Mke Kumsujudia Mume Wake.

Egypt's Dar Al-Ifta

Mke Kumsujudia Mume Wake.

Question

 Mimi ni msichana wa Kihindi niliingia katika Uislamu tangu muda mrefu, na kuanzia wakati huo ninatekeleza Swala kwa utaratibu wake unaotakiwa, na ninafunga mwezi wa Ramadhani, na nilimsujudia mume wangu bila ya kukusudia kwa mujibu wa hisia yangu ya ndani na bila ya kujua hukumu ya kitendo hiki. Baadaye nikajua kwamba kitendo cha kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu kinasababisha mtu kutoka katika Dini, kwa kuwa ni aina ya ushirikina, na ni juu ya mtu kuingia katika Uislamu upya, mimi sijui nifanyeje? Je, nilipata dhambi? Hali ya kuwa mimi nilikuwa sijui hukumu ya kitendo hiki wakati wa kufanya hivyo.
Tafadhalini mniongoze njia iliyonyooka, nahitaji msaada wenu, na huwenda nikawa nimetoka katika dini yangu kwa kitendo hicho. Je kuna njia ya kujitakasa itakayo nifanya nirudi tena katika dini yangu?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu, na rehma na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu, jamaa zake, maswahaba wake na wanaomfuata. Na baada ya hayo:

Hapana, ewe dada mwema! Wewe hujatoka katika dini yako kwa kitendo cha kumsujudia mume wako; kwani dini ni akida thabiti katika moyo wa Mwislamu hawezi kuipoteza ila anapobadili akida hii na kutoka katika imani ya Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W, au akaenda kinyume na akida hii thabiti na kitendo cha kusujudia kinachomtoa mtu katika mila ni sijida ya Ibada, lakini sijida ya maamkizi na kumfadhilisha ni haramu tu na wala si ukafiri. Na Malaika walimsujudia Baba yetu Adamu na ndugu za Nabii Yusufu A.S. walimsujudia, na hukumu hii ilifutwa katika sheria yetu kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Basi msilisujudie jua wala mwezi, bali msujudieni Mwenyezi Mungu aliyeviumba} [FUSSILAT, 37],
Lakini hukumu hii haifikii daraja la ukafiri bali ni haramu tu. Na sharti ya dhambi katika mambo ya haramu ni kujua kwamba ni haramu, kwa hivyo hapati dhambi anayefanya hivyo hali ya kuwa hajui kwamba hukumu yake ni haramu, na wala haimtoi mtu katika mila kwa kufanya hivyo, kwa dalili ya kuwa Moadhi Ibn Jabal R.A. alipokuja kutoka Yemen alimsujudia Mtume S.A.W, kama ilivyotajwa na Ibn Majah na kusahihishwa na Ibn Haban Na Mtume S.A.W alimkataza kufanya hivyo - lakini hakusifu kitendo chake kuwa ni miongoni mwa ushirikina au ukafiri, na kimantiki kwamba Moadhi R.A. - Ndiye mwenye elimu zaidi katika Umma kwa mambo ya haramu na ya halali kama alivyosifiwa na Mtume S.A.W. – Alikuwa anajua kwamba sijida ni ibada na ibada haijuzu kutekelezwa kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, lakini kwa kuwa sijida inaweza kumaanisha maana nyingine mbali ya ibada kwa mwenye kusujudiwa, basi haiwezekani kuchukulia kwa sifa ya ibada hasa inapotokea na Mwislamu au kumkufurisha kwa hali yeyote ile, na katika suala hili anasema Mwanachuoni mkubwa Kadikhan mfuasi wa madhehebu ya Abu-Hanifa: "Mtu angemsujudia Sultani akiwa na nia ya kumtakasa na kumpa maamkizi bila ya kukusudia ibada, basi halo haliingii katika hukumu ya ukafiri, na asili ya hukumu hii ni kuwa Malaika walimsujudia Baba yetu Adamu na ndugu za Nabii Yusufu A.S. walimsujudia" [Mirkat Al-Mafatih, Mula Ali Al-Kari, 6/369, chapa ya Dar Al-Kotub Al-Elmiya], na alisema Al-Hafidh Al-Zahabi mfuasi wa madhehebu ya Shafi: "Huoni kwamba Masahaba kutokana na mapenzi yao kwa Mtume S.A.W. walisema: Je, tukusujudie? Basi Mtume S.A.W. akasema: Hapana.
Na angeliwaruhusu kumsujudia wangelimsujudia sijida ya kumtakasa na kumheshimu siyo sijida ya ibada, kama walivyomsujudia nduguze Yusufu A.S., na pia kauli katika sijida ya Mwislamu juu ya kaburi ya Mtume S.A.W. kwa kusudio la utakaso na heshima, basi kitendo kicho hakimwingizi katika ukafiri, bali akifanya anakuwa miongoni mwa waasi, basi ijulikanwe kwamba kitendo hicho ni miongoni mwa mambo yaliyokatazwa, kama vile kusali mbele ya kaburi" kutoka kitabu cha: [Mujam Ash-Sheukh na Imam Al-Zahabiy uk 56].
Na hitilafu kati ya kumsujudia asiyekuwa Mwenyezi Mungu kati ya Mwislamu na asiyekuwa Mwislamu ni kwamba: Mwislamu anaamini kwamba ibada haijuzu kutekelezwa ila kwa Mwenyezi Mungu peke yake, ama mshirikina anaamini uwezekano wa kutekeleza ibada kwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu.
Na kwa hivyo basi tunapomwona Mwislamu anatekeleza ibada kwa viumbe badala ya Mwenyezi Mungu inapasa kuchukua kitendo hicho kwa maana inayokwenda sambamba na itikadi yake kuwa ni Mwislamu; kwani aliyeingia katika Uislamu kwa uyakinifu hatoki katika Uislamu kwa shaka au dhana.
Na hiyo inategemea kanuni ya kisheria isemayo: Asili ya vitendo vilivyotokea kwa Mwislamu huchukuliwa kwa maana zisizoenda kinyume na msingi wa upwekeshahi, na haijuzu kumkufurisha au kumpa wasifu wa kuwa mshirikina; kwani Uislamu wake ni hoja imara inayotulazimisha kutofahamu kuwa vitendo vyake vinamwingiza katika ukafiri, na msingi huu ni kwa Waislamu wote, na kwamba wanapaswa kushikamana nao kwa kuviangalia vitendo vyote vya Waislamu wenzao.
Naye Imam Malik Imamu wa Dar Al-Hijrah - Mwenyezi Mungu amrehemu - aliyaelezea hayo kwa kauli yake: "yeyote anayefanya mambo yanayoweza kufasiriwa na sura tisini na tisa za ukafiri na sura moja tu ya imani, basi inapaswa kufasiriwa kwa sura ya imani tu”.
Basi kuwa na matumaini ewe dada mwema. Hujapoteza dini yako kwa kitendo chako, bali hujapata dhambi kabisa, kwani umekifanya kitendo hicho bila ya kukusudia na wala hukujua kwamba kitendo hicho ni haramu wakati wa kukifanya, mbali ya hayo umepata thawabu juu ya kusudio na nia yako ya kutaka upendo wa mume wako na kuishi naye kwa wema.
Naye Mtume S.A.W, alihimiza mke kumheshimu mume wake pamoja na kujua haki yake akasema: "Ningekuwa ninaamirisha mtu kumsujudia mwengine, basi ningemwamrisha mke amsujudie mume wake” imepokelewa na kusahihishwa na Al-Tirmiziy. Kwa hivyo basi ninakupa pole sana na kuwa mtulivu. Mwenyezi Mungu Akuthibitishe katika dini yake, na Akuongoze kwenye mambo ya kheri na Akupe furaha ya milele hapa duniani na kesho Siku ya Mwisho.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi ya wote.

 

Share this:

Related Fatwas