Mwanamume Humwosha Mke Wake aliyefa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Mwanamume Humwosha Mke Wake aliyefariki Dunia.

Question

Je, Inajuzi kwa mwanamume kumwosha mke wake?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Kuosha katika lugha ya kiarabu ni: mzizi wa ameosha kwa kuweka shadda (mkazo), kwa maana kwamba; ni kuondosha uchafu katika kitu kwa kumwagia maji juu yake. Na katika istilahi za wanazuoni: ni kueneza maji katika mwili wa maiti kwa njia ya Sunna. Na kuzika katika lugha maana yake ni kufunika na kusitiri, yasemwa kuwa: amemzika maiti yaani amemsitiri na ameuzika mwili wake: kwa maana kuwa ameuficha. [Lisaan El Arab 1397/17, kidahizo cha Dafan, Ch. Dar Al Maarif]
Na maana yake katika istilahi ni kumzika maiti kaburini. [Al Sharhu Al Kabeer kwa Al Darderiy 407/1, Ch. Eisa Al Halabiy]

Na kumuosha maiti na kumzika ni faradhi ya kutoshelezeana ambapo watakapoifanya baadhi ya watu basi jukumu lake litafutika kwa wengine pia. Ad Darderiy amesema katika kitabu cha [As Sharhu Al Kabeer kwa Muhtasari wa Khalil]: "Na Swala juu yake ni faradhi ya kutoshelezeana kama vile kuzika kwake na kumvika sanda" [As Sharahu Al Kabeer 407/1, Ch. Eisa Al Halabiy]. Na Al Bukhariy walisimulia kutoka kwa Hadithi ya Umm Atia Nasibah Al Ansaariyah, kwamba alisema: Binti mmoja miongoni mwa mabinti ya Mtume S.A.W. alikufa, basi akatoka Mtume na akasema: "Mwosheni mara tatu au mara tano au zaidi ya idadi hiyo iwapo mtaona hivyo, kwa maji na majani ya mkunazi, na mlifanye josho la Mwisho liwe kwa kafuri au kitu kinachotokana na hiyo kafura"

Na Abu Dawud alipokea Hadithi kutoka kwa Al Hasswen Bin Wahawah kuwa Twalha Bin Al Baraa alipata ugonjwa basi Mtume S.A.W. alikuja kwake kwa ajili ya kumhudumia na akasema: "Mimi simuoni Twalha isipokuwa amepatwa na umauti, basi nipeni idhini mimi kwa ajili yake na muharakishe kwani haifai kwa mfu mwislamu afungiwe kati ya pande mbili za kuta za watu wake"

Na hamwoshi mwanamake isipokuwa mwanamke mwenzake, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu aliharamisha kuutazama uchi wa mwanamke na kumgusa mwili wake. {Waambie Waumini wanaume wainamishe macho yao, na wazilinde tupu zao. Hili ni takaso bora kwao.} [An Nuur 30]

Na AS Syutiy alipokea Hadithi katika kitabu cha [Al Jaami'I Al Sagheer] kutoka kwa Maqal Bin Yasaar Al Mazniy: "Ni bora kwa mtu achomwe kwa sindano ya chuma katika kichwa chake kuliko kumgusa mwanamke asiye halali kwake."

An Nawawiy amesema katika kitabu cha [Raudhat At Twalibeen] "Basi kwa hiyo asili ni kwamba wanaume wawaoshe wanaume wenzi wao na wanawake wawaoshe wanawake wenzi wao ni bora zaidi kuliko mwanamke kuoshwa kwa hali zote nyingine" [Raudhat At Twalibeen kwa AN Nawawiy 105/2, Ch. Al Maktab Al Islamiy]

Na inajuzu kwa mume kumwosha mke wake hata kama hakumwingilia baada ya kufunga nae ndoa, Ibn Majah amepokea Hadithi kwamba Mtume S.A.W. alimwambia Bi Aisha R.A.: "Nini kitakachokudhuru kama lau wewe ungelifariki kabla yangu na mimi nikakusimamia na nikakuosha, nikakuvika sanda nikakuswalia na nikakuzika" Basi Mtume S.A.W. akajiwekea jukumu hilo juu yake, na hiyo ni dalili ya kujuzu ya kumwosha mke wake.

Ibn Al Munzer alipokea Hadithi: Kwamba Ali Bin Abi Twalib Mwenyezi Mungu autakase uso wake, alimwosha Bi Fatuma R.A. na masahaba wote walikubaliana juu ya tukio hilo.

Al Sheikh Zakariya Al ansaariy alisema katika kitabu cha [Sharh Manhaju Al Twulaabi] "Na mke ana haki ya kumwosha mume wake, kwani katika ndoa yao umauti hauondoshi haki, kwa kuwepo dalili ya kurithiana" [Sharh Manhaja Al Twlaabi kwa Al Sheikh Zakariya Al Nsaariy150/ 2, Ch. Dar Al Fikr].
Ibn Qudamah amesema katika kitabu cha [Al Mughniy]: "Na Hadithi mashuhuri kutoka kwa Imamu Ahmad ni kuwa: mume anapaswa kumuosha mke wake". Na hili ni tamko la Alqamah, na Abdulrahmaan Bin Yazid Bin Al Aswad, na Jaber Bin Zaid, na Sulaimaan Bin Jasaar, na Abiy Salmaha Bin Abdulrahmaan, na Qatadah, Hammad, Malik, Al Awzaiy, Al Shafiy na Ishaaq; "Na kwa kuwa ni mmoja wa wanandoa wawili basi amehalalishiwa kumuosha mwenzake, na maana iliyomo ndani yake ni kwamba kila mmoja kati ya wana ndoa wawili ni rahisi kwake kumwangalia mwenzake uchi wake pasina ya kuwa hivyo kwa mtu baki kwa jinsi walivyokuwa wakati wa uhai wao. Na humuogesha mwenzake vizuri zaidi kutokana na kuwa na upendo na huruma kwake" [Al Mughniy kwa Ibn Qudamah 290/2, Ch. Maktabat Al Qahirah]

Al Kharashiy almesema: "Na wana ndoa wawili wametangulizwa kama ndoa yao ilikuwa sahihi isipokuwa ikitolewa fatwa ya kuiharibu ndoa hiyo, kwa hukumu za kisheria inamaanisha kwamba kila mmoja kati ya wana ndoa wawili atakapokufa mmoja wao basi ajitangulize katika kumuosha mwenzake kwa kuwatangulia walezi wake wote na hukumu itatolewa ikimpendelea yeye kama patatokea mvutano kati yake na walezi, kwani yule ambaye haki ya asili imemthibitikia, basi anapendelewa na hukumu. Hii ni kama ndoa itakuwa sahihi baina yao, iwe pametuka ujenzi au hapana." [Sharh Al Kharashiy juu ya Muhtasari wa Khalil 114/ 2, Ch. Dar Al Fikr].

Na kama hawakupatikana wanawake wa kumuosha na wala hakuna mume basi ataoshwa na ndugu wa karibu kwani inajuzu kwa ndugu huyo kumwangalia na inajuzu pia kumgusa katika uhai wake, na hali hii ya kujuzu haikatishwi na kifo, na atamkosha kwa sharti la kutomgusa kwa mkono mtupu isipokuwa kwa kitambaa kizito atakachokizungushia mkononi mwake na atamwosha akiwa chini ya nguo ili izuie kumwangalia.

Al Kharashiy alisema katika kitabu cha [Sharh Muhtasari wa Khalil]: "Kisha atamwosha ndugu wa karibu katika wanaume, chini ya kitambaa kizito atakachokizungushia mkononi mwake na atamwosha akiwa chini ya nguo ili izuie kumwangalia na wala hatamgusa kwa mkono wake mtupu." [Sharh Al Kharashiy juu ya Muhtasari ya Khalil 117/ 2, Ch. Dar Al Fikr].

An Nawawiy amesema katika kitabu cha [Raudhat Al Twalbeen]" "Na uwazi wa maneno ya Al Ghazaliy ni kujuzisha wanaume ndugu wa karibu kuwaosha wanawake pamoja na kuwa wanawake wapo, lakini wafuasi wote kwa ujumla wa madhehebu ya Shafi wanasema kuwa ndugu wa karibu baada ya wanawake, ni bora zaidi [Raudhat At Twalibeen kwa AN Nawawiy 103/2, Ch. Al Maktab Al Islamiy].

Na ikiwa wanawake hawatapatikana, wala mume au ndugu wa karibu, basi mwanaume asiye ndugu amsafishe mwanamke kwa tayamamu kwa kumpangusa uso na mikono yake. Na dalili ya hayo ni yale yaliyopokelewa na Al Bihaiqiy katika kitabu cha [Al Sunan Al Kubra] kutoka kwa Makhuol kwamba Mtume S.A.W. alisema: "Pindi anapokufa mwanamke akiwa na wanaume na hakuna mwanamke mwingine isipokuwa yeye, na akifa mwanaume akiwa na wanawake na hayuko na mwanaume isipokuwa yeye aliyekufa tu, basi watamsafisha maiti kwa tayamamu na kumzika. Nao watakuwa katika hukumu ya mtu asiyekuwa na maji" Na kwa kuwa kumwosha maiti ni amrisho na usafi kwa njia ya Tayamumi ni mbadala wa josho na maeneo ya tayamumi sio maeneo ya uchi. [Tazama: Bidayat Al Mujtahed kwa Ibn Rushd 241/1, Ch. Dar Al Hadithi]

Ad Darder akasema katika kitabu cha [As Sharhu Al Sagheer]: Kisha kama hakuna ndugu wa karibu basi maiti itasafishwa kwa tayamamu hadi katika nguyu mbili za mkono na wala sio vifundo viwili vya miguu. [As Sharhu Al Sagheer kwa Ad Darder 545/1, Ch. Dar Al Maarif].

Ibn Qudamah alisema katika kitabu cha [Al Mughniy]: "Na iwapo mwanaume atafariki dunia akiwa kati ya wanawake wasio ndugu wa karibu au mwanamke akafariki akiwa na wanaume wasio ndugu wa karibu au alikufa katika mazingira ya Kuwa kwake huntha asiyejulikana vyema, basi atasafishwa kwa tayamamu." Na hili ni tamko la Saidi Bin Al Musaib, Al Nukhaiy, Hammad, Malik, na wenye rai, na Ibn Al Munzer, kwa kwa Hadithi iliyopokelewa na Tammam Ar Raziy katika kitabu cha [Fawaid] kwa isnadi yake kutoka kwa Mak-huuli, kutoka kwa Wailah alisema: Mtume S.A.W. anasema: "Iwapo mwanamke atafariki hali ya kuwa na wanaume na hakuna kati yao mtu wa karibu basi atasafishwa kwa tayamamu kama wanavyofanyiwa wanaume". Kwani josho bila ya kugusa halisafishi na wala haliondoshi najisi bali huwenda iliongezeka na hawezi kukwepa usingaliaji kwa hiyo kutumia tayamamu ni bora zaidi kama vile hakuna maji. [Al Mughniy kwa Ibn Qudamah 391/2, Ch. Maktabat Al Qahirah]

Ama atakaemzika mwanamke na kumbeba katika maziko na kumshusha kaburini ni ndugu zake wa karibu katika wanaume na watangulizwe wa karibu zaidi, pamoja na mume wake, nao ni wale ambao ilikuwa inaruhusiwa kwao kumuona wakati wa uhai wake na alikuwa akiweza kusafiri nao. Kwa Hadithi iliyopokelwa na Al Khalal katika [Sanad yake] kutoka kwa Omar R.A. kwamba alisimama kwenye Mimbari ya Mtume S.A.W. alipokufa Zainab Binti Jahsh R.A. na akasema; "Hakika mimi nimemuagiza mtu katika wanawake atakaemwingiza kaburini, nao wakamtuma: aliyekuwa na ruhusa ya kumwona maiti wakati wa uhai wake nikawaona wamesema kweli" [Tazam; Al Mughniy kwa Ibn Qudamah 383/2, Ch. Dar Al Kitaab Al Arabiy].

Kwani mke wa Omar Radhi za Mwenyezi Mungu ziwafikie wote wawili, alipofariki dunia Omar aliwaambia ndugu zake: "Nyinyi mna haki zaidi kwake; kwa kuwa wao ni watu bora zaidi kwa usimamizi katika uhai wa marehemu na hivyo ndivyo inavyokuwa katika umauti wake, kisha mume; kwa sababu yeye ni sawa na ndugu zake wa karibu kwa nasaba kuliko mtu asiyekuwa ndugu yake, na kama hakuna kati yao watu wa karibu basi hapana ubaya wowote kwa wasio ndugu kumweka kaburini na wala hapahitajiki kuwaleta wanawake mazikoni". Kwani Mtume S.A.W. katika hadithi iliyopokelewa na Al Bukhariy kutoka kwa Anas Bin Malik R.A. kuwa alipokufa binti yake akamwomba Aba Twalaha, basi nae akashuka kaburini mwa binti yake, na yeye sio ndugu, [Tazama; Al Mughniy cha Ibn Qudamah 383/2, Ch. Dar Al Kitaab Al Arabiy].

An Nawaiy alisema: "Ni sunna maiti kuwekwa chini ya kaburi kwa namna ambapo kichwa chake kinakuwa mbele ya mtu aliye kaburini kisha anageuzwa upande wa kichwa chake mgeuzo mdogo. Na hawaingii kaburini isipokuwa wanaume tu wakiwapo. Awe marehemu huyo ni mwanaume au mwanamke. Na wabora wao kwa maziko ni wabora wao katika swala isipokuwa mume ana haki zaidi ya kumzika mkewe kisha baada yake ni ndugu wa karibu, ambao ni baba, babu, mtoto wa kiume, kisha mtoto wa kiume wa mtoto wa kiume, kisha kaka, kisha mtoto wa kaka, kisha baba mdogo, na kama hakuna yeyote kati ya hao, basi ndugu wa upande wa kikeni ambao hawana usimamizi watachukua nafasi hiyo. Na kama hawapo basi watu wema wasio ndugu." [Raudhat At Twalbeen kwa An Nawaiy 133/2 Ch. Al Maktab Al Islamiy].

An Nafrawiy Al Malikiy amesema: "Akataja mwenye Risala kama vile Khalili: Kumtanguliza mmoja wa wana ndoa katika kumwosha mwenzake, na wakanyamazia iwapo aliyekufa aliwahi kutaka rafiki yake ateremke kaburini. Na wengine wakabainisha jambo hili kwa kusema kuwa: kama aliye hai ni mume basi hakika atatangulizwa katika kumteresha mke wake kaburini. Atawatangulia wengine kwa maamuzi ya kisheria. Ama kwa upande wa mke, yeye hatangulizwi kumshusha mume wake kaburini bali jambo hili ni la walezi wake" Ibn Arafah amesema: Na mume ana haki zaidi ya kuuingiza mwili wa mke wake kaburini na kama haikuwa hivyo basi ndugu zake wa karibu na kama hawapo basi imesemwa kuwa ni wanawake na ikasemwa kuwa ni watu wema. [ Al Fawakeh Al Dawani Sharh Ar Resala 287/1, Ch. Dar Al Fikr].

Na juu ya hivyo: ni bora kwa mwanamke kumuosha mwanamke mwenzake, na inajuzu kwa mume kumwosha mkewe, na kama hakuwapo, basi wanaume ndugu wa karibu wa marehemu watafanya hivyo. Na mwanaume atakaemkosha mwanamke nduguye wa karibu asitumie mikono mitupu bali atajifunga kizuizi kama vile kitambaa, na wala hatamwangalia bali atamwosha akiwa amefunikwa na nguo mwili mzima, na pindipo atakuwa sio ndugu wa maiti na hakupatikana wa kumuosha maiti huyo basi atamsafisha kwa tayamamu, kwa kumpangusa uso na mikono yake miwili kwa udongo ulio safi na anayemzika mwanamke ni ndugu zake wa karibu wa kiume pamoja na mume wake na hao ni bora zaidi kwake. Na kama hakuna mume wala ndugu wa karibu basi watu wema wanaofaa kufanya kazi hiyo watamzika.
Na Mwenyezi Mungu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas