Misingi ya Kutendeana na Quraani Tu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Misingi ya Kutendeana na Quraani Tukufu

Question

Ni ipi misingi ambayo sisi tunapaswa kuitumia tunapotendeana na Quraani tukufu?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Mwislamu katika mambo yake ya kijamii au kibinadamu anahitaji uongozi wa Quraani Tukufu na maelekezo yake, kwa hiyo Mwislamu lazima aamini kuwa Quraani Tukufu ni Kitabu kilichoteremshwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu ambacho kinakusanya ndani yake uongofu; “Kitabu cha Hidaya”. Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Kwa (kitabu) hicho Mwenyezi Mungu huwaongoza wenye kufuata radhi Yake katika njia za salama, na huwatoa katika kiza kuwapeleka katika nuru kwa amri Yake, na huwaongoza katika njia iliyonyooka}[AL MAIDAH, 16]. Kutokana na hayo; Mwislamu analazimika kushikamana na maelekezo yafuatayo:

Kwanza: Quraani Tukufu ni kitabu cha uongofu, na hii inamaanisha mambo mawili;
La kwanza: Quraani Tukufu inatoa uongofu hasa katika masuala yenye kutofautiana na maoni ya hitilafu, kwa hiyo Mwislamu anaikabidhi akili yake kwa Quraani Tukufu ili akili hiyo ifuate misingi na njia iliyonyooka ya Quraani Tukufu.

La pili: kitabu hiki cha Quraani si kitabu cha taarifa, hata zikiwa taarifa nyingi sana zinapatikana ndani yake kwani kitabu hicho kimsingi hakikuteremka kiwe kitabu cha elimu za Kemia na Fizikia n.k. aidha hakikuteremka kiwe kitabu cha elimu za kisiasa, kijamii au kiuchumi n.k. ingawa misingi ya elimu hizo zote zinapatikana ndani ya Aya zake hata zikiwa na ufupisho ila Aya hizo zina mjumuisho wa maana nyingi katika maneno machache.

Quraani Tukufu ni kitabu cha uongofu kwani kinatoa mfumo kamili (jumuishi) wa vipengele vya kufikiria kwa upande wa elimu kwa akili ya mwenye kuokoka na uongofu ili atambue kila anachojifunza na kuweza kutoa hukumu juu yake.

Mwislamu kama hahitalifiani na Sigmund Frued mtaalamu wa saikolojia katika suala la kutambua hali halisi kwa nafsi ya mtu inayosumbuliwa na uchusa, kukata tamaa na matatizo ya kisaikolojia, lakini mtafiti Mwislamu anaweza kuhitalifiana naye katika suala la hukumu jumuishi; yaani kuziangalia nafsi zote kuwa ni katika aina moja tu na zina hukumu moja, aidha katika jambo la utatuzi wa matatizo hayo ya kisaikolojia. Tofauti baina ya Frued na Quraani Tukufu ni kwamba Frued aliweka misingi yake na akaitekeleza juu ya nafsi ya kibinadamu kiujumla lakini katika Quraani Tukufu tunakuta sifa za nafsi ya kibinadamu zinatofautiana, aidha sifa zile za nafsi ambazo alizitaja Frued ziko karibu zaidi na nafsi yenye kuamrisha maovu licha ya kuwa aina hiyo ya nafsi ya kibinadamu inaenea zaidi katika jamii ya kibinadamu ila nafsi inayojilaumu inakuwepo.

Aidha, kufuata matamanio au kuidhinisha ngono hautakuwa utatuzi wa matatizo ya kisaikolojia kwa namna aliyoitaja Frued kwani utatuzi unaotokana na uongofu wa Quraani ni tofauti kabisa. Mwislamu akiangalia sura ya nafsi ya kibinadamu na hali yake kwa mujibu wa maoni ya Frued kisha akaziangalia katika Quraani Tukufu atazikuta zinatofautiana kutoka nafsi zilizotiwa muhuri, nafsi yenye kuamrisha maovu, nafsi ya kukaripia, nafsi iliyofunguliwa heri kisha nafsi iliyoridhika na nafsi yenye utulivu. Quraani ilitaja nafsi ya mwanadamu na aina zake pamoja na kubainisha njia zinazotakikana kuziongoza kutoka katika giza, upofu, dhiki na kushindwa kwenda katika mwangaza, ujuzi wa kweli, uongofu, faraja na usalama.

Utatuzi wa kingono kwa matatizo ya vijana hauafikiani kabisa na kitabu cha uongofu, kwani utatuzi unaofaa ni ule unaotokana na maneno ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na wajizuilie na machafu wale wasiopata cha kuolea, mpaka Mwenyezi Mungu Awatajirishe katika fadhila Zake}{AN-NUR, 33}, na maneno yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Waambie Waislamu wanaume wainamishe macho yao (wasitazame yaliyokatazwa), na wazilinde tupu zao, hili ni takaso kwao; bila shaka Mwenyezi Mungu Anazo habari za (yote) wanayoyafanya* Na waambie Waislamu wanawake wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao, wala wasidhihirishe viungo vyao isipokuwa vinavyodhihirika (nao ni uso na vitanga vya mikono – na wengine wanasema na nyayo). Na waangushe shungi zao mpaka vifuani mwao, na wasionyeshe mapambo yao ila kwa waume zao, au baba zao, au baba za waume zao, au watoto wao, au watoto wa waume zao, au kaka zao, au wana wa kaka zao, au wana wa dada zao, au wanawake wenziwao, au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume (watumwa wao), au wafuasi wanaume wasio na matamanio (kwa wanawake) au watoto ambao hawajajua mambo yanayohusu uke. Wala wasipige miguu yao ili yajulikane wanayoyaficha katika mapambo yao. Na tubieni nyote kwa Mwenyezi Mungu, enyi Waislamu ili mpate kufaulu}[AN-NUR, 30, 31].

Ufupishio: tunaweza kusema kwamba Quraani Tukufu si kitabu cha kutambua hali ilivyo au maarifa ya uwepo, bali ni ufunuo unaodhibiti utambuzi huo, kutoa njia ya kuitambua na kurekebisha hali ili iwe bora kuliko ilivyo pamoja na kuainisha mielekeo iliyo bora zaidi inayofaa kwa hali ilivyo.

Pili: kutendeana na Quraani Tukufu kuwa ni “msingi wa juu” ambao unaufanya moyo na akili kusikia raha ili mtu aweze kuufuata pamoja na kutoa hukumu na maoni yake katika shughuli zake za kiakili, kinafsi na kitabia:

1) Mtafiti wa kijamii Mwislamu anatendeana na Quraani Tukufu kwa ajili ya kutohoa misingi na kanuni, kama kuondosha mambo mazito: Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini} [AL-HAJJ, 78]. Mazito yanaleta mepesi, na baada ya dhiki ni faraja: Mwenyezi Mungu Mtufukufu Amesema: {Mwenyezi Mungu Anakutakieni yaliyo mepesi wala hakutakieni yaliyo mazito} [AL BAQARAH, 185]. Uhuru wa imani: Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Hakuna kulazimishwa (mtu kuingia) katika dini}[AL BAQARAH, 256]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Basi anayetaka naamini na anayetaka naakufuru}[AL KAHF, 29], Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Waite (waite watu) katika njia ya Mola wako kwa hekima na mawaidha mema, na ujadiliane nao kwa namna iliyo bora}[AN NAHL, 125], Amesema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Ondosha (ubaya unaofanyiwa kwa mema); tahamaki yule ambaye baina yako na baina yake kuna uadui atakuwa kama ni jamaa (yako) mwenye kukufia uchungu} [SAJDAH, 34], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wanaume wanafiki na wanawake wanafiki, wote ni hali moja; huamrisha yaliyo mabaya na huyakataza yaliyo mazuri, na kuizuilia mikono yao (hawasaidii mambo ya kheri); wamemsahau Mwenyezi Mungu (wamepuuza amri Zake); na Yeye pia Amewasahau (Amewapuuza). Hakika wanafiki ndio wavunjao amri * Mwenyezi Mungu Amewaahidi wanafiki wanaume na wanafiki wanawake na makafiri, moto wa Jahanamu kukaa humo daima. Huo unawatosha (kuwaadhibu); na Mwenyezi Mungu Amewalaani; nao wana adhabu itakayodumu * (Makafiri nyinyi ni) sawa na wale waliokuwa kabla yenu (tutakuangamizeni kama tulivyowaangamiza wao. Bali) wao walikuwa wana nguvu zaidi kuliko nyinyi na wana mali nyingi zaidi na watoto wengi zaidi kuliko nyinyi. Basi walistarehea sehemu yao, na nyinyi mnaistarehea sehemu yenu kama walivyostarehea kwa sehemu yao wale waliokuwa kabla yenu; na mkazama katika maovu kama walivyozama wao. Hao ndio ambao matendo yao yameharibika katika dunia na Akhera; na hao ndio waliokula hasarai * Je, Hazikuwajia, habari za wale walikuwa kabla yao; watu wa Nuhu na Adi na Thamud, na watu wa Ibrahimu, na watu wa Madyan, na (watu wa) miji iliyopinduliwa chini juu? Mitume wao waliwajia kwa hoja zilizo wazi (wakakataa kufuata. Basi Mwenyezi Mungu Akawaangamiza); na Mwenyezi Mungu hakuwa Mwenye kuwadhulumu, bali wao walikuwa wakijidhulumu wenyewe * Na waumini wanaume na wanawake, ni marafiki wao kwa wao} [AT TAWBA, 67: 71]. Katika kitabu kitakatifu kuna sentensi jumuia na sentensi hali zote ambapo mwenye sifa ya kilugha anaweza kutohoa misingi.

2) Kutohoa “kanuni za kiungu” zinazoendesha shughuli za binadamu na jamii ambazo zinasaidia kutambua hali ilivyo na mambo yenye kubadilika juu ya msingi ya kuwa: “kila kiumbe kimeumbwa kwa kiasi”, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Kwa hakika Sisi Tumekiumba kila kitu kwa kiasi (chake makhsusi)} [AL-QAMAR, 49]. Na Mwenyezi Mungu Ana kawaida na sheria yake katika kuendesha dunia na mambo yake, pamoja na kuendesha hali ya watu, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Basi hawangoji ila desturi (ya Mungu) iliyokuwa, (Aliyoipitisha) kwa watu wa zamani! Wala hutapata mabadiliko katika kawaida (desturi) ya Mwenyezi Mungu (Aliyoweka) wala hutakuta mageuko katika kawaida ya Mwenyezi Mungu} [FATIR, 43]. Pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Zimepita adabu namna kwa namna walizotiwa waliokuwa kabla yenu. Basi safirini katika nchi na mwone ulikuwaje mwisho wa wale waliokadhibisha} [AALI IMRAN, 137].
Miongoni mwa kanuni hizo za kiungu ni “kuwakinga watu wenyewe kwa wenyewe”, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na kama Mwenyezi Mungu Asingaliwakinga watu, baadhi yao kwa wengine, bila shaka yangalivunjwa mahekalu na makanisa na nyumba nyengine za ibada na misikiti ambamo jina la Mwenyezi Mungu hutajwa kwa wingi} [AL HAJJ, 40]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Alisema: {Na kama Mwenyezi Mungu Asingalizuia watu, baadhi yao kwa wengine, kwa yakini ardhi ingaliharibika} {AL BAQARAH, 251}. Aidha “kanuni ya kuhitalifiana” kama Alivyobainisha Mwenyezi Mtukufu Mungu: (Kwa hivyo wataendelea tu kuhitalifiana} [HUD, 118], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na katika Ishara Zake (za kuonyesha uweza wake) ni kuumba mbingu na ardhi, na kuhitalifiana lugha zenu na rangi zenu na (mengine yenu, na hali ya kuwa Muumbaji ndiye huyo huyo mmoja). Kwa yakini katika haya zimo Ishara kwa wenye ujuzi} [AR-RUM, 22]. Pamoja na kanuni ya: {Na mwisho (mwema) ni kwa wamchao} [AL AARAF, 128]. Na kanuni ya kubadilishana watu baada ya watu kama Alivyobainisha Mwenyezi Mungu :{Na siku za namna hii tunawaletea watu kwa zama}[ALLI IMRAN, 140].

3) Kutohoa hukumu za kisheria ambazo zinaelekeza mielekeo na tabia kwa upande wa shani iliyochunguzwa. Kwa hiyo, mtafiti wa sekta yoyote (kiujumla) analazimika kuweka Quraani Tukufu kuwa ni “msingi jumuia” ili aweze kudhibiti mielekeo yake ya kimaana na ya kitabia.

4) Kutohoa “makusudio ya kisheria ya kiujumla” nayo ni malengo ya juu ya kisheria ambayo ni kiini chake. Aidha yanadhibiti njia za kutafakari na kutohoa licha ya kutendeana na sheria yenyewe; nayo ni kuhifadhi nafsi, dini, kizazi, akili, mali na kila kilichomilikiwa na mtu. Kwa hiyo mtafiti yoyote katika utafiti wake hakiri siasa au mfumo wa nchi au mtu au jamii unaopinzana na hayo makusudio ya kisheria ya kiujumla ambayo ni “mipaka ya Mwenyezi Mungu na vitu Vyake vitakatifu”: utakatifu wa nafsi ya kibinadamu: Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Wala msimwue mtu ambaye Mwenyezi Mungu Ameharimisha (kuuawa), ila ikiwa (imetokea) haki ya kuuawa} [AL AN-AM, 151], pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Kwa sababu ya hayo tukawaandikia wana wa Israili ya kwamba atakayemwua mtu bila ya yeye kuua mtu, au bila ya kufanya ufisadi katika nchi, basi ni kama amewaua watu wote; na mwenye kumwacha mtu hai (kumsaidia kuishi) ni kama amewaacha hai watu wote} [AL MAIDAH, 32]. Hiyo ni hukumu ya kiujumla kwa kila nafsi, na imeharamisha mtu kujitoa akili kwa kisingizio chochote. Hayo ni malengo ya kiujumla yanayokuwa na malengo kadhaa ndani yake kama kuhifadhi afya ya mwili, usafi wa mazingira, kupambana na uchafuzi wa mazingira na kuhifadhi akili kutokana na matamanio.

Tatu: kutendeana na Quraani Tukufu lazima kuwe na vidhibiti madhubuti vya kutambua:
1. Kitabu chenyewe: nacho ni hoja iliyo wazi na baadhi yake inakuwa hoja juu ya sehemu zake nyengine, na kwa maana nyengine: lazima tukusanye baina ya dalili na matini (Aya) katika kila suala ili tusianguke katika jambo Alilolibainisha Mwenyezi Mungu Mtukufu katika maneno Yake: {Je! Mnaamini baadhi ya Kitabu na kukataa baadhi (yake)? Basi hakuna malipo kwa mwenye kufanya haya katika nyinyi ila fedheha katika maisha ya dunia; na siku ya Kiyama watapelekwa katika adhabu kali. Na Mwenyezi Mungu si mwenye kughafilika na yale mnayoyatenda} [AL BAQARAH, 85]. Jambo la kukusanya Aya linasaidia kuleta ufahamu licha ya kutenganisha masuala Muhkam (rahisi kufahamika) na yanayobabaisha, masuala maalum na masuala makuu, yenye masharti na yasiyokuwa na masharti, yanayofuta na yanayofutwa. Kwa hiyo mtafiti lazima awe na utambuzi asikosee kufahamu na kupata dalili za kisheria.

2. Sunna: ni udhibiti mwengine unaomsaidia mtafiti kufahamu na kuelewa Quraani Tukufu na kutohoa hukumu; maana Sunna inafasiri na kubainisha maana ya Quraani Tukufu, kwa hiyo Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na hatukukuteremshia Kitabu (hiki) isipokuwa uwabainishie yale ambayo wanahitalifiana, na (pia kiwe) uongozi na rehema kwa watu wanaoamini} [AN NAHL, 64]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na tumekuteremshia Kitabu hiki kielezacho kila kitu, na ambacho ni uongofu na rehema, na habari za furaha kwa wanaojisalimisha (kwa Mwenyezi Mungu) Waislamu} [AN NAHL, 89]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Na tumekuteremshia mawaidha ili uwabainishie watu yaliyoteremshwa kwao, na ili wapate kufikiri} {AN NAHL, 44}. Pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Hakika tumekuteremshia Kitabu (hiki), hali ya kuwa kimeshikamana na haki ili upate kuhukumu baina ya watu kama alivyokufahamisha Mwenyezi Mungu; wala usiwe mwenye kuwatetea wale wafanyao khiyana} [AN NISAA, 105].

3. Lugha ya Kiarabu: Quraani ni kitabu kwa lugha ya Kiarabu iliyo wazi, Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Hakika Sisi tumeiteremsha Quraani kwa Kiarabu ili mpate kufahamu} [YUSUF, 2]. Aidha Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {(Hiki ni) Kitabu kinachopambanuliwa (vizuri kabisa) Aya zake cha kusomwa kwa Kiarabu kwa watu wanaojua} [FUSWILAT, 3]. Pia Mwenyezi Mungu Mtukufu Amesema: {Kwa lugha ya Kiarabu waziwazi (fasihi)}[ASH-SHURAA, 195]. Na hii kwa ajili ya kubainisha na kuweka wazi. (Na hatukumpeleka Mtume yoyote isipokuwa kwa lugha ya watu wake ili apate kuwabainishia} [IBRAHIM, 4].

4. Ijmai (makubaliano ya wanazuoni): ni jambo ambalo Umma au wanazuoni wa enzi wanakubaliana juu ya ufahamu wake; kwa hiyo inawajibika juu ya kila anayejua hayo makubaliano ayatekeleze bila ya kupinga.

5. Makusudio ya kisheria: hukumu yake ni kama Ijamai.
Hizo ni funguo ambazo yoyote akizipata (kwa kuwajibika na kuzitumia) zinakuwa ni mfumo wake, basi anaweza kutendeana na Quraani Tukufu kwa njia sahihi; maana mwenye funguo hizo hatakuwa mwenye kasoro (pungufu) kwa kujinyima katika lafudhi na matini ya Quraani Tukufu bila ya kuangalia na kuelewa maana zake, mwenye funguo hizo hatakuta anazuiliwa na vizingiti vya tafsiri iliyotegemea mtazamo wa uwazi wa maana, tena hawezi kwenda mbali (na tafsiri yake) na mipaka ya Quraani Tukufu au kwenda mbali na matakwa ya Mwenyezi Mungu au hata kwenda mbali na madhumuni na maana ya maneno ya Mwenyezi Mungu. Aidha, mtafiti wakati wa kutendeana na Quraani Tukufu lazima azidishe ufahamu wake wa Quraani Tukufu pamoja na ujuzi na ufahamu wake wa elimu zinazoambatana na Quraani Tukufu kama elimu za lugha za Kiarabu, visomo vya Quraani Tukufu, tafsiri, Sunna n.k. aidha mtafiti hawajibiki kujua kila kinachohusiana na elimu hizo zote kama kwamba aliyebobea, bali ajue mambo ya elimu hizo kiujumla na kila akitaka kuangalia suala arudi kulichunguza katika tawi lake la elimu.
Marejeo: Dr. Ali Juma (Mufti wa Misri): ATWARIYQU ILAA FAHMI TURATHI.
 

Share this:

Related Fatwas