Hukumu ya kisheria katika kuombaomba
Question
Ni ipi hukumu ya kisheria katika kuombaomba? Na ni ipi hukumu ya kuwasaidia ombaomba waliozagaa maeneo mbalimbali?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Asili ya neno "tasawwul katika lugha ya kiarabu" ni kulilaza tumbo, na maana yake ni "kuomba" na "kuomba msaada wa haja". Na maana nyingine ya neno hili, pia kuwaomba watu sadaka. Na hayo yote ni "kuombaomba" [Rejea: Al Kamus Al Muheett na Al Mujam Al Wajeez, kidahizo cha "Sawal"]
Na asili ya kuombaomba watu bila ya kuwa na shida au dharura inayowafanya waombe ni jambo linalochukiza katika Sheria ya Kiislamu. Na Imamu Muslim amepokea kutoka kwa Auf Bin Malik Al Ashjaiy R.A. amesema: tulikuwa watu saba, wanane au tisa pamoja na Mtume S.A.W, nae akasema: "Je hamumuungi mkono Mtume wa Mwenyezi Mungu? "Na tulikuwa wapya katika Uislamu. Basi tukasema "Hakika tumekuunga mkono ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kisha akasema: "Je hamumuungi mkono Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Basi tukasema tumekuunga mkono ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, halafu akasema: "Je hamumuungi mkono Mtume wa Mwenyezi Mungu?" Akasema: "Tukakunjua mikono yetu na kusema: Hakika tumekuunga mkono ewe mtume wa Mwenyezi Mungu, je tunakuunga mkono kwa jambo gani? Akasema: "Kuwa mnamwabudu Mwenyezi Mungu Mtukufu, na wala hamumshirikishi mwingine yeyote, na mnatekeleza mambo matano, na kutii!" Akanong’ona neno la siri "wala msiwaombe watu kitu chochote". Msimulizi akasema: "Hakika nimewaona baadhi ya watu hao pindi mmoja wao anapodondosha fimbo yake, basi hamuombi mtu yeyoye amuokotee.
Na Imamu Ahmad amepokea na Ibn Habaan – tamko hili ni lake- kutoka kwa Abi Huraira R.A kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Hajifungulii mtu yeye mwenyewe mlango wa kuomba isipokuwa Mwenyezi Mungu humfungulia mlango wa ufakiri, mtu kubeba kamba na kuelekea majabalini na akakata kuni na kuzibeba mgongoni mwake na akala kwa kazi hiyo, basi kwake ni bora zaidi kuliko kuwaomba watu akapewa au akanyimwa."
Na watu wana hali zinazotofautiana katika jambo hili, na kwa kutokana na tofauti za hali zao, hukumu zao pia zinatofautiana. Kwa hivyo mtu anaeombaomba bila ya kuwa na haja ya kuomba, kwa kuwa mtu huyu ana mali, ujuzi wa mikono au kwa kutengeneza kitu chochote, na akawa anaonesha ufakiri na umasikini ili watu wamsaidie, basi kuomba kwake ni haramu. Na dalili ya hayo ni uwazi wa hadithi zilizotajwa katika kukataza kuombaomba watu; na miongoni mwake ni yaliyopokelewa na Imamu Al Bukhariy na Muslim kutoka kwa hadithi ya Ibn Omar R.A. kwa wote wawili, kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Ataendelea mmoja wenu kuombaomba mpaka akakutana na Mola wake mtukufu hali ya kuwa katika uso wake hakuna hata kipande cha nyama".
Al Qadhi Aiyaadh Mwenyezi Mungu amrehemu amesema katika kitabu cha [Ikmaal Al Mualem 574/3, Ch. Dar El Wafaa]: "Inasemekana: maana yake atakuja mtu siku ya Kiama akiwa dhalili aliyeporomoka hana uso mbele ya Mwenyezi Mungu. Na inasemekana: na kwa uwazi wake, atafufuliwa hali yakuwa uso wake ni mifupa mitupu isio na nyamanyama, na hii ni alama ya dhambi zake kwa kombaomba kwake kwa uso wake, kama ilivyokuja katika Hadithi nyingine za adhabu ya viungo ambavyo alivitumia katika maasi.. na hii ni kwa yule aliyeomba bila ya dharura na kwa kutaka kujilimbikizia mali".
Na katika kitabu sahihi cha Muslim kutoka kwa Abi Huraira R.A. kuwa Mtume S.A.W. amesema: "Atakayewaomba watu mali zao kwa ajili ya kujilimbikizia basi anaomba jiwe la moto, basi na apunguze au aongeze" (aongeze anachokiomba ili jiwe la moto liwe kubwa au apunguze ili jiwe la moto liwe dogo. Na yote mawili ni ya kuachwa). Al Qadhi Aiyaadh akasema katika kitabu cha [Ikmaal Al Mualem 575/3, Ch. Dar El Wafaa]: "Ina maana ya kumuadhibu kwayo motoni; kwa kuwa amejidanganya yeye mwenyewe na kujichumia kisicho halali yake kwa jina la umasikini… na inawezekana jiwe likawa katika uso wake, kwa maana kuwa kinarejeshwa kile alichokichukua kama jiwe la moto na likawa lake kama ilivyokuja kwa anayezuia zaka".
Na Abu Dawud amepokea kutoka katika Hadithi ya Sahl Bin Al Handhaliyah R.A. kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Na atakayeomba hali ya kuwa anacho kinachomtosha, basi atakuwa anajiongezea moto – au: jiwe la moto wa Jahannam." Basi Maswahaba wakauliza, na ni nini hicho kinachomtosha? Akasema: "Kiasi cha chakula cha kumtosha mchana na jioni-, au akawa na kinachomshibisha usiku na mchana, au kwa siku nzima."
Na miongoni mwake ni Hadithi iliyopokelewa na Attabaraniy katika kitabu cha [Al Kabeer] kutoka kwa Masoud Bin Amru R.A. kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Mja haachi kuombaomba huku anajitosheleza, mpaka uso wake ukazoea tabia hiyo na akawa hana tena uso mbele ya Mwenyezi Mungu".
Na Al Baihaqiy amepokea katika kitabu cha [Al Shaub] kutoka kwa Ibn Abaas R.A. kwao wote wawili, kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Atakayewaomba watu bila ya yeye kukumbwa na ufukara au akawa hawezi kuwalea watoto wake, basi atakuja siku ya Kiama kwa uso wake usiokuwa na nyama."
Na Ibn Khuzaimah amepokea katika kitabu chake sahihi kutoka kwa Habashiy Bin Janadah R.A. kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Atakayeomba hali ya kuwa anacho cha kumtosha, basi hakika atakula jiwe la moto". Imepokelewa na Al Baihaqiy katika kitabu cha [Al Sheab] kwa tamko la: "Anayeomba bila ya kuwa na haja ni kama vile mtu anayeokota jiwe la moto."
Na tamko la kuharimisha katika hali hii, ni namna wanachuoni wa Madhehebu ya Shafi walivyolitaja; Sheikh wa Usilamu Zakariyah Al Ansariy amesema katika kitabu cha: [Isny Al Mattalib 407/1, Ch. Dar Al Kitaab Al Islamiy]: (Ni haramu juu yake) yaani tajiri kuichukua – yaani sadaka - "Ikiwa atajifanya kuwa yeye ni fakiri” na kwa huyu, wamemchukulia kama ilivyo katika Hadithi ya yule aliyekufa miongoni mwa wenye sifa hiyo na akaacha dinari mbili, basi Mtume S.A.W akasema zote mbili ni moto" Bali Imamu Ibn Hajar Al Haitamiy aliizingatia katika kitabu chake [Al Zawajer 304/1, Ch. Dar Al Fikr] ni miongoni mwa madhambi makubwa.
Na kama mwombaji atakuwa na dharura kutokana na umasikini wake au haja yeyote iliyomtokea au kwa kushindwa kujichumia riziki basi ni halali kwake wakati huo kuomba na wala si haramu. Na dalili ya hayo ni mapokezi ya Abu Dawud na Ibn Majah ya Hadithi ya Anas Bin Malik R.A. kutoka kwake na kutoka kwa Mtume S.A.W. kwamba amesema: "Hakika kuomba hakusihi isipokuwa kwa watu watatu: kwa fukara aliyepindukia, au mwenye deni kubwa mno au mwenye mikono yenye damu (yaani mtu aliyeua mtu) na ndugu wa marehemu wakawa na uchungu mwingi wakitaka fidia ya mauaji ya ndugu yao". Na ufukara uliopindukia ni ufukara mkubwa, na deni kubwa yaani deni zito lenye kuhitaji fedha nyingi mno. Na damu inayotia uchungu mwingi ni ile inayowasononesha wafiwa na kuwauma sana, wakitaka fidia ya mauaji ya ndugu yao aliyeuawa. Na hapo ndipo inapozuka fitina na ugomvi baina yao. [Aun Al Maboud kwa Al Adheem Abadi 38/5, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah].
Imamu Al Nawawiy –rehema ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake – amesema katika [Al Majmou Sharh Al Muhazab 239/6, Ch. ya Al Mattba'a Al Membariyah: "Ama kuomba kwa mwenye haja asiyeweza kufanya kazi, basi si haramu wala haichukizi."
Bali wakati mwingine kuomba kunaweza kuwa ni lazima kwa mtu kama fukara au asiyeweza kujichumia pato lake mwenyewe na maisha yake yakawa yanategemea kuwaomba watu wengine kiasi cha fedha kitakachomsaidia katika maisha yake na kama hakuwaomba ataangamia, na juu ya hayo huchukua yaliyopokelewa na Abu Nuaim katika mji wa Al Hella kutoka kwa Sufiyaan Al Thawriy "Aliyekuwa na njaa na akashindwa kuwaomba watu hadi akafa basi ataingia motoni."
Kwa upande wa kuwasaidia ombaomba, sio pale wanapoonekana tu, yaani hapo kwa hapo, bali kuna tegemea na dhana yenye nguvu kuwa wana haja ya kusaidiwa na pia kusadikika kwa dhana hiyo, na iwapo mtoaji ataona kuwa afanye uchunguzi wa hali ya ombaomba basi na afanye hivyo, hasa katika mali za Zaka ambazo Mwenyezi Mungu alilazimisha zitolewe kwa wanaostahili. Na umuhimu wake unaonekana katika baadhi ya maeneo ambayo ombaomba wamekuwa wakiyatumia kuombea, kama kazi yao wanajipatia pato kutokana na kazi hiyo, bali ni kazi inayofanywa kwa kuwatumia watoto, pia husukumwa watoto hao ili wajifunze wakiwa wadogo, na hakuna shaka kuwa hiyo ni dalili yenye hatari juu ya amani ya jamii na usalama wake.
Na kuenea kwa omba omba na kuwa kwake ni tukio kubwa ni dalili ya watu kurejea nyuma kimaendeleo, na ni ushahidi tosha wa uchache wa kuleana na kusaidiana kati ya watu. Pande zinazohusika zinapaswa kutafuta sababu ya tatizo hili ili kufanya kazi ya kulimaliza kwa kuwatoshelezea mafukara na wenye kuhitaji, mahitaji yao muimu, na kumzuia yule mwenye kutaka kuisukuma nafsi yake awe ombaomba, na kisha kuwabughudhi watu bila ya haja ya kufanya hivyo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni mjuzi zaidi kuliko wote.