Kuendelea Kuacha Sunna Zilizotiliwa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuendelea Kuacha Sunna Zilizotiliwa Mkazo

Question

Nini hukumu ya kuendelea kuacha Sunna zilizotiliwa Mkazo? 

Answer

Wanachuoni wa Misingi ya Fiqhi wanazigawanya hukumu za kisheria katika migawanyo mitano, nayo ni: Wajibu, Mustahabu, Haramu, Makuruhu, na Mubaha. Walifafanua Mustahabu kuwa: Ni ile ambayo mtendaji wake hupata thawabu, na haadhibiwi mwenye kuiacha, nayo ina misamiati mingine kama vile: Inayotakiwa, Sunna, na Ziada, na mifano yake ni: Sala ya Witri, Mswaki. Kusukutua maji mdomoni mara nyingi, Kuvuta maji puani, Kuosha kati ya vidole wakati wa Udhu, Futari ya tende kwa mwenye kufunga, Kufanya Hija na Umra mara nyingi, Kusaidia wanaohitaji, n.k.
Wanachuoni walibainisha kuwa Sunna hizi hazina ngazi moja katika kutakiwa kwake, ambapo zingine ni zenye kutiliwa Mkazo zaidi kuliko zingine, lakini zote zinashirikiana na Mustahabu kiutekelezaji, na kutoadhibiwa mja katika hali ya kuziacha.
Az-Zarkashi katika kitabu Al-Bahr anasema: “Yumkini kuwa baadhi ya Mustahabu zinatiliwa Mkazo kuliko nyingine, kwa hiyo wanasema: Sunna zilizotiliwa Mkazo. Ibn Daqiqil-Idi katika Sharhul-Ilmami anasema: “Haifichiki kuwa ngazi ya Sunna ni tofauti kwa mtazamo wa kutilia mkazo. Na hizi zinagawanyika katika ngazi ya juu, ya kati, na ya chini, kutokana na dalili zinazoonesha hitajio”. [1/376-387, Ch.ya Dar Al-Kutbiy].
Wanachuoni wamezigawa Sunna kwa mtazamo wa kuziendeleza Mtume S.A.W, kuzitekeleza ziwe: Sunna zilizotiliwa Mkazo, Ibn Nujaim Al-Hanafiy, Mwenyezi Mungu amrehemu, baada ya kunukulu kauli kadhaa za wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy katika ufafanuzi wa Sunna, pamoja na kuzipinga anasema: “Maoni yangu ni: Sunna iliyoendelezwa na Mtume S.A.W, na bila kuiacha hata siku moja, basi ndio iliyotiliwa Mkazo, lakini ikiwa na iliachwa baadhi ya nyakati, basi ni Sunna isiyotiliwa Mkazo”. [Al-Bahru-Raaiq: 1/18, Ch.ya Dar Al-Kitaab Al-Islamiy].
Kuendelea kwa Mtume S.A.W kukitekeleza kitu, hata ikiwa si wajibu, ni kigezo cha kuwa hicho kitu ni Sunna iliyotiliwa Mkazo. Na kuigawa Sunna kuwa ya kutiliwa Mkazo na kutokuwa ya kutilia mkazo ni aina ya istilahi ambayo haina tofauti, na ufafanuzi huu umechukuliwa na kufuata kwa vitendo vya Mtume S.A.W, katika minasaba mbali mbali, na kwa hivyo basi ni jinsi alivyoendelea kuzitekeleza kama vile Rakaa mbili za Alfajiri. Na maana ya istilahi hii, jambo muhimu hapa ni kuthibitisha hali ya kuiendeleza, na dalili yake ni jinsi walivyoeleza masahaba, mfano wake, kama alivyopokea Bibi Aisha R.A,: “Mtume S.A.W, hakuwa na shime ya kusali sala ya Sunna kuliko kusali Rakaa mbili za Alfajiri’. [Muttafaq].
Kinyume cha ilivyopokelewa na Mtume S.A.W, kuwa akihimiza kutekeleza tendo fulani, lakini hakuendelea kulitekeleza, mfano wake kufuatana kati ya Hijja na Umra, kama kauli yake S.A.W: “Fuatanisheni kati ya Hija na Umra kwani huwa zinaondosha ufakiri na madhambi, kama tanuri la moto liondoavyo takataka za chuma, dhahabu na fedha”. [Imepokelewa na Ahmad, At-Tirmidhiy na An-Nasaaiy].
Na inafaa kuashiria kuwa Sunna iliyotiliwa Mkazo inaitwa na wafuasi wa Madhehebu ya Hanafiy kama: Sunna ya uongofu, Ibn Abidiin anasema: “Sunna ni aina mbili; Sunna ya uongofu, na kuacha kwake kunawajibika uovu na kuchukuliwa, kama kuacha sala ya jamaa, adhani, kusimamisha sala, n.k; Sunna ya ongezo: Kuacha kwake hakuwajibiki hivi, kama vile kuigiza Mtume S.A.W, katika mavazi yake, kusimama kwake na kukaa kwake”.
Anasema pia: “Sunna ya uongofu ni miongoni mwa Sunna zilizotiliwa Mkazo, iliyo karibu na Wajibu”. [Rad-Dul Muhtaar: 1/103, Ch.ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Msomaji wa matini ya wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy, hasa waliokuja mwishoni, wataona kuwa wao wanafanya sawa kati ya istilahi ya (Sunna iliyotiliwa Mkazo) na istilahi ya (Wajibu), kwa upande wa kulazimisha kutenda na kutahadharisha kuacha, yaani; kuadhibiwa anayeacha, na kupatiwa thawabu anayetenda, na hii ni wazi katika maneno yao ya Sala ya jamaa.
Al-Kasaniy baada ya kutaja kauli ya wengi kuwa Sala ya jamaa ni Wajibu, anasema kuwa: “Dalili ya kauli ya wengi hivi ni kutokana na Kitabu, Sunna, na matendo ya umma… kuhusu matendo ya umma, umma kutoka zama za Mtume S.A.W, mpaka siku hivi sasa, waliendelea kuitekeleza, na wakawakana wanaoiacha, na kuendelea kwa sura hii ni dalili ya Uwajibikaji, pia hii siyo tofauti, isipokuwa lafudhi tu; kwa sababu Sunna iliyotiliwa Mkazo na Wajibu ni sawa, hasa inayohusu ibada za Uislamu, na huoni kuwa Imamu Al-Karkhiy aliiita Sunna, kisha akaieleza kwa Wajibu, akisema: Sala ya jamaa ni Sunna, na hairuhusiwi mtu ye yote kuiahirisha isipokuwa dharura. Na hii ni maana ya Wajibu kwa maoni ya wengi”. [Badaaiu’-Sanaii’: 1/155, Ch.ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Al-babertiy anasema: (Sala ya jamaa ni Sunna iliyotiliwa Mkazo) maana yake ni yenye imara inayolingana na Wajibu katika Mkazo yake, hata kuendelea kuitekeleza ni dalili ya kuwepo imani, kinyume cha masuala mengine ya Sheria, kwa hiyo, wanachuoni wanaiita Sunna ya uongofu, yaani kuitekeleza ni uongufu, na kuiacha ni upotofu, na kauli yake Mtume S.A.W, ikiashiria hivi: “Sala ya jamaa ni miongoni mwa Sunna ya uongofu, na haiachi isipokuwa mnafiki”. [Al-Inayah: 1/345, Ch. Dar Al-Fikr].
Katika Hashiyat Ash-Shilbiy Ala Tabiyn Al-Haqaiq: “Kauli yake: (Wengi wa mashekhe wetu walisema: Ni wajibu…) na katika Mykhtasar Al-Bahr Al-Muhiit: Ni Sunna iliyotiliwa Mkazo, na kama watu wa mahali fulani wangaliiacha watapata dhambi, na ni wajibu kuwapiga kwa silaha; kwani ni miongoni mwa ibada za Uislamu. Katika Shrhu Khawahir Zadah: Ni Sunna iliyotiliwa Mkazo, upeo wa Mkazo. Al-Kamal anasema: Inasemwa kuwa: Sala ya jamaa ni Sunna iliyotiliwa Mkazo kama wajibu. Na Miongoni mwa waliosema kuwa ni Sunna iliyotiliwa Mkazo: Al-Kakhiy, Al-Quduriy, na miongoni mwa dalili ya kuwa ni kama Wajibu: kauli ya mtungaji wa Tuhfah, kama alivyotaja Muhammad katika mapokezi yasiyokuwa ya misingi kuwa ni Wajibu, na baadhi ya wanachuoni wetu waliiita Sunna iliyotiliwa Mkazo, na hizi mbili ni sawa”. [1/133, Ch. ya Al-matba’a Al-Amiriyah].
Burhanu-Din Al-Bukhariy Al-Hanafiy anasema: “Sala ya jamaa ni Sunna iliyotiliwa Mkazo, na haijuzu kwa mtu kuiacha isipokuwa dharura, na asili yake ni kauli yake SAW,: “Ningefikiri kumwamuru mtu yeyote aongoze sala, kisha niwatazame watu ambao wameacha sala ya jamaa, ili nizichome nyumba zao”, na mfano wa tishio hili hakika linaambatana na mwenye kuacha Wajibu au Sunna iliyotiliwa Mkazo”. [Al-Muhiit Al-Burhaniy: 1/428, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Baadhi ya wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy waliweka Sunna iliyotiliwa Mkazo mahali pa Wajibu, katika Sharhul Ashbaah, na Al-Hamawiy, kwenye maneno ya Ibn Nujaim kuhusu Sunna ya kudumu, na kuwa miongoni mwake ni Rakaa mbili za Alfajiri, Al-Hamawiy anasema: “Kauli yake: Rakaa mbili kabla ya Alfajiri”, katika Al-Khulasah anasema: Walikubaliana kuwa sala ya Rakaa mbili za Alfajiri akiketi bila ya dharura haijuzu, lakini Sunna zingine inajuzu kuzisali kwa kuketi bila ya dharura hata Sala ya Tarawehe, na hii ni rai iliyo sahihi na kuchaguliwa. Imesemwa kuwa:Kauli hii ni kutokana na kauli ya kuwa ni Wajibu, kinyume cha Sunna zingine, kwa hiyo, baadhi yao walifahamu maelezo haya kuwa Sunna ya Alfajiri haijuzu kiketi , yaani haijuzu kuisali kwa kuketi, na hii ni kosa, kwa sababu tulitaja kuwa kuna rai ya kuwa ni Wajibu, kama ilivyokuja katika Sharh At-Tahawiy kuwa hii ni Sunna iliyotiliwa Mkazo, lakini ina Mkazo zaidi, kupendeza, kuhofisha, na tishio, kwa hiyo ikawa kama Wajibu, na ni wazi kuwa haijuzu hapa inamaanisha: haisihi’. [1/120, Ch. ya, Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Mbali na istilahi ya wafuasi wa madhehebu ya Hanafiy, sala za Sunna zilizotiliwa Mkazo baadhi yake hazifuatani na faradhi, na baadhi yake hufuata. Kwa hiyo, zinazofuata au zina wakati maalumu na zisizo za faradhi, huitwa sunna za kudumu.
Kuainisha Sunna za kudumu na Mustahabu katika kuzitekeleza, kuna Hadithi nyingi, miongoni mwake Hadithi ya Ibn Umar RA, anasema: “Nilihifadhi kutoka kwa Mtume S.A.W, Rakaa kumi: Rakaa mbili kabla ya Adhuhuri, Na Rakaa mbili baada yake, na Rakaa mbili baada ya Magharibi nyumbani kwake, na Rakaa mbili baada ya Isha nyumbani kwake, na Rakaa mbili kabla ya Asubuhi”. [Ameipokea Bukhariy].
Imepokelewa na Aisha RA, alisema: “Mtume SAW, alikuwa haziachi Rakaa nne kabla ya Adhuhuri”. [Ameipokea Bukhariy].
Imepokelewa na Umu Habiba R.A, alisema: Nilimsikia Mtume S.A.W, akisema: “Aliyesali Rakaa kumi na mbili katika siku moja na usiku mmoja, itajengwa nyumba katika Pepo kwa ajili yake”, na Umu Habiba alisema: Sikuziacha sala hizi, tangu niliposikia kutoka kwa Mtume S.A.W. [Ameipokea Muslim]. Na At-Tirmidhiy amezidisha: “Rakaa nne kabla ya Adhuhuri, na Rakaa mbili baada yake, na Rakaa mbili baada ya Magharibi, na na Rakaa mbili baada ya Isha, na rakaa mbili kabla ya sala ya Alfajiri”.
Sunna za kudumu hazina ngazi moja ya kutilia Mkazo, na kigezo chake, kama tulivyosema, ni kudumu kwa Mtume S.A.W, katika kuzitekeleza, kwa hiyo baadhi yake ni kutiliwa Mkazo zaidi kuliko zingine, na Rakaa kumi zinazotajwa katika Hadithi ya Ibn Umar ni miongoni mwa Sunna za kudumu na zinazotiliwa Mkazo, hasa Rakaa mbili za Alfajiri, ambazo zimetiliwa Mkazo zaidi kuliko zote; kwa kauli ya Aisha R.A: “Mtume S.A.W hakudumisha kuzitekeleza Sala za Sunna isipokuwa rakaa mbili za Alfajiri”. [Muttafaq], na katika lafudhi nyingine: “Yeye hakuziacha katu siku zote”.Pia imepokelewa naye kuwa Mtume S.A.W, anasema:“Rakaa mbili za Alfajiri ni bora kuliko Dunia na vilivyomo ndani yake”. [Ameipokea Muslim}. Kwa hiyo, imenukuliwa kwake S.A.W, kuwa hakuziacha katu Rakaa mbili za Alifajiri, na Katika Al-Musannaf, na Ibn Abi—Shaibah, kutoka kwa Hadithi ya Aisha, anasema: “Sala isiyoachwa Katu na Mtume S.A.W, akiwa mzima au mgonjwa, msafiri au siyo msafiri, mbali au karibu, ni Rakaa mbili za Alfajiri”.
Ibn Al-Qaiym anasema: “…kwa hiyo, Mtume S.A.W, hakuziacha, yaani sala hii na Witri, akiwa msafiri au siyo, na alikiwa katika safari akidumisha kuzitekeleza, yaani Sunna ya Alfajiri na Witri, kuliko sala nyingine za Sunna, na haikunukuliwa naye, wakati wa safarini, kuwa akisali sala ya Sunna na ya kudumu isipokuwa hizi”. Zaad Al-Ma’ad: 1/305, Ch. ya Muassasat Ar-Risalah].
Zaidi ya hayo, Sala zote za Sunna, miongoni mwake ni Sala za Sunna za kudumu hakika zimewekwa kama sheria kwa ajili ya kurekibisha kasoro na kukamilisha upungufu uliopo katika swala za faradhi, katika Hadithi: “Hakika kitu cha kwanza anachohesabiwa mja Siku ya Qiyama ni Sala zilizofaradhiwa, zikiwa zimetimia ni sawa, ikiwa kinyume na hivyo, pataulizwa kuwa: Je Mja huyu ana sala ya Sunna? Akiwa na Sala ya Sunna, basi Faradhi zitaunganishwa na Sunna, kisha itafanywa hivi hivi kwa swala zote za faradhi zilizobakia”. [Wameipokea: Ahmad, Abu-Dawuud, na Ibn Majah]. Pamoja na kuwa Kuhifadhi sala za Sunna na kudumu kuzitekeleza ni kuangalia dini ya Mwenyezi Mungu na kuzingatia Sheria yake na kumfuata Mtume S.A.W, na kutekeleza kauli ya Mwenyezi Mungu: {Bila shaka mnao mfano mwema (ruwaza nzuri) kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu, kwa mwenye kumuogopa Mwenyezi Mungu na siku ya Mwisho, na kumtaja Mwenyezi Mungu sana}.[Al Ahzab: 21]. Pia kuendelea kuziacha bila ya dharura kunaonesha uzembe wa Sunna ya Mustafa S.A.W, na wanachuoni walitaja kuwa mwenye kuziacha Sunna za kudumu kwa uwazi, haikubaliwi shahada yake kutokana na kuanguka uadilifu wake, kwa sababu ya upungufu wa dini yake. Imamu Nawawi anasema: “ Aliyeendelea kuziacha Sunna za kudumu au tasbihi za Rukuu na Sujudu, shahada yake haikubaliki kwa ajili ya uzembe wake wa Dini”. [Al-Majmuu: 4/30, Ch. ya Dar Al-Fikr].
Imenukuliwa na Imamu Ahmad kuwa: Mwenye kuiacha Witri kwa makusufi ni mtu mwovu, kwa sababu Witri ni sunna iliyotiliwa Mkazo. [Rejea: Al-Mubdii’ na Ibn Muflih: 2/21, Ch. ya Dar Al-kutub Al-Ilmiyah].
Imamu Al-Bahutiy kwenye kubainisha sharti za wanaokubaliwa shahada zao, anasema: “(Sita: Uadilifu ni: Uwiano wa hali yake), yaani mtu yeyote (katika dini yake, kauli na matendo yake) na huo una (vitu viwili) kwanza ni: Uadilifu wa Dini) na huo ni aina mbili: (Kutekeleza faradhi) yaani Sala tano na Ijumaa. Niliongeza: Ilivyowajibika kama Saumu, Hijja, Zaka, na mengineo (kwa ngazi zake yaani Sunna za Sala za kudumu, na Abu-Talib amenukulu kuwa: Witri ni sunna iliyotiliwa Mkazo, kutokana na Mtume S.A.W, na aliyeacha Sunna, yaani siku sote yeye ni mtu mbaya (kwa hiyo, haikubaliki shahada ya mwenye kuziacha siku zote) kwa sababu uzembe wake unaonyesha kuwa kutohifadhi sababu za dini yake, na inawezekana uzembe huo kumpelekea uzembe wa faradhi, lakini shahada inakubalika kutoka kwa mwenye kuziacha baadhi ya wakati”. [Sharhu Al-Muntaha: 3/5899, Ch.ya Aalam Al-Kutub].
Hakuna lawama wala kosa kwa mwenye kuacha Sunna ya kudumu na iliyotiliwa Mkazo, sharti asiendelee kuziacha siku zote na milele, lakini akiendelea kuziacha kwa kila mara, basi atalaumiwa kwa sababu ya uzembe wake wa kuiacha Sunna ya Mtume S.A.W, hasa kwa kuendelea na kudumisha kufanya kitu maana yake ni kukusudia na kuwa na shime, na aliyekusudia kuacha Sunna ya Mtume S.A.W, iliyotiliwa Mkazo na kuiendeleza hali hiyo, hapana shaka kuwa ni uzembe wake katika mambo ya dini yake.
Hata hivyo, Imamu Ash-Shatibiy anauelekea mwelekeo mwingine katika suala la kuacha Sunna, akatofautisha kati ya kuacha Sunna kwa mtazamo wa kuiangalia kama kamili, na au kuiangalia kama sehemu tu ya Sunna hiyo, yeye anasema: “Miongoni mwa uhalisia wa Mustahabu ni kutolingana na Wajibu katika kutekeleza, hali kadhalika haulingani na baadhi ya mubaha katika kuacha kwa uwazi na bila ya kubainisha; kama ingekuwa kuna mlingano kati yao, basi ingefahamika kuwa kuacha ni kisheria, na isingefahamika kuwa ni Mustahabu tu. Na huu ni upande, na kwa upande mwingine ni kuwa: Kuacha Mustahabu ni kasoro ya jambo kamili ndani yake, ingawa baadhai ya Mustahabu ni wajibu kiukamilifu; kwa hiyo, kuuacha kwa uwazi, hupelekea kasoro ya Wajibu, lakini lazima kuutekeleza ili ubainike kwa watu na wautekeleze, na hii inatakiwa na wanaoigwa kama ilivyokuwa hali ya Salaf walio wema”. [Al-Muwafaqaat; 1/108, Ch.ya Dar Ibn Affan].
Anasema mahali pengine: “Ikiwa sehemu ya tendo ni Mustahabu litakuwa Wajibu kwa ukamili wake, kama vile Adhana katika misikiti na mahali pengine, sala ya jamaa, Sala ya Idi mbili, Sadaka ya kujitolea, ndoa, Witri, Alfajiri, Umra, na Sunna zote za kudumu. Hizi zote zimependelewa kwa sehemu yake, na kama zikiachwa kwa ukamili wake, basi mwenye kuziacha anapata dhambi, je, huoni Adhana ni kudhihirisha ibada za Uislamu, kwa hiyo, watu wa mahali fulani wakiacha Adhana, watastahiki kupigwa vita? Kama vile sala ya jamaa, aliyeiacha siku zote atapata dhambi, na haikubaliki shahada yake, kwa sababu kuacha kwake ni kwenda kinyume cha udhihirishaji wa dini, na Mtume S.A.W, aliwatishia wenye kuiacha jamaa, hata akafikiri azichome nyumba zao. Pia Mtume S.A.W, alikuwa hapigani vita na watu mpaka papambazuke, akisikia Adhana anajizuia, pia ndoa haifichi makusudio yake ambayo ni ongezeko la kizazi na kuhifadhi uwepo wa binadamu, n.k. na kuacha vitu hivi kwa ujumla wake huathiri katika hali za dini. Lakini ikiwa ni kwa muda mfupi, basi haiathiri na pia haikatazwi”. [1/211].
Imamu Ash-shatibiy kwa mtazamo wake huu, anafanya Mustahabu ni (Mustahabu wa kutoshelezeana) kama mkabala wa (Wajibu wa kutoshelezeana), na kwa mujibu wa hayo, wenye kuacha aina hii ya Mustahabu ni wenye dhambi, wakiiacha wote pamoja, bali yeye anapanua nadharia yake hii, anaona kuwa Mustahabu wa kutoshelezeana kwa mtazamo kamili ni Wajibu, kama ilivyo wazi katika mifano aliyoitaja katika andiko lake la mwisho.
Kwa Mujibu wa hayo: Kuendelea kuacha Sunna iliyotiliwa Mkazo kwa uwazi kunaathiri uadilifu wa mwenye kuiacha, na mwenye kuiacha katika baadhi ya siku au wakati basi hana kosa. Lakini haijuzu kwa jamii yote kuziacha Sunna za kutoshelezeana, ambazo ni miongoni mwa Ibada za Uislamu.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

Share this:

Related Fatwas