Mfumo wa maadili ya Kiislamu -sifa ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mfumo wa maadili ya Kiislamu -sifa zake

Question

Ni zipi sifa maalumu za mfumo wa maadili katika Uislamu?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Mfumo wa Kiislamu wa maadili una sifa maalumu kadhaa ambazo muhimu kati ya hizo ni kama ifuatavyo: Maumbile- Ukamilifu- Uimara-Ukweli-Ujumuishaji.

Tuzizungumzie sifa Moja baada ya nyingine, kwa ufafanuzi zaidi kama ifuatavyo:
1) Sifa ya Maumbile: Miongoni mwa sifa za Mfumo wa Kielimu wa Kiislamu ni kuwa unamsemesha binadamu kwa lugha anayoifahamu bila tabu yoyote, na kwa muonjo maalumu unaomjenga kimawazo bila ya kuwepo uzito wowote, na fikra anayoizingatia bila ugumu wowote wa kueleweka kwa fikra hiyo, na mambo ya ukweli ambayo moyo hufunulika kwayo bila ya uzito, na maana ambazo huingia moyoni mwake bila ya kuzikana. Na huwenda baadhi ya watu wakajiuliza, iwapo jambo hili lina uyakini kwa kiasi hiki, kwa nini basi watu wengi wanazikadhibisha aya hizi na dalili zake, na wanazikwepa, ingawa zote ni ukweli ulio wazi? Wanazungumza maneno batili na porojo wakiwa kati ya mwenye kutia shaka na mkanushaji?

Hakika swali hili ndani yake linabeba swali jingine kuhusu maumbile ya mwanadamu, kwanini mtu anakwenda kinyume na maumbile hata kama kinachohusika ni cha kweli na lazima kifuatwe? Na kwa nini mtu anapingana na kanuni ya Mwenyezi Mungu ingawa kanuni hiyo inakwenda sambamba na maumbile ya mwanadamu na inaleta kheri iliyo bora? Na kwa nini huwa daima hata kwa yule anaeuamini Mfumo wa Kiislamu kuna pengo –huwa linapungua na kupanuka- kati ya elimu na kazi, na kati ya fikra ya nadharia na mwenendo wa kiutendaji, na kati ya sheria na ukweli? Na ikiwa Dini ya Kimaadili ni ya kimaumbile kwa watu wote kwanini mwanadamu anakwenda kinyume nayo na kujidhulumu yeye mwenyewe? Na kwa nini hafuati maumbile aliyopewa na Mwenyezi Mungu?

2) Hakika mtu mwenye kuzingatia Aya za Mwenyezi Mungu Mtukufu anapata jibu la wazi lisilojificha juu ya swali hili, na kama alivyosema Mwenyezi Mungu kwa kauli ya Mtume wetu Ibrahimu A.S. {Isipokuwa yule ambaye ameniumba hakika yeye ndiye atakayeniongoza} [AZ ZUKHRUF: 27], kwa hivyo basi, pamoja na kuwepo kwa maumbile ya kibinaadamu, kukwepa au kuwajibika nayo huja kutokana na tofauti za watu katika Uongofu na Upotofu, Uchamungu na Uasi, Ikhlasi na Shirki, Utiifu na Uasi, katika nafsi na nguvu yake ya matamanio, na moyo na nguvu yake ya Mola, na nafsi ya binadamu huhimiza uasi kama ifanyavyo katika uchamungu {Na kwa nafsi na kwa aliyeitengeneza! Kisha akaifahamisha uovu wake na wema wake} [ASHAMS:7-8]

3) Kwa hivyo kuna hali ya kimaumbile iliyokamilika ndani ya mwanadamu isipokuwa pale atakapofuata miumbiko ya nafsi basi udhaifu wa kibinadamu humlemea, na pia hutawaliwa na matamanio yake, na kasahau kabisa na kughafilika kuhusu jambo la Mwenyezi Mungu na akatii udanganyifu wa akili yake na kufuata upotofu ya shetani. Na ikiwa atapambana na nafsi yake pamoja na shetani basi atanyooka na kuwa katika njia ya haki na rehma ya Mwenyezi Mungu pamoja na kuongozwa mpaka kufikia hali yake ya kimaumbile iliyosalimika.

