Maadili Baina ya Mgaumbile na Kujifunza
Question
Kuna tifauti gani baina ya tabia na mazoea? Na je, tabia ya binadamu ya kimaadili inaweza kubadilika na kunyooshwa?
Answer
Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., watu wake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:
1) Kuna tofauti kati ya tabia ya kimaumbile na mazoea, kwani tabia ya kimaumbile ni ile inayokuwa ya asili ya kimaumbile ambayo mwanadamu ameumbiwa, wakati ambapo mazoea ni hali ya nafsi ambayo nafsi hiyo kusababisha kuifanya bila ya kufikiri au kuona. Na asili ya neno tabia ya kimaumbile katika lugha ya Kiarabu ni kutokana na kutengeneza upanga na kuwa na umbile lake kamili na maalumu linalotokana na madini ya chuma, na kwa ajili hii tuna kazi ya kuwaza ugumu wa kubadilika kwake na upeo wa kinachohitajika kufanyika kufikia lengo hilo la mabadiliko kutokana na kupambana vikali na nafsi. Lakini mabadiliko yake hayo yanawezekana. Ama kwa upande wa mazoea yenyewe hutokana na kukariri kitendo mara kwa mara na katika lugha ya Kiarabu neno hili linatokana na kitenzi aada kwa maana amerudi au amerejea. Na tumelizungumzia jambo hili katika maudhui inayojitegemea. Na hapa hebu tuzungumzie tabia ya kimaadili.
2) Na tabia za mwanadamu za kimaadili kwa mujibu wa aonavyo marehemu Prof/Dkt. Muhammad Dhiaau Din Alkurdiy, mwalimu na mkuu wa kitengo cha Akida ya Kiislamu na Falsafa, Katika Chuo Kikuu cha Al-Azhar anasema: "tabia ya aina hii inaweza kubadilishwa na kunyooshwa na kuilea. Na kauli ya kuwa tabia hii haikubali mabadiliko kama yalivyo madhehebu ya baadhi ya wanafalsafa" inazifanya risala za Mwenyezi Mungu na Mitume wake kuwa ni upuuzi mtupu usiokuwa na faida yoyote. Vipi basi Mwenyezi Mungu Mtukufu alete Mitume wake duniani ili waje kubadilisha jambo ambalo haliwezi kugeuzwa wala kubadilishwa!
3) Na ukweli ni kuwa mtu ambaye hajawahi kuonja ladha ya juhudi za kimaadili na wala hajawahi kuyashinda maadili hayo ndiye aliyetoa tamko la kutowezekana kubadilishwa au kugeuzwa kwake. Na aliyejua aina hii ya juhudi na akasimama kidete katika njia yake ndiye aliyesema kuwa kuna uwezekano wa kufanyiwa marekebisho na kugeuzwa. Na marejeo ya haya ni kuwa, Mwenyezi Mungu Mtukufu ameziumba nyoyo zinachangaya baina ya dawa na matamanio yake na wala haziwezi kujizuia na machafu yake. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu amewaelezea watu hawa kwa sifa mbali mbali katika Quraani Tukufu, Allah S.W. anasema: {Mwenyezi Mungu amepiga muhuri juu ya nyoyo zao na juu ya masikio yao, na juu ya macho yao pana kifuniko. Basi watapata adhabu kubwa}. [Baqarah: 7], Na nafsi hizi zinaujua ukweli na zinauficha. {wanaujua ukweli kama wanavyowajua watoto wao na wapo miongoni mwao wenye kuuficha ukweli huku wakijua} [Baqarah:146]. Na Mwenyezi Mungu ameziumba nyoyo zingine zinazoujua ukweli na zinajaribu kuufanyia kazi kwa kiasi cha uwezo wake na ubora wake na maandalizi yake na kwa ajili hii Mtume S.A.W. amesema: "Kile nilichokukatazeni jiepusheni nacho na kile nilichokuamrishe kifanyeni kwa kiasi muwezacho", akakifanya kile kinachoamrishwa kufanywa kuwa ni wajibu kukifanya kwa kiasi cha uwezo wa mja, na kile alichokikataza kuwa ni lazima kukiacha na hakuna udhuru wowote unaokubalika kukifanya.
