Takbira za Idd Mbili.

Egypt's Dar Al-Ifta

Takbira za Idd Mbili.

Question

 Nini hukumu ya Takbira za Idd mbili? Ni wakati gani wa kuanza na kwisha? Na je kuna utoaji wa Takbira ndani ya masiku ya tashriiq? Na je mtu anatoa Takbira peke yake au katika hali ya pamoja? Na je hizo Takbira zinakuwa ni baada ya Sala za Lazima? Na muundo wake upo vipi?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya hayo:
Takbira kwa upande wa lugha maana yake ni utukuzaji [Kamusi ya Lisan Al-Arab, 5/127, chapa ya Dar Sadir, na kusudio katika Takbira za Idd ni kumtukuza Mwenyezi Mungu Mtukufu, na kuthibitisha ukubwa wa Mwenyezi Mungu kwa tamko la (Allah Akbar) ikiwa na maana ya upweke wake katika Uungu, kwa sababu kutukuza kunalazimisha upungufu kwa asiyekuwa Mungu, na upungufu haukubaliki kwa Mwenyezi Mungu, kwa sababu ukweli wa Mwenyezi Mungu haukutani na upungufu wowote, na kwa sababu hiyo, Takbira zimewekwa kwenye Sala ili kubatilisha kusujudiwa asiyekuwa Mwenyezi Mungu, na zimewekwa Takbira wakati wa kuchinja wanyama kipindi cha hijja ili kubatilisha yale masanamu waliyokuwa wakijikurubisha kwayo makafiri, na vile vile zimewekwa Takbira baada ya kumalizika ibada ya funga kwa kauli yake Mola Mtukufu: {Na mtimize hiyo hesabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni}[AL BAQARAH: 185].
Na kutokana na hivyo imekuwa ni sunna kwa Waislamu kutoa Takbira wakati wa kuelekea kwenye Sala ya Idd na Imamu anatoa Takbira katika hotuba ya Iddi, na Takbira kwa kauli ya Muslim inakuwa (Allahu Akbar) ni ishara ya kuwa Mwenyezi Mungu Anaabudiwa kwa ibada ya funga na yeye Mola Mtukufu ameepukana na ubaya wa ibada za masanamu. [Rejea: At Tahrir wa At Tanwiir 2/17 chapa ya Dar at Tunisia]
Na Takbira kwenye Idd mbili ni Sunna kwa Makubaliano ya Jamhuri ya wanachuoni. Amesema Mwenyezi Mungu baada ya Aya za Funga: {Na mtimize hiyo hesabu, na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni} [AL BAQARAH: 185].
Na ikachukuliwa Takbira kwenye Aya kuwa ni ile Takbira ya Idd Al-Fitri, na Mwenyezi Mungu Mtukufu Anasema: {Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hesabiwa} [AL BAQARAH: 203]. Na Akasema pia: {Ili washuhudie manufaa yao na walitaje jina la Mwenyezi Mungu katika siku maalumu juu ya nyama hoa alio waruzuku} [AL HAJJ 28]. Na akasema Mola Mtukufu: {Namna hivi tumewadhalilisha kwenu ili mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa alivyo kuongoeni} [AL HAJJ 37]. Na imechukuliwa neno Dhikri “utajo” na Takbira katika Aya hizo zilizopita kwamba ni zile zinazokuwa katika Idd Al-Adh’ha.
Amesema Imamu Shafiy R.A. katika yale aliyoyanukuu kutoka kwa Khatwib As sharbiny katika kitabu cha: [Mughniy Al-Muhtaj] amesema: "Nimemsikia aliyekubalika katika wanachuoni kwenye Qur`ani anasema: kusudio la neno “hesabu” ni hesabu ya siku za kufunga, na kwa Takbir ni pale wakati wa kukamilishwa kwa hesabu ya siku za kufunga".
Na dalili ya Pili: kwa maana ya Takbira za Idd Al-Adh’ha – ni kipimo cha Takbira za kwanza - yaani Takbira za Idd Al-Fitri, na kwa ajili hiyo Takbira za Idd ya kwanza zilikuwa ni msisitizo wa andiko lake, [Mughniy Al-Muhtaj, 1/593, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Na akasema Ibn Hazmi: “Takbira usiku wa Idd Al-Fitri ni lazima, nazo katika usiku wa Idd Al-Adh’ha zimependekezwa. Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema: {Na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni ili mpate kushuruku} [AL BAQARAH: 185], kwa kukamilisha hesabu ya kufunga Ramadhani ni lazima kutoa Takbira, na yatosha kwa ibada hiyo ya funga kuleta Takbira [Kitabu Al-Muhalla, 3/304, chapa ya Dar Al- Fikr].
Na kutoa Takbira ndani ya masiku ya Tashriiq ni jambo la kisheria kwa kauli yake Mola Mtukufu: {Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazohesabiwa} [AL BAQARAH: 203]. Pamoja na kukubaliana wanachuoni juu ya usheria wa kuleta Takbira ndani ya masiku ya Tashriiq, isipokuwa wanatofautiana katika hukumu yake, kwa upande wa madhehebu ya Imamu Hanbali Imamu Shafiy na baadhi ya wafuasi wa Imamu Abu Hanifa kuwa ni sunna kwa kudumu nayo kwake Mtume S.A.W, nayo kwa upande wa Imamu Maliki inapendeza, na usahihi kwa upande wa Abu Hanifa ni lazima, kwa amri ya kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na mtajeni Mwenyezi Mungu katika zile siku zinazo hisabiwa} (Angalia: Kashaf Al-Iqnaa, 2/85, chapa ya Dar Al-Fikr, na kitabu Al-Majmuu, 5/31 chapa ya Dar Al-Kutub Al- Elmiya, na Al-Hawy Al-Kabir, 2/485, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya, na Al-Bahr Ar-Raaiq, 2/177 chapa ya Dar Al-Kitab Al-Eslamy, na Badai As-Sanai, 1/195, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya).
Wametofautiana wanachuoni juu ya wakati wa kuleta hizo Takbira, kwa upande wa muda wa kuanza wamekubaliana wanachuoni ni kabla ya kuanza kwa masiku ya Tashriq, na kutafautiana kwao ni kuwa kwake wakati wa Adhuhur siku ya kuchinja kama anavyosema Imamu Malik na baadhi ya watu wa madhehebu ya Imamu Shafiy, au wakati wa alfajiri siku ya Arafa kama anavyosema Imamu Hanbali na wanachuoni wa Abu Hanifa. [Angalia: Sharh Al-Kabir Ala Mukhtasar Khalil, 1/401, chapa ya Dar Al-Fikr, na Majimuu, 5/31, chapa ya Dar Al-fikr, na Kashaf Al- Iqnai, 2/58, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elmiya].
Ama kwa upande wa kumalizika, Imamu Hanbal, Abi Yussuf na Muhammad mfuasi wa madhehebu ya Abu Hanifa, na katika kauli ya Shafi na Malik mwisho wake unakuwa ni wakati wa Swala ya Asiri ya mwisho wa siku ya Tashriiq, na wafuasi wa Imamu Malik wao wanaona kuwa kauli yenye kutegemewa kwao ni kukamilishwa Takbira wakati wa Al-Fajiri ya mwisho ya siku za Tashriq. [Angalia: Al-Dar Al-Mukhtar, 2/180, chapa ya Dar Al-Fikr na Majmuu, 5/34, na Sharh Muntahi Al- Iradat, 1/329, chapa ya Aalam Al-Kutub].
Na kwa upande wa kutoa Takbira kwa sauti na kwa pamoja, hii imekuwa ni katika alama za Idd. Bila shaka, Takbira ya pamoja ina nguvu na sauti kubwa, na imekuwa ni katika alama sahihi ya Idd, na wanachuoni wa Madhehebu ya Imamu Abu Hanifa wamekokotezea utoaji wa Takbira ndani ya masiku ya Tashriq kwa wanaume na wanawake angalau mara moja, na ikiwa watazidisha zaidi ya mara moja basi itakuwa ni bora zaidi, na hutolewa hizo Takbira kwa pamoja au kwa mtu mmoja mmoja, na kwa upande wa wanaume zinakuwa kwa sauti, na kwa upande wa mwanaumke zinakuwa kwa sauti ndogo. [Hashiyat Ibn Aabideen Ala Ad-Dar Al-Mukhtar, 2/177 – 179].
Ama kwa upande wa Imamu Malik yeye anaona inapendeza kuleta Takbira kwa pamoja na mtu mmoja mmoja. Amesema As-Sawiy katika kitabu chake: “Inapendeza kuleta Takbira ya mtu anapokuwa peke yake pale anapokuwa njiani kuelekea kusali, ama kuleta Takbira kwa pamoja ni pale watu wanapokuwa wamekaa sehemu ya kusalia na hili ndilo linalopendekezwa lifanyike. Amesema Ibn Naajy: watu wa Qairawani wamegawanyika makundi mawili, kundi la Abi Amru Al-Farisy na kundi la Abi Bakr ibn Abdulrahman, linapomaliza kundi moja kuleta Takbira kundi lingine linaleta Takbira, na kwa ajili hiyo, wakaulizwa juu ya hilo? Wakasema: kufanya hivyo ndio bora zaidi”. [Hashiyat as-Sawiy Ala Sharh Al-Kabir, 1/529, chapa ya Dar Al-Maarif].
Amepokea Imamu Malik ndani ya kitabu cha Al-Muutwiu kutoka kwa Umar Ibn Khattab kuwa alitoka wakati wa asubuhi siku ya kuchinja wakati jua likiwa limepanda kidogo huku akileta Takbira na watu wakaleta Takbira kwa kufuata Takbira yake, kisha akatoka mara ya pili siku hiyo hiyo baada ya mchana kuongezeka kidogo akaleta Takbira na watu wakaleta Takbira kwa Takbira yake, na akatoka mara ya tatu wakati jua lilipokuwa linawaka na akaleta Takbira kisha watu nao wakaleta Takbira kwa kufuata Takbira yake mpaka zikaungana Takbira na kufika sauti majumbani na kufahamika kuwa Umar ametoka kwenye kurusha vijiwe. Amesema Imamu Malik: “Kwetu sisi kuleta Takbira ndani ya masiku ya Tashriq ni baada ya Sala ya Faradhi, na mwanzo wa hiyo Takbira ni Takbira ya Imamu na watu wakimfuatia na kuitoa pamoja naye mwishoni mwa Sala ya Adhuhur kuanzia siku ya kuchinja, na Takibra ya mwisho ya Imamu na Waumini ni mwisho wa Sala ya Al-Fajiri ya mwisho ya siku za Tashriiq kisha Takbira zinakatishwa”.
Na akasema pia “uletaji wa Takbira katika masiku ya Tashriiq kwa wanaume na wanawake wakiwa pamoja au mtu mmoja mmoja wakiwa Mina au sehemu nyengine yoyote ni jambo la lazima, na watu watakamilisha wakiwa hija na pale wanapokuwa Minaa kwa sababu pindi wanaporudi na kumaliza kazi za kuhirimia hija watakamilisha nao na kuwa kama wao, ama yule ambaye hayupo kwenye ibada za hija basi hatokamilisha nao isipokuwa atakamilisha Takbira ndani ya masiku ya Tashiriiq”. [Angalia: Al-Istidhkar, 4/337, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiya, na Al-Muntaqaa, 3/42, chapa ya Dar As-Saada, na Sharh Az-Zarqaniy Ala Al-Muutwii, 2/548 – 549, chapa ya Dar At-Thaqafa Ad-Diniya].
Ama kwa upande wa Imamu Shafi yeye anaona kuwa inapendeza kwao kuleta Takbira kwa pamoja na kwa sauti. Amesema Sheikh Al-Islam Zakaria Al-Ansary: “Ama Takbira pasipokuwa sehemu hizo mbili – yaani kwenye Sala na hotuba – ni aina mbili: ya kwanza ni ya moja kwa moja isiyofungana na hali yoyote, na ya pili ni ile inayoletwa mwishoni mwa Swala maalumu, aina ya kwanza inaanza pale linapozama jua usiku wa Idd, yaani Idd Al-Fitri na Idd Al-Adh’ha, na dalili ya kwanza ni kauli yake Mola Mtukufu: {Na mtimize hiyo hesabu} yaani hesabu ya siku za funga ya Ramadhani na mumtaje Mwenyezi Mungu, yaani pale zinapokamilika, inadumu mpaka anapo hirimia Imamu Swala ya Idd, Takbira ya kwanza anayoshughulika nayo ni kwa sababu ya kumtaja Mwenyezi Mungu na alama ya siku hiyo, ikiwa mtu atasali peke yake mazingatio ni kuhirimia kwake. (na watu kuinua sauti zao) inapendekezwa ili kuonesha alama ya siku ya Idd tofauti na siku zingine, pamoja na majumbani, barabarani, misikitini, masokoni, usiku na mchana, ila inaondolewa hali ya kuinua sauti kwa mwanamke, na uwazi ni kuwa sehemu yake mwanamke ni pale anapokuwa amehudhuria Sala ya Pamoja na wala hakuna wale maharimu, na mfano wake ni kama vile khuntha”. (Asnaa Al-Matalib, 1/284, chapa ya Dar Al-Kitab Al-Islamiy).
Amesema Imamu Shafi: “Pindi wanapoona mwezi wa mwandamo wa mfunguo mosi imependeza watu walete Takbira kwa pamoja na hata mtu mmoja mmoja Misikitini, masokoni, barabarani, majumbani, wasafiri na wenyeji katika hali zote na popote walipo wanatakiwa kuleta Takbira” [Kitabu Al-Umm, 1/264, chapa ya Dar Al-Maarifa].
Imamu An-Nawawiy ameelezea kuwa kundi la Masahaba na waja wema waliotangulia walikuwa wanaleta Takbira pindi wanapotoka kuelekea kwenye Sala ya Idd mpaka wanapofika msikitini hunyanyua sauti. [Kitabu Sharh An-Nawawiy Ala Sahih Muslim, 6/179, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Ama madhehebu ya Imamu Hanbali wao wanaona kutoa sauti kwa Takbira ni sunna kwa upande wa wanaume tofauti na wanawake, hakuna sunna kwao kutoa sauti kwa Takbira. [Matalib Uli Al-Nuha, 1/802 chapa ya Al-Maktab Al-Islamiy].
Wanachuoni wakatoa dalili juu ya kupendezeshwa Takbira za Idd kuwa kwa pamoja na kwa sauti kwa dalili nyingi, miongoni mwa hizo ni Hadithi iliyopokelewa na Bukhary katika sahihi yake: “Omar R.A. alikuwa analeta Takbira pale anapokuwa Kuba ya Minaa na alikuwa akisisikika na watu waliomo msikitini, nao wanaleta Takbira, na watu waliomo sokoni walikuwa wakileta Takbira mpaka Mina yote ikawa imeenea Takbira.
Na alikuwa Ibn Omar R.A. naye akileta Takbira Mina siku hizo akiwa kwenye Swala, na anapokuwa kitandani, kwenye makazi yake na maeneo yote kwa siku hiyo anayopita. Na alikuwa analeta Takbira siku ya kuchinja. Na wanawake walikuwa wanaleta takbira nyuma ya Abaan Ibn Uthman na Umar Ibn Abdulaziz ndani ya masiku ya Tashriiq pamoja na wanaume msikitini”.
Amesema Al-Hafidh Ibn Hajar katika sherehe ya Hadithi: “sauti yake inagongana na kupaa, nayo ni maelezo ya kukusanyika na kutoa sauti”[kitabu Fat’h Al-Bary, 2/464, chapa ya Dar Al-Maarifa].
Hakuna shaka kuwa sauti za pamoja ni zenye nguvu zaidi kuliko sauti ya mtu mmoja mmoja, hili linaonesha juu ya usahihi wa kuleta Takbira kwa pamoja, na kwa vile imethibiti kuwa inafaa kuleta Takbira katika Sala ya Idd kwa pamoja kutoka kwa Masahaba na waja wema waliotangulia pamoja na wanachuoni wa madhehebu mbali mbali, sura iliyofikiwa katika hilo inakuwa ni kwa kukubaliana kuleta kwa pamoja kwa sauti moja, ikiwa kundi limekaa chini na kuleta Takbira kwa pamoja na kwa sauti pasi na kukubaliana, hilo litapelekea kuibuka hali ya ushawishi ambao unaharibu makusudio ya utajo kwa kubatilisha, ambapo hali ya unyenyekevu inaondoka.
Kuleta Takbira mwishoni mwa Sala hakuna tofauti kati ya wanachuoni katika uhalali wake ndani ya masiku ya Tashriiq. Na Takbira ni sunna kwa Jamhuri ya wanchuoni, na ni wajibu kwa madhehebu ya Imamu Abu Hanifa.
Amesema Imamu Malik: “Kwetu sisi Takbira ndani ya masiku ya tashriiq ni kila baada ya Sala” [kitabu Muutwii Malik simulizi ya Yahya Allaythy, 1/404, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Ama kwa upande wa maneno ya Takbira katika sunna takatifu, ni kwamba hakuna maneno yaliyopokelewa maalumu kwa takbira, lakini hata hivyo imepokelewa kutoka kwa baadhi ya Masahaba, miongoni mwao ni Salman Al-Farisy maneno ya Takbira kama ifuatayo: “Allahu Akbaru Allahu Akbaru Allahu Akbaru, Laa ilaaha illa llah Allah Akbaru, Allahu Akbaru walillahil hamdu” na Takbira zenyewe ni zaidi ya hapo, kwa sababu tamko lililopokelewa katika hizo Takbira ni kauli yake tu Mola: {Na mumtukuze Mwenyezi Mungu kwa kuwa amekuongoeni} [AL BAQARAH: 185]. Na kitu kilichokuja bila kikomo kwenye amri yake basi huchukuliwa katika hali hiyo hiyo mpaka litakapokuja tamko linalohusishwa kisheria, na imekuja kwenye kitabu cha: [Ghamz Uyun Al-Basair” cha Hamuwy, 2/217, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiya] kuwa: “kitu kilichokuja kimeachiwa bila mipaka kwenye amri yake hufanyiwa kazi katika hali ya uhuru isipokuwa pale inapokuwepo dalili".
Wamisri wameupokea tokea hapo zamani muundo unaofahamika hivi sasa ambao ni: (Allah Akbar Allah Akbar Allah Akbar, La ilah illa Allah Allah Akbar, Allah Akbar walillahil hamd. Allah Akbar kabira wal hamdulillah kathira wasubhana Allah bukratan wa aswila, la ilaha ila Allah wahdah sadaqa waadah wanasara abdah wa aaza jundah wahazam al-ahzaba wahdah, la ilah ila Allah wala na’abudu ila iyah mukhlisina lahul Din walau karhal kafirun, allahumma sali ala sayidina Muhammad, waalaa aali sayidina Muhammad waalaa as-hab sayidina Muhammad, waalaa ansari sayidina Muhammad, waalaa azwaji sayidina Muhammad, waalaa dhuriyat sayidina Muhammad, wasallim tasliman kathira).
Ni utaratibu wa kisheria na ulio sahihi. Amesema Imamu Shafiy R.A: “ikiwa mtu ataleta Takbira kama vile wanavyoleta watu hivi sasa basi itapendeza, na ikiwa atazidisha basi pia itapendeza, na ikiwa atazidisha zaidi ya hivi katika kumtaja Mwenyezi Mungu basi mimi ninapendelea hivyo zaidi” [Angalia: kitabu Al-Umm, 1/276, chapa ya Dar Al-Maarifa].
Na kuongeza kumsalia Mtume, jamaa zake, Masahaba wake, watetezi wake, wake zake na kizazi chake mwishoni mwa Takbira ni jambo la kisheria, kwani utajo ulio bora ni ule unaokusanya utajo wa Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W, kama ambavyo kumtakia rehema na amani Mtume S.A.W, kunafungua milango ya kukubalika kwa maombi, kwani maombi hukubalika siku zote hata kama mwombaji ni mnafiki kama walivyoelezea hilo watu wa elimu.
Kutokana na maelezo yaliyotangulia, kuleta Takbira ni jambo la sunna kwa makubaliano ya Jamhuri ya wanachuoni, na kunaanzia kabla ya kuanza masiku ya tashriiq, pamoja na kutofautiana mwanzo wake kati ya Adhuhuri siku ya kuchinja na wakati wa Alfajiri siku ya Arafa, na mwisho wake ni wakati wa Alasiri siku ya mwisho ya masiku ya tashriiq. Na inafaa – kwa mujibu wa yale tuliyo yaelezea hapo nyuma – kuwa katika hali ya pamoja au mtu peke yake, na kuleta Takbira kwa pamoja ni bora zaidi kama tulivyoelezea, na hakuna maneno maalumu yaliyopokelewa katika Sunna takatifu, ambapo maneno yanayofahamika na ambayo yamepokelewa na Wamisri ni ya kisheria na yapo sahihi, na mwenye kudai kuwa msemaji wake amezusha, basi yeye mwenyewe atakuwa karibu zaidi na uzushi, ambapo atakuwa amelibana lililopana na kukifinya kile alichokitanua Mwenyezi Mungu na Mtume wake S.A.W. na kukifunga kilichohuru pasi na dalili. Na inatutosha katika hilo kile kilichofanywa kwa urefu na waja wema waliotangulia miongoni mwa mazuri mfano wa maneno haya na kukubalika kwake na watu wa kawaida sawa na kukubalika kwenye Sheria Takatifu na kutopingana, na kukataza kwa mwenye kuyakataza hayo sio jambo sahihi, na wala hazingatiwi.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.

 

 

Share this:

Related Fatwas