Imamu kumwachia Mtu Mwingine Akami...

Egypt's Dar Al-Ifta

Imamu kumwachia Mtu Mwingine Akamilishe sehemu ya Sala iliyobakia.

Question

Nini hukumu ya imamu atakaekumbuka wakati wa Sala kuwa hana twahara, pale alipoanza kusali, na je kwa wakati huo atamwachia mtu mwingine miongoni mwa walio nyuma yake (maamuma) ili akamilishie sehemu ya Sala iliyobakia au watu wote wanalazimika kusali upya?

Answer

 Sifa zote njema ni zake Mwenyezi Mungu, rehma na amani zimfikie Mtume Muhammad S.A.W., jamaa zake, masahaba wake na waliomfuata. Ama baada ya hayo:

Kwa hakika Sala ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu, na imefaradhishwa ili imwasilishe mtu na Mola wake, na ni lazima mtu anayrsali awe na twahara kamili kwa maana ya kutokuwa na hadathi na uchafu wowote ule.

Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema kuwa: {Enyi mlio amini! Mnaposimama kwa ajili ya Sala basi osheni nyuso zenu, na mikono yenu mpaka vifundoni, na mpake vichwa vyenu, na osheni miguu yenu mpaka vifundoni. Na mkiwa na janaba basi ogeni. Namkiwa wagonjwa au mmo safarini, au mmoja wenu ametoka chooni au mmewagusa wanawake, na hamkupata maji, basi tayamamuni vumbi lilio safi, na mpake nyuso zenu na mikono yenu. Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu; bali anataka kukutakaseni na kutimiza neema yake juu yenu ili mpate kushukuru}. [AL MAIDAH 6].

Na Mtume S.A.W alisema katika Hadith iliyopokelewa na Al Bukhariy na wengineo, kutoka kwa Abi Huraira kutoka kwa Mtume S.A.W. anasema: "Mwenyezi Mungu haikubali Sala ya yoyote miongoni mwenu hadi atakapotawadha." Na katika Hadithi iliyopokelewa na Imamu Muslim kutoka kwa Ibn Omar R.A. anasema: Mtume S.A.W amesema: "Mwenyezi Mungu haikubali Sala isipokuwa kwa usafi, na wala hakuna sadaka yoyote kwa (kutoa) chakula kilichooza."

Na iwapo mtu anayesali hajatwaharika na hadathi ndogo au kubwa, au uchafu wowote au najisi basi akisali na hali hiyo hakika Sala yake imeharibika na atalazimika kuirejea tena.

Na iwapo imamu hatakuwa na twahara na akakumbuka akiwa katika Sala atalazimika kukata Sala kisha amwachie mwingine atakayeikamilisha Sala hiyo. Na waumini walio nyuma ya imamu huyo, hawalazimiki kusali upya kwa sharti kwamba asifanye kitendo chochote miongoni mwa vitendo vya Sala baada ya yeye kukumbuka kuwa ana hadathi, la sivyo Sala yake itabatilika na pia Sala ya wengine walio nyuma yake, kwani yeye katika hali hii amekusudia kusali Sala akiwa na hadathi kwa hiyo ni batili.

Na dalili ya hayo, ni yale yaliyopokelewa katika Sahihi mbili: " Mtume S.A.W alimwachia Abu Bakar R.A. mara mbili; mara alipokuwa mgonjwa, na mara nyingine alipokwenda Mtume S.A.W ili kusuluhisha baina ya Bani Amro Bin Auf, na Abu Bakar akawasalisha watu, basi Mtume S.A.W alikuja naye akiwa anasali, Abu Bakar akarejea nyuma na kumwachia Mtume S.A.W, (asalishe sehemu ya Sala iliyobakia). [Rejea: Al Majmou' Sharh Al Muhazab 138 /4, Ch. Al Miniriyah]

Ibn Abdulhadi amepokea kutoka kwa Al Barraa' Bin Aazib katika kitabu cha [Tanqieh Tahqiq Al Ta'aleeq] akasema: "Mtume S.A.W. alisalisha watu bila ya kutawadha, na Sala ya watu hao ikatimia. Na Mtume S.A.W akasali upya (baada ya kutawadha)."

Na dalili ya kutobatilika Sala ya aliyesali nyuma ya imamu mwenye janaba iwapo imamu atasahau kuwa ana hadathi hiyo, ni Hadithi iliyopokelewa na Malik katika kitabu chake [Al Muwata'] kutoka kwa Sulaiman Bin Yasaar: Hakika Omar Bin Khatwab aliteremkia makondeni na akakuta kuna alama za maji ya manii katika nguo yake yanayotokana na kuota usingizini, akasema hakika mimi nimepatwa na mtihani kwa kuota, tangu nilipowaongoza watu (katika Sala), basi akaoga na akakiosha kile alichokiona kwenye nguo yake kutokana na kuota. Kisha akasali baada ya jua kuchomoza. Kwa hivyo basi, Omar akailipa Sala na wala hakuwaamrisha watu kuilipa Sala hiyo.

Sahnun amepokea Hadithi kutoka kwa Ibn Al Qaasem kwamba amesema: Na Omar amewasalisha watu alipokuwa na janaba, halafu akalipa Sala yake hiyo na wala hakuwaamrisha watu kuilipa Sala yao hiyo. [Al Modawanah 138/1, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]

Na pale Omar R.A alipochomwa na mkuki alimwachia Abdulrahman Bin Auf (amalizie kuwasalisha watu sehemu iliyobakia), na kama Sala yake ingeliharibika basi Sala ya watu wote ingelikuwa imeharibika, na asingelimwachia mtu yoyote mwingine kuimalizia, na kwa kuwa tukio hilo lilimtangulia bila ya yeye kusababisha kwa hivyo limekuwa ni kama tukio la kimbingu. [Al Mabssutt 196/1, Ch. Dar Al Maarifa]

Na Imamu atamwachia mtu mwingine akamilishe Sala ya watu hao kwa kufuata kipimo cha madaraka ya ukadhi, kwa kuangalia masilahi yote na kuondosha migogoro. [Al Fiqh Al Malikiy Wa Adillatuhu, cha Al Habeeb Bin Taher 353/1, Ch. Dar Bin Hazm]

Na katika kitabu cha [Al Mudawanah 138/1]: "Na Imamu Malik amemzungumzia mtu mwenye janaba anaewasalisha watu huku anajua kuwa ana janaba na akawasalisha rakaa moja au mbili au tatu kisha akakumbuka kuwa ana janaba anasema Imamu: aondoke mtu huyo, na amwachie mwingine atakayewaongoza watu sehemu ya Sala iliyobakia, na Sala ya watu hao waliomfuata imamu huyo mwenye janaba ni sahihi na imetimia, akasema Imamu: na ikiwa atamaliza Sala bila ya kukumbuka kuwa ana janaba mpaka mwisho wa Sala, basi Sala ya waliokuwa nyuma yake ni sahihi na Sala yake yeye tu ndio imeharibika na lazima asali tena."

Al Hattaab amesema katika kitabu cha [Mawaheb Al Jaleel]: "Al Mussanif: (au mwenye janaba akikusudia au mfuasi wake akijua) suala hili limeandikwa. Amesema katika kitabu cha Twahara: Na iwapo imamu, baada ya kumaliza Sala, alikumbuka kuwa alikuwa na janaba basi yeye peke yake atairejea tena Sala yake, na Sala ya waliosali nyuma yake ni sahihi na imekamilika. Na iwapo atakumbuka kuwa ana janaba kabla ya kukamilisha Sala yake basi na amwachie mwingine akamilishe (sehemu ya Sala iliyobakia), na iwapo ataendelea na Sala baada ya kujua kwake, kwa ujinga au kwa kuona haya au kuna kitu kimemtokea na kuivuruga Sala yake, kisha akaendelea na Sala hiyo au akaanza kuwasalisha watu huku akikumbuka kuwa ana janaba, basi atakuwa amejivurugia Sala yake na amewavurugia wenzake, na ni lazima kwa walio nyuma yake kusali upya kuanzia pale walipojua (kuwepo kwa tatizo hilo), au wale waliojua kuwa imamu ana janaba miongoni mwa wale aliowaongoza katika Sala, huku imamu mwenyewe akiwa amesahau kuwa ana janaba, na akaendelea na Sala, basi Sala yake imeharibika, atairejea tena hata kama ameimaliza." [Mawaheb Al Jaleel kwa Al Hattaab 96/2, Ch. Dar Al Fikr].

Ibn Qudamah amesema katika kitabu cha [Al Mughniy]: "(Na iwapo imamu amesahau na akawasalisha watu akiwa na janaba, yeye peke yake ataisali tena Sala yake, na ujumla wake ni kwamba imamu atakapoisalisha jamaa akiwa na hadathi au janaba bila ya kujua kuwa nayo, si yeye wala anayewaongoza waliojua hivyo hadi akakamilisha Sala yake walijua kuwa ana hadathi au janaba, basi Sala yao ni sahihi na Sala ya imamu imeharibika. Hayo yamepokelewa kutoka kwa Omar, Othmaan, Ali na Ibn Omar R.A ziwafikie wao wote, na hivyo ndivyo walivyosema hawa wafuatao: Al Hasan, Said Bin Jubeer, Malik, Al Awzaiy, Al Shafiy, Sulaimaan Bin Harb na Abu Thaur."

Halafu akasema: "Dalili yetu ni masahaba wote R.A. ziwe kwao wote, kuwa imepokelewa kwamba Omar R.A. alisalisha watu Sala ya Asubuhi, kisha akatoka na kuelekea kondeni, na kisha akajimwagia maji, na akakuta kwenye nguo yake kuna manii kwa sababu ya kuota, basi akasali tena. Na wale aliowasalisha hawakuisali tena (Sala yao na ilikamilika). Na kutoka kwa Muhammad Bin Amr Bin Al Mussttaliq Al Khozai, kuwa Othman aliwasalisha watu Sala ya Alfajiri, na baada ya kucha na kuingia mchana akajikuta na athari za janaba na akasema: nimefanya kosa kubwa kwa kweli, nimefanya kosa kubwa kwa kweli! basi akasali tena, na wala hajawaamrisha waliosali nyuma yake kuirejea Sala yao.

Na kutoka kwa Ali amesema: Mtu mwenye janaba akiwasalisha watu na akakamilisha Sala yao nitamwamrisha aoge na asali tena na wala sitawaamrisha waliosali nyuma yake kuirejea Sala yao.

Na kutoka kwa Ibn Omar R.A. kuwa aliwasalisha watu Adhuhuri halafu akakumbuka kwamba alikuwa anasali bila ya kutawadha, basi akairejea Sala yake na wao hawakuirejea Sala yao. Hayo yote yamepokelewa na Al Athrem. Na jambo hili linajulikana, na wala hapajawahi kupokelewa kinyume cha hivyo, na hivyo limekuwa ni katika makubaliano ya wanachuoni wote. [Al Mughniy kwa Ibn Qudamah 219-220/1, Ch. Dar Ihyaa Al Turaath Al Arabiy]

Ibn Hazm amesema: "Na iwapo imamu atapatwa na hadathi au akakumbuka kuwa yeye si msafi basi atatoka na atampa uimamu mtu mwingine na atakuwa amefanya vizuri." [Al Mahaliy 137/3, Ch. Dar Al Fikr]

Na kutokana na hayo: Imamu atakapokumbuka akiwa katika Sala kuwa yeye si msafi basi atamwachia mtu mwingine awasalishe watu sehemu ya Sala iliyobakia, na Sala ya imamu huyo itabatilika, na maamuma Sala yao haitabatilika na hawalazimiki kuisali tena.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi.

Share this:

Related Fatwas