4) Na Mtume S.A.W. ametoa mfano wa tofauti ya jinsi watu walivyo katika kuyapokea mabadiliko ya kimaadili, na akasema: "Mfano wa kile alichonituma mimi Mwenyezi Mungu katika uongofu na elimu ni kama mfano wa mvua nyingi iliyonyeesha katika ardhi pakawepo katika ardhi hiyo sehemu iliyoyapokea hayo maji ya mvua na ardhi hiyo ikaota mimea na majani kwa wingi, na kuna sehemu ya ardhi hiyo iliyazuia maji na Mwenyezi Mungu akawanufaisha watu kwa maji hayo, wakayanywa na wakayalimia, na pakawepo sehemu ya ardhi ambayo haishiki maji wala haioti kitu chochote".
5) Na Miongoni mwa yale yanayooesha hivyo ni simulizi ya Raghib Al-Asfahaaniy, tamko lake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {hakika amefaulu Yule aliyeitakasa nafsi yake, na ametoka patupu Yule aliyeipuuza nafsi yake}, na kama isingelikuwa hivyo basi faida ya mawaidha na nyasia ingebatilika, pamoja na ahadi, onyo, amri na katazo, na wala akili isingejuzisha kuambiwa au kuulizwa mukallafu (mtu mkubwa kisheria) kwanini umefanya hivi? Na kwa nini umeacha?. Na vipi jambo hili lishindikane kwa mwanadamu wakati ambapo linawezekana kwa wanyama kubadilisha tabia zao kwa kuwafuga na kuwapa mafunzo.
6) Lakini watu wanatofautiana kwa tabia zao za kimaumbile kwani wao miongoni mwao waliumbwa kwa maumbile ya kukubali haraka na wengine wameumbwa kwa maumbile ya kukubali taratibu, huku wengine wakiwa na maumbile ya kukubali kati kwa kati yaani kati ya haraka na taratibu. Na wote hawawezi kuepukana na athari za kukubali hata kama ni kidogo.
7) Na mwisho kabisa, Imamu Ghazali anasema katika kitabu chake muhimu, cha [Ihyaau Uluumi Diin]: "Tambua kuwa baadhi ya watu walioshindwa na uvivu waliifanya juhudi, mazoezi na kujishughulisha katika kuitakasa nafsi na kuipa mafunzo ya maadili kwa jambo zito lisilowezekana, na wala nafsi zao hazikuruhusu iwe hivyo kutokana na kuzembea kwao na upungufu wao na uchafu wa undani wake na mpaka akadhani kuwa maadili hayafikiriki kuwa yanaweza kubadilika kwani tabia ya kimaumbile haibadiliki. Na akabadilisha katika hayo kwa mambo mawili;
La kwanza: Ni kwamba maadili ni picha ya undani wa mja na pia maadili ni picha ya nje ya mja. Kwa hivyo umbile ni mwonekano usioweza kubadilishwa. Kwa mfano, mtu mfupi hawezi kujibadilisha akawa mrefu na wala mrefu hawezi kujibadilisha na akawa mfupi, wala mtu mbaya wa sura hawezi kujibadilisha na akawa mzuri, na hivyo ndivyo ulivyo ubaya wa ndani ya nafsi, nao unapita njia hii hii.
La pili: Ni kwamba wamesema (wanazuoni) kuwa tabia njema huyakandamiza matamanio na hasira. Na tumejaribu kufanya hivyo kwa kuwa na juhudi za muda mrefu na tukajua kuwa hivyo hutokana na hali ya hisia na tabia ambayo daima haiepukani na binadamu na kwa hiyo kujishughulisha nayo ni kupoteza muda wake bila ya faida yoyote. Kinachotakiwa ni kukata mawasiliano ya moyo kuelekea katika furaha za haraka (za mpito) na jambo hili kuwepo kwake haiwezekani.
Na sisi tunasema; kama maadili yangekuwa hayakubali mabadiliko basi nyasia, mawaidha na mafunzo ya adabu yasingekuwa na kazi yoyote, … na vipi jambo kama hili (la kubadilisha tabia) likanushwe kuwezekana kwake kwa binadamu wakati ambapo tabia ya mnyama inawezekana kubadilishwa! Ambapo ndege aina ya Kipanga anatolewa katika mazingira ya umwitu na kuwa katika ukaribu na binadamu, na mbwa hutolewa katika shari yake ya kupenda kula na akawa na adabu na kujizuia pamoja na kujiepusha (na anayokatazwa kuyasogelea) na farasi kutoka katika mazingira ya kupambana na kuwa mtulivu na anafuata maagizo, na yote haya ni mabadiliko ya tabia za wanyama.
Na tamko linalofichua siri ya hayo ni kuwa: vitu vinagawanyika migawanyiko miwili; wa kwanza ni vile ambavyo mwanadamu hawezi kuingilia na kuwa na chaguo katika asili yake na ufafanuzi wake, kama vile mbingu na sayari, bali pia viungo vya mwili wake nje na ndani, na vile vile sehemu mbali mbali za wanyama. Kwa ujumla kila kinachopatikana kimekamilika, uwazi unatokea kutokana na kuwepo kwa kitu hicho na kukamilika kwake.
Na mgawanyiko wa pili ni wa vile vilivyokuwepo kwa uwepo pungufu na vikajaaliwa ndani yake uwezo wa kukubali ukamilifu iwapo sharti lake litatimia. Na sharti hilo linaweza kufungamanishwa na chaguo la mja, kwani hakika chembe ya uhai si tunda la tufaha wala mtende isipokuwa imeumbwa kwa umbile ambalo linaweza kugeuka na kuwa mtende iwapo itawekewa malezi, na wala chembe hiyo haiwi tufaha kiasili isipokuwa kwa malezi maalumu, na iwapo chembe hiyo itabadilika na kuwa ni yenye kuathirika kwa kuchagua mpaka izikubali baadhi ya hali fulani na kuzikataa zingine, na hivyo ndivyo ilivyo kwa hasira na matamanio kama tungelitaka kuvikandamiza na kuvitenza nguvu kwa ujumla hadi pasibakie athari yeyote ile ambayo hatujaiweza kiasili, na kama tungelitaka kuviingiza na kuviongoza kwa mazoezi na juhudi pevu basi tungefanikiwa. Na tumeamrishwa kufanya hivyo mpaka ikawa ni sababu ya kuokoka kwetu na kufika kwa Mola wetu tukufu.
Ndio maumbile ni ya aina nyingi, baadhi yake huwa na kasi ya kupokea na baadhi yake huwa hayana kasi hiyo ya mapokezi, na tofauti hii ina sababu kuu mbili, sababu ya kwanza: ni nguvu za matamanio katika asili ya maumbile yenyewe na urefu wake katika muda wa uwepo wake, kwani nguvu za matamanio, hasira na kujivuna zipo ndani ya mwanadamu, lakini kati ya hizo, iliyo ngumu na yenye uzito mkubwa wa kuibadilisha kuliko zote ni nguvu ya matamanio, kwani hii ndio ya tangu na tangu kabla ya zingine, katika uwepo, kwani mtoto mdogo katika msingi wa maumbile yake, huumbiwa matamanio, na kisha baada ya miaka saba huwenda akaumbiwa hasira, na kisha baada ya hapo huumbiwa nguvu za kupambanua.
Na sababu ya pili: ni kuwa maadili yanaweza kuwa na uhakika wa kupatikana kwake kwa kuwepo utendaji mwingi kwa mujibu wa maadili hayo, na kuyatii, na kwa kuamini kuwa kwake ni jambo zuri na lenye kuridhisha, na watu katika hili wamegawanyika makundi manne:
Kundi la kwanza ni binadamu aliyeghafilika ambaye hawezi kupambanua kati ya haki na batili, na kati ya uzuri na ubaya, bali ameendelea kuwa kama alivyoumbwa yuko mbali na aina zote za itikadi, na matamanio yake bado hayajakamilika pia ufuasi wa nafsi yake, na hali hii inakubali haraka mno tiba yake, kwani haihitaji isipokuwa mwalimu au mwongozaji, au msukumo kutoka kwake yeye mwenyewe katika kujitahidi na kupambana, akaboresha tabia zake kwa kipindi kifupi sana.
Na wa pili: awe amekwishatambua baya zaidi ya mabaya lakini akawa hajazoea kufanya kazi nzuri, bali isitoshe, akawa amepambiwa uovu na akawa anaufanya kwa kufuata matamanio yake na kwa kukwepa rai sahihi kutokana na kutawaliwa na matamanio hayo, kwani anapaswa kwanza kuachana na yale yaliyotuama kwenye nafsi yake kwa kuuzoea kwake uovu, na mwisho anatakiwa ajijengee ndani ya nafsi yake sifa ya mazoea ya kurekebishika, lakini tu kwa ujumla awe na uwezo wa kufanya mazoezi iwapo atayapatia nafasi kwa ufanisi na uamuzi kwa kweli.
Na tatu: Aamini kuwa katika tabia mbaya kuwa ni wajibu unaopendwa, na kwamba ni haki na ni uzuri na hutumika katika malezi, na hali inakaribia kuwa na ugumu wa kuitatua na wala hakuna matumaini ya kuirekebisha isipokuwa kwa nadra sana, na inatokana na ongezeko la sababu za kupotea.
Na nne: awe katika kukua kwake kuna rai iliyoharibika na amelelewa katika kuifanyia kazi rai hiyo kiasi kwamba akawa anaona ubora unapatikana kwa kuzidisha shari na kwa kuangamia kwa nafsi za watu, na akawa anajigamba kwayo, na kudhani kuwa hivyo ni kumpandisha cheo, na kiwango hichi ndio kigumu mno kuliko vyote.
Na katika mfanowe imesemwa: na katika tabu ni kufanya mazoezi uzeeni, na katika kuadhibu kuna kumpa mafunzo mbwa mwitu.
Na Kwanza: na miongoni mwa hawa ni Mjinga tu.
Na wa pili: ni mjinga aliyepotea.
Na wa tatu: ni Mjinga, aliyepotea na mwovu. Na wanne: ni Mjinga, aliyepotea, mwovu na mshari.
Na kwa upande wa wazo jingine ambalo wamelitumia kutolea dalili ni kwamba: tamko lao eti mwanadamu akiwa katika hali ya uhai wake hawezi kuachana na matamanio na hasira, kupenda dunia na tabia zingine nyingi kama hizi, hili ni kosa kabisa ambalo limetokea kwa kundi la watu ambao walidhani kuwa kinachokusudiwa katika jitihada ni kuzikandamiza sifa hizi kiukamilifu, na kuzifuta kabisa na baada ya hivyo! Kwani matamanio yameumbwa kwa faida maalumu nayo ni lazima kuwepo kwake katika maumbile, na kama matamanio ya chakula yangelikatika kabisa basi mwanadamu angeliangamia, na kama matamanio ya kuingiliana yangelikatika basi ukoo ungelikatika, na kama ghadhabu isingekuwepo kwa ujumla basi mwanadamu asingechukua hatua za kujilindana na yale yanayoweza kumuangamiza, na angeangamia.
Na vyovyote vile, iwapo asili ya matamanio itakuwepo basi mapenzi ya mali yanaendelea kuwepo bila kizuizi ambayo humfikisha mtu katika matamanio mpaka yampeleke katika kuzuia mali hiyo. Na kinachotakiwa si kuepusha jambo hili kiujumla bali kinachotakiwa na kulirejesha katika uwiano ambao ni kati ya kuzidisha na kupoteza.
Na kinachotakiwa katika sifa ya hasira ni kujilinda vyema kwa njia ambayo mtu aepukane na uzembe pamoja na woga, ajiepushe na vyote viwili. Kwa ujumla, awe na nguvu katika nafsi yake, na kwa nguvu zake hizo afuate akili. Na kwa ajili hii, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Wana nguvu mbele ya makafiri na wanahurumiana wao kwa wao}, na akawasifu kuwa na nguvu kwani nguvu hutokana na hasira, na kama hasira isingekuwa na maana yoyote basi jihadi nayo ingekosa maana. Iweje pakusudiwe kujiepusha na hasira pamoja na matamanio kwa ujumla! Wakati ambapo Mitume S.A.W. hawakuachana na sifa hizi mbili, na Mtume S.A.W. amesema: "Hakika mimi ni binadamu ninakasirika kama wanavyokasirika watu wengine".
Na alikuwa, pindi anapoyazungumzia yanayomkera hukasirika hadi sehemu za juu za mashavu yake zinakuwa na rangi nyekundu, lakini hasemi isipokuwa ukweli. Akawa S.A.W ghadhabu yake haimpelekei kuacha ukweli. Na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu {na wanajizuia na ghadhabu na ni wasamehevu kwa watu}, na wala hajasema waliokosa ghadhabu, kwa hivyo jibu la ghadhabu na matamanio linapaswa kuwa la wastani kwa namna ambayo si moja kati ya mawili haya huishinda akili, bali akili inakuwa ndio mdhibiti mkuu wa hasira na matamanio na ikaweza kuyashinda, na ndio maana hasa ya kugeuza tabia, kwani mwanadamu huenda akazidiwa na matamanio kwa namna ambayo inamfanya kutokuwa na akili yenye nguvu kwa ajili ya kuondosha matamanio hayo, na hivyo kujikuta kuwa anatumbukia katika maovu kiurahisi. Na kwa mazoezi hurejea matamanio hayo katika hali ya uwastani, na imeoneshwa kuwa jambo hili linawezekana.
