Hukumu ya Kugeuka Upande wa Kulia n...

Egypt's Dar Al-Ifta

Hukumu ya Kugeuka Upande wa Kulia na Upande wa Kushoto Wakati wa Adhana Katika Kipaza Sauti.

Question

 Je! Ni ipi hukumu ya kugeuka upande wa kulia na upande wa kushoto wakati wa kutoa adhana katika kipaza sauti?

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu.
Maana ya Adhana katika lugha ni: kutangaza, maana yake kufuatana na Sheria ni: maneno maalumu yanayotangaza mwanzo wa wakati wa swala ya faradhi. [Mughni Al-Muhtaj kwa Al-Khatib Al-Sharbini: 1/317, Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Na Al-Haialtan maana yake ni kusema: (Hayya alas-swalaah) na: (Hayya Alal-falaah). [Lisan Al-Arab kwa Ibn Mandhuur: 11/705, Dar Swadir].
Na inapendekezwa kugeuka upande wa kulia na upande wa kushoto wakati wa adhana kufuatana na kukiri kwa Mtume S.A.W. na kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhariy na Muslim kutoka kwa Aoun Ibn Abu Juhaifah, kutoka kwa baba yake alisema: "Nilimjia Mtume S.A.W., kwenye Makkah, wakatai alipokuwa katika kuba nyekundu, akasema: na Bilal aliadhini, nikaufuatilia mdomo wake huku na huku, kuelekea upande wa kulia na upande wa kushoto akisema (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), na katika mapokezi ya Abu Dawud kuwa: “Nilimwona Bilal akitoka nje akaadhini, na alipofikia (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah) akageuza shingo yake upande wa kulia na upande wa kushoto, na hakugeuza mwili wake”, wala hakuna ubaya kuhusu kipaza sauti kwani kinasikiza watu adhana tu, wala hakizuii kufuata Sunnah ya kugeuka katika adhana, kama alivyosema Ibn Abidin katika maelezo yake: “Kugeuka ni miongoni mwa Sunnah za adhana, hairuhusiwi kwa mwadhini kuziacha Sunnah hizi, hata kama akiwa peke yake, au hata katika adhana ya mzaliwa pia inalazimishwa kwa mwadhini kugeuza shingo yake”. [Maelezo ya Ibn Abidin Ala Al-Durr Al-Mukhtar: 1/387, Dar Al-Kutub Al-Elmiyah].
Al-Hafidh Ibn Hajar alisema: “Hali hii ina kizuizi cha kugeuka katika adhana, na wakati wake aliposema mwadhini (Hayya Ala As swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah). Ibn Khuzaymah aliweka kichwa cha maudhui hii akisema kugeuka kwa mwadhini wakati wa kusema (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), kwa mdomo wake si kwa mwili wake mzima, alisema, lakini inawezekana kugeuka kwa mdomo na uso tu.”. [Fath Al-Bariy Sharh Sahih Al-Bukhariy: 2/115, Dar Al-Maarifa].
Al-Aini alisema: “Kauli yake Al-Bukhariy: (Je, anageuka?) Yaani: Je, mwadhini anageuka katika adhana? Ndiyo anageuka: maneno hayo yanathibitishwa na mapokezi ya Ismaili yaliyotajwa hapo juu, na mapokezi ya Abi Dawud pia inathibitisha hivyo, na maana ya kugeuka ni kugeuza shingo tu, wala hageuzi mwili wake mbali na upande wa kibla, wala hageuzi miguu yake kutoka mhala pake, na rai hii ilichaguliwa pia na Al-Thawri, Al-Awzai, Abu Thawr, na Ahmed katika mapokezi moja. [Umdatul Qarii: 5/147, Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabi].
Al-Haskafiy alisema katika kitabu cha: [Al-Durr Al-Mukhtar]: “Inageuzwa katika adhana kwenye upande wa kulia na upande wa kushoto tu, ili kibla kisigeuzwe na kukipa mgongo katika kauli ya mwadhini (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), hata kama akiwa peke yake, au katika adhana ya mzaliwa; kwani ni Sunnah ya adhana”. [Al-Durr Al-Mukhtar – Maelezo ya Ibn Abidin - 1/259 Ihyaa Al-Turath].
Al-Babratiy Al-Hanafiy alisema: “Mwadhini anageuza uso wake anaposema: (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), upande wa kulia na upande wa kushoto kwa sababu ni taarifa kwa watu kwa hivyo mwadhini anaelekea kwao. Ilisemekana kuwa: ikiwa hali ni hiyo, basi anaweza kuelekea nyuma yake pia; kwa sababu watu wako nyuma pia, na ilijibiwa kwamba: mwadhini hakuelekea nyuma; ili kibla isigeuzwe na kukipa mgongo, wakati ambapo adhana inaita kuelekea kibla, kwa hiyo, mwadhini imetosha kugeuza shingo yake upande wa kulia na upande wa kushoto tu ili kufikisha sauti yake kwa watu”. [Al-Inayah Sharhul Hidayah kwa Al-Babratiy: 1/244, Dar Al-Fikr].
An Nawawiy wa Kishafiy alisema katika kitabu cha: [Al-Majmuu] kuwa: “Miongoni mwa Sunnah za adhana ni kugeuka kwa mwadhini katika upande wa kulia na upande wa kushoto aliposema (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), akiwa juu ya ardhi au mnarani, na ameeleza namna gani inageuzwa, kuwa mwadhini anaelekea upande wa kulia akisema: (Hayya Ala As Swalaah) mara mbili, kisha anaelekea upande wa kushoto akisema: (Hayya Ala Al Falaah), mara mbili, na rai hii ilichaguliwa na Al-Nakh'iy, Al-Thawriy, Al-Awzaiy, Abu Thawr, nayo ni mapokezi ya Ahmed”. [Al-Majmuo' Sharhul Muhadhab: 3/115, Ch. Al-Maktba’ah Al-Muniriyah].
Al-Khatwib Al-Sherbiniy alisema: “Ni Sunnah kugeuza shingo tu katika kauli ya mwadhini: (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), siyo kwa mwili, wala kwa kuondoka mahala akiwa mnarani akielekea upande wa kulia akisema: (Hayya Ala As Swalaah) mara mbili, kisha anaelekea upande wa kushoto akisema: (Hayya Ala Al Falaah) mara mbili, na mwadhini anaelekea wakati wa kusema hivyo tu, kwani ni mwito wa kuwenda kuswali kinyume na maneno yaliyobaki katika adhana. [Mughni Al-Muhtaj 1/322].
Ibn Qudaamah Al-Hanbali alisema katika kitabu cha: [Al-Mughni" kuwa: “Inapendekezwa kugeuzwa kwa uso upande wa kulia, kama akisema: (Hayya Ala As Swalaah) na kugeuzwa upande wa kushoto, kama akisema: (Hayya Ala Al Falaah), wala hageuzi miguu yake nyuma ya kibla kwa mujibu wa Hadithi ya Abu Jahfah aliposema: "Nilimwona Bilal akiadhini, nikaufuatailia mdomo wake huku na huku, na vidole viwili vyake viko masikioni mwake". Hadithi hii Imekubaliwa. Katika mapokezi mengine alisema: "alipofikia kauli yake: (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), akaelekea upande wa kulia na upande wa kushoto kwa shingo tu," Imepokelewa kutoka kwa Abu Dawud. [Al-Mughni: 1/309, Ch. Maktabat Al-Qahirah].
Kulingana na yaliyotangulia hapo juu: kugeuka kwa mwadhini anaposema: (Hayya Ala As Swalaah) na: (Hayya Ala Al Falaah), ni jambo linalopendekezwa, halihusiani kama akiwa mwadhini anaadhini katika kipaza sauti au la, basi jambo hili ni Sunnah linalohusiana na jinsi ya kuadhini katika hali zote.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas