Kusahau Baadhi ya Aya Katika Kuhiti...

Egypt's Dar Al-Ifta

Kusahau Baadhi ya Aya Katika Kuhitimisha Qur'ani.

Question

Imamu wa swala ya Tarawehe anafanya nini pindi anaposahau baadhi ya Aya za Qur'ani wakati wa kisomo cha kuhitimisha katika sala ya Tarawehe? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, na sifa njema ni zake, na rehema na amani zimshukie Bwana wetu Mjumbe wa Mwenyezi Mungu, na Aali zake na Masahaba wake na wafuasi wake, na baada ya hayo:
Ramadhani ni msimu wa kutii, na miongoni mwa ibada muhimu ndani yake ni Saumu na Sala ya usiku, iliyoitwa kwa kawaida Sala ya Tarawehe. Watu wengi wamezoea kuhitimisha kusoma Qur'ani tukufu katika Sala ya Tarawehe, kwa ajili ya kupata heshima ya kuihitimu, na kuomba dua mwishoni mwa kusoma, kwa kutazamia ikubaliwe baada ya kuimaliza, lakini huenda msomaji akasahau kusoma baadhi ya Aya, hapo watu wanaulizia hukumu za kuzirejea.
Inajulikana kuwa miongoni mwa mambo ya kupendeza kwa kawaida ni kuihitimu Qur'ani tukufu, hasa katika mwezi wa Ramadhani, na imepokelewa katika mlango huu Hadithi iliyopokelewa na Ibn Abbas, akisema: Mtume S.A.W., alikuwa mkarimu sana kuliko watu wote, ukarimu hasa ulipita kiasi katika mwezi wa Ramadhani, hasa alipokuwa akishukiwa na Malaika Jibril. Malaika alikuwa akionana naye kila mwaka katika Ramadhani, ulipokuwa mwisho wake Mtume anasoma Qur'ani mbele ya Jibril. Wakati huo ukarimu wake kwa kutoa heri ulikuwa zaidi kuliko kuvuma kwa upepo wa mvua. [Muttafaq].
Inapendeza kuwa kusoma ni katika usiku, kwa ilivyopokelewa katika Aya za Qur'ani na Hadithi ya Mtume S.A.W., miongoni mwake, kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Kwa yakini wamchao Mwenyezi Mungu watakuwa katika Mabustani na chemchem. Wanapokea aliyowapa Mola wao, kwa hakika wao walikuwa wakifanya mema kabla ya haya, Walikuwa wakilala kidogo tu usiku. Na wakiomba maghufira, (msamaha) nyakati za kabla ya alfajiri} [ADH DHARIYAT; 15-18], na kauli yake Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Na waja wa Mwenyezi Mungu (anaowapenda ni wenye sifa hizi):- Ni wale wanaokwenda (na kurejea) ulimwenguni kwa unyenyekevu; na wajinga wakisema nao (maneno mabaya) huwajibu (maneno ya salama). Na wale wanaopitisha baadhi ya saa za usiku kwa ajili ya Mola wao kwa kusujudu na kusimama}. [AL FURQAAN: 63-64].
Na imepokelewa kutoka kwa Salim, kutoka kwa Ibn Umar kuwa Mtume S.A.W, alisema: “Abullahi ni mtu mwema anaejishughulisha kusali sala ya usiku. Salim akaongeza kusema kuwa baada ya haya Abdullahi hakuwa akilala ila kidogo tu” [Wameipokea: Bukhariy na Muslim}. Na Adullahi bin Amr bin Alaas., alisema kuwa Mtume S.A.W, alimwambia: “Ewe Abdullahi usiwe kama mtu fulani aliyekuwa akifanya Ibada ya usiku, na baadaye akaacha kusali hivi” [Wameipokea Bukhariy na Muslim].
Inatakiwa kuendelea kufanya hivi hasa katika Ramadhani, na hii inayoitwa Sala ya Tarawehe, imepokelewa kutoka kwa Abi-Hurairah R.A., kuwa Mtume S.A.W., alisema: “Atakayesali Sala ya Tarawehe katika mwezi wa Ramadhani kwa uaminifu na kwa nia ya kupata thawabu, dhambi zake zote za zamani zitasamehewa”. [Muttafaq].