Jaribio pamoja na ushuhudiaji ni dalili tosha ya jambo hili na kinachothibitisha hivyo ni kuwa kinachotakiwa ni uwastani wa maadili bila ya kumili zaidi upande mmoja kati ya pande mbili na kwamba utoaji ni moja kati ya tabia njema kisheria nayo ni uwastani baina ya ubadhirifu na ugumu wa kutoa.
Na Mwenyezi Mungu mtukufu ameilielezea jambo hili katika kauli yake aliposema; {na wale ambao wanapotoa mali zao hawafanyi ubadhirifu wala ubahili na wanakuwa baina ya hayo}, na anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {wala usiufanye mkono wako kama uliofungwa shingoni mwako wala usiukunjue wote kabisa…}, na vile vile kinachotakiwa katika matamanio ya chakula ni kuwepo uwastani bila ya kuzidisha au kupunguza mno, anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu {na kuleni na kunyweni na wala msifanye israfu kwani Mwenyezi Mungu hawapendi wabadhirifu}, na anasema Mwenyezi Mungu kuhusu hasira: {wana nguvu mbele ya makafiri na wanahurumiana wao kwa wao}, na Mtume S.A.W anasema: "Ubora wa mambo ni uwastani wake".
Na hii ni siri na maafanikio, nayo ni kuwa furaha inatokana na moyo kusalimika na mambo ya dunia hii. Anasema Mwenyezi Mungu mtukufu: {Isipokuwa Yule atakaemwendea Mwenyezi Mungu kwa moyo uliosalimika} na ubahili ni miongoni mwa mambo ya dunia hii, na ubadhirifu pia ni miongoni mwa mambo ya dunia, Moyo ili usalimike ni sharti ujiepushe na vyote viwili, kwa maana kuwa moyo usiangalie mali na wala usiwe na shime ya kuitumia mali hiyo au kuikama, kwani mtu mwenye shime ya kuitumia mali moyo wake huvutiwa na matumizi na na mtu mwenye kujizuia na ukamataji wa mali moyo wake huvutiwa na hali hiyo ya kujizuia na kwa hivyo ukamilifu wa moyo hupatikana kwa kujizuia na viwili hivyo vyote.
Na kama hali hiyo haikuwa duniani basi tutataka kile kinachofanana zaidi na kutokuwepo kwa sifa hizi mbili, na mbali na pande hizi mbili, nacho ni hali ya wastani kwani kilicho na uvuguvugu si cha moto wala si cha baridi bali ni kati ya hali hizi mbili na ni kama vile kitu hicho hakina sifa hizo mbili. Na pia utoaji mzuri ni ule ulio kati ya ubadhirifu na ubahili. Na ushujaa ni kati ya woga na ushambuliaji. Na kutosheka ni kati ya kujiaachia sana na kujibana sana.
Na hivyo ndivyo ilivyo kwa maadili mengine yote, kwani pande zote mbili za mambo si nzuri, na hili ndilo linalotakiwa na linawezekana. Ndio, ni wajibu kwa shekhe kiongozi kwa anaemwongoza achukizwe na hasira kuanzia ngazi za juu, na akemee uzuiaji wa mali kuanzia ngazi za juu na wala asimruhusu kufanya chochote katika hivyo. Kwani shekhe kiongozi akiruhusu kufanyika kitu kidogo tu basi mtu huyo atakitumia kama kisingizio cha kuuendeleza ubahili na hasira zake na hata akadhani kuwa hicho ni kiasi kilichoruhusiwa.
Na iwapo atakusudia asili ya jambo hili na kisha akalizidisha na ikawa hakuna wepesi kwake isipokuwa kuondosha uzio wake kwa namna ambayo itamrejesha katika uwastani, kwahivyo kilicho sahihi hapa kwake ni kuwa akusudie kuachana na asili ya jambo hilo ili pawepo na wepesi katika kiwango kinachokusudiwa haifichui siri hii kwa mwongozwaji kwani mtu huyo yuko katika mazingira ya kudanganyika kwa walio na upumbavu kwani anadhani katika nafsi yake kuwa hasira zake ni haki yake na kujizuia nayo ni haki yake pia)).
1. Chanzo: Alraaghibu Al-asfahaaniy, Adhariy’a Ilaa Makaarim Shariy’a. Prof/Dkt Abulyaziid Al-ajamiy, (Uk wa 113-116).
2. Prof/Dkt Muhamad Dhiyaau Din Alkurdiy, Al-akhlaaqu Islaamiyya Waswuwfiyya, Cairo: Mat Alsaada, mwaka wa 1989/1409, (uk: 22-23).
3. Alghazaliy, Ihyaau Uluumi Din. T. Alhalabiy, (uk:252-256).