Kusamehewa kwa Kiasi Kidogo ya Madh...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusamehewa kwa Kiasi Kidogo ya Madhii kwa Vijana.

Question

 Je, kinasameheka kiasi kidogo cha madhii kwa vijana?

Answer

 Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu..
Watu wengi hasa vijana hutokwa na Madhii, na huwenda wakawa wanasumbuka sana kufua nguo zao kutokana na Madhii hayo, kwa sababu huwa yanawatoka mara kwa mara, na hupata usumbufu zaidi wanapokuwa nje ya nyumba kwao.
Madhii ni maji mepesi yatokayo kwa kuchezeana baina ya mume na mke, na rangi yake inakaribiana na weupe.
Al-Mawardiy anasema: “Madhii ni maji mepesi yasiyotoka kwa wingi kama manii, lakni hutoka tone kwa tone katika hali ya matamanio”. [Al-Hawiy; 1/215, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Ilmiyah].
Imamul-Haramain anasema: “Madhii ni maji mepesi yatokayo kwa nguvu na hayafuatiwi na uvivu”. [Nihayat Al-Matlab: 1/143].
Kuhusu suala la kuosha Madhii, wanazuoni wa fiqhi wanazungumza katika kitabu cha Tahara, ambapo wanataja aina za najisi na namna ya kuzisafisha kwake.
Hukumu ya madhii pale mtu anapotokwa nayo ni kunyunyizia maji, na kama nguo zitapatwa na Madhii, basi inatosha kunyunyizia maji, yaani bila ya kuzifua, na kiwango kidogo Madhii kinasameheka, na hasa katika hali ya mtu kutokwa nayo mara nyingi.
Kigezo cha uchache wa Madhii ni desturi ya watu na jinsi waonavyo, kama ilivyo katika mifano yake kwenye mlango wake. Al-Baijuriy anasema: “(Hakuna kitu cho chote cha najisi kinachosameheka) yaani kila aina ya najisi; (isipokuwa kiwango kidogo… n.k.) yaani kiwango kikubwa cha najisi hakisameheki. Ikiwa najisi ni nyingi… na kigezo cha kuujua uchache wa Madhii na wingi wake ni desturi ya watu na jisni waonvyo”. [Hashiyat Al-Baijuriy Ala sharh Ibn Qasim Al-Ghuzziy: 1/103, Ch. ya Issa Al-halabiy]
Dalili ya hayo ni kwamba: Madhii ni miongoni mwa vitu ambavyo Sharia imeamuru viondoshwe kwa kufua au kwa kunyunyizia maji, na dalili ya kuondosha kwa kufua ni ile iliyopokelewa kutoka kwa Ali, aliposema: nilikuwa ninatokwa na Madhii kwa wingi, nikamwambia mtu amuulize Mtume S.A.W., kwa sababu mimi ni mume wa mtoto wake, akamuuliza, na Mtume akasema: “Tawadha na uoshe tupu yako”. [Muttafaq}.
Na dalili ya kunyunyizia maji ni kama ilivyopokewa kutoka kwa Sahl Ibn Hunaif, akisema: nilikuwa nikipta shida na taabu kwa kutokwa na Madhii, nikawa ninajiosha mara nyingi, nikamwambia Mtume S.A.W., na nikamuuliza, akasema: “inakutosha kutawadha”, nikamwambia: ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu: inakuwaje pale nguo zangu zinapopatwa na madhii? Akasema: “inatosha kuchukua maji kiasi cha kitanga cha mkono kisha kunyunyizia sehemu yenye Madhii”. [Wameipokea Abu Dawuud, At-Tirmidhiy, na akasema: Hadithi hii ni Hassan na ni Sahihi. Hatutambui isipokuwa kwa mapokezi ya Muhammad Ibn Is-haaq kuhusu Madhii. Wanazuoni wamehitilafiana kuhusu Madhii yanapokuwa nguoni, baadhi yao wanasema: haifai nguo hiyo isipokuwa kwa kuoshwa, na hii ni kauli ya Shafiy, Is-haaq, na wengine wanasema: inatosha kunyunyizia maji. Na Ahmad anasema: ninaona kuwa inatosha kunyunyizia maji].
Kama tukielekea kuwa kufuliwa ni kinyume cha kunyunyiziwa maji, kama ilivyo wazi, basi kufuliwa ima kuwe wajibu na kunyunyizia maji kuwe ni ruhusa, kwa basi hakuna kosa lolote kwa mtu atakaetekeleza ruhusa, kwa jinsi ilivyopokelewa na Ibn Umar kuwa Mtume S.A.W., anasema: “Hakika Mwenyezi Mungu anapenda kutumiwa ruhusa zake, kama ambavyo anachukia kuyafanya maasi”. [Hadithi hii imepokewa na Imamu Ahmad pamoja na wapokezi wengine].
Au kunyunyizia maji kukawa ni wajibu na kufuliwa kukawa bora zaidi kwa anayeweza, hapo basi itatosha kunyunyizia maji, kwa mujibu wa asili ya hukumu, na kufanya hivyo ni vizuri na bila ya kulaumiwa.
Madhii kwa vijana wengi ni mtihani mkubwa; kwa hiyo inafaa kuwepo ruhusa kwa ajili ya kuondosha uzito na taabu juu yao, na haya ni miongoni mwa mambo mazuri ya Sharia tukufu, kama alivyosema Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Hapendi Mwenyezi Mungu kukutieni katika taabu}. [AL MAIDAH: 6], na pia anasema: {Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika dini}. [AL HAJJ: 78].
Ibn Qudamah anasema: “Kuhusu Madhii, mate ya nyumbu na punda, na jasho lao, wanyama na ndege wakali, na mkojo wa popo, kuna mapokezi mawili, kwanza: kusamehewa uchache wake, kwa sababu ya ugumu wa kujiepusha nayo, na Madhii ni mengi kwa vijana, na mwenye wanyama hasalimiki na kuwagusa mara kwa mara, kwa hiyo husameheka uchache wa najisi hizo, kama vile damu. Ya pili: hakusameheki kwa kutokuwepo dalili ya Sharia”. [Al-Kafiy: 1/170, Ch. ya Dar Al-Kutub Al-Elmiyah]
Ibn Rajab Al-Hanbaliy anasema: “Madhii yakiwa sehemu za mwili isipokuwa tupu au nguo, wanazuoni wengi wanaona kuwa ni najisi kama mkojo na lazima yaoshwe. Kuna mapokezi kutoka kwa Ahmad kuwa: kiwango kidogo cha najisi kama damu kinasameheka. Na kuna mapokezi ya tatu kuwa: najisi yake ni nyepesi na inatosha kunyunyizia maji kama mkojo wa mtoto mchanga asiyekula chakula, kwa sababu ya kutokea kwake mara kwa mara, na uzito wa kujiepusha nayo.
Na kuna hadithi kutoka kwa Sahl Ibn Hunaif, kutoka kwa Mtume S.A.W., kuwa: aliulizwa juu ya nguo kuwa na madhii, akasema: “chukua maji kiasi cha kitanga cha mkono na uyanyunyizie mahali palipo na madhii hayo”. Imepokelewa na Maimamu: Ahmad, Abu dawuud, Ibn Majah, na At-Tirmidhiy, na wakasema: kuwa Hadithi hii ni Hassan na ni Sahihi, na hatuijui isipokuwa kwa mapokezi ya Ibn Is-haaq. Imamu Ahmad katika mapokezi ya Al-Athram alisema: sijui kitu chochote kinyume na hivyo. Imepokelewa kutoka kwake akisema: hakuipokea ila Ibn Is-haq, na mimi ninamheshimu. Na mara nyingine alisema: Hadithi hii ikiwa imethibiti, basi inatosha kunyunyizia maji. Na kutoka kwa Ahmad amesema kuwa: Madhii ni tahiri kama manii, na ni kauli ya Abi Hafs Al-Barmakiy naye ni mwenzetu, ambaye anaona kuwa panyunyiziwe maji kiibada… Na imepokelewa kutoka kwa Mtume S.A.W., kuwa alisema juu ya Madhii: “Tawadha na uusafishe utupu wako kwa maji”, Hadithi hii imepokelewa na Imamu Muslim pamoja na wapokezi wengine.
Baadhi ya wanazuoni walifahamu kuwa kumwagia maji kunamaanisha kuosha, kutokana na lafudhi nyingine: “Tawadha na uuoshe utupu wako”, na wengine miongo mwao walifahamu kuwa ni: kumwagia maji baada ya kutawadha, kwa madhumuni ya kupunguza matamanio na kujiepusha na wasiwasi. Katika mapokezi mengine kuna uwazi wa maana hii, lakini Isnad yake ni dhaifu. Kwa hiyo amri ya kunyunyizia maji ni ya hiari”. [Fath Al-Bariy, na Ibn Rajab: 1/305, Ch. ya Maktabat Al-Ghurabaa’ Al-Athariyah, Al-Madinah Al-Munawarah].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia kusemwa hapo juu, inafahamika kuwa kiwango kidogo cha Madhii kinasameheka, na hasa kwa vijana.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

 

 

 

Share this:

Related Fatwas