Na kumaliza kusoma Msahafu ni ada ya waja kwa kipindi cha mwaka kutokana na fadhila za Ramadhani, na As-Sayutiy anasema: “Waja wema waliotangulia (Salaf) walikuwa na ada nyingi kuhusu jambo hili, na miongoni mwa mapokezi ni kuwa: wapo waliokuwa wanaohitimisha Msahafu mara nane kila mchana na usiku; nne ndani ya usiku na mfano wake ndani ya mchana; na wapo waliokuwa wanauhitimisha mara nne kila mchana na usiku; kisha mara tatu, mbili, na hitima moja… kisha wanafuatia wanaohitimisha kila nyusiku mbili, kisha wanaofuata wanaohitimisha kila nyusiku tatu; na hii ni nzuri…
Na wamepokea Ahmad na Abu-Ubaidah kutoka kwa said Ibn Al-Mundhir- na huyu hana Hadithi isipokuwa hii- alisema: Nilimuuliza Mtume S.A.W, Je, naweza kusoma Qur'ani kila siku tatu? Akasema: Naam, ukiweza. Kisha anafuatia aliyehitimu kila siku mara nne, kila siku mara tano, kila siku mara sita, kila siku mara saba, na hii ya mwisho ni ya kati na kati, tena nzuri kuliko zote, na pia ni kitendo cha Masahaba wengi na wengineo. Bukhariy na Muslim walipokea kutoka kwa Abdillahi Ibn Amr, alisema: Mtume S.A.W., aliniambia; Soma Qur'ani kila mwezi, akasema: Nina nguvu ya kuzidi, akasema: Isome kila siku kumi, nilijibu hivi hivi, akasema: isome kila siku saba na usizidi kuliko hivi.
Abu-Ubaid na wengineo walipokea kwa njia ya Wasii’ Ibn Hibban, kutoka kwa Qais ibn Abi-Sa’sa’ah- na huyu hana Hadithi isipokuwa hii- kuwa alisema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu, muda gani naweza kusoma Qur'ani? Akasema: kupitia siku kumi na tano, nikasema: Nina nguvu zaidi kuliko hivyo, akasema: Isome kila Ijumaa. Kisha aliyehitimu kila siku nane, kisha kumi, kisha mwezi mmoja na miezi miwili.
Ibn Abi-Dawuud amepokea kutoka kwa Mak-Huul alisema: Masahaba wa Mtume S.A.W, wenye nguvu walikuwa wakisoma Qur'ani kila siku saba, na baadhi yao kila mwezi, na baadhi yao kila miezi miwili, na baadhi yao kupitia ziada ya hivi. Na Abul-Laith katika Al-Bustaan anasema: Ni afadhali kwa msomaji ahitimu mara mbili kwa mwaka, asipoweza kuzidisha . Na Al-hasan Ibn Ziad amepokea kutoka kwa Abi-Hanifa kuwa alisema: Aliyesoma Qur'ani mara mbili kwa mwaka, basi ametekeleza haki yake, kwa kuwa Mtume S.A.W, aliisoma mbele ya Jibrili mara mbili, ndani ya mwaka aliokufa.
Na wengine walisema; Inachukiza kuichelewesha hitima zaidi ya siku arobaini bila ya sababu, na hii ni kauli ya Ahmad, kwa sababu Abdullahi Ibn Umar alimuuliza Mtume S.A.W: Je, muda gani twaweza kuihitimisha Qur'ani? Akasema: Ndani ya Muda wa siku arobaini. Ameipokea Abu-Dawuud.
