Binadamu ni Kiumbe Mwenye Maadili
Question
Kuna Uhusiano gani baina ya binadamu na maadili?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
1. Tunaweza kumuelezea binadamu kuwa ni kiumbe mwenye maadili -kama alivyosema Prof. Abdel Hamid Madkur Profesa na Mkuu wa zamani wa kitengo cha falsafa ya Kiislamu, kitivo cha Dar al U’lum- binadamu anaweza kusifika kwa sifa nyingi mbalimbali kwa mujibu wa mtazamo ambao tunautumia kumsifu na kuainisha na elimu inayotumika kufafanua sifa hizo, ambapo anasifika kwa mujibu wa nyanja za maarifa kuwa ni kiumbe kinachoweza kutamka; kiumbe mwenye akili na fikra, hali kadhalika binadamu anaweza kusifika kutokana na elimu ya sosholojia kuwa ni kiumbe mwenye ustaarabu kimaumbile. wanavyuoni wa elimu ya historia wanamsifu binadamu kuwa ni kiumbe mwenye historia; ana uwezo wa kuangalia na kuandika historia yake kuirithisha kwa vizazi vijavyo. Hivyo basi, sifa za binadamu zinatofautiana kwa mujibu wa nyanja na mitazamo tofauti inayotumika kuziainisha sifa zake.
2. Kutokana na elimu ya maadili, tunaweza kumpa binadamu sifa ya kuwa ni kiumbe mwenye utashi; ana uwezo wa kupambanua baina ya kheri na shari, mambo mema na mambo mabaya. Kisha baada ya hayo, anachagua anavyotaka kufanya kwa hiari yake. na hili ndilo linalomfanya binadamu awe bora zaidi ya viumbe vyengine, ambapo anakuwa na jukumu kuhusu kila anachokitenda.
3. Hivyo, inamaanisha kwamba, binadamu katika chaguo lake na tabia yake hanyenyekei hisia “utashi” au tabia thabiti inayomlazimisha kuwa na mienendo asiyeweza kuiacha; kwani binadamu anaweza kuiacha akitaka akiwa na sababu zinazomfanya ajiepushe na mienendo hiyo; maana tabia yake inaweza kubadilika kutoka uzuri kwa kuufuata ubaya au kutoka ubaya kwa kuufuata uzuri, na mienendo yake inatofautiana baina ya kufanya na kutofanya, kwenda mbele na kurudi nyumba, na kitendo chake kinaainishwa katika kila hali kwa sifa ya inachokifaa akiwa anakitenda kwa hiari na uhuru wake. Hali kadhalika jukumu lake la kimaadili linategemea chaguo lake licha ya kuwepo malipo ya baadaye. Mwenyezi Mungu Anasema: {Kisha Akaifahamisha uovu wake na wema wake * Bila shaka amefaulu aliyeitakasa (nafsi yake) * Na bila shaka amepata hasara aliyeiviza (nafsi yake)}[ASH- SHAMS, 8,9,10]. Kadhalika Mwenyezi Mungu Amesema: {Hakika sisi tumemuongoa, (tumembainishia) njia (zote mbili hizi; kuwa hii ndiyo ya kheri na hii ndiyo ya shari). Basi (mwenyewe tena) atakuwa mwenye shukurani au awe mwenye kukufuru, (kukanusha)}[AL INSAAN, 3].
4. Ikiwa binadamu ana sifa hiyo; sifa ya mwenye matakwa na uwezo wa kuchagua, basi anaweza kusifika kuwa ni kiumbe mwenye maadili na utashi wa kuyafanya yanayoelekeza kufanya jambo la kheri au la shari.
5. Binadamu alifadhilishwa juu ya viumbe vyengine kwa sifa hiyo ambapo vitendo vyake vinabadilika, haviko S.A.W.a, na vitendo vya viumbe vyengine vinakwenda sambamba na mwelekeo mmoja havibadiliki. Vitendo hivyo vinaweza kuwa vya kheri wala haviwezi kuelekea kwenye njia ya shari kabisa kama vile vitendo vya Malaika ambao wanasifika katika Quraani kwa sifa nyingi na miongoni mwazo ni kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu anaposema: {Na makafiri wanasema: “(Mwenyezi Mungu) Mwinyi wa rehema Amejifanyia mtoto”. Ametakasika (Mwenyezi Mungu!) bali (hao Malaika) ni waja (wa Mwenyezi Mungu) waliotukuzwa * Hawamtangulii kwa neno (lake Analosema), nao wanafanya amzri zake (zote) * (Mwenyezi Mungu) Anayajua yaliyo mbele yao (hao Malaika) na yaliyo nyuma yao. Na (hao Malaika) hawamuombei (yo yote) ila yule anayemridhia (Mwenyewe Mwenyezi Mungu), nao kwa ajili ya kumuogopa wananyenyekea}[AL ANBIYAA, 26, 27, 28]. Hali kadhalika vitendo hivyo vinaweza kuwa ni vya shari kiujumla havina kheri, kama vile vitendo vya shetani ambapo anawapambia watu wafanye shari licha ya kuingia katika ukafiri na uasi, na anawakataza wasifanye kheri akawaamuru wafanye uovu waache mema, utiifu na ihsani. Aya za Quraani Tukufu zinazungumzia shetani na ung’ang’anizi wake katika njia ya shari na udanganyifu wake kwa watu. Na miongoni mwa Aya hizo ni: {Akasema: “Kwa kuwa umenihukumia upotofu (upotevu) basi nitawakalia (waja Wako) katika njia Yako iliyonyooka (ili niwapoteze)” * “Kisha nitawafikia kwa mbele yao na nyuma yao na kuumeni (kuliani) kwao na kushotoni kwao; wengi katika wao hutawakuta (hutawaona) ni wenye kukushukuru”}[AL AARAF, 16, 17]. Tena vitendo hivyo pengine vinaweza kuwa vinatokana na silika kama vile vitendo vya wanyama ambavyo havina fikra wala utashi; kwani mnyama hana sifa hizo, na vitendo hivyo vinatokana na silika ya kimaumbile ambayo haina chaguo au inaweza kuwa na chaguo lakini kwa kiwango duni mno, na kwa hiyo, vitendo vyake haviwezi kuwa na sifa za maadili, tena vinakuwa bila ya jukumu la kimaadili wala la kungojea kupata malipo, kwa sababu tu ya kutokuwepo sharti. Aina hizi za vitendo haviingii katika elimu ya sosholojia inayohusika na mwenendo wa kibinadamu.
6. Kwa kuwa Binadamu ana upande huu wa utashi unaoelekea kheri na shari, jambo ambalo linamtofautisha na viumbe vingine, kwa hivyo basi hapa lazima tuashirie kwamba vitendo vinavyoingia katika uwanja wa hukumu ya kimaadili ni vile vitendo vinavyoambatana na upande wa utashi. Ama vile vitendo ambavyo haviambatani na utashi, basi binadamu hawi na jukumu la kimaadili kwa kuvitenda.
7. Na miongoni mwa mifano ya Vitendo vitendo vya kimwili vinavyotokea bila ya utashi, ni kama vile kazi za moyo, ini, matumbo, kiu, miayo n.k. Aidha, vitendo vinavyofanywa na mtoto ambaye akili yake bado haijakomaa, na kichaa asie na akili uwianifu. Tena hukumu hii inahusiana na aliyelazimishwa akiwa hana nafasi ya kuwa na utashi au kuchagua. Kwa hiyo basi, vitendo vya wale wote tuliowataja, vinakuwa nje ya upande wa kubeba jukumu la kimaadili, kwa sababu ya kutokuwepo sharti la utashi kamili. Na iwapo watu hawa watakuwa na hadhi ya kuchagua angalau kwa kiwango kidogo, basi watakuwa na jukumu linalolingana na kiwango hicho. Kwa mfano aliyekunywa dawa za kulevya kwa makusudi, basi hubeba jukumu la kila jambo analolifanya; kwani yeye mwenyewe ndiye aliyesababisha kuwepo hali hiyo ya kupoteza fahamu yake kwa utashi wake yeye mwenyewe, na pia yule mwenye kulazimsihwa kwa kiasi kidogo, basi kwa namna ambayo anakuwa na jukumu linalokuwa S.A.W.a na kiwango cha utashi wake. Wanazuoni wa Elimu ya Fiqhi ya Kiislamu na wataalamu wanasheria, wana tafiti zinazostahiki kuzingatiwa katika suala hilo.
8. Binadamu aliyetunukiwa na Mwenyezi Mungu sifa ya utashi wa kheri na shari, alijaribiwa kwa mtihani na mabalaa ya kila aina tangu kuumbwa kwake, jambo ambalo linamaanisha kwamba binadamu aliingia katika jaribio la kimaadili linalohusiana na utashi na nia yake tangu mapema. Hivyo basi, Mwenyezi Mungu Alipomwambia Nabii Adam A.S. akae bustanini na achukue ahadi ya utiifu na unyenyevu kwa Mwenyezi Mungu pamoja na kutomtii iblisi ambaye alikataa kumsujudia Nabii Adam A.S. alipoamrishwa na Mwenyezi Mungu: {Na Tulipompa ahadi (Nabii) Adamu zamani, lakini alisahau, wala Hatukuona kwake azma kubwa (kama za wale Mitume wengine) * Na (kumbukeni) Tulipowambia Malaika, “Msujudieni Adamu”, wakatii isipokuwa Iblisi, alikataa * Tukasema: “Ewe Adamu! Hakika huyu ni adui yako na wa mke wako. Basi asikutoeni Peponi mtaingia mashakani” * “Hakika hutakuwa mwenye njaa humo wala hutakuwa uchi” * “Na kwa yakini hutapata kiu humo wala hutapata joto” * (lakini) Shetani alimtia wasiwasi, (alimchokoachokoa) akamwambia “Ewe Adamu, je! Nikujulishe mti wa umilele na wa ufalme usiokoma?” * Basi wakaula wote wawili, na uchi wao ukawadhihirikia na wakaanza kujibandika majani ya Peponi (humo). Na Adamu akamkosa Mola wake, na akapotea kidogo njia * Kisha Mola wake Akamchagua na Akamkubalia toba yake na Akamuongoa * (Mwenyezi Mungu) Akasema: “Ondokeni humu nyote, hali ya kuwa ni maadui nyinyi kwa nyinyi; (vizazi vyenu vitakuwa maadui wenyewe kwa wenyewe). Na ukikufikieni kutoka Kwangu uwongofu, basi atakayeufuata uwongofu Wangu huo hatapotea wala hatataabika” * “Na atakayejiepusha na mawaidha yangu (hayo), basi kwa yakini atapata maisha yenye dhiki, na siku ya Kiama Tutamfufua hali ya kuwa kipofu”}[TA HA, 115: 124].
9. Hilo linamaanisha kwamba binadamu anaweza kupata mtihani akiingia katika kheri au shari ili kupata mtihani (atahiniwe) kuhusu utashi wake na nia aliyonayo, na huo mtihani unakuwa ni msingi wa kubeba jukumu la kimaadili. Vile vle kupatwa na mtihani wa kimaadili haukuwahusu Nabii Adam na Bi. Hawwa A.S. peke yao, bali ni mtihani unaoendelea kutokea kwa vizazi vyao vitakavyowafuata. Mwenyezi Mungu Anasema: {Ambaye Ameumba mauti na uhai ili kukujaribuni (kukufanyieni mtihani); ni nani miongoni mwenu mwenye vitendo vizuri zaidi. Naye ni Mwenye nguvu na Mwenye Msamaha}[AL-MULK, 2].
10. Ingawa Adam A.S. na vizazi vyake wakafanya maasi ila sisi tunaweza kusema kwamba tabia ya kibinadamu inayoweza kumfanya aelemee upande wa shari na kheri inakuwa kwa upande wa kheri zaidi kuliko shari. Huo ni mtazamo ambao unasifiwa na wanafalsafa na wana fikra kuwa ni mtazamo wa matumaini, ule mtazamo unaoafikiana na Aya za Quraani Tukufu ambazo zinampa binadamu sifa ya kuwa ni kiumbe kilichoumbwa kwa umbo lililo zuri, Mwenyezi Mungu Anasema: {Bila shaka Tumemuumba mwanadamu kwa umbo lililo bora kabisa}[Al TYN, 4]. Kadhalika, mtazamo huu unakwenda sambamba na Sunna sahihi za Mtume S.A.W. ambapo zimetilia mkazo hali ya kuwa binadamu anazaliwa akiwa na hulka yake (maumbile ya Kiislamu), hulka hiyo inasifika kwa ukamilifu na usafi mbali na maafa na aibu. Kwa hiyo, hulka hiyo inamwelekeza binadamu kwa Muumbaji wake kuhakikisha kuwa anakifikia cheo cha juu zaidi cha ukamilifu wa kidini na wa kimaadili unaotakikana. Mtume S.A.W. anasema: “Kila mtoto anazaliwa juu ya maumbile (fitra) Na wazazi wake humfanya awe yahudi, mkiristo au mshirikina … ”(imepokelewa na Imamu Bukhari 1293 na Imamu Muslim 2658 kutoka kwa Abu Huraira R.A.).
11. Hapa inawezekana kabisa kuifananisha nafsi ya Binadamu katika asili yake (asili ya kuumbwa kwake) kuwa ni kama mbegu nzuri ambayo Mwenyezi Mungu Ameiwekea ndani yake sifa na nyenzo za makuzi na hatimae kutoa matunda yake; kwa hivyo mbegu hizo zimeandaliwa katika asili ya kuwepo kwake kwa ajili hiyo, lakini ukuaji huo na utoaji wa matunda yake maana una masharti yanayopelekea kufanikiwa kwa masharti za mazingira bora yanayofaa kwa ajili yake, na yanaporahisika, hutokea katika ulimwengu huu kile kilichokuwa undani wake, na katika hali hii nafsi imeandaliwa kwa ajili ya kheri, tena inakuwa na utashi wa kuelekeza kheri lakini mazingira yanayomzunguka binadamu pamoja na jamii yanaweza kumpotoa binadamu huyo.
12. Hilo halimaanishi kwamba nafsi inashikamana na maadili kwa njia ya msukumo wa kimaumbile, bali inahitaji uvumilivu na juhudi kwa ajili ya kuyasifikia hayo.
13. Kutokana na yaliyotangulia, inaonekana wazi kuwa uhusiano wa binadamu na maadili unatuwezesha kusema kwamba binadamu ni kiumbe mwenye maadili.
Rejeo: Prof. Abdel Hamid Madkur, Chunguzi katika Elimu Maadili, Cairo, Dar Al Hany, 2005, uk. 1: 5 (imechukuliwa kwa kifupi).