzi ya kisasa wamemchukua kama kigezo kwao, na wamechukua maana zao kutoka utenzi wake, [Al-Kaukab Al-Durriyi Fi Madhi Khairi Al-Bariya], unaojulikana kwa jina la (Al-Burda), utenzi huo ni miongoni mwa mashairi mazuri sana ya Kiarabu, na ni miongoni mwa mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W yaliyo bora sana kuliko mashairi mengine, nayo ni mashairi yaliyotungwa na washairi wakongwe katika Uislamu, watafiti wengi sana wamekubaliana kwamba utenzi huo ni bora sana kuliko tenzi za kumsifu Mtume S.A.W. kama vile utenzi wa Kaab Ibn Malik (Al-Burda ya kwanza) hata inasemekana kwamba: utenzi huo ni maarufu sana kuliko zote katika mashairi ya Kiarabu kati ya watu wa kawaida na wengine. Mshairi ametaja katika utenzi huo mwenendo wa Mtume S.A.W tangu kuzaliwa kwake mpaka kifo chake, na ameeleza kuhusu miujiza yake na sifa zake.
Na baada ya kusoma kasida na mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W kwa kufuatilia kiwango cha kihistoria na kisanii inaonekana kwamba mashairi hayo yalichukua mada zake za ubunifu, na mtazamo wake ni wa Kiislamu kutoka Quraani Tukufu kwanza, kisha kutoka Sunna ya Mtume Muhammad S.A.W, pia kuna chanzo muhimu katika kutunga mashairi ya kumsifu Mtume S.A.W. nacho ni kutegemea Sira ya Mtume S.A.W. ambayo imeeleza maisha ya Mtume S.A.W kwa maelezo yake, kwa mfano [Siratu Nabawiyya Li Ibn Hisham], [Siratu Nabawiyya Li Ibn Hibban), (Al-Wafa BiAhwali Al-Mustafa] cha Abu Faraj Abdul Rahman Ibn Al-Jawzi, na [ASh-Shifa Bitaarif Hukuki Al-Mustafa] cha Al-Qadhi Iyadh n.k.
Na kwa mujibu wa yaliyotangulia hapo juu, mashairi ya kumsifu Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. ni miongoni mwa matendo makuu ya ibada, na kuyaimba kuna thawabu kubwa, na mashairi hayo hayahusu kikundi cha watu maalumu, bali ni kwa Waislamu wote.
Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi.