Madaraka ya Warithi Kuhusu Kodi ya Kifaransa Inayorithiwa
Question
Mume wa jirani yangu mwanamke alikufa ghafla, akaacha shirika la ujenzi, na alikuwa na madeni mengi kwa serikali ya Ufaransa; kwa sababu yeye hakulipa kodi pamoja na makato mengine kwa muda wa mwaka mmoja na nusu. Mke wake alikataa mirathi yake, kwa hiyo, hana madaraka kuhusu mali yake, na madeni yake yakawa katika hisa za watoto wake wadogo ambao pia wanaweza kukataa urithi wa baba yao. Swali ni:
Je mtu aliyefariki analazimika kulipa madeni ya serikali Siku ya Kiyama? Kwa sababu kama jibu litakuwa: Ndio, naweza kuwatolea wito watoto kulipa madeni ya baba yao baada ya kupata kazi.
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Siku zote wanachuoni wanazungumzia suala hili katika mlango wa Jeneza; wanapozungumzia mirathi ya aliyekufa, namna ya kuigawanya, na kumsalia maiti mwenye deni. Pia wanaitaja katika mlango wa Dhamana, na baadhi yao wanaitaja katika Sifa za Mtume SAW, katika maudhui ya aliyekufa mwenye deni. Hukumu yake ni kuwa hakuna mirathi ila baada ya kulipa madeni ya aliyekufa, na hakuna mgawanyo wa mirathi kwa warthi isipokuwa baada ya kulipwa kwa deni la aliyekufa, na ikiwa kiasi cha mirathi kinatosha kulipia deni, basi hakuna kitakachogawanywa kwa warithi, na kikibakia kitu kitagawanywa kwao, na kama kiasi cha deni kikizidi mirathi haiwajibiki warithi kulipa kutokana na mali zao, lakini inapendeza kwao wafanye hivyo, au yeyote anayetaka kuchukua deni la aliyekufa anaweza kufanya hivyo.
Dalili ya hayo kuwa asili ya dhima ya mtu mzima ni huru na hakuna madaraka ya dhima isipokuwa kwa dalili, na haikupokelewa kinachoonesha kuwa mrithi analipa kwa mali yake deni la anayerithiwa, na Mtume S.A.W alipohudhuria mazishi ya mtu mwenye deni alikataa kumsalia, na hakuwaamuru jamaa zake au kuashiria kuwa wanawajibika kulipa deni la mtu huyo aliyefariki, na kuahirisha ufafanuzi baada ya wakati wake haikujuzu, kama ilivyokuja katika Hadithi nyingi miongoni mwake ni ile iliyopokelewa na Abi-Hurairah R.A kuwa: Mtume S.A.W aliletewa mtu aliyekufa mwenye deni alikuwa akiuliza:“Je aliacha mali ya kulipa deni?” Akijibiwa kuwa ameacha mali ya kulipa basi humsalia, kama si hivyo basi aliwaambia waislamu: “Msalieni ndugu yenu”, na ilipozidi mali ya ngawira, Mtume akasema: “Mimi ni walii wa waumini kuliko nafsi zao, basi yeyote aliyekufa kati yao, akaacha deni mimi nitalilipa, na yeyote atakaeacha mali itakuwa haki ya warithi wake”. [Muttafaq].
Ibn Qudamah anasema: “Na huharakishwa malipo ya deni ya aliyekufa, kwa Hadithi iliyopokelewa na Mtume S.A.W kuwa amesema: “Nafsi ya muumini inaambatana na deni lake mpaka lilipwe”. At-Tirmidhiy anasema: Hadithi hii ni Hassan. Iwapo atashindwa kulipa deni lake hapo hapo, ni bora kwa warithi wake kulilipa kwa niaba yake, kama alivyofanya Abu-Qatadah wakati lilipoletwa jeneza kwa Mtume S.A.W hakulisalia, lakini Abu-Qatadah akasema: Ewe Mtume Swali! na mimi nitalipa deni, basi Mtume S.A.W akamswalia”. Imepokelewa na Bukhariy. [Al-Mughniy, 2/337, Maktabat Al-Qahirah].
Kwa mujibu wa hayo, Hailazimiki watoto hawa kulipa deni la baba yao ambaye mali yake haitoshi kulilipia deni hilo.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.