Swala ya Sunna Katika Hali ya Kukaa...

Egypt's Dar Al-Ifta

Swala ya Sunna Katika Hali ya Kukaa Bila ya Sababu na Imamu Akiwa Anaswalisha Hali ya Kuwa Kasimama.

Question

Je, maamuma anaruhusiwa kuswali kwa kukaa katika Swala ya Sunna bila ya sababu wakati ambapo Imamu anaswalisha akiwa amesimama? 

Answer

Kwa jina la Mwenyezi Mungu, sifa njema ni zake, na rehema na amani zimwendee bwana wetu Mtume wa Mwenyezi Mungu na Jamaa zake na Masahaba wake na wafuasi wake. Na baada ya utangulizi huu:
Swala ni mojawapo ya nguzo za Uislamu, nayo ni msingi wa dini, anayeuharibu amehaibu dini nzima. Maana ya Nafilah katika lugha: ni ziada ya Sunna, nayo ni mambo yanayofanywa na mtu yasiyo ya lazima kwake, Mwenyezi Mungu Mtukufu amesema: {Na amka usiku kwa ibada; ni ziada ya sunna hasa kwako wewe. Huenda Mola wako Mlezi akakunyanyua cheo kinacho sifika.} [ISRAA 79].
Na maana yake katika istilahi: Sunna ni ile isiyokuwa ya faradhi – yaani kama kuswali, kufunga na kutoa sadaka -, na inaitwa Sunna, jambo lililopendekezwa, jambo zuri, jambo linalotakiwa, jambo linalopendelewa, majina haya yote yana maana moja tu kufuatana na mtazamo ulio maarufu. [Nihayatul Muhtaj 2/100, Al-Halabi].
Na kusimama kwa ajili ya kupiga takbira ya kuingia kwenye Swala (ihraam) na kusoma Suratul Fatiha ni nguzo ya Swala ya faradhi, basi aliyeswali katika Swala ya faradhi akiwa amekaa pasi na sababu, Swala yake ni batili, kwa mujibu wa kauli ya Mwenyezi Mungu Mtukufu: {Zilindeni Swala, na khasa Swala ya katikati, na simameni kwa ajili ya Mwenyezi Mungu nanyi ni wenye kuqunuti} [AL BAQARAH: 238], yaani: wenye kunyenyekea, na amri hii inapelekea faradhi, kwa sababu kusimama hakukulazimishwa nje ya swala, basi ni wajibu kusimama katika Swala ya faradhi, kwa mujibu wa matini ya Aya hiyo kadiri inavyowezekana, na Sunna imethibitisha uwajibikaji wa kusimama kama ilivyopokelewa kutoka kwa kundi la Wananvyoni -isipokuwa Imamu Muslim-, imepokewa kutoka kwa Imran Ibn Hussein alisema: Nilikuwa nikiugua bawasiri. Nikamuuliza Mtume kuhusu kuswali. ‎Akasema: “Swali ukiwa umesimama! Ikiwa huwezi basi swali hali ya kuwa umekaa. Ikiwa huwezi basi swali hali ya kuwa umelala ubavu.”
Lakini katika Swala ya Sunna kusimama sio wajibu, inaruhusiwa kuswali kwa kukaa kwa sababu au bila ya sababu, lakini thawabu ya mwenye kukaa ni nusu ya mwenye kusimama, kwa mujibu wa Hadithi ya Al-Tirmidhi kutoka kwa Imran Ibn Husein kwamba alimuuliza Mtume S.A.W, kwa Swala ya mtu akiwa amekaa kitako alisema: “Mwenye kuswali akiwa amesimama ni bora zaidi, na mwenye kuswali akiwa amekaa kitako atapata nusu ya thawabu, na mwenye kuswali akiwa amelala atapata nusu ya thawabu ya mwenye kuswali akiwa amekaa kitako”, na hii ni kwa aliyeswali akiwa amekaa kitako pasina sababu; kwa sababu mtu huandikwa aliyo kuwa akiyafanya kama akizuiliwa na udhuru, kwa mujibu wa Sahih Al-Bukhari kutoka kwa Abu Musa R.A, kwamba Mtume, S.A.W, alisema: “kama mja akipatwa na ugonjwa au akisafiri Mwenyezi Mungu humwandikia vile alivyokuwa akifanya wakati wa kuwa mzima na mkazi”.
