Mavazi ya Kiislamu Kisheria

Egypt's Dar Al-Ifta

Mavazi ya Kiislamu Kisheria

Question

Je, Uislamu umefaradhisha mavazi maalum kwa mwanamume na mwanamke? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Uislamu haukufaradhisha mavazi maalumu kwa mwanamume wala mwanamke, bali umeyaachia mazingira ya zama na wakati pamoja na mahali. Lakini Uislamu umeweka masharti kwa ujumla kwa kila vazi, na kwa hivyo basi ni lazima mavazi hayo yasitiri uchi wa mwanadamu na kuufunika mahali pake. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Enyi wanaadamu! Tumekuteremshieni nguo za kuficha tupu zenu, na nguo za pambo} [AL AARAF 26] Na mavazi hayo hayapaswi kuwa mepesi yanayodhihirisha kilicho ndani ya mwili.
Na Abu Dawud amepokea Hadithi kutoka kwa Aisha R.A. "Kwamba Asmaa Bint Abi Bakr R.A. aliingia ndani kwa Mtume S.A.W. huku akiwa amevaa nguo nyepesi na Mtume S.A.W, akamkwepa, na akasema: ewe Asmaa, Hakika mwanamke anapobaleghe na kutokwa hedhi haifai kwake kuonekana sehemu za mwili wake isipokuwa hapa na hapa, akaashiria usoni na katika viganja viwili vya mikono. Na lazima mavazi yasiwe mepesi yanayouonesha mwili kwa kuyavaa kwake.
Na Ahmad ameipokea Hadithi katika kitabu chake: [Musnad Ahmad], kutoka kwa Usama Bin Zayed R.A. Alisema: "Mtume S.A.W. alinivalisha vazi zito la Kimisri miongoni mwa mavazi aliyopewa na Duhiyat Al Kalbiy, kwa hivyo basi nikamvalisha mke wangu, basi Mtume S.A.W. akaniuliza na kusema: Kwa nini wewe hauvai vazi la Kimisri? nikamwambia; Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Nimemvalisha vazi hilo mke wangu, basi Mtume S.A.W. akaniambia hivi: Mwambie mke wako avae kitambaa kizito chini ya vazi hilo, kwani ninaogopa kwamba vazi hilo linaonesha mwili na mifupa yake.
Na hii ni dalili ya kukataza mavazi yanauonesha mwili kama ulivyo, na mwanamume na mwanamke ni sawa katika jambo hilo.
Baada ya hayo, yapo mambo mengine yanayolazimishwa katika mavazi. Miongoni mwake ni kama vile; wanaume hawaruhusiwi kuvaa mavazi ya wanawake na wanawake hawaruhusiwi kuvaa mavazi ya wanaume. Na maelezo haya ni kwa mujibu wa yaliyopokelewa na Imamu Bukhariy kutoka kwa Ibn Abaas Rafhi zake Mwenyezi Mungu ziwafikie wote wawili, akasema: Mtume S.A.W. amewalaani wanaume wanaoshabihiana na wanawake, na wanawake wanaoshabihiana na wanaume."
Na ni karaha yakawa mavazi ni yenye umaarufu na umashuhuri, nayo ni mavazi yaliyo mashuhuri kwa watu na mvaaji huashiriwa kwa vidole,ili isiwe hiyo ni sababu ya kumsengenya basi (ikiwa atafanya hivyo,mvaaji na msengenyaji) watashirikiana katika dhambi ya usengenyo.
Na katika nguo za umashuhuri inaingia kila nguo siyokuwa vazi lake la kawaida, kama vile ambaye alivaa mavazi yanayogeuza au mavazi tofauti ya mavazi ya watu wa mji wake. [Tazama: Kashafu Al Qinai kwa Al Bahutiy 279/1, Ch. Dar Al Kutub Al Elmiyah].
amepokea katika kitabu cha: [Ashuab], kutoka kwa Abi Hurairah na Zayed Bin Thabet R.A. wote wawili, kwamba Mtume S.A.W. amekataza vitu viwili inasemekana Mtume aliulizwa: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Vitu viwili mashuhuri/vinavyojulikana ni nini? Basi akasema: Nguo nyepesi na nzito yake, ulaini wake na ukwaruzo wake, urefu wake na ufupi wake, lakini ni kuwa kati baina ya mawili hayo na kutofanya israfu."
Na kadhalika inaharamishwa kwa wanaume kuvaa Hariri safi, lakina inajuzu kwa wanawake kuvaa hariri hiyo, kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa na Anasaiy kutoka kwa Abi Musa kwamba Mtume S.A.W. amesema: "Hariri na dhahabu zimehalalishwa kwa wanawake wa Umma wangu na zikaharamishwa kwa wanaume wa umma huu."
Na kwa Hadithi iliyotolewa na Ibn Majah kutoka kwa Ali R.A.: "Kwamba Mtume S.A.W. alichukuwa dhahabu katika mkono wake wa kulia na Dhahabu katika mkono wake wa kushoto kisha akainua mikono yake, na akasema: kwamba hizo zote mbili ni haramu kwa wanaume wa Umma wangu na ni halali kwa wanawake ".
Na kutokana na hayo, Uislamu haukufaradhisha mavazi maalumu kwa wanaume na wala kwa wanawake. Lakini umeweka masharti na vidhibiti kwa ujumla vya nguo zao. Kisha ukaacha sifa zao kwa mujibu wa zama na mahali walipo, zikawa zinatofautiana kutokana na watu, hali, nyakati na mahali.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.


 

Share this:

Related Fatwas