An-Nawawiy katika Al-Adhkar anasema: Rai inayochaguliwa kuwa jambo hili linatofautiana na hali ya watu: Mtu aliyekuwa akitafakari katika maana na maarifa yake, basi afadhali kusoma kadiri ya awezavyo mtu kufanya hivyo; na huyu alikuwa akishughulikia kueneza elimu na kutoa hukumu katika mtangamano wa watu n.k. Miongoni mwa mambo muhimu ya dini na masilahi ya umma, basi afadhali mtu asome kadiri ya kutoisababisha kasoro katika kazi kama hizi wala kuahirisha masilahi; lakini mtu asipokuwa miongoni mwa wale waliotajwa hapo juu, ni bora kwake akazidisha kwa kiasi kiwezekanavyo, bila ya kusababisha tabu wala hangaisho la kusoma Quran”. [Al-Itqan Fi Uluum Al-Quran: 1/360].
Miongoni mwa fadhila za hivi: Kuomba dua mwishoni mwa kusoma, kwa mapokezi yaliyoashiria kuwa inatakiwa hivi. As-Sayutiy anasema: Afadhali kuihitimisha mwanzoni mwa mchana au mwanzoni mwa usiku, kwa ilivyopokelewa na Ad-Darimiy, kwa Isnadi hasan, kutoka kwa Saad Ibn Abi-Waqas alisema: Akihitimu Qur'ani mwanzoni mwa usiku, basi Malaika atamsalia mpaka asubuhi, na kama akihitimu mwanzoni mwa mchana, basi malaika atamsalia mpaka jioni. Alisema katika Al-Ihyaa: hitima ya mwanzoni mwa mchana inakuwa katika Rakaa mbili za alfajiri, na ya mwanzoni mwa usiku katika Rakaa mbili za Sunna ya Magharibi.
(Suala): kutoka kwa Ibn Al-Mubarak; Inatakiwa kuhitimisha mwanzoni mwa usiku kupitia msimu wa kipupwe, na mwanzoni mwa mchana katika msimu wa kaskazi. (Suala): Ni Sunna kufunga Saumu siku ya kuhitimisha, na hii imepokelewa na Ibn Abi-Dawud, kutoka kwa wengi wa Tabi’ina, pamoja na kuhudhuria ndugu zake wa karibu na marafiki.
At-Twabaraniy amepokelea kutoka kwa Anas kuwa: Wakati akihitimu anawaita ndugu zake wa karibu na kuomba dua. Na Ibn Abi-Dawuud kutoka kwa Al-Hakam Ibn Utaibah alisema: Mujahid aliniita, akiwa na Ibn Abi-Umamah, na wao walisema: tulimuita kwa sababu tulitaka kuihitimsha kisomo cha Qur'ani, na kuomba dua wakati huo kunakubalika. Na amepokea kutoka kwa Mujahid alisema: walikuwa wakikutana kwenye kuhitimisha Qur'ani, akisema: Wakati huu rehema zinateremka. [Al-Itqan Fi Uluum Al-Quran: 1/382, Ch. Ya Al-haiah Al-Masriyah Al-A’amah Lil-Kitab]
Ibn Qudamah anasema: “Al-Fadhl Ibn Ziad alisema: Nilimuuliza Aba-Abdillahi, nikisema: nahitimu Qur'ani, Je, naihitimu katika Sala ya Witri au Sala ya Tarawehe? Akasema: Ihitimu katika sala ya Tarawehe, hata tuombe dua kati ya wawili. Nikasema: vipi ninafanya? Akasema: Ukimaliza mwisho wa Qur'ani, inua mikono yako kabla ya kurukuu, omba dua wakati sisi tuko katika sala, na refusha kusimama. Nilisema: Naomba dua ya nini? Akasema: unavyotaka. Akasema; Nilifanya alivyoniamuru, wakati yeye yuko nyuma yangu akisimama kuomba dua na kuinua mikono yake.
Hanbal anasema: Nilisikia Ahmad akisema katika kuhitimisha Qur'ani: Ukimaliza kusoma {Ninajikinga kwa Bwana Mwenye kuwalea}. [AN NISAA: 1], basi inua mikono yako hali ya kuomba dua na kabla ya kurukuu; nikasema: Nini dalili yako? akasema: Niliona watu wa makkah wakifanya hivi, na Sufyaan Ibn Uyainah akiifanya pamoja nao Makkah. Al-Abbas Ibn Adul-Adhiim anasema: Vile vile tumeona watu wa Al-Basrah na Makkah, na watu wa madinah wamepokelea habari katika jambo hili, kisha alitaja Uthmaan Ibn A’affaan”. [Al-Mughniy: 2/125, Ch. Ya Maktabat Al-Qaahirah].
Inajulikana kuwa kwenye kuhitimisha huenda msomaji akasahau baadhi ya Aya, hapo ni bora akazisoma upya, kwa ajili ya kukamilisha Hitima. Na haikupokelewa hukumu maalumu katika sheria inayoainisha njia ya kufanya hivyo, kwa hiyo inarejea katika kujitahidi kwa wanazuoni. Na miongoni mwa njia hizi: ni kuwa na msomaji aliyesimama nyuma ya Imamu (ili amkumbushe), na hii imechukuliwa kutoka katika Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Said Ibn Abder-Rahmaan Ibn Abziy, kutoka kwa baba yake, alisema: Siku moja Mtume S.A.W, alisali Sala ya Alfajiri, akaacha Aya, akasema: (Ubaiy Ibn Kaab yuko wapi?”, na Ubaiy akasema: Ewe Mtume (ulisahau Aya fulani, ama sivyo au Aya imefutwa?), na Mtume akasema: (Niliisahau). An-Nasaiy ameipokea Hadithi hii katika As-Sunan Al-Kubra.
Dalili hapa ni kuwa: Mtume S.A.W, alimuulizia Ubaiy Ibn Kaab kwa kuwa yeye ni miongoni mwa maswahaba waliohifadhi Qur'ani, na Ubaiy alisikitika kuwa hakumkumbusha Mtume S.A.W, Aya iliyosahaulika, kwa kudhani huenda Aya hii ikawa imefutwa katika Qur'ani.
Miongoni mwa mapokezi ya Salaf yaliyopokelewa na Ibn Hazim akisema: “Nilimwona Ibn Siriin akisali hali ya kuwa ameketi, na Msahafu uko kando yake, na yeye akisahau Aya fulani, basi huitazama katika Msahafu”. [Al-Masaahif: 461, Ch. ya Al-faruuq Al-Hadiithah]
Na hii ni dalili ya kujaribu kuisoma sura kwa ukamilifu, lakini pasipokuwepo hali hiyo, basi inatakiwa kusoma Aya zinazosahaulika nje ya sala, au ndani yake, ni sawa sawa iwe katika rakaa zijazo au mwishoni mwa Hitima. Na rai ya pili imepokelewa na baadhi ya Salaf, Ibn Qudamah anasema: (Suala): Abu-Abdillahi aliulizwa kuhusu Imamu katika mwezi wa Ramadhani huacha baadhi ya Aya za Sura: Je, afadhali kwa aliye nyuma yake azisome? Akasema: Naam, ni bora zaidi afanye hivyo, na watu wa Makkah walikuwa wakimwandaa mtu anayeandike kila kilichosahauliwa na Imamu, ikiwa herufi au kingine, na katika usiku wa kuhitimisha Imamu azisome upya, na inatakiwa ifanyike hivyo kwa ajili ya kukamilisha Hitima, na pia thawabu iwe kamili. [Al-Mughniy: 2/127, Ch. Ya Maktabat Al-Qahirah]
Miongoni mwa mambo mazuri katika mlango huu, ni ilivyotajwa na As-Sayutiy kwa kauli yake: “Ibn Bas-haan ikiwa kumrejesha msomaji kitu alikiacha na hakukijua, basi alikiandika, na ikifika wakati wa kuihitimu Hitima na kuomba idhini kwa ajili ya hivi, hapo Ibn Bas-haan akamwuulizia vitu alivyowahi kuvisahau, kama akivijua akamtoa idhini, na asipovijua akamwomba aihitimu Hitima nyingine”. [Al-Itqaan: 1/357].
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia: kuna urahisi katika suala la usahaulifu wa Imamu kwa baadhi ya Aya katika kuhitimisha Sala ya Tarawehe, na inatakiwa katika hali ya kusahu, arejee upya aliposahau, na hakuna ubaya wowote kuwa mmoja wa wanaosali nyuma yake, naye amehifadhi Qur'ani, amkumbushe Imamu alichokisahau.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.

 

 

 

 

Share this:

Related Fatwas