Ukatili wa Kifamilia.

Egypt's Dar Al-Ifta

Ukatili wa Kifamilia.

Question

Ni ipi hukumu ya kisheria kuhusu ukatili/unyanyasaji wa kifamilia uliodhihiri katiki kipindi cha hivi karibuni?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, masahaba wake na wanaomfuata, na baada ya hayo:

Imeenea katika zama zetu hali ya ukatili au unyanyasaji wa kifamilia, na kilichokusudiwa ni ile hali ya ukatili ambayo imezunguka tabia za mume kwa mkewe, tabia za mke kwa mumewe, tabia za wazazi wawili kwa watoto, na tabia za watoto kwa wazazi wote wawili, na pamoja na ndugu zao miongoni mwao, kisha tabia za wanafamilia kwa jirani zao, na kwa ndugu wa karibu, na katika maisha kwa ujumla. Hizi hali kumi baadhi yake au zote zimezingirwa na  ukatili, na watu wengi wanauliza kuhusu hukumu ya kisheria katika ukatili huu kwa upande mmoja, na sababu ya hali hii na namna ya kuishughulikia kwa upande wa pili. Na pia kuhusu athari zake zenye kuangamiza kwa upande mwingine.

1-   Ama hukumu ya hali hii inahesabiwa kuwa ni ukiukwaji wa vipimo vyote vya dini ya Kiislamu, sawa sawa iwe kwa mtu mmoja, au ngazi mbali mbali za kijamii. Ama kwa ngazi ya mtu mmoja, Mtume ametuamrisha kuwa wapole, katika hadithi tukufu: “Hakika Allah anaupenda upole katika mambo yote” ([1]), na akasema Mtume S.A.W.: “Hakika upole hauwi katika kitu isipokuwa utakipamba, na hauondolewi katika kila kitu isipokuwa utakiharibu”([2]), “Hakika dini hii ni imara basi iendeeni kwa upole” ([3]).

Na akatuamrisha Mtume S.A.W. kuunga undugu, kwa upande wa mume: Mtume S.A.W. alimuelekeza akasema: “Mbora wenu ni mbora wenu kwa mke wake na mabinti zake” ([4]), na Bi Aisha R.A. akamsifia Mtume kwamba: “Alikuwa katika kusaidia kazi za wakeze” ([5]), maana yake, alikuwa S.A.W. akifanya kazi kumsaidia mke katika kazi zake; akiufundisha umma wake ni vipi watafanya kazi ndani ya familia, na anasema Anas Bin Maalik: “Nimemtumikia Mtume S.A.W. miaka kumi, naapa kwa jina la Allah Mtukufu hakuwahi kunikemea hata mara moja, wala kuniambia kwa kitu kwanini umefanya hivi? Na je kwa nini usigefanya hivi?” ([6]), na akamuamrisha mke kuufanya uhusiano wake na mume wake uwe ni uhusiano wa Mungu, akitafuta thawabu za Mwenyezi Mungu kabla ya chochote. Na kutaraji kwa Mwenyezi Mungu Mtukufu amlipe duniani na akhera, kwa yale anayomvumilia. Anasema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na ingeli wadhuru nini wao lau wangeli muamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na wakatoa katika aliyo waruzuku Mwenyezi Mungu? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kuwajua vyema} [AN NISAA: 39]. Na anawaelekeza wazazi akisema: “Sio miongoni mwetu asiyewahurumia wadogo wetu” ([7]), na anawaelekeza wataoto na anafanya jambo la kuwafanyia wema wazazi wawili ni tawhid. {Na wafanyieni wema wazazi wawili na jamaa na mayatima na masikini na jirani wa karibu na jirani wa mbali, na rafiki wa ubavuni na mpita njia, na walio milikiwa na mikono yenu ya kulia. Hakika Mwenyezi Mungu hawapendi wenye kiburi wanao jifakhiri} [An-Nisaai: 36]. Kisha anawaamrisha wote kuwa na ujirani mwema, anasema: “Wallahi haamini, wallahi haamini, wallahi haamini). Ikasemwa: ni nani ewe Mjumbe wa Allah? Akasema: (Mtu ambaye jirani yake hatakuwa na amani kutokana na vitimbi vyake” ([8]), na anaamrisha kuunganisha udugu, na kufanya mambo ya kheri, amesema Mtume S.A.W.: “Enyi watu, toleaneni salamu,na lishaneni chakula, na unganisheni udugu, na salini na watu wakiwa wamelala, mtaingia peponi kwa amani”([9]), amesema Mola wetu Mtukufu: {Enyi mlio amini! Rukuuni na msujudu, na muabuduni Mola wenu Mlezi, na tendeni mema, ili mfanikiwe} [HAJJ: 77]. Na ili tusimamishe matini hizo za kisheria yatupasa kuingiza ndani ya hisia zetu thamani na maana ya kusameheana, hakika kusameheana ni njia yenye mafanikio katika kuhakikisha upole mapenzi na mashirikiano, ambayo kwa kufanya hayo tunaweza kukomesha ukatili katika familia na katika maisha yetu yote, zinapatikana matini nyingi za Quraani na Sunna katika kupandikiza mema hayo katika kuwalingania sana waumini kujipamba na tabia hizo, na mfano wa matini hizo, ni yale aliyomuamrisha Allah Mtukufu Mtume wake S.A.W. kusamehe; pale aliposema: {Na hatukuziumba mbingu na ardhi na vilivyomo ndani yake ila kwa ajili ya Haki. Na hakika Kiyama kitafika. Basi samehe msamaha mzuri} [HIJRI: 85]. Mwenyezi Mungu aliamuru msamaha katika kuuwa nafsi, akasema aliyetukuka: {Na anaye samehewa na ndugu yake chochote basi ashikwe kulipa kwa wema, na yeye alipe kwa ihsani} [AL BAQARA: 178]. Akaamrisha pia kuwasamehe wasiokuwa waislamu, na katika hali ya uhasama wa hali ya juu wa kuuchukia Uislamu, akasema Mola Mtukufu:     {Wengi miongoni mwa watu wa Kitabu wanatamani lau wangekurudisheni nyinyi muwe makafiri baada ya kuamini kwenu, kwa ajili ya uhasidi uliomo ndani ya nafsi zao, baada ya kwishawapambanukia Haki. Basi sameheni na wachilieni mbali mpaka Mwenyezi Mungu atapo leta amri yake. Hakika Mwenyezi Mungu ni Muweza wa kila kitu} [AL BAQARAH:109].

Na Mweneyezi Mungu kamuamrisha Mtume S.A.W. kuwasemehe waumini akasema: {Basi ni kwa sababu ya rehema itokayo kwa Mwenyezi Mungu ndio umekuwa laini kwao. Na lau ungeli kuwa mkali, mwenye moyo mgumu, bila ya shaka wangeli kukimbia. Basi wasamehe, na waombee maghfira, na shauriana nao katika mambo} [AL IMRAN: 159]. Akamuamrisha pia kuwasamehe Mayahudi pamoja na sifa zao mbaya, akasema Mola Mtukufu: {Basi wasamehe na waache. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema} [AL MAIDAH: 13], na akabainisha Mola wetu kuwa msamaha ndio njia ya kupata msamaha wa Allah Mtukufu akasema: {Na wasamehe, na waachilie mbali. Je! Nyinyi hampendi Mwenyezi Mungu akusameheni? Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe Mwenye kurehemu} [ANUUR: 22]. Na Mwenyezi Mungu akasifia msamaha na wale wenye kujipamba nao, akasema: {Ambao hutoa wanapo kuwa na wasaa na wanapokuwa na dhiki, na wanajizuia ghadhabu, na wasamehevu kwa watu; na Mwenyezi Mungu huwapenda wafanyao wema} [AL IMRAN: 134], akasema tena: {Na anayesubiri, na akasamehe, hakika hayo ni katika mambo ya kuazimiwa} [SHURA: 43].

2-    Hii ndiyo mifumo ya kisheria inayolinda kutokana na ukatili wa kifamilia kwa ngazi ya mtu mmoja au kuenea kwake katika jamii, kutotilia umuhimu wa kuwaelimisha vijana juu ya maana hizi, na kujenga ubinafsi hata katika kutangaza chakula na peremende kwa watoto, vinaongeza mvutano wa maisha kutokana na kelele na kasi ya harakati za mipango ya kila siku ya mwanadamu, na ukosefu wa mavazi ambayo yameakisi vibaya katika akili yake, na matatizo mengi ya kiuchumi, kijamii na kisiasa, yote haya yalikuwa ni katika sababu zilizopelekea kutengana kwa familia, tabia mbaya na kupelekea ukatili wa kifamilia.

3-   Na hapa inapatikana tiba ambayo inaanzia kwenye mchakato wa malezi, na malezi ni mchakato uliopangiliwa na unanyanja zake, na nguzo zake, haushii tu katika kufundisha wala katika kutoa mafunzo, wala haushii shuleni, isipokuwa hakuna budi kuvishikirisha vyombo vya habari, na kutengeneza utamaduni utakao enea katika jamii utakaoilinda jamii kutokana na hali hii mbaya, na kupelekea kupatikana kwa utulivu na usalama, na hii inahitaji kutilia umuhimu zaidi. Na kuna hali zilikuwepo tokea miongo minne iliyopita zilipigwa vita na kuzingirwa kwa kila njia kiasi kwamba tumekuwa hatuzisikii kwa sura ambayo ilikuwapo hapo awali, na zikazorota sana kwa sababu ya juhudi zilizotolewa kwa ajili ya kupambana na hali hizo. Miongoni mwa hali hizo ni: Tabia ya kugushi kwa pamoja, tabia ya ukatili kwa wanafunzi hasa kati ya wasichana, tabia ya uadui wa pamoja dhidi ya majengo ya shule au wanafunzi, nayo ni mambo ambayo hayapo katika kiwango kilichokuwepo hapo awali, na zinaelekea kutokomea kabisa ikiwa kama bado hazijatokomea.

Huenda Mwenyezi Mungu akazimaliza tabia hizi katika jamii zetu, na jamii zote za kiislamu, na duniani kote kwa kuwa yeye ni mpole kwa waja wake.

Chanzo: kitabu cha “Simaat Al Asri, cha Mufti wa Zamani wa Misri Dk. Ali Juma

 ([1]) Wamekubaliana juu yake; kaitoa Bukhary katika (Al Adab) mlango (upole katika kila kitu) hadithi (6024), na katika kitabu (Istiidhan) mlango (vipi utajibu salaamu kwa watu wa dhimmiy) hadithi (6256), na katika kitabu (Daawat) malango (kuwaombea dua washirikina) hadith (6395), na Imam Muslim katika kitabu (Al Salaam) mlango (Katazo la kuwaanza kwa Salaam Ahlu Kitaab) Hadithi (2165) katika Hadithi ya Aisha R.A.

([2]) Ameitoa Muslim katika kitabu (Al Birru wa Al Sillah wal Adaab) mlango (Fadhila za upole) hadithi (2594) katika hadithi ya Aisha R.A.

([3]) Ameitoa Imam Ahmad katika Musnad yake (3/198) hadithi (13074) kutoka katika hadithi ya Anas Ibn Maalik R.A., na amaitaja El Haythamiy katika (Majmaa zawaaid) (1/62) na akaisahihisha.

([4]) Ameitoa Al Bayhaqiy katika (Al Shaab) (6/415) hadithi (8720), na Ibn A’adiy katika (Kaamel) (7/265) katika hadithi ya Abu Hurairah R.A.

Hadithi( 6039).

([5])   Ameitoa Bukhary katika kitabu (Al Adab) mlango (vipi anakuwa mtu kwa watu wake?)

([6]) Wamekubaliana juu yake,ameitoa Bukhary katika kitabu cha (Al Adab) mlango (Tabaia njema na ukarimu na ubakhili unaochukiwa) hadithi (6038), na Muslim katika kitabu (Al Fadhaail) mlango (alikuwa Mtume S.A.W. ni mbora wa watu kwa tabia) hadith (2309).

([7]) Ameitoa Al Tirmidhiy katika kitabu (Al Birru wa Al Silah) mlango (yaliyokuja katika kuwaurumia watoto) hadithi (1920) kutoka katika hadithi ya Amru bin Shuaibu kutoka kwa baba yake kutoka kwa babu yake, na akasema Al Tirmidhiy: (hadithi ya Mohamad ibn Is-hak kutoka kwa Amru Ibn Shuaibu ni hadithi sahihi).

([8]) Ameitoa Bukhary katika kitabu (Al Adab) mlango (Madhambi ya mtu amabaye jirani yake hatulii kutokana na vitimbi vyake) hadithi (6016) katika hadithi ya Abi Al shuraih Al Khazaai R.A.

([9]) Ameitoa Ibn Maajah katika kitabu (Al Atiimah) mlango (kulisha chakula) hadith (3251), na Al Daaramiy katika kitabu (Asswalaa) mlango (Fadhila za swala za usiku) hadithi (1460) na katika kitbu (Al Istiidhan) malngo (kutoleana salaam) hadith (2632), na Al Haakim (Fil al Mustadrak)(3/14) hadithi (4283) na akaisahihisha kutoka katika hadithi ya Abdillahi Bin Salaam R.A.

Share this:

Related Fatwas