Uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu...

Egypt's Dar Al-Ifta

Uwezekano wa kumuona Mwenyezi Mungu Mtukufu

Question

Je, inawezekana kumuona Mwenyezi Mungu katika maisha haya ya Dunia na maisha baada ya kifo?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:
Maana ya kuona katika Lugha ni: kuangalia kwa jicho au kwa moyo. Al-Zubaidiy amesema katika kitabu cha [Tajul- Arus, 38/102] na kinachofuatia baada yake, ni mlango wa herufi ya "Yee" somo la herufi ya "Raa". Baraza la Taifa la Utamaduni na Sanaa la Kuwait: "(Kuona) ni: kufahamu kinachotazamwa, na jambo hili lina aina kadhaa kwa mujibu wa nguvu ya nafsi: Kwanza: kuangalia kwa jicho, ambalo ni kiungo cha hisia, na kila kinachofanana na hali hiyo. Na kuhusu jambo hili, Mwenyezi Mungu anasema: {Na sema: Tendeni vitendo. Na Mwenyezi Mungu, na Mtume wake na waumini wataviona vitendo vyenu.} [AT TAWBAH: 105] basi aina hii inazingatiwa kama kuona kwa jicho, kwa hiyo kumuona Mwenyezi Mungu kwa kiungo cha hisia ambacho ni jicho hakuwezekani. Kwa hivyo, Mwenyezi Mungu anasema: {Hakika yeye na kizazi chake wanakuoneni, na nyinyi hamuwaoni} [AL AARAF: 27], na aina ya pili ni: Kuona kwa mawazo na kufikirika, kwa mfano kama nikisema: Naona kwamba Zaid anakwenda. Aina ya tatu ni: Kama Mwenyezi Mungu anavyosema: {Mimi naona msiyo yaona} [Al-Anfal: 48]. Na aina ya nne ni: Kuona kwa moyo, yaani kwa akili, kama Mwenyezi Mungu anavyosema: {Moyo haukusema uwongo kwa uliyo yaona} [AN-NAJM: 11] na pia kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na akamwona mara nyingine} [AN-NAJM: 13].
Abu Hilal amesema katika kitabu cha: [Al-Furuq, uk. 263, Taasisi ya uchapishaji ya kiislamu nchini Iran]: “Kuona katika lugha kuna njia tatu: Ya kwanza ni: Kuona, kama Mwenyezi Mungu alivyosema: {Na Sisi tunaiona iko karibu} [AL-MAARIJ: 7] yaani:. Tunafahamu Siku ya Kiama, hivyo, kila kinachokuja ni karibu, ya pili ni: Kwa maana ya dhana, kama Mwenyezi Mungu anavyosema {Hakika wao wanaiona iko mbali} [AL-MAARIJ: 6] yaani: wao wanaidhani tu, na hali hii haina maana ya kufahamu; kwa sababu haiwezekana kuwa wao wanaijua kuwa iko mbali ambapo ni karibu kwa ujuzi wa Mwenyezi Mungu, na kutumia neno "kuona" katika njia hizi mbili ni kwa maana iliyoazimwa. Na ya tatu ni: Kuona kwa jicho nayo ni uonaji wa kweli”.
Wanazuoni wa Elimu au Tauhidi wametofautiana kuhusu kuainisha maana ya kuona, ambapo wafuasi wa madhehebu ya Sunni wanasema ni: Nguvu ambayo Mwenyezi Mungu anawajaalia viumbe wake, na wala hakuna sharti ndani yake la kuwasiliana mionzi ya jua, au kukutana na kinachoonwa au chochote kingine, hakika kuona ni aina ya kutambua ambako Mwenyezi Mungu Mtukufu anaumba wakati wowote anaotaka na kwa chochote anachotaka [Rejea: Ithaf Al-Murid Sharhu Jawhartul Tawhiid na Abdul Salam Al-Laqany, uk 202, Dar Al-kutub Al-Elmiya.
Suala la kumuona Mwenyezi Mungu ni miongoni mwa masuala ambayo wanazuoni wametofautiana kati ya Madhehebu ya Sunni, Al-Ashairah na Maaturidiyah, na madhehebu mengine ya Kiislamu miongoni mwao Al-Muutazilah, Mashia na Ibadhi.
Masunni wamekubaliana bila ya upinzani kwamba kumuona Mwenyezi Mungu, kunaingia katika vitu vinavyowezekana, na kwamba akili haizuii kuwa waja watamwona Mola wao, na suala hili ni miongoni mwa masuala ambayo kutofautiana ndani yake hakupelekei ukafiri au kuritadi ingawa kwenda kinyume na Masunni kunapelekea maasi na kutoka kwenye haki.
Na wanaokanusha suala la kumuona Mwenyezi Mungu wamesema kuwa: Kuona ni hisia ya picha ya kinachoonekana ndani ya mboni ya macho, na miongoni mwa masharti ni kuwepo kwa anayetazamwa katika upande maalumu wa pahala, mpaka mboni ya macho iweze kumwona. Inajulikana kwamba Mwenyezi Mungu si umbo wala hakuna upande wowote unaomzunguka, na kwa hivyo, kusudio lao la kuona linakuwa ni kwa maana inayopatikana kati ya viumbe, ambayo inahitaji kuwepo kwa upande, upande mwingine na pia mambo mengine ambayo yanahitaji kufananishwa, ambayo Mwenyezi Mungu anaepukana nayo.
Al-Kramiyah na Al-Mujassimah, wamejuzisha kumwona Mwenyezi Mungu kwa kumuelekea; kwa kuamini kwao kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu yukatika mwelekeo na mahali maalumu, na jambo hili linakiuka imani waliyonayo waislamu wote
Kwa madhehebu ya Al-Ashairah hakuna mfungamano kati ya kuona na kufananisha, kwa hivyo wao wanathibitisha kumwona Mwenyezi Mungu lakini siyo kama jinsi tunavyoviona vitu mbali mbali duniani kwa hiyo jinsi uonaji unavyopatikana hii leo hauwi isipokuwa kwa namna miongoni mwa namna nyingi. Mwenyezi Mungu aliyetukuka alikuwa na anaendelea kuwa na uwezo wa kufungamanisha uhakika wa kuona kama atakavyo, na imekuwa kawaida yetu katika kuonana sisi kwa sisi –kwa maana ya: yale yanayotuka kati ya matukio na mambo yawezekanayo– pawepo na utangulizi unaoambatana na wazo la picha inayoonekana katika jicho la mtazamaji, na hali hii huwa kile kinachoonekana kinakuwa upande mwingine wa yule anayekiona kwa mkabiliano wa kieneo , na umbali kati ya mwonaji na kinachoangaliwa ukawa na kiwango maalumu kwa mujibu wa uwezo wa macho, yawe macho hayo yana nguvu au dhaifu, kisha pakatokea mchoro wa picha inayoangaliwa mbele ya macho ya mwenye kuona, au kutoka nuru kwenye macho ya mwenye kuona na kuelekea kwenye kile kinachoonekana, na hayo yote hayatokei isipokuwa kwa upande wa muafikiano wa kawaida, na wala siyo kwa njia ya kushurutika kiakili. Mwenyezi Mungu aliyetukuka ana uwezo wa kuumba picha ya kitu chochote bila ya utangulizi huu, kwa hiyo basi utangulizi huu siyo sharti la kiakili ambalo haiwezekani kwenda kinyume nalo bali hii ni aina ya mipangilio ya kawaida inayopatikana kwa utashi wa Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kama Mwenyezi Mungu Mtukufu angetaka kutoyafanya hivyo basi angelifanya.
Sheikh Mohammed Al-Husseini Al-Zawahri anasema, “Maana ya kuona ambako tunadai kwamba inajuzu: Ni hali ambayo binadamu hupata wakati wa kuona jambo baada ya kulifahamu, kwa hiyo anatambua tofauti kati ya hali hizi mbili, na kwamba tofauti hii haitokani na kuchorwa kwa picha ya kinachoonekana katika macho, au mawasiliano ya nuru kutoka kwenye macho kwenda kwa kinachoonekana, bali ni hali nyingine iliyo tofauti na elimu, inaweza kupatikana bila ya kuchoreka picha na kutoka miale ya mwangaza ambayo Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaumbia viumbe hai. Na wala hapashurutishwi mwanga, mkabiliano au chochote kingine kisichokuwa viwili hivi miongoni mwa masharti” [Al-Tahkik Al-Taam fi elmul-Kalaam uk 97].
Kwa hivyo basi, kumuona Mwenyezi Mungu Mtukufu siku ya Kiyama, maana yake:
Ni yeye kujifichua kiukamilifu siku ya Kiyama kwa waja wake waliomuamini. Na wala sio lazima kuoneka kwake Mwenyezi Mungu Mtukufu kuwe kwa upande maalumu, kwani ametakasika Mwenyezi Mungu na jambo hilo.
Bali waumini watamuona si kwa upande maalumu, kama wanavyofahamu kuwa yeye Mwenyezi Mungu hana upande maalumu. Daktari Mohamad Al-Butwiy anasema: "Pamoja na kuwa Mwenyezi Mungu Mtukufu hana umbo wala uwepo katika upande miongoni mwa pande mbali mbali, hakika ni kwamba kuna uwezekano akaonekana kwa ajili ya waja wake, muonekano kama wa mbalamwezi, kama ilivyopokelewa katika Hadithi Sahihi, na watamuona mwenyewe muonekano wa kweli sio wa kufananisha. Na muonekano huu, kwa utashi wa Mwenyezi Mungu, utapatikana bila ya kuwapo masharti yeyote ya kuonekana kwake. [Kobra Al-Yaqinaat Al-Kawniyah 171,Dar Al-Fikr Al-Muasir]
Madhehebu ya Sunni yametoa dalili ya uwezekano wa kumwona Mwenyezi Mungu siku ya mwisho katika Qur’ani, Hadithi na makubaliano ya wanavyuoni:
Kuhusu dalili zao, wametoa dalili kutoka katika aya nyingi:
Dalili ya Kwanza: Ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Zipo nyuso siku hiyo zitakazong'ara * Zinamwangalia Mola wao Mlezi} [ALQIYAMAH: 22.23]. Dalili katika aya hii ni kwamba: Maana ya kuona ni kutazama kama walivyosema Masunni, au ni kugeuza mboni ya macho kuelekea kinachoonekana kwa ajili ya kukiona. Maana ya kwanza ndiyo inayotakiwa, na maana ya pili haiwezekani kuzingatiwa kwa maana yake iliyo wazi, kwa sababu kugeuza mboni ya macho kuelekea kinachoonekana kunalazimisha kuwapo katika upande na mahali maalumu, kwa maana ya pili ya kuona. Na kutamkwa sababu na kukusudiwa msababishaji ni miongoni mwa njia za Maana iliyoazimwa [Al-Tahkik Al-Taam fi Elmul Kalaam uk. 97].
Aya ya pili: Ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi} [MUTAFFIFIN: 15].
Dalili yao ni: Kwamba Mwenyezi Mungu amewaambia makafiri wote kwa vitisho katika aya hii kwamba wao hawaoni kama hii ni adhabu kwao. Na hiyo inaonesha kuwa waumini hawazuiliwi na Mola wao, au itakuwa hakuna faida katika kutaja habari za makafiri kwa vitisho hivyo.
Dalili ya tatu: Ni kauli ya Mwenyezi Mungu: {Kwa wafanyao wema ni wema na zaidi} [YUNUS: 26]. Wema: Ni pepo, na hii ziada: Ni kuuangalia uso wake Mola Mtukufu kama walivyosema wataalamu wengi wa Tafsiri. [Rejea: Tafsiri ya Al-Alusi 11/102, Dar Ihiyaa Al-turaath Al-Arabi].Tafsiri hii inatia nguvu Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Suhayb (R.A) kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, (S.A.W) anasema: "Wakishamalizika watu wa Peponi kuingia Peponi, Mwenyezi Mungu atawauliza: “Mnataka kitu chochote kingine cha ziada?” Watajibu: “Si Umeshasafisha nyuso zetu! Umeshatuingiza Peponi, na Umeshatukinga na Moto!" "Basi Mwenyezi Mungu Atainua pazia ili wamuone!” Watajua kwamba hawajapata kupewa kitu chochote kizuri kuliko kupewa uwezo wa kumuona Mola wao Mlezi!". [Imepokewa na Muslim].
Aya ya nne: {Na alipo kuja Musa kwenye miadi yetu, na Mola wake Mlezi akamsemeza, alisema: Mola wangu Mlezi! Nioneshe nikutazame. Mwenyezi Mungu akasema: Hutoniona. Lakini utazame huo mlima. Ukibaki pahala pake basi utaniona. Basi alipo jionesha Mola Mlezi wake kwa mlima, aliufanya uvurugike, na Musa akaanguka chini akazimia. Alipo zindukana alisema: Subhanaka, Umetakasika! Natubu kwako, na mimi ni wa kwanza wa Waumini} [AL-AARAF: 143]. Wametoa dalili ya Aya hii kwa njia mbili:
Ya kwanza ni: Kwamba Mussa (A.S) alimwomba Mola wake amwone, na kama jambo hili haliwezekani, basi swali la Mussa lilikuwa na ujinga au ubatilifu; kwa sababu Mtume anajua nini kilicho wajibu kwa Mwenyezi Mungu, kilicho muhali na kinachojuzu. na kwa hivyo basi, haijuzu kwa yeyote katika Mitume kutokijua kitu chochote katika hukumu za Uungu, lakini kitendo cha Mussa (A.S) kuomba kumwona Mwenyezi Mungu tu, ni dalili ya kwamba jambo hili linajuzu.
Ya pili ni: Kwamba kumwona Mwenyezi Mungu kunategemea jambo linalowezekana, Mwenyezi Mungu Mtukufu amelifanya jambo hili la kuona litegemeane na utulivu wa mlima pale yeye Mtukufu atakapojitokeza mbele ya mlima huo, na hili ni jambo linalowezekana kama lilivyo kidharura, kwani utulivu wa mlima kwa upande wake ni jambo linalowezekana, na kila kinachotegemeana na kinachowezekana hakiwi isipokuwa kinawezekana, na kwa hiyo kinakuwa kile kilichotegemeana na utulivu wa Mlima kuwa kinawezekana, kwa hiyo kumwona Mwenyezi Mungu Mtukufu kunawezekana.
Pia wametoa dalili za Hadithi zifuatazo:
Ya kwanza: Imepokewa kutoka kwa Jarir Ibn Abdullah kwamba amesema: Tulikuwa pamoja na Mtume, (S.A.W) na siku moja nyakati za usiku akaingalia mbalawezi, yaani mwezi uliokamilika, akasema: "Hakika nyinyi mtamwona Mola wenu kama mnavyouona mwezi huu pasipo na tabu yoyote ya kumwona, na ikiwa mtaweza kumcha kwa sala kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa kwake. Basi fanyeni hivyo. kisha akasoma: {Na mtakase kwa kumsifu Mola wako Mlezi kabla ya kuchomoza jua na kabla ya kuchwa} [QAAF: 39]". [na Hadithi hii imekubaliwa].
Ya pili: Imepokelewa kutoka kwa Jarir Ibn Abdullah kwamba alisema: Mtume, (S.A.W) amesema: ((Hakika mtamuona Mola wenu kwa uwazi)) [Imepokewa na Al-Bukhari].
Dalili yao katika Hadithi hizi mbili ni wazi, Ibn Al-Qayyim amesema: “Hadithi za Mtume zinazothibitisha kuonwa kwa Mwenyezi Mungu ni nyingi, zimepokelewa kutoka kwa Abu Bakr, Abu Huraira, Abu Said Al-Khudry, Jarir Ibn Abdullah Al-Bajali, Suhayib Ibn Sinan Al-Roumi, Abdullah Ibn Masoud Al-Hadhli, Ali Ibn Abi Talib, Abu Musa Al-Al-Ashiariy, Adi Ibn Hatim Al-Tai, Anas Ibn Malik Al-Ansariy, Buraidah Ibn Husayb Al-Aslamiy, Abu Raziin Al-Aqaili, Jabir Ibn Abdullah Al-Ansariy, Abu Umamah Al-Bahli, Zaid Ibn Thaabit, Ammar Ibn Yasir, Aisha, mama wa waumini, Abdullah Ibn Omar, Omara Ibn Rouibah, Salman Al-Farisiy, Huzaifa Ibn Al-Yaman, Abdullah Ibn Abbas, Abdullah Ibn Amr Ibn Al-Aas, na Hadithi yake ina hukumu ya Mauquufu, na Ubai Ibn Kaab, Kaab Ibn Ojarah, Fudhalah Ibn Obeid, na Hadithi yake ina hukumu ya Muquufu, na mtu mmoja miongoni mwa maswahaba wa Mtume lakini jina lake halijulikani. [Hadi Al-Arwah uk. 205, Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Imam Malik amesema: “Na atapowawekea kizuizi hawataweza kumwona na atajitokeza kwa waja wake wachamungu mpaka wakaweza kumwona, na kama waumini hawatamwona Mola wao siku ya Kiama basi asingeliwawekea makafiri kizuizi cha kumwona. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hasha! Hakika hao siku hiyo bila ya shaka watazuiliwa na neema za Mola wao Mlezi} [AL-MUTFFIFIN: 15]."
Imam Al-Shafiy amesema: “Wakati watu wanapozuiliwa kwa ghadhabu ya Mwenyezi Mungu, hali hii ni dalili ya kwamba kuna watu watamwona kwa kuridhika. Mohammed Ibn Al-Fadil amesema: Kama Mwenyezi Mungu alivyowazuia na kuwaweka mbali na nuru yake duniani, basi atawazuia wasimwone Akhera.” [Rejea: Ithaf Al-Muriid Sharhu Jawhartul Tawhiid, Abdul Salam AL-Llaqani, uk. 206.].
Ama kuhusu makubaliano, Maswahaba (R.A) walikuwa na kauli moja juu ya tukio la kumwona Mwenyezi Mungu Akhera, na kwamba Aya na Hadithi zilizotajwa zimezingatiwa kwa mujibu wa matini zake tu.
Sheikh Al-Husseini Al-Zawahiri anasema: “Kama vile mimi kwako wewe, baada ya kusoma sehemu hii na kutoa dalili kama ulivyoona, unaweza kuona kwamba waliyoyasema Al-Ashaariy kuhusu kumwona Mwenyezi Mungu na dalili zao ambazo zimethibitisha hivyo ni kitu kingine tofauti na suala la kumwona ambalo Al-Muutazilah wamelitolea dalili ambazo zinathibitisha kwamba si sahihi, basi labda mgogoro huu unakaribia kuwa sio halisi.” [Al-Tahkik Altaam fi Elmil kalam uk. 106].
Kuhusu kumwona Mwenyezi Mungu duniani, wanavyuoni wengi wamesema kwamba inajuzu kiakili kumwona Mwenyezi Mungu katika dunia na Akhera, na swali la Mussa kuhusu jambo hili ndilo dalili ya kujuzu kwake, ambapo hakuna Mtume yeyote ambaye hajui nini kinachoruhusiwa au kisichoruhusiwa kwa Mola wake kama ilivyoelezwa hapo kabla. Ama kuhusu kusikia hivyo duniani, Madhehebu ya Sunni yametofautiana kuhusu suala hili la kumuona kwa yeyote miongoni mwa watu hapa duniani: Baadhi yao wamesema, haikuwahi kupokelewa isipokuwa kuhusu kumwona Mwenyezi Mungu Akhera tu, bali jambo ambalo limekuja kwa kusikika kwake ni mtu yeyote katika watu kutomwona Mola wake kabla ya kufa kwake. Kwa hivyo, kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu kwamba amesema: "Jifunzeni kwamba hakuna yeyote miongoni mwenu atakaemwona Mola wake mpaka afe" [imepokelewa kutoka kwa Imam Muslim]. Wanavyuoni wengi wanaona kwamba imesikika kuwa kuna dalili ya kujuzu kumuona Mwenyezi Mungu duniani, na jambo hili halikuthibitika hapa duniani isipokuwa kwa Mtume wetu, (S.A.W), na mtazamo sahihi zaidi ni kwamba Mtume (S.A.W) amemwona Mola wake kwa macho yake mwenyewe si kwa moyo wake [Sharhu Imam Muslim kwa Al-Nawawi 3 / 5, Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabi], na miongoni mwa dalili zao ambazo ni muhimu zaidi kuhusu Hadithi ya Al-Israa na Al-Miraaj, na kauli ya Mwenyezi Mungu: {Na hatukuifanya ndoto tulio kuonesha ila ni kuwajaribu watu} [AL-ISRAA: 60]. Kuhusu Hadithi: "Jifunzeni kwamba si yoyote katika nyinyi atakaemwona Mola wake isipokuwa mpaka afe" Ingawa Hadithi hii inatoa dalili ya kwamba kumwona Mwenyezi Mungu hapa duniani, na hata kama hali hii inajuzu kiakili, lakini imezuilika kwa kusikia. Lakini anayeithibitisha hali hii kwa Mtume, (S.A.W) anaweza kusema kwamba: Mzungumzaji ambaye ni Mtume (S.A.W) haingii katika ujumuishaji wa kauli yake hii.
Abdullah bin Abbas pamoja na maswahaba wengi ni miongoni mwa wale ambao wanasema kwamba tukio la kumwona Mwenyezi Mungu kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, (S.A.W), na miongoni mwa Hadithi zilizopokelewa katika suala hili ni: “Je, mnashangaa Upendo wa Mwenyezi Mungu kuwa kwa Ibrahim?, na Mwenyezi Mungu huyo kuzungumza na Mussa? na Muhammad (S.A.W) kumwona Mwenyezi Mungu?!” Na imepokelewa kutoka kwa Bwana wetu Al-Hassan (R.A) kwamba alikuwa akiapa kuwa Muhammad (S.A.W) alimwona Mola wake. Pia imepokelewa kutoka kwa Abu Dhar na Kaab (R.A), na wengine wamesimulia Hadithi kama hii, imepokelewa kutoka kwa Ibn Masud, Abu Hurayrah, Ahmad Ibn Hanbal. Imam Al-Nawawiy anasema: “Uthibitisho wa jambo hili hawauchukui isipokuwa kwa kuusikia kutoka kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu( S.A.W) tu, na hili ni katika mambo ambayo haifai kuyatilia shaka.” [Sharhu Imam Muslim 3/5].
Bi Aisha (R.A), amekanusha kwamba Mtume (S.A.W) amemwona Mola wake katika Dunia hii, na imepokelewa suala hili kutoka kwa Abu Huraira na Ibn Masoud.
Bi Aisha (R.A), hakukanusha suala hili kwa mujibu wa hadithi yeyote ya Mtume (S.A.W), na kama alikuwa nayo Hadithi yeyote, basi angeitaja, lakini alitegemea kufahamu Aya za Qur’ani tu. Suala hili ni miongoni mwa masuala ambayo wanavyuoni wametofautiana. Ibn Taymiyyah anasema kuhusu suala hili: “Wanavyuoni wametofautiana kuhusu masuala ya kielimu na ya kiitikadi; kama vile, mtu aliyekufa kuisikia sauti ya aliye hai, na mfu kuteswa kwa kosa la jamaa zake kulia, na Muhammad kumuona Mola wake kabla ya kufa kwake. Moja kati ya masuala haya mawili ya Wanavyuoni ni kosa lisilopingika, lingine ni sahihi kwa wanavyuoni wengi, wafuasi wa Salaf, yaani waliotutangulia, na hilo lingine linapelekea kwa kile kilicho wajibu kwa mujibu wa uwezo wa kudiriki. Je mtu husemwa kuwa amepatia au amekosea? Jambo hili lina mgogoro. Na kuna watu wanaowaona kuwa watu wote wanapatia na wala hakuna hukumu yeyote katika jambo hilo hilo. Na madhehebu ya Sunni yanaona kuwa hakuna dhambi yeyote kwa mwenye kujitahidi hata kama atakosea. yanasemekana maoni haya ni sahihi au makosa? Yana migogoro”. "[Majmuu Al-Fatawa 19/122, Majmaa Al-Malik Fahd katika Riyadh].
Suala hili la –Mtume Muhammad (S.A.W) kumuona Mola wake duniani– lina ikhtilafu baina ya maswahaba wao wenyewe, na hakuna katika mlango wa Imani kinachopelekea kutoa maamuzi ya mwisho kwa kauli moja kati ya kauli mbili, ingawa sisi tunakubali katika jambo hili, mwelekeo wa maswahaba wote kisha wale waliokuja baada yao miongoni mwa wanazuoni wa kiislamu, nalo ni uwezekano wa kumwona Mwenyezi Mungu Mtukufu duniani bali kuna dalili za kutokea kwa jambo hili kutoka kwa Mtume (S.A.W)
Lakini mtu mwingine yeyote aliyedai kumwona Mwenyezi Mungu Duniani tena akiwa macho, basi huyo ni mpotezu. baadhi ya wanavyuoni wanaona kuwa mtu huyo ni kafiri. Pia hakuna mgogoro kuwa suala hili linatokea katika ndoto; Kwa sababu shetani hajitokezi katika ndoto katika picha ya Mwenyezi Mungu kama ambavyo pia hajitokezi katika picha ya manabii (A.S), Al-Khalal amesimulia katika kitabu chake: [Al-Majaalis Al-Asharah Al-Amali, uk 50, Dar Al-Sahabah Lilturath- Tanta] Imepokewa kwamba Imam Ahmad Ibn Hanmbal alimwona Mwenyezi Mungu mara tisini na tisa, alisema, na naapa kwamba nikimwona mara mia kamili nitamwuliza. Akamwona akasema: Bwana wangu Mola wangu jambo gani ambalo watu ambao ni karibu nawe wanaweza kulifanya kwa ajili ya kuwa karibu nawe zaidi? Akasema, kusoma maneno yangu. Akasema: Kwa ufahamu au pasipo na ufahamu? Akasema: Ewe Ahmad kwa ufahamu na pasipo na ufahamu.
Kwa mujibu wa yaliyotangulia hapo juu, inajuzu kiakili na kisheria kumwona Mwenyezi Mungu Akhera, kwa mujibu wa makubaliano ya wafuasi wa Madhehebu ya Sunni, lakini katika Dunia, hakuna mzozo kuhusu usahihi wake katika ndoto na kusihi kwake, masahaba na wanavyuoni waliokuja baada yao wametofautiana kuhusu kutokea au kutotokea suala hili wakati mtu anapokuwa macho. Kwa upande wa kuwa macho, maswahaba wametofautiana kuhusu kutokea au kutotokea kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, (S.A.W). kwa upande wa mtu mwingine, akidai kwamba amemwona Mwenyezi Mungu katika akiwa macho , basi huyo ni katika watu waliopotea.
Na Mwenyezi Mungu anajua zaidi.

Share this:

Related Fatwas