Kumlakinia mtu aliyekaribia kufa na...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kumlakinia mtu aliyekaribia kufa na aliyekufa.

Question

Je, ni ipi hukumu ya kisheria kumlakinia aliyekaribia kufa na aliyekufa?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, Maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya utangulizi huu:

Maana ya kulakinia ni kufahamisha kwa njia ya maneno; Ni sawa yawe matamshi au maandishi. Na pia imesemwa alimlakinia: Maana yake alimwambia maneno ili ayaseme kama alivyoambiwa. Na matumizi ya neno hili la talkini kwa wanazuoni hayaepuki maana hizi za kilugha.

Na imesuniwa kwa mtu aliyekaribia kufa kulakiniwa shahada mbili bila ya kumuamrisha kuzitaja, na kutozidisha, ili yawe ndio maneno yake ya mwisho, na kupatikana ile furaha ya kuingia peponi, na kufukuzwa Mashetani ambao huwa wanamsogelea kwa ajili ya kumuharibia imani yake na kuigeuza. Na dalili ya hayo ni kauli yake Mtume (S.A.W) aliposema: "Walakinieni ndugu zenu wanaokufa kwa Laa Ilaaha Illa llahu" [Imetolewa na Muslim.]

An Nawawiy amesema katika kusherehesha Hadithi hiyo; maana yake aliyekaribia kufa. Na lengo ni kukumbushwa kuwa Hakuna Mola mwingine anayestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu, ili yawe maneno yake ya mwisho duniani, kama ilivyotajwa katika Hadithi: "Na yeyote ambaye maneno yake ya mwisho yatakuwa Laa Ilaaha Illa llahu (Hakuna Mola mwingine anaestahiki kuabudiwa isipokuwa Mwenyezi Mungu) basi ataingia peponi. [Haithi hii imetolewa na Abu Dawud katika kitabu chake cha Sunna (3118), Na Al Haakim akaitaja katika kitabu chake Al Mustadrak na akasema kuwa Hadithi hii ina hukumu ya usahihi katika Isnadi/Utaratibu wa mapokezi yake, na hakuitoa (1247)]

Na jambo la kumlakinia mtu anayekaribia kufa ni sunna, na wanazuoni wamekubaliana juu ya Talkini hii, na wakakataza kuzidisha mno na kufululiza, ili isimsumbue kwa hali mbaya aliyonayo, na tabu ya machungu yake, basi huenda akachukizwa na hayo moyoni mwake na kuzungumza mambo yasiyofaa. Na akishaisema mara moja basi isikaririwe kwake isipokuwa atakapozungumza maneno mengine, basi atarejeshwa kwa kulakiniwa tena ili iwe ndio maneno yake ya mwisho. Na Hadithi hii inakusanya kuwepo mahali alipo mtu anayekaribia kufa, ili kumkumbusha na kumliwaza, na kuyafumba macho yake, na kumtekelezea haki zake. Na hivi ndivyo walivyokubaliana wanazuoni wote. [Sharhu An Nawawiy katika kitabu cha Sahihi Muslim 219/6, Ch. Dar Al Turaath Al Arabiy].

Anapokufa mwislamu na akawa hajalakiniwa shahada, basi hakuna ubaya wowote, na wala hali hii haimaanishi kuwa yeye sio mtu mwema. Na atakayekuwa katika uhai wake ameshikamana na dini ya Mwenyezi Mungu na sheria zake ipasavyo, na akafa katika hali hiyo, basi ni matumaini kuwa huyu ni mtu wa kheri, na hudhaniwa hivyo – Kwa utashi wake Mwenyezi Mungu – Na haswa kama alionekana kuwa ni mtu mwema mbele ya watu wote. Basi Mtume (S.A.W) lilipopita jeneza, watu walimsifu maiti kwa kheri, Mtume akasema: "Yeyote mtakaemdhania kheri basi pepo humuwajibikia". [Imetolewa na Muslim]

Na kumlakinia maiti baada ya kumzika. Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa inapendeza kufanya hivyo. Walitoa dalili kwa yaliyopokewa na Atabaraniy kutoka kwa Abu Umamah Al Bahiliy (R.A) kwamba alisema: "Kama mimi nikifa basi nifanyieni kama alivyotuamrisha Mtume (S.A.W) kwamba tuwafanyie maiti wetu. Mtume (S.A.W) amesema: Iwapo mtu mmoja miongoni mwa ndugu zenu atakufa na mkamaliza kumzika basi mmoja wenu asimame sehemu ya kichwa katika kaburi lake na aseme: Ewe Fulani mtoto wa Mwanamke fulani, hakika yeye humsikia msemaji na wala hawezi kumjibu, kisha aseme: Ewe Fulani mtoto wa Mwanamke fulani na atasema: Ametuongoza Mwenyezi Mungu akurehemu, lakini wao hawahisi. Na aseme: Kumbuka kile ulichokitoa duniani ambacho ni tamko la Shahada kuwa: Ninashuhudia kuwa hakuna Mola mwingine isipokuwa Mwenyezi Mungu na kwamba Muhammad ni Mtume wake. Na kwamba wewe umeridhia Mwenyezi Mungu kuwa ndiye Mlezi wako, na Uislamu kuwa ndio dini yako, na Muhammad kuwa ndio Mtume wako, na Qur-ani kuwa ndio muongozo wako, hakika Malaika Munkari na Nakiiri, kila mmoja kati ya Malaika hawa humshika mkono mwenzake na kusema: Tuondoke, ni nini kinachotuweka kwa yule aliyelakiniwa kama hoja kwake? Mmoja wa Maswahaba alimuuliza Mtume: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, kama mama yake hajulikani je? Akasema (S.A.W): Anasibishwe na mama yake Hawa, aitwe ewe fulani mtoto wa Hawa."

An Nawawiy amesema katika kitabu cha: [Almajmu'I 274-275/5, Ch. Dar Al Fikr] "Kundi la wafuasi wetu limesema: inapendeza kumlakinia maiti baada ya kuzikwa kwake. Mmoja akae mbele ya kichwa chake na aseme: …." Kisha akaitaja Hadithi.

Halafu akasema: "Talkini hii kwa wao inapendeza. Na miongoni mwa waliotoa kauli ya kupendeza kwake ni Kadhi Husein, Al- Mutawaliy, Sheikh Naswer Al- Muqdisiy, Al-Rafiiy na wengineo. Na imenukuliwa na Al- Kadhi Husein kutoka kwa wafuasi wetu. Na Sheikh Amru Bin Aswalah Mwenyezi Mungu Amrehemu, amesema: "Talkini ni ile tulioichagua na kuifanyia kazi, akasema: Tumepokea Hadithi kutoka Hadithi ya Abi Umamah, utaratibu wa mapokezi yake haukunyooka lakini Hadithi hiyo imetiwa nguvu na ushahidi mwingi na kwa kufanyiwa kazi na watu wa Shamu hapo zamani. Na hii ni kauli ya Abu Amru. Nilisema kuwa hadithi ya Abi Usama ilipokelewa na Abu Al Qasim Atwabaraniy, katika kitabu chake: [Al Mu'ujam] kwa utaratibu wa mapokezi yaliyo dhaifu, na tamko lake ni….. na akaitaja hii Hadithi ".

Akasema: "Nikasema: Hadithi hii hata kama ni Dhaifu inaweza kutumiwa kama kiliwazo. Na wanazuoni wa Hadithi na wengineo wamekubaliana juu ya kuruhusu matumizi ya Hadithi kwa mambo mazuri ya kuvutia na kukemea, na imetiwa nguvu kwa ushahidi mwingi wa Hadithi, kama vile Hadithi: "Na Mwombeeni msimamo thabiti" Na wasia wa Amru Bin Alaas na hayo yote mawili ni sahihi tumekwishayaeleza hapo kabla. Na watu wa Shamu bado wanaendelea kuitumia katika zama hizi na ni wenye kuifuata mpaka sasa. Na Talkini hii kiuhakika ni haki ya Maiti aliyebaleghe. Mtoto halakiniwi. Na Mwenyezi Mungu ni mjuzi zaidi"

Na Ibn Taimiyah aliulizwa juu ya Talkini ya maiti katika kaburi yake baada ya kumaliza mazishi yake, je iko Hadithi sahihi kutoka kwa Mtume (S.A.W) au kutoka na Maswahaba wake juu ya Talkini ya Maiti? Na je, kama hakuna hadithi, inajuzu kufanya Talkini au hapana?

Basi akajibu: "Talkini hii iliyotajwa imenukuliwa kutoka kwa Kundi la Maswahaba wa Mtume kwamba wao ambao waliamrishwa kuitumia, kama Abu Umamah Al Bahiliy na wengineo, na imepokewa Hadithi kutoka na Mtume (S.A.W) lakini Hadithi hiyo haina hukumu ya usahihi wake, na Maswahaba wengi hawakuwa wakifanya hayo, kwa hiyo Imamu Ahmad na wengineo wakasema: "Hakika Talkini hii haina ubaya wowote, kwa hiyo wakairuhusu, na wala hawakuamrisha kuitumia, na baadhi ya wanazuoni miongoni mwa Wafuasi wa Ashafiy na baadhi ya wafuasi wa Maliki waliifanya kuwa inapendeza kuitekeleza na wengine wakasema kuwa inachukiza".

Na yaliyopo katika Kitabu cha Sunnan kutoka kwa Mtume (S.A.W) Kuwa yeye alikuwa akisimama katika kaburi la kila Swahaba aliyezikwa na kusema: "Mwombeni kauli iliyothabiti, kwani yeye hivi sasa anaulizwa. Na imethibiti kwa Imamu Bukhari na Imamu Muslimu kuwa Mtume (S.A.W) amesema: "Walakinieni/Wasomeeni Laa Ilaaha Illa llahu, ndugu zenu wanaokaribia kufa".

Kwa hiyo kumlakinia mtu anayekaribia kuiaga dunia ni Sunna iliyoamrishwa. Na imethibiti kuwa aliye kaburini huulizwa maswali, na hutahiniwa, na kwamba tunaamrishwa kumwombea Dua. Na kwa ajili hii pamesemwa: Kwamba Talkini inamfaa Maiti, kwani yeye anasikia wito". Kama ilivyothibiti katika Hadithi Sahihi kuwa kutoka kwa Mtume (S.A.W) amesema: "Kwani yeye husikia milio ya viatu vyao", Na akasema: "Nyinyi hamsikii kwa yale niyasemayo kutokana na wao", Na Mtume (S.A.W) ametuamrisha kuwatolea salamu waliokufa na akasema: "Na haiwi kwa mtu yeyote apitae katika kaburi la mtu aliyekuwa anamjua duniani na akamsalimia isipokuwa Mwenyezi Mungu humrejeshea roho yake hadi atakapoijibu salamu hiyo". [Al Fatawa Al Kubra kwa Ibn Taimiah 24-25/3, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah]

Na kutokana na yaliyotangulia, kumlakinia mtu aliyekaribia kufa ni jambo lililothibiti na wala hakuna shaka yeyote. Na kulifanya jambo hilo ni Sunna kwa mwislamu amfanyie nduguye mwislamu wakati anapokaribia kukata roho na pia wakati wa kumzika, na yote hayo humnufaisha maiti, kwa utashi wa Mwenyezi Mungu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

Share this:

Related Fatwas