Matibabu kwa Kutumia Maada Zitokanazo na Nguruwe
Question
Mwanangu anasumbuliwa na ugonjwa wa kansa ya damu na tiba yake inayotakiwa ni kuchoma sindano ya dawa ya Heparin kwa uchache mara mbili kwa siku, ukiongezea pia na dawa zingine pamoja na kuhamisha damu. Na sisi tunaisha nchini Ujapani ambapo njia pekee ya kupata hiyo Heparin ni kupitia nguruwe, kama ambavyo pia damu inachangiwa na Wajapani wanaojitolewa.
Je, ni halali au hapana? Na kama haitakuwa halali ni ipi njia mbadala?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:
Kwanza: Kuhamisha damu kutoka kwa kafiri kwenda kwa Mwislamu na kinyume chake ni jambo linalofaa na wala hakuna ubaya wowote, kwa sababu ni upande wa tiba, na tiba ni jambo la kisheria kutokana na mapokezi ya Abu Daud na Tarmidhy kutoka kwa Usama Ibnu Sharik R.A. amesema: Nilikwenda kwa Mtume S.A.W. na maswahaba zake kana kwamba vichwani mwao kuna ndege, nikasalimia kisha nikakaa. Basi wakaja waarabu na wakasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Je, tunaweza kufanya dawa? Mtume akasema: “Fanyeni dawa, kwani Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuleta ugonjwa isipokuwa ameleta na dawa yake isipokuwa ugonjwa mmoja: nao ni uzee” Hadithi hii imekuja kuhimiza watu kuwa huru kufanya matibabu moja kwa moja pasi na kizuwizi. Na kanuni inasema jambo lililoachwa huru hufanyika kwa uhuru wake, mpaka lije tamko la kuzuia.
Amesema Imam Al-Khattaby katika kitabu cha Maalimu As-sunan 4/217 chapa ya Halab: “Katika Hadithi hii kuna uthibitisho wa ruhusa ya kufanya tiba au matibabu, na kutumia dawa ni halali na wala haichukizi”.
Pili: Ikiwa maada ya “Heparin” inatokana na nguruwe na kubadilishwa na kuwa maada nyengine kwa kutumia kemikali au maada zengine, basi hakuna kizuizi kutumia kwa sindano, kwa sababu kwa mchanganyiko huo inakuwa imebadilika kutoka katika uhalisia wake wa unguruwe na kuwa katika uhalisia mwingine mpya. Kubadilisha uhalisia ni moja ya njia ya usafishaji wa kitu kilichokuwa najisi au kichafu, na asili ya hilo ni kukubalika kuwa pombe inapogeuka yenyewe na kuwa siki inakuwa twahara kwa maana ya usafi, basi linganisha hali hiyo na vitu vingine.
Ama maada hii inapokuwa hivyo hivyo pasi na kubadilika basi kufaa kutumika kwake kunafungamana na kutokuwepo kwa dawa mbadala, au ikapatikana lakini kwenu haitoshelezi basi hakuna kizuizi kuitumia, kwa sababu jambo la dharura uhalalisha lililozuiliwa, na hakika Anasema Mola Mtukufu: {na hali Amewabainishieni waziwazi Alivyowaharimishieni - isipokuwa vile mlivyovishurutishwa?}[AL ANA'AM, 119].
Na Anasema tena: {lakini aliyeshurutishwa, bila kutamani wala kupita kiasi, basi yeye hana dhambi; hakika Mwenyezi Mungu ni Msamehevu, Mrehemevu}[AL BAQARAH, 173].
Na inapaswa kutambua kuwa jambo la dharura huwa linakadiriwa kwa kiasi chake wala hakizidishwi kiasi hicho kwa kile kinachopelekea udharura, kwa sababu asili ya dharura ni kuhalalisha kilichopigwa marufuku kutumika, inapoondoka asili tawi pia huondoka, na kurejea kwa kilichopigwa marufuku kutumika na kuwa si halali, ikiwa mgonjwa hajapata dawa badala ya ile iliyotokana na maada ya “Heparin” inayotokana na nguruwe basi yafaa kwake kwa kiwango cha kuondoa ugonjwa pasi na kuzidisha.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.