Kuomba Dua Kati ya Hotuba Mbili za Ijumaa.
Question
Tunaona kwamba katika hotuba ya Ijumaa baadhi ya wasalio wanaomba dua wakati Imamu anapokaa kati ya hotuba mbili wanadhani kwamba wakati huu dua inatarajiwa kujibiwa, wakati tunaona baadhi yao wanakataa kufanya hivyo, je, hali gani ni sahihi kuhusu jambo hili?
Answer
Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Siku ya Ijumaa ni miongoni mwa siku maalumu kwa Umma wa Mtume Muhammad S.A.W, imetajwa katika Hadithi ya Mtume S.A.W, kwamba: “Mwenyezi Mungu Mtukufu hakuwaongoa watu waliokuwa kabla yetu kwa siku ya Ijumaa, Wayahudi walikuwa na siku ya Jumamosi, Wakristo walikuwa na siku ya Jumapili, kisha Mwenyezi Mungu alituongoa siku ya Ijumaa, na akafanya siku ya Ijumaa, kisha Jumamosi na Jumapili, pia Wayahudi na Wakristo watatufuata sisi siku ya Kiyama, sisi ndio umma wa mwisho kutoka watu wa dunia na sisi ndiyo wenye kutangulia siku ya Kiyama tuliyoiamirishia kabla ya viumbe”. [Hadithi hii imekubaliwa na imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim]. Pia siku ya Ijumaa ni siku ya sikukuu ya Waislamu kama ilivyotajwa na Mtume S.A.W (imepokelewa kutoka kwa Imamu Ahmad), nayo ni siku bora ya wiki, Mwenyezi Mungu ameisifu siku hii kwa sifa nyingi kwa fadhila zake ambazo ni zaidi na ili kueleza nafasi yake, imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslimu kutoka kwa Abu Hurayrah R.A kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W, alisema kuwa: “Swala tano na Ijumaa mpaka Ijumaa ni kafara baina yake muda wakuwa hakujafanywa madhambi makubwa”, (imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim).
Vile vile imepokelewa kutoka kwa Abu Hurayrah R.A kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W, alisema kuwa: “Siku iliyo bora ambayo imechomozewa na Jua ni siku ya Ijumaa, ndani ya siku hiyo aliumbwa Nabii Adam, ndani ya siku hiyo aliingizwa peponi, ndani ya siku hiyo alitolewa peponi, na siku ya Kiyama haikuwa isipokuwa katika siku ya Ijumaa”, (imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslim). Na mwenye kufariki siku ya Ijumaa au usiku wa Ijumaa Allah atamkinga na fitna za kaburini, kama ilivyopokelewa kutoka kwa Abdullah Ibn Amr R.A, aliposema kuwa: Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W, alisema: “Hakuna yeyote mwislamu atafariki siku ya Ijumaa au usiku wa Ijumaa isipokuwa Allah atamkinga na fitna za kaburini." (Imesimuliwa na Ahmad na Tirmidhi).
Kwa ajili ya fadhila hizi Mwenyezi Mungu aliwapendekezea Waislamu kufanya baadhi ya kazi katika siku ya Ijumaa, miongoni mwao ni kuoga, kuvaa nguo nzuri, na iliyo bora zaidi ni nyeupe, na kujitia manukato kwa wanaume, na kufika msikitini mapema siku ya Ijumaa kwa ajili ya kuswali, na kumswalia Mtume mara nyingi, S.A.W, na kusoma Suratul Kahf, pia miongoni mwa kazi za siku ya Ijumaa kutafuta saa ya kujibiwa kwa dua, kwani imetajwa katika Hadithi kadhaa kuwa: katika siku ya Ijumaa, ipo saa ambayo dua hairudishwi, na maneno ya Hadithi hizi yametofautiana, na kulingana na tofauti hii, wanavyuoni wametofautiana kuhusu kuainisha wakati huu, Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W alisema kuwa: “Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna wakati, haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah Kheri, ila Mwenyezi Mungi humpatia” (imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslimu kutoka kwa Abu Hurayrah), na katika baadhi ya Hadithi: “nayo ni saa rahisi”.
Na imepokelewa kutoka kwa Abu Musa Al-Ash'ari R.A kwamba alisikia Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W, anazungumzia kuhusu saa iliyopo katika siku ya Ijumaa ina maana: saa ambayo dua inajibiwa ndani yake, akisema: “Saa hii iko kati ya kukaa kwa imamu mpaka kumaliza sala” (Imepokelewa kutoka kwa Imam Muslim) .
Vile vile Mtume S.A.W, alisema: “Hakika katika Siku ya Ijumaa kuna wakati, hawafikishwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah chochote, ila Mwenyezi Mungi humpatia” (imepokelewa kutoka kwa Imamu Ahmad kutoka kwa Abu Hurayrah), na katika Hadithi nyingine: “Tafuteni saa iliyotarajiwa katika siku ya Ijumaa kuanzia baada ya alasiri mpaka kuchwa jua” (Imepokewa kutoka kwa Al-Tirmidhi kutoka kwa Anas).
Miongoni mwa Hadithi nyingine ni kauli ya Mtume S.A.W: “Siku ya Ijumaa ni masaa kumi na mbili, miongoni mwao ni saa moja haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah chochote, ila Mwenyezi Mungi humpatia, basi tafuteni saa hii baada ya Al-Asiri”. [Imepokewa kutoka kwa Abu Dawood, Al-Nasaa'i na Al-Hakim kutoka kwa Hadithi ya Jaabir].
Na kauli yake S.A.W: Siku ya Ijumaa ni masaa kumi na mbili, miongoni mwao ni saa moja haafikiwi Muislamu na wakati huo hali akiwa anamuomba Allah chochote, ila Mwenyezi Mungi humpatia, Masahaba walisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, saa hii ni ipi? Akasema: “Kuanzia kusali mpaka kumaliza swala”. (Imepokewa kutoka kwa Al-Tirmidhi na Ibn Majah kutoka kwa Amr ibn Auf).
Na Imepokewa kutoka kwa Anas R.A, kwamba Mtume, S.A.W alisema: “Tafuteni saa iliyotarajiwa katika siku ya Ijumaa kuanzia baada ya alasiri mpaka kuchwa jua”, (Imepokewa kutoka kwa Al-Tabarani katika Al-Kabiir).
Na kauli yake S.A.W: “Nilikuwa nikijua wakati wa saa ile iliyoko katika siku ya Ijumaa, kisha nikasahaulishwa kama nilivyosahaulishwa Lailatu Al-qadr (Usiku wa cheo)”. (Imepokelewa kutoka kwa Ibn Majah, Ibn Khuzaymah, na Al-Hakim kutoka kwa Abu Said).
Na kauli yake S.A.W: “Saa ambayo dua itajibiwa iko kati ya kukaa kwa Imamu mpaka kumaliza swala” (Imepokelewa kutoka kwa Imamu Muslimu kutoka kwa Abu Musa) .
Ni wazi kutoka kwenye Hadithi hizi kwamba inathibitishwa kuwa katika siku ya Ijumaa iko saa ambayo dua hairudishwi ndani yake, na Hadithi hizi zimetaja sifa ya saa hii kama ilivyotajwa katika Hadithi ya Abu Hurayrah kuwa ni saa rahisi, na Hadithi ya Al-Twabaraaniy iliyotajwa hapo juu kutoka kwa Anas, na ilitajwa katika mapokezi ya Salamah ibn Alqamah iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhari: Mtume S.A.W akaweka ncha ya kidole chake juu ya kidole cha kati au cha mwisho. Tukasema: anaipunguza. Kutokana na hivyo inafahamika kuwa wakati ambao dua inajibiwa katika siku ya Ijumaa si muda kubwa, bali ni muda rahisi na haongozwi kwake isipokuwa aliyefanikiwa tu, hivyo kwa mujibu wa sifa yake, ama kuhusu kuainisha wakati wake, basi mitazamo ni mingi, Ibn Hajar katika Fath Al-Bari amesema mitazamo hii inafikia arobaini na tatu [2/416 na kurasa zilizo baada yake, Dar Al-Maarifa], lakini alisema baada ya hivyo: “Hakuna shaka kuwa mitazamo iliyo sahihi zaidi iliyotajwa katika Hadithi ya Abu Musa na Hadithi ya Abdullah ibn Salam”.
Mitazamo hii miwili ni kwamba saa ile iko kati ya swala ya Ijumaa na mwisho wa swala, au saa baada ya Al-Asiri mpaka kuchwa jua, kila wakati miongoni mwa masaa haya mawili inatarajiwa dua inajibiwa ndani yake.
Imam Ahmad alisema: “Hadithi nyingi zaidi zilitaja kuwa wakati huo uliotarajiwa kujibiwa dua uko baada sala ya Al-Asiri, na unatarajiwa pia baada ya kuchwa jua” (Sunan Al-Tirmidhi, 2/360, Mustafa Al-Halabi.).
Kuainisha kwa wakati wa kujibu dua katika siku ya Ijumaa ni suala la utata, hata wanavyuoni waliochagua mtazamo fulani hawahukumu kuwa wengine wamekosea. Kuhusu jambo hili Ibn Hajar anasema: “Ibn Al-Qayim alichagua mtazamo mwengine akisema kuwa wakati wa kujibu kwa dua uko katika moja ya masaa mawili yaliyotajwa, na kwamba mmoja wapo ulikuwa si kinyume na mwingine, kwa uwezekano kwamba Mtume S.A.W alionesha moja wapo katika wakati mmoja na mwiingine katika wakati mwingine, hii ni kama kauli ya Abdul Barr: inapaswa kujitahidi katika kuomba dua katika masaa haya mawili yaliyotajwa, na Imamu Ahmad alipendekeza mtazamo huu, Ibn Al-Muniir alisema katika maelezo yake kuwa: Kama ikifahamika kwamba faida ya kutoainisha saa hii na usiku wa cheo ni kulifanya mwenye kuomba dua anaswali swala nyingi na kuomba dua nyingi, na kama akiainisha saa hii watu wataitegemea na wataacha swala na dua katika masaa mengine, ni ajabu basi wanaofanya juhudi katika ombi la kuiainisha” [Fathul Bari 2/422].
Kuainisha wakati maalumu na kushikamana nao na kudai kwamba wakati huu ni wakati wa kujibiwa dua katika siku ya Ijumaa na kukataa kuwa masaa yaliyobaki katika siku ile siyo wakati wa kujibiwa dua, hali hii sio sahihi, mja lazima awe mwenye bidii katika kuomba dua siku nzima ili alipwe malipo makubwa.
Ikiwa hali hii haijulikani, basi hakuna ubaya wowote kuomba dua wakati Imamu anapokaa kati ya hotuba mbili. Wakati huu ni pamoja na wakati wa kujibiwa dua katika siku ya Ijumaa yaani kati ya adhana ya Ijumaa na kumalizia swala ya Ijumaa. Hivyo, kuomba dua wakati wa kukaa Imamu kati ya hotuba mbili ni halali kwa ajili ya kuomba dua katika saa ya kujibiwa dua kufuatana na mtazamo mmoja. Na sio lazima kukataa kwa wale wanaofuata mtazamo huu au waliouacha. Suala hilo ni la utata na hakuna mtazamo maalumu ambao ni sahihi zaidi kuliko mwingine.
Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.