Vile vile inaruhusiwa kuswali raka moja akisimama na raka moja akikaa kitako, na dalili ya hivyo ni Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa mama wa waumini Aisha, R.A: kwamba Mtume wa Mwenyezi Mungu, S.A.W., alikuwa akiswali amekaa kitako, akisoma hali ya kuwa amekaa, kama zikibaki Aya za Qur`ani karibu thelathini au arubaini- akasimama na akazisoma, kisha akarukuu, halafu akasujudu, akafanya hivyo hivyo alivyofanya katika rakaa ya pili, kama akimaliza swala yake anaangalia: Kama nikiwa nimeamka anazungumza nami, na kama nikiwa nimelala analala..
Al-Baji alisema katika kuelezea Muwatta akitoa maoni juu ya Hadithi hii: “Hivyo kwa yule aliyeanza Swala ya Sunna hali ya kuwa amekaa kitako, kisha akataka kusimama inaruhusiwa hivyo, na kama akianza Swala hali ya kuwa kasimama, kisha akataka kukaa, inaruhusiwa hivyo kwake kufuatana na maelezo ya Ibn Al-Qasim, kwani hali hii inamruhusu kuanza Swala hali ya kuwa amekaa, basi ruhusa ya kuanza Swala hali ya kuwa amekaa ni kama mtu mwenye udhuru, kisha akasema: kauli yake Aisha R.A.: “kisha akafanya hivyo hivyo alivyofanya katika rakaa ya pili”, kauli yake hii inaonesha kwamba inaruhusiwa kukaa katika Swala ya Sunna baada ya kusimama pamoja na kuwa anaye swali anaweza kusimama kwa sababu Aisha alieleza tendo lake S.A.W lilikuwa la mara kwa mara na alisema kwamba Mtume S.A.W. alikuwa akianza kusoma hali ya kuwa amekaa, kisha anasimama kwa ajili ya kusoma Aya zilizobaki katika kila rakaa, Na kwamba hali hii ilikuwa hali yake ya mara kwa mara.”. [Al-Muntaqa Al-Baji Sharhul Muwatta 1/243, Ch. Dar Al-Kitab Al-Islamiy].
Kuruhusiwa kuswali Swala ya Sunna hali ya kukaa kitako ingawa anaweza kusimama huu ni mtazamo wa wengi wa Wanavyuoni, na kufuatana na mtazamo huu Wanavyuoni walielekea katika kauli za Abu Barakat Al-Dardeer alisema katika Al-Sharhul Kabiir: “Inaruhusiwa kwa mwenye kuswali Swala ya Sunna kuswali hali ya kuwa amekaa ingawa anaweza kusimama mwanzoni mwa Swala, na hata katikati ya Swala baada ya kufanya baadhi ya vitendo vyake kwa kusimama, na ametegemea hivyo kwa kuegemeza kwake jambo lililo bora zaidi”. [Al-Sharhul Kabiir kwa Al-Dardeer 1/262, Dar Ihyaa Al-Kutub Al-Arabia].
Malik alisema: aliyeanza Swala ya Sunna hali hya kuwa amekaa kisha akataka kusimama, au aliianza Swala yake hali ya kuwa amesimama kisha akataka kukaa, basi inaruhusiwa kwake kufanya hivyo. [Tahdhib Al-Mudawanah kwa Al-Baradhai 1/246, Dar Al-Buhuth kwa Masomo ya Kiislamu –Dubai].
Sheikh Al-Islam Zakaria Al-Answariy alisema: “Inaruhusiwa kwa mwenye uwezo wa kusimama kusali Swala za Sunna (akikaa kitako lakini kwa nusu ya thawabu ya mwenye kusimama) kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Al-Bukhari: “Mwenye kuswali akiwa amesimama ni bora zaidi, na mwenye kuswali akiwa amekaa kitako atapata nusu ya thawabu ya mwenye kuswali akisimama, na mwenye kuