Swala ya Sunna Wakati wa Swala ya F...

Egypt's Dar Al-Ifta

Swala ya Sunna Wakati wa Swala ya Faradhi.

Question

{Pindi inapokimiwa Swala hakuna Swala isiokuwa Swala ya Faradhi} ni nini maana ya maneno haya? Na je ikikimiwa Swala ya Faradhi au ya lazima na mtu akawa anaswali Swala ya Sunna au Swala ya Maamkizi ya msikiti anapaswa kuikata ili aingie kwenye Swala ya Pamoja? 

Answer

 Namshukuru Mwenyezi Mungu, rehma na amani ziwe kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu pamoja na jamaa zake Masahaba wake na wale waliomfuata, baada ya hayo.
Hakika Mwenyezi Mungu Amefaradhisha Swala tano na kuzitukuza zaidi kuliko Swala zingine za Sunna, lakini pia imetukuzwa zaidi ya ibada zingine, Swala ikafanywa kuwa ni nguzo ya Dini, imepokelewa na Al-Baihaqiy kutoka kwa Umar Ibn Khattab R.A. amesema: Amesema Mtume S.A.W.:- "Swala ni nguzo ya Dini" ibada inayomuweka karibu zaidi mja kwa Mwenyezi Mungu ni Swala za Lazima na zile za Sunna, imepokelewa na Imamu Bukhari toka kwa Abi Huraira kuwa Mtume S.A.W. amesema kwenye Hadithi Al-Qudusy toka kwa Mola Mtukufu:
"Hajajiweka karibu kwangu mja wangu kwa kitu ninachokipenda zaidi kwangu kuliko ibada niliyoilazimisha kwake, na wala mja wangu hatoacha kujiweka karibu kwangu kwa ibada za sunna mpaka ninakuwa nampenda, pindi ninapompenda ninakuwa msikivu wake ambaye anasikia, na jicho lake ambalo anatazamia, na mkono wake ambao anachukulia, na mguu wake ambao anatembelea, ikiwa ataniomba nitampa, na ikiwa atataka kinga basi nitamkinga".
Na umuhimu wa ibada ya Swala, Amesema Mtume S.A.W. katika Hadithi ambayo imepokelewa na Imamu Muslim kutoka kwa Abi Huraira R.A. amesema: Amesema Mtume wa Mwenyezi Mungu S.A.W.: - "Pindi inapokimiwa Swala, basi hakuna Swala isipokuwa ni Swala ya Faradhi". Inapokimiwa Swala, basi inachukiza mtu kuingia kwenye Swala ya Sunna, na hii ni kutokana pia na Hadithi iliyopokelewa na Imamu Bukhariy na Muslim Hadithi itokanayo na Abdallah Ibn Malik Ibn Bahina R.A. amesema: "Siku moja Mtume alipita na kulikuwa na mtu anaswali na tayari Swala ya Alfajiri ilikuwa imeshakimiwa Mtume akamwambia kitu sisi hatukufahamu ni kitu gani hiko, tulipoondoka tukawa tunasema: Mtume wa Mwenyezi Mungu Amekwambia nini? Akasema: ameniambia: anahofia mmoja wenu akaswali Swala ya Asubuhi rakaa nne} na imepokelewa na Ibn Habbani na Ibn Khuzaima kutoka kwa Ibn Abbas R.A. amesema: "Ilikimiwa Sala ya Asubuhi, basi nikasimama kusali rakaa mbili, Mtume akanichukuwa kwa mkono wake S.A.W. na akasema: Je utaswali Swala ya Asubuhi rakaa nne".
Na imepokelewa na Imamu Muslim kutoka kwa Abdallah Ibn Sarjas R.A. amesema: "Kuna mtu mmoja aliingia msikitini na Mtume wa Mwenyezi Mungu alikuwa anaswali Swala ya Alfajiri, basi akasali rakaa mbili pembezoni mwa msikiti, kisha akajiunga na Swala ya Mtume S.A.W., baada ya Mtume kutoa salamu akasema: ewe fulani ni ipi kati ya Swala mbili uliyoisali, ni Swala yako ya peke yako au Swala yako ya pamoja na sisi?"
Hadithi zote hizi zinaonesha kuchukiza kuingia mtu kwenye Swala ya Sunna pindi inapokimiwa Swala ya Lazima.
Amesema Al-Bahutiy Al-Hanbaliy ndani ya kitabu cha: [Kashaafu Al-Iqnaau]: “Pindi inapokimiwa Swala – kwa maana ya mwadhini ameshaanza kukimu Swala, kwa mapokezi ya Ibn Habbani kwa tamko: “Pindi mwadhini anapokimu Swala” ambaye anataka kuswali na imamu – basi hakuna Swala isipokuwa ni Swala ya Lazima, wala hatakiwi mtu kuingia katika Swala ya Sunna, au Sunna ya Swala ya Alfajir au Sunna nyingine ndani ya msikiti” [Kashaf Al-Qinai, Bahutiy Al-Hanbaliy, 1/459, chapa ya Dar Al-Kutub Al-Elamiya].
Na akasema mwenye kitabu cha: [Al-Mughniy]: “Na pindi inapokimiwa Swala mtu asijishughulishe na Swala ya Sunna, ni sawa sawa kwa kuhofia kupitwa na rakaa ya kwanza au kutohofia, kwa kauli ya Mtume S.A.W.: Pindi inapokimiwa Swala, basi hakuna Swala isipokuwa ni Swala ya Faradhi” imepokelewa na Imamu Muslim, na kitakachompita kwa Imamu ni bora zaidi kuliko atakacho kileta, hivyo asilete chochote. [Al- Mughniy cha Ibn Qudama, 1/272, chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy]
Na akasema Imamu An-Nawawiy katika Majmuui: “Pindi inapokimiwa Sala inachukiza kushughurika na Sala ya Sunna ni sawa sawa iwe Sala ya maamkizi ya msikiti sunna ya ya alfajiri na zenginezo” [Al-Majmuu Sharhu Al-Muhadhab, 3/550 chapa ya Matbaa Al-Munira].
Ama mtu akiwa ameingia kwenye Swala ya Sunna kisha ikakimiwa Swala, ikiwa atahofia kupitwa na Swala ya Pamoja (Jamaa), basi ataikatiza Swala yake na kujiunga na Swala ya Pamoja, kwa sababu kuipata Swala ya Lazima (faradhi) ni bora zaidi, na kuipata Swala ya Pamoja ni kuna thawabu nyingi kuliko Swala ya peke yako, Anasema Mtume S.A.W. katika Hadithi Al-Qudusy kutoka kwa Mola Mtukufu: “Mja wangu hatojiweka karibu kwangu kwa kitu nikipendacho zaidi kuliko kutekeleza ibada niliyo ifaradhisha kwake” na anasema Mtume S.A.W. katika Hadithi iliyopokelewa na Imamu Bukhariy na Muslim kutoka kwa Abi Saad Al-Khudriy R.A. amesema: Amesema Mtume S.A.W.:- “Swala ya Pamoja inaizidi Swala ya mtu peke yake kwa daraja ishirini na tano” na katika mapokezi mengine “daraja ishirini na saba”
Amesema mwandishi wa kitabu cha: [Al-Mughniy]: "Ama ikiwa Swala imekimiwa na mtu bado yupo kwenye Swala ya Sunna, na wala hakuhofia kupitwa na Swala ya Pamoja “Jamaa”, basi ataikamilisha bila kuikata, kwa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu pale Aliposema: {Na wala msiviharibu vitendo vyenu} [MUHAMMAD: 33]. Na ikiwa atahofia kupitwa na Swala ya Pamoja, basi kuna kauli mbili, ya kwanza inasema atakamilisha Swala yake ya Sunna, na kauli ya pili, ataikatisha Swala yake ya Sunna, kwa sababu atakacho kiwahi kwenye Swala ya Pamoja kina malipo makubwa zaidi na thawabu nyingi kuliko kinachompita kwa kuendelea na Swala ya Sunna, kwa sababu Swala ya Jamaa inazidi Swala ya mtu peke yake daraja ishirini na saba) [Al-Mughniy, Ibn Qudama, 1/272 chapa ya Dar Ihyaa At-Turath Al-Arabiy].
Amesema As-Shairaziy katika kitabu cha: [Al-Muhadhab]: “Ikiwa mtu ameingia kwenye Swala ya Sunna kisha ikakimiwa Swala ikiwa hatahofia kupitwa na Swala ya Pamoja, basi atakamilisha Swala yake kisha ataingia kwenye Swala ya Pamoja, na ikiwa atahofia kupitwa na Swala ya Pamoja ataikatiza Swala ya Sunna kwa sababu Swala ya Pamoja ni bora zaidi” [Al-Muhadhab, 4/1033 chapa ya Matba Al-Munira].
Na kutokana na yaliyopita basi inachukiza mtu kuingia au kuanza Swala ya Sunna pale inapokuwa imekimiwa Swala ya Lazima, kwa ushahidi wa Hadithi zilizotajwa na kuzungumza katika hilo, na pindi inapokimiwa Swala baada ya kuwa mtu ameshaingia kwenye Swala ya Sunna, basi ikiwa ni mwenye kuhofia kupitwa na Swala ya Pamoja ataikatiza Swala yake ya sunna, na kujiunga na Swala ya Pamoja, lakini kama hatahofia kupitwa na Swala ya Pamoja, basi ataikamilisha na kujiunga na Swala ya Pamoja.
Naye Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi Zaidi.


Share this:

Related Fatwas