Kuzimwa kwa kipaza sauti wakati wa ...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kuzimwa kwa kipaza sauti wakati wa swala

Question

 Kipaza sauti kinapozimwa katikati ya swala, na maamuma akawa hajui kama Imamu anarukuu, anasujudu au anasoma, katika hali kama hii, maamuma atafanyaje?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Katika wakati wa swala ya jamaa huwenda kipaza sauti kikazimika, kwa sababu moja au nyingine, Kama vile kwa kukatika umeme wa kipaza sauti, kutokana na hali hii sauti ya Imamu haitasikika, na hakuna njia kwa maamuma ya kuweza kujua hali ya Imamu.
Wanavyuoni wamesema kuhusu suala hili katika sura ya (Swala ya jamaa), ambako walitaja masharti ya kusihi swala nyuma ya Imamu.
Hukumu ya kuswali nyuma ya Imamu ni kwamba inaruhusiwa kwa maamuma kusali nyuma ya Imamu kama akimwona au akiwaona baadhi ya maamuma au akimsikia Imamu au anayeikariri sauti ya Imamu kwa maamuma au akiwasikia wao kwa pamoja.
Kama maamuma hasikii sauti ya Imamu au anayeikariri sauti yake, basi hairuhusiwi kuswali nyuma ya Imamu kwa sababu ya kutojua hali ya Imamu, kwa hivyo anapaswa kunuia kuswali peke yake na amalize swala yake.
Dalili ya kuruhusiwa kwa kuswali nyuma ya Imamu ambapo maamuma atakuwa anajua baadhi ya hali ya Imamu ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Aisha R.A, aliposema: Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W, alikuwa akiswali usiku katika chumba chake, na ukuta wake ulikuwa mfupi, watu wakamwona Mtume S.A.W. akiswali. Baadhi ya watu wakasimama wakaswali kwa kumfuata Yeye, ilipofika asubuhi wakayazungumzia hayo, (kuhusiana na Swala ya Mtume S.A.W) Mtume S.A.W. akasimama kuswali usiku wa pili, wakasimama watu wakamfuata katika swali yake, wakafanya hivyo kila siku usiku kwa muda wa siku mbili au tatu – na baada yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W. akakaa na hakutoka. Ilipofika asubuhi watu wakayasema hayo akasema: ((Hakika nimeogopa isije ikafaradhishwa juu yenu swala ya usiku)). [Imepokelewa kutoka kwa Al-Bukhari].
Ushahidi ni kwamba Masahaba hawajaona swala nzima ya Mtume S.A.W., lakini walikuwa wakiona baadhi ya sehemu za swala hii, hata hivyo, Mtume, S.A.W. alikubaliana nao katika vitendo vyao.
Vile vile ilipokelewa kutoka kwa baadhi ya Wanavyuoni waliotangulia dalili ya suala hili, Imamu Ahmad Al-Bayhaqi alisema: Abu Zakariya, abu Bakr, na Abu Said walisema kuwa: Abu Al-Abbas alituambia kuwa: Al-Rabii alituambia akisema: Ashafiy alituambia kuwa: Ibn Abi Yahya alituambia kutoka kwa Salih Mtumwa wa Al-Tawamah alisema: Niliona Abu Hurayrah alikuwa akiswali juu ya msikiti peke yake kwa kuifuata swala ya Imamu. Na katika mapokezi ya Abi Said katika kitabu cha Imamu alisema: tuliambiwa na Ibrahim Ibn Mohammad naye ni Ibn Abi Yahya alisema: Salih Mtumwa wa Al-Tawamah, kuwa alimwona Abu Hurayrah akisali juu ya msikiti kwa swala ya Imamu ambaye alikuwa msikitini. Imamu Ahmad (naye ni Al-Bayhaqi) alisema: Alifuatiwa na Ibn Abi Dhib, kutoka kwa Salih. Al-Shafii alisema katika Hadithi iliyopokelewa na Abu Said: Niliona baadhi ya waadhini, (watoaji adhana) wanaoswali kwa kuifuata swala ya Imamu juu ya msikiti, nilimuuliza Muslim ibn Khalid kuhusu hilo akasema, inaruhusiwa hivyo, lakini kama wakiwa chini hali hii ndiyo ninayoipendekeza mimi. Ashafiy alisema: Ibn Abbas haoni lolote baya kuswali katika msikiti kwa kuifuata swala ya Imamu. [Maarifat Al-Sunan Wal Athaar: 4/190, Chuo Kikuu cha Masomo ya Kiislam - Karachi].
Kuhusu dalili ya kuruhusiwa kutomaliza swala ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Jabir Ibn Abdullah: kuwa Muadh Ibn Jabal R.A, alikuwa akiswali pamoja na Mtume S.A.W, kisha hurudi kwa watu wake ili aswali pamoja nao mara nyingine, akasoma Surat AL BAQARAH, alisema: mtu mmoja akaswali haraka, basi Muadh alijua hivyo, akasema: mtu huyu ni mnafiki, mtu yule akajua hivyo, akaja kwa Mtume S.A.W. akasema: “Ewe Mtume wa Allah, sisi ni watu tunaofanya kazi kwa mikono yetu, na tunaleta maji kwa ngamia wetu, hakika Muadh alituswalisha jana, akasoma Surat Al-Baqarah, mimi nikaswali peke yangu haraka, akadai kuwa mimi ni mnafiki, Mtume S.A.W. akasema: “Ewe Muadh wewe unafitinisha -akasema hivyo mara tatu- Soma Surat Ash-Shams, Surat Wadh-Dhuha, nk.”. [Hadithi hii (ina hukumu ya Mutafaqu alaihi) imekubaliwa].
Al-Hafidh Ibn Hajar akasema: “Na mapokezi yote ya Hadithi yanaonesha kuwa mtu yule hakutoka katika swala, lakini aliendelea kuswala peke yake, Ar-Rafii alisema katika Sharhul Musnad kuhusu mapokezi ya Ashafiy kutoka kwa Ibn Uyaynah katika Hadithi hii kwamba: mtu mmoja nyuma yake (Muadh) aliamua kuketi mbali na akaswali peke yake. Maana ya Hadithi hii inawezekana kuwa mtu yule alikata swala yake (nyuma na Muadh) akakaa mbali, akaendeleza swala ya peke yake, ingawa faradhi hairuhusiwi kukatwa baada ya kuanzwa, kwa hivyo Wanavyuoni wa madhehebu ya Imamu Al-Shaafi wanaona kwamba maamuma anaruhusiwa kukata swala na kuendeleza swala peke yake”. [Fathu Al-Bari kwa Ibn Hajar 2/194, Dar Al-Maarifa]. Baadhi ya Wanavyuoni wamekubaliana na mtazamo huu tulioutaja, miongoni mwao ni:
Al-Khatib Al-Sherbini alisema: “(na) sharti la pili kutokana na masharti ya kumfuata Imamu ni kwamba maamuma (anahitaji kujua mabadiliko ya Imamu); ili aweze kumfuata (kwa kumwona au) kuona (baadhi ya safu au kuisikia sauti yake au sauti ya maamuma anayeikariri sauti ya Imamu), hata kama asipokuwa pamoja na maamuma, ingawa maneno ya Sheikh Abu Muhammad katika kitabu cha Al-Furuq yana maana kuwa anayeikariri sauti ya Imamu ni lazima awe mwaminifu kama alivyoeleza Ibn Al-Ustadh katika Sharul Wasiit na Sheikh Abu Mohammed katika kitabu cha Al-Furuq, ingawa imetajwa katika kitabu cha [Al-Majmuu] katika Sura ya Adhana kwamba Wanavyuoni wa Umma walisema: habari ya kijana inakubaliwa kama njia yake ni kutazama au kwa kuongozwa na mwaminifu akiwa ni kipofu au kiziwi au anaona katika giza au kama hivyo.” [Mughni Al-Muhtaj Ila Marifat Maani Alfadh AlMinhaj: 1/494, Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Sheikh Al-Dardeer alisema: “(na) inaruhusiwa (kwa abiria wa Majahazi) wakiwa karibu hata Majahazi haya yakiwa yanatembea baharini inaruhusiwa (kumfuata Imamu) mmoja kwa sharti la kuweza kusikia takbira yake au kuyaona matendo yake au kusikia sauti ya anayeikariri takbira yake (na) inaruhusiwa (kujitenga kwa maamuma) mbali na Imamu wake (kwa mto mdogo) kwa sharti la kutozuiliwa kumsikia Imamu au maamuma wake au kuona matendo yao ya swala”. [Al-Sharhu Alkabiir kwa Sheikh Al-Dardair pamoja na Hashiyat Al-Dosoki: 1/336, Dar Al-Fikr].
Ibn Qudaamah alisema: “Kama maamuma akitamka Takbira ya kuhirimia, kisha akanuia kumwacha Imamu wake, na kumaliza swala peke yake kwa ajili ya udhuru, inaruhusiwa, kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Jabir, aliposema: Muadh alikuwa akiswali pamoja na Mtume S.A.W. swala ya Isha, kisha anarudi kwa watu wake ili kuswali pamoja nao mara nyingine, Mtume S.A.W. akachelewesha swala ya Isha akaswali pamoja naye, kisha akarudi kwa watu wake akasoma Surat Al-Baqarah, mtu mmoja akachelewa akaswali peke yake, akaambiwa kuwa kafanya unafiki: Akasema: sikufanya unafiki, lakini nitakwenda kumwambia Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W. Akaja kwa Mtume S.A.W, akamwambia hivyo. Mtume akasema: “Je, unafitinisha wewe Muadh? Je, unafitinisha wewe Muadh? -akasema hivyo mara mbili- (Soma Sura fulani na Sura fulani) alisema: (Surat AL BURUJ, Surat AL LAYL, Suart AT-TWARIQ, na Surat AL GHASHIYAH). Hadithi hii imekubaliwa. Mtume hakumwamuru mtu yule kuiswali tena swala yake, wala hakukanusha kitendo chake, na nyudhuru ambazo kwa ajili yake maamuma anaweza kutoka katika swala, ni kama vile kuhisi ugumu wa kurefusha Imamu muda wa kusoma Qur’ani, au (maamuma kuwa) mgonjwa, au hofu ya kuzidiwa na usingizi, au kitu kinachobatilisha swala yake, au hofu ya kukosa mali au kuharibiwa kwa mali yake, au kuwakosa wenzake, au yeyote anayetoka nje ya safu na hakukuta mwingine atakayesimama pamoja naye, n.k. Kama maamuma akifanya hivyo bila udhuru, basi kuna mitazamo miwili: wa kwanza ni kwamba swala yake imebatilika, kwa sababu ameacha kumfuata Imamu wake pasipo na sababu yeyote. Mtazamo wa pili ni kwamba swala yake ni sahihi kwa sababu kama mtu anayeswali peke yake akinuia kuwa maamuma, basi swala yake ni sahili, nia ya kuswali peke yake ni bora zaidi kuliko nia ya maamuma, basi maamuma anaweza kugeuka kuswali peke yake pasipo na nia, naye ni aliyetanguliwa katika swala kama Imamu akimaliza swala, na mwingine hageuki kuwa maamuma pasipo nia”. [Al-Mughni kwa Ibn Qudaamah: 2/171, Maktabat Al-Qahira].
Pia inawezekana kupima suala hili kwa masuala yanayofanana nayo katika mlango wa kuswali Imamu, miongoni mwa masuala haya ni: udhu wa Imamu ukitenguka, basi maamuma wanaweza kuikamilisha swala kila mmoja peke yake ikiwa hakuna Imamu mwingine wa kukamilisha.
Al-Bahwatiy alisema: “(Kama hakuna Imamu mwingine wa kukamilisha) na maamuma (wakasali kila mmoja peke yake) (inaruhusiwa) hivyo (pia inaruhusiwa kama wakitanguliwa na Imamu mwingine) anayekamilisha swala pamoja nao, basi inaruhusiwa pia kama Imamu atamtanguliza maamuma ili kukamilisha sala)”. [Kaashaf Al-Qinaa an Matn Al-Iqnaa: 1/322, Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Na katika kitabu cha: [Sharh Mukhtasar Khalil” kwa Al-Khrashy [2/36, Dar Al-Fikr]: “(na) inaruhusiwa kwa abiria wa majahazi wakiwa karibu, inaruhusiwa kumfuata Imamu mmoja kwa sharti la kuweza kusikia takbira yake na kuyaona matendo yake, kama wakiwa wanatembea baharini au wamesimama, kwa mujibu wa rai ya Wanavyuoni iliyochaguliwa, kwa sababu asili ni kutokwepo kwa yanayosababisha kujitenga kati yao kama upepo au mfano wa hivyo, ikiwa upepo umewatawanya wanaweza kuchagua Imamu miongoni mwao ili kumaliza swala na wanaweza pia kumaliza swala kila mmoja peke yake, kama wakikutana mara nyingine wanaweza kumfuata Imamu wao wa kwanza, lakini kama wakiswali kila mmoja peke yake haruhusiwi mtu kurudi kwa Imamu wao wala haruhusiwi kufuta waliyoyafanya, kinyume na aliyetanguliwa katika (matendo ya swala) swala na akadhani kwamba Imamu amemaliza swala, akasimama ili kumalisha swala yake akajua kwamba alikosea (katika kudhani kwake), anaweza kurudi na kufuta (vitendo vya swala) alivyofanya.
Vile vile kama maimamu wakichagua Imamu mwingine ili awakamilishie swala yao, hawaruhusiwi kumfuata Imamu wao wa kwanza, kwa sababu tayari wameshamwacha, na kwa sababu wao hawana uhakika wa kujitenga kati yao mara nyingine kama alivyosema Abd Al-Haq”. Sheikh Al-Adawi anasema katika maelezo yake: “Kauli yake: (lakini kama hawakuswali peke yao) ni lazima kumfuata Imamu wao wa kwanza, na kama hawakuswali peke yao, wala hawakumfuata Imamu wao wa kwanza, wala hawakumfuata Imamu mwingine, basi swala yao ni batili”.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia hapo juu, inajulikana kwamba inaruhusiwa kwa maamuma kumfuata Imamu kama wanamwona au wanawaona maamuma wengine wanaomwona Imamu vizuri, au wanasikia takbira ya Imamu au wanasikia sauti ya maamuma anayeikariri takbira ya Imamu, lakini kama hali hizi hazikutokea, basi hairuhusiwi kumfuata Imamu katika wakati huo, kwa sababu hawaijui hali ya Imamu, na ni lazima kwa maamuma kunuia kumwacha Imamu, na kumalizia yaliyobakia katika swala yake.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.


Share this:

Related Fatwas