4) Kwahivyo mwanadamu daima huhitaji jihadi katika kutafuta elimu na kufanya mema na kuzingatia ndani ya nafsi yake, na katika Uumbaji na Ulimwengu wote kwa ujumla ili viende sambamba na hali ya maumbile yake, na aongoke kuelekea katika njia iliyonyooka na uadilifu. Anasema Mwenyezi Mungu {Na wanaofanya juhudi kwa ajili yetu, Sisi tutawaongoa kwenye njia zetu. Na hakika Mwenyezi Mungu yu pamoja na watu wema} [AL ANKABUUT: 69]

5) Pili: Ukamilifu: hakika Mfumo wa Kiislamu ambao Misingi yake inatokana na Quraani Tukufu na Sunna ya Mtume, ndio mwongozo ulio bora zaidi kuliko yote, ambao unaweza kuchaguliwa na mwanadamu katika dunia hii, kwa sababu una sifa ya kipekee ya ukamilifu katika kila kitu. Mtu yoyote anayeuzingatia kwa makini hawezi kamwe kukuta aina yoyote ya mkanganyo ndani yake au aina yoyote ya upungufu au kwenda mrama kama tunavyokuta katika mifumo mingine ya kibinadamu {Hakika wale mnaowaomba badala ya Mwenyezi Mungu, hawatoumba hata nzi ijapokuwa watajumuika kwa hilo} [AL HAJI: 73]

6) Na miongoni mwa Ukamilifu wa Mfumo wa Kiislamu ni kwamba haumuachi mtu peke yake bila ya kumsaidia, akawa anachelea kuharibikiwa huku akishikwa na butwaa, na wala haufuati mfumo huu hali ya kuwa amekata tamaa na amezongwa na shaka shaka, akiwa hana hamu ya kuendelea kwa kuzingirwa na mawazo potofu, isipokuwa muumini wa mfumo huu wa Kiislamu humtegemea Mwenyezi Mungu mmoja anaetegemewa na kuwa ndio matumaini yake na ndilo lengo lake, na huwa na hisia zenye nguvu kuwa hakika Mwenyezi Mungu Mtukufu yu pamoja naye na ndiye anayemsaidia na kumpa utulivu moyoni mwake, huku akiamini kauli ya Mwenyezi Mungu isemayo: {Na Sisi tuko karibu naye kuliko mshipa wa shingoni mwake} [QAAF: 16], na kuwa yeye Mwenyezi Mungu Mtukufu kamwe hatamwacha peke yake katika dunia hii bila ya huruma, akipotea bila mwongozo, mnyonge asiye na msaidizi, na kwamba kila pale anapokosea basi Mwenyezi Mungu humuongoza, na kila anapojikwaa humsimamisha, na kila anapoghafilika humzindua. Anasema Mwenyezi Mungu: {Kwani hakukukuta yatima akakupa makaazi? Na akakukuta umepotea akakuongoa? Akakukuta mhitaji akakutosheleza?} [AD DUHA: 6-8]

7) Hakika ukamilifu unaoletwa na Imani kwa kufuata mfumo wa Mwenyezi Mungu hauwezi kuletwa na mfumo wowote mwingine miongoni mwa mifumo ya kibinadamu iliyoandaliwa na binadamu kwa namna yoyote ile ambayo mfumo huu utampa picha mwanadamu kuwa ni mfumo wenye lengo la uadilifu na haki, na hii inatokana na kwamba mengi miongoni mwa yaliyomo ndani ya mifumo ambayo imetengenezwa na binadamu huenda kinyume na yale ambayo ni ya kweli kiungu, kwani mfumo huo wa kibinadamu haufuati hekima ya Mwenyezi Mungu isiyo na kifani {Ishara yoyote tunayoifuta au tunayo isahaulisha tunailetea iliyo bora kuliko hiyo, au iliyo mfano wake. Hujui kwamba Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu?}[AL BAQARAH: 106].

8) Hakika Ukamilifu katika Mfumo wa Mwenyezi Mungu wa uundaji sheria unambebea mwanadamu utukufu iwapo mwanadamu huyo atafuata njia iliyonyooka, uadilifu, utendaji wa haki na ukweli. Na ukamilifu huu unakwenda kwa mfumo wa wastani wenye uadilfu na ambao hauna ubadhirifu ndani yake, wala hauna israfu wala ukiukaji, isipokuwa ni heri yenye ubora ambao huonesha ubora na ukweli katika kila kitu. Kwa hivyo ukamilifu unaokusudiwa hapa ni kufuata mfumo wa wastani katika kila kitu ambao ni njia iliyonyooka. Kama ulivyo ulimwengu huu unafuata wastani, kwa hivyo umma wa Kiislamu pia ni Umma wa Mfumo wa wastani. Na tuliwahi kuzungumzia Mfumo wa wastani katika maudhui maalumu isemayo (Mfumo wa wastani kwa mtazamo wa Maadili ya Kiislamu). Kwa hivyo, Mfumo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu na Sheria yake ni ujumbe uliokamilika na kutimia. {Leo nimekukamilishieni dini yenu, na nimekutimizieni neema yangu, na nimekupendeleeni UISLAMU uwe ndiyo dini} [AL MAIDAH: 3]

9) Tatu: Miongoni mwa sifa maalumu za Mfumo wa Kiislamu wa Maadili ni Kutotetereka: Hakika mifumo mingine yote iliyoundwa na binadamu hukumbwa na tatizo la kuyumbishwa. Ni sawa mifumo hiyo iwe Madhehebu ya Kiakili, Kiroho, Kihisia au hata kimajaribio, huwa hauwezi kutulia na hujikuta ukikumbwa na kudhihiri kwa nadharia mpya kila baada ya kipindi fulani, nadharia ambazo huzivunja hoja zake na kubainisha uchache wa ukweli wake na baadhi ya wanachuoni hutoa nadharia mpya zinazoivunja mifumo ya zamani na kufuta misingi yake. Na mwanadamu, mbele ya adui huyu wa kushangaza, anahitaji maana na fikra mpya zinazokinzana na za zamani na zilizo tofauti, jambo ambalo humzibia njia mbele yake, akawa haelewi ni yepi kati ya madhehebu haya ayafuate, na mpaka akaishia kuwa na msimamo wa kuyakataa baada ya kutafiti kwa kina, na akawa anayatilia shaka yote kwa ujumla na huwenda akafuata matamanio ya akili yake na kujikuta anakanusha kila kitu. Na iwapo Mwenyezi Mungu atamwongoza aelekee katika kuuzingatia mfumo wake na akabahatika kupata neema ya kumwamini na akamfanya Mtume S.A.W kuwa ndiye kiongozi na mfano wake wa kuuiga, basi atakuwa ameiokoa nafsi yake, na moyo wake utakuwa umetulizana katika haki na atasalimika na shari za upotofu wa njia iliyonyooka {Walio muitikia Mola wao Mlezi watapata wema} [AR RAD: 18].

10) Na pale mwanadamu anapokuwa na uhakika na yakini kwa namna ya kimaumbile isiyo na kasoro, kuwa njia ya Mwenyezi Mungu ndio njia ya kweli basi hakika mtu huyu humfungamanisha Mwenyezi Mungu na moyo wake. Kwa hivyo basi, mtu huyu halitilii shaka jambo lolote la Mwenyezi Mungu na wala hasiti katika njia yake, kwani njia hufunguliwa mbele yake kama alivyoahidi Mwenyezi Mungu {Enyi mlio amini! Mkimnusuru Mwenyezi Mungu naye atakunusuruni na ataithibitisha miguu yenu} [MUHAMAD: 7]. Kwa hivyo mtu ambaye anashikamana na mfumo wa Kiislamu wa Maadili huongozwa njia ya elimu sahihi, na huthibitisha kwa kauli isiyoterereka, na Mwenyezi Mungu humpa utulivu wa ndani ya moyo na mwelekezo wa kimalaika. Mtu huyu kamwe hawezi kuikosa njia ya amani na usalama {Mwenyezi Mungu huwatia imara wenye kuamini kwa kauli ya imara katika maisha ya dunia na katika akhera} [IBRAHIM: 27]

11) Na Mfumo wa Kiislamu ni imara kwa mambo yake ya kweli ambapo muumini hupata nafasi ya kupanda vyeo, na siku hadi siku elimu yake, maaarifa na uyakinifu huongezeka. Na Mwenyezi Mungu hamwangushi na hamwachi kabisa ikiwa tu mtu huyu atadumisha njia yake ya kumpwekesha Mwenyezi Mungu na Imani {Mwenyezi Mungu atawainua walioamini miongoni mwenu, na waliopewa elimu daraja za juu. Na Mwenyezi Mungu anazo khabari za mnayoyatenda} [AL MUJADALAH: 11]

12) Na huu ndio mwendo wa Mwenyezi Mungu kwa watu wote na wala haubadiliki, kwani mwendo wake Mwenyezi Mungu Mtukufu haubadiliki wala haugeuziki, kwani namna ulivyo ni imara na wala hauyumbi kamwe. {Hebu hawangojei yaliowasibu watu wa kale? Basi hutapata mabadiliko katika mtindo wa Mwenyezi Mungu. Wala hutapata mageuko katika mwendo wa Mwenyezi Mungu} [FAATWIR: 43] {Huo ndio mwendo kwa Mitume tuliowatuma kabla yako. Wala hupati mabadiliko katika mwendo wetu} [AL ISRAA: 77]

13) Nne: Na miongoni mwa sifa maalumu za Mfumo wa Kiislamu wa Maadili ni: Ukweli: Hakika Ukweli wa Mfumo huu wa Kiislamu katika kutibu nafsi ya binadamu namna ulivyo, hutokana na kuwa kwetu na yakini kwa kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu {Na ni nani msema kweli kuliko Mwenyezi Mungu?} [AN NISAA: 87] {Na nani mkweli zaidi kwa usemi kuliko Mwenyezi Mungu} [AN NISAA: 122]. Na Mwenyezi Mungu amejaalia miongoni mwa alama za usahihi wa mfumo wa Kiislamu ni kuwa kwake kweli na kwenda kwake sambamba na Sheria za Mwenyezi Mungu za kabla ya Uislamu {Na tumekuteremshia wewe, kwa haki, kitabu hiki kinachosadikisha yaliyokuwa kabla yake katika Vitabu na kuyalinda} [AL MAIDAH: 48] Naye Mwenyezi Mungu ndiye aliyetuumba na ndiye mjuzi zaidi wa yanayozifaa nafsi zetu na yasiyozifaa. Kwa upande wa ukweli unaopigiwa kelele na mifumo ya kutengenezwa na mwanadamu huwa tunayagundua makosa yake haraka mno. Kinachothibitishwa kuwa kweli leo na watafiti, hudhihirika kesho uongo wake na kutokwenda sambasamba na uhalisi wa hali. Ingawa mfumo wa majaribio unafaa kwa ajili ya kuufikia ukweli wa maumbile ya kitu na namna njia yake inavyofunikwa na giza kwa kufanyika majaribio na kutumia vipimo na matokeo yake na mfano wa vyombo kama hivyo na njia mbali mbali za kisayansi ambazo husaidia kufichua na kufanya tafiti na kudurusu, hakika mwanadamu sio kile kitu ambacho hakina uhai na ambacho kinafaa kufanyiwa aina hii ya utafiti, na iwapo mfumo huu utafanikiwa kudadisi hali halisi basi hakika ni kuwa hautaweza kupendekeza fumbuzi sahihi za kutibu nafsi ya mwanadamu, na kwa ajili hii fumbuzi za kuundwa kwa ajili ya kutibu mwenendo wa binadamu, huyathibitisha makosa yake haraka sana, na huthibitisha pia kutokuwa na uwezo wa kubadilisha mwenendo mbovu wa mwanadamu. Na kama sisi tunalazimika kunufaika na mifumo ya kisasa na uwezo wake wa kudadisi uhalisia wa hali, mabadiliko na matatizo, basi chanzo cha ufumbuzi sahihi hakitapatikaia isipokuwa kwenye Mfumo wa Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa ajili ya kuitibu nafsi ya mwanadamu. Mfumo ambao unatoa asili yake inatokana na Sheria ya kweli ambayo Mwenyezi Mungu ameitengeneza {Yeye ndiye ajuaye Siri na kilichojificha} [AT TAWBAH 7], na yeye Mwenyezi Mungu anaangalia yaliyojificha kwenye nafsi ya Mwanadamu, {Na hakika Mola wako anayajua yale yaliyofichikana katika vifua vyao na yale wanayoyadhihirisha} [AN NAML: 74] {Anayajua yaliyofichikana machoni na yafichwayo vifuani} [GHAAFIR: 19]. Na kwa ajili hii, hakika tamko la Mwenyezi Mungu la kweli ndilo chanzo pekee chenye furaha ya mwanadamu na tiba ya matatizo yake. {Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu. Hapana awezaye kuyabadilisha maneno yake. Na Yeye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua.} [AAL ANAAM: 115]
14) Na miongoni mwa matokeo ya ukweli wa Mfumo wa Kiislamu ni kuwataka daima wale wote wanaoufanyia kazi kuwa wakweli kila wakati. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu {Amesema Mwenyezi Mungu siku hii ukweli ndio utakaowasaidia wasema kweli} [AL MAIDAH: 119]

15) Na utaratibu wa Kiislamu wa Kimaadili –katika mfumo wake –daima hutaka muumini wa kweli kukimbilia ukweli katika dogo na kubwa miongoni mwa mambo ya maisha. {Na sema: Mola wangu Mlezi! Niingize muingizo mwema, na unitoe kutoka kwema. Na unipe nguvu zinazotoka kwako zinisaidie} [AL ISRAA: 80]. Na Mwenyezi Mungu anatunabahisha kuwa sisi tunabeba jukumu la ukweli huu. {Ili awaulize wakweli kutokana na ukweli wao} [AL AHZAAB: 8]. Ikiwa mkweli ataulizwa kutokana na ukweli wake, sembuse sisi tusiokuwa wakweli! Ukweli ni jambo la lazima lililo wajibu hata pamoja na utiifu kwa Mwenyezi Mungu na utendaji wema. {Utiifu na kauli njema. Na jambo likishaazimiwa, basi wakiwa ni wakweli kwa Mwenyezi Mungu, bila ya shaka itakuwa ni kheri kwao} [MUHAMAD: 21]

16) Kwa hivyo ukweli ni wa Mwenyezi Mungu katika Mfumo, Utunzi wa Sheria na Hukumu, na kutokana na Mfumo huu, ni wajibu kwa wale wote wenye kubeba majukumu kisheria waufuate katika kila jambo lao. Na ukweli kwa upande wa kiakili unamaanisha uadilifu, na uadilifu ni msingi wa uelewa. Na ukweli kwa upande wa Maadili una maana Kweli na Hakika kwa hivyo, Ukweli huu unakuwa na sura kamili kwa mwenye elimu kwa upande wa kiakili na kimwenendo, au kwa upande wa Kielimu na Kiutendaji, au kwa upande wa Dhati na Maudhui. Kwani ukweli katika mweleweko wa Kiislamu ni picha ya maarifa iliyoboreka na ambayo huanzia katika ukweli na kuishia katika ukweli huo.

17) Hakika ukweli una nguzo zake ambazo ni tatu: 1– Mifano ya Juu. 2– Ujuzi wa Siri. 3– Upevu wa kuona. Kwani kila mtu anatofautiana na mtu mwingine kimielekeo na maandalizi yake, na hivyo kutofautiana katika bahati yake ya Mfano wa Juu, na Mkweli zaidi katika watu ndiye anayeweza kuzingatia zaidi Mifano hii ya Juu. Na kuizingatia Mifano hii humsaidia mtu katika mazuri yaliyo bora na kumfanya awe na tabia nzuri, na kilele cha Mifano hii ya Juu ni Majina Matukufu ya Mwenyezi Mungu Mtukufu, ambayo sisi tunapaswa kujipamba kwayo kitabia – kwa yale ambayo inajuzu kwetu sisi kujipamba kwayo kama vile Upole, Uadilifu, Wema, Ukweli… -au kumuamini Mwenyezi Mungu kwa sifa hizi kama vile –Utenzaji nguvu, na Utukufu- kwa hivyo, kuifanyia kazi mifano ya juu iliyopo katika majina ya Mwenyezi Mungu Mtukufu na kuyafanya kuwa kigezo kwa mwanadamu kitabia na kwa Kiimani humletea maisha ya utulivu wa moyo, na humpatia tabia za kijamii zilizo bora.

18) Na nguzo ya pili miongoni mwa nguzo za Ukweli wa Mfumo wa Kiislamu wa Maadili ni kuwa: Umejengeka kwa Ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kuwa kwetu na yakini kuwa huo ni Ulimwengu wa Siri ambazo zipo chini ya Hekima ya Juu ya Mwenyezi Mungu. {Na yametimia maneno ya Mola Mlezi wako kwa kweli na uadilifu.} [AL ANAAM: 115] {Sema Mwenyezi Mungu amesema kweli} [AALI IMRAAN: 95], kwa hivyo basi, Ukweli wa Mfumo wa Kiislamu wa Maadili unajengeka kwa kumwamini Mwenyezi Mungu Mtukufu ambaye anajua siri zote na yaliyofichikana, na anayajua yaliyojificha vifuani na yaliyotulizana katika nafsi za watu, naye Mwenyezi Mungu ni mjuzi wa yasiyoonekana na yanayoonekana.

19) Msingi wa tatu miongoni mwa misingi ya Ukweli wa Mfumo Kiislamu wa maadili: Upevu wa kuona moyoni. Ni upevu ambao Mwenyezi Mungu humpa mja wake ambaye ameikamilisha misingi miwili ya mwanzo miongoni mwa misingi ya ukweli: Mifano ya Juu na Uyakini kwa namna ambayo yeye Mwenyezi Mungu amempa siri miongoni mwa siri zake zilizomo katika Hekima na Sheria yake. Na upevu huu kwa maana hii ni tunu ambayo mtu anayeutumia Mfumo huu wa Kiislamu hubahatika kuwa nayo na hupatikana kutokana nao. Kwa hivyo basi, humpa kina cha Uzingatiaji katika mambo ya ulimwengu kwa upande mmoja, na katika Imani na Uyakini wa kumwamini Mwenyezi Mungu, Elimu yake na kutokuonekana kwake, na kila pale mwanadamu anapofanikiwa kuwa na Ukweli zaidi pamoja na kuwa kwake upande wa Mwenyezi Mungu, basi Upevu wake wa kuona moyoni mwake nao pia huongezeka.

20) Na miongoni mwa sifa za Mfumo wa Maadili wa Kiislamu ni Ujumuishaji wake na Ueneaji:
Mfumo wa Kiislamu unasifika kipekee kwa kuwa na misingi yenye sifa ya Ujumuishaji wa kila kitu kilichopo katika Ulimwengu huu. Na hii ni moja tu kati ya sifa za kipekee za Mfumo huu wa Kiislamu {Na kwamba Mwenyezi Mungu amevizunguka vitu vyote kwa elimu yake} [TWALAAQ: 12]. Kwa hivyo Mfumo wa Quraani Tukufu unafungamanisha kati ya Mafunzo ya Kimaadili na Mfumo wa ulimwengu, kwa hivyo Uislamu unalingania kuwa na Msimamo (katika Dini) na kufuata kheri wakati ambapo Aya za Quraani zinaashiria Ubora wa Uumbaji wa mbingu na Ardhi, na yale yaliyodhalilishwa kwa ajili ya mwanadamu kama vile mito, bahari, wanyama, majabali n.k, na hufungamanisha vyote hivi na nasaha pamoja na mazingatio, na kwa ajili hii Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Sema: Tembeeni ulimwenguni, kisha mtazame ulikuwaje mwisho wa wanaokanusha. Sema: Ni vya nani viliomo katika mbingu na katika ardhi? Sema: Ni vya Mwenyezi Mungu. Yeye amejilazimisha nafsi yake kurehemu. Hakika atakukusanyeni Siku ya Kiyama isiyo kuwa na shaka.Waliojitia hasara wenyewe hawaamini. Na ni vyake viliotulia usiku na mchana. Naye ndiye Mwenye kusikia na Mwenye kujua} [AL ANAAM: 11-13]. Na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na mwanaadamu huomba shari kama vile aombavyo kheri, kwani mwanaadamu ni mwenye pupa. Na tumefanya usiku na mchana kuwa ishara mbili.Tena tukaifuta ishara ya usiku, na tukaifanya ishara ya mchana ni yenye mwangaza ili mtafute fadhila itokayo kwa Mola wenu Mlezi, na mpate kujua idadi ya miaka na hisabu. Na kila kitu tumekifafanua waziwazi. Na kila mtu tumemfungia matendo yake shingoni mwake. Na Siku ya Kiyama tutamtolea kitabu atakachokikuta kiwazi kimekunjuliwa} [AL ISRAA 11-13] na Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na Ufalme wa mbingu na ardhi ni wa Mwenyezi Mungu; na Mwenyezi Mungu ni Mwenye uwezo juu ya kila kitu. Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi na kukhitalifiana usiku na mchana ziko ishara kwa wenye akili, Ambao humkumbuka Mwenyezi Mungu wakiwa wima na wakikaa kitako na wakilala, na hufikiri kuumbwa mbingu na ardhi, wakisema: Mola wetu Mlezi! Hukuviumba hivi bure. Subhanaka, Umetakasika! Basi tukinge na adhabu ya Moto} [AALI IMRAAN: 189-191]

21) Kwa hivyo Quraani Tukufu hutibu zaidi ya maudhui moja kwa wakati mmoja bila ya kuchanganyika maana huku njia zake zikiwa tofauti, ukweli ni kuwa maudhui zake huunganishwa kwa mjengeko uliowekwa kwa njia ya Muujiza katika mtindo wa Ujumuishaji Mkuu, {Hiki ni Kitabu ambacho Aya zake zimewekwa wazi, kisha zikapambanuliwa, kilichotoka kwa Mwenye Hekima na Mwenye Khabari} [HUD: 1]

22) Na maneno ya Mwenyezi Mungu kwa waja wake ni Muujiza ulio katika mtindo wake wa kipekee kwa balagha na maana zake, mpaka unamfanya kila anaesoma maneno ya Mwenyezi Mungu au kuyasikia, ahisi kana kwamba maneno hayo anaambiwa yeye peke yake, ingawa watu wametofautiana kitamaduni, kimila na desturi na kitabia, na Muumini huhisi kweli kuwa aya za Mwenyezi Mungu zilizo wazi kwa hakika zinakwenda sambamba na mambo nyeti ya maisha yake ya kila siku na uhalisia wake uliopo. Na ndani ya maneno hayo, daima huwa kuna dawa inayotibu magonjwa yake yote na kukijaza kifua chake kwa utulivu, amani na matumaini. {Sema: Hii Quraani ni uwongofu na dawa kwa wenye kuamini. Na wasioamini umo uziwi katika masikio yao, nayo kwao imezibwa hawaioni. Hao wanaitwa kutoka sehemu iliyo mbali} [FUSWILAT: 44]

23) Ujumuishaji na Ueneaji katika mfumo wa Kiislamu ni moja kati ya sifa maalumu za mfumo huu, kwa kuwa watu wanatofautiana kimaandalizi na kinyenzo, mazingira na uungwana wao, na mabadiliko ya fikra na mielekeo yao, kwa hivyo mfumo huu wa Kiislamu kwa kujumuisha na kuenea kwake, una uwezo wa kuwasemesha watu wote kwa namna ambayo inawakinaisha wote sawa sawa, wawe watu wa kawaida au wabora wao, wawe wasomi wao au wasio wasomi, wateule wao na wanafikira na wanafalsafa wao. Na kwa sababu hii, usemeshaji wa Quraani husemesha nguvu za nyenzo za mwanadamu kwa ngazi zake zote, kwa hivyo basi, huvisemesha viungo vya hisia na huisemesha akili, na huusemesha undani wa mtu pamoja na moyo na roho. Kwa hivyo basi, usemeshaji wa Quraani ndio pekee unaofaa kwa kundi fulani la watu kama ni tiba na dawa na huwafaa wengine kwa ajili ya kuongeza elimu huku ukiwafaa wengine kwa ajili ya muelekezo na mwongozo. Kwa hivyo basi, kila usemeshaji wa Quraani kutoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hufaa sehemu zote, na watu wote huyafahamu maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu kwa kutegemea kiwango cha uwezo wao. Na maneno yote yanayotoka kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yana hekima kubwa ndani yake kwa ajili ya watu wote bila ya ubadhirifu au upunguzaji wowote, hakika mambo yalivyo ni kuwa kufikisha kwake kwa kauli na kwa maana kunalenga upeo wenye hekima na kusudio lenye uadilifu na lenye kufaa kwa nyakati na zama zote.

24) Kwa hivyo basi, watu wote wanaweza kuuona uzuri wa viumbe vya Mwenyezi Mungu Mtukufu katika ulimwengu wake, na vile alivyovipambia Mbingu na vile alivyoviotesha ardhini, na mwenye elimu miongoni mwao huwa anafikiria kwa mazingatio. Dalili zote hizo za ulimwengu kwa kuangalia hekima ya hali ya juu iliyomo ndani yake. Na iwapo tutatoka kwenye hisia na kuhamia katika akili na tukatoka katika kujihisi na kuelekea katika mazingatio, tunakuta kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu anamsemesha wale waliozama na kubobea katika elimu na ambao wamekusanya kati ya nyenzo za utambuzi wa kihisia na uzingativu wa kiakili na muonjo wa undani wa moyoni. {Tutawaonyesha Ishara zetu katika upeo wa mbali na katika nafsi zao wenyewe mpaka iwabainikie kwamba kweli. Je! Haikutoshi kwamba Mola wako Mlezi kuwa Yeye ni Shahidi wa kila kitu?} [FUSWILAT: 53]

25) Kwa hivyo Mwenyezi Mungu Mtukufu kama inavyoonekana kwa maelezo yaliyokwishatangulia, anamsemesha kila mtu kwa njia inayomfaa mtu huyo, na kwa mfumo wa Kiislamu na kwa njia hii iliyo ya wazi yenye mfumo uliokamilika ambao hautuami katika upande mmoja tu ulimwenguni au katika maumbile kama ifanyavyo mifumo mingine ya kibinadamu iliyobuniwa na yenye muono mfupi.

Marejeo: Prof/Dkt Hassan Sharkawiy, Al-Akhlaqu Islaamiya, Kairo: Taasisi ya Mukhtaar ya Uchapishaji na Usambazaji, toleo la 1, 1988, (Uk 87-109).

 

Share this:

Related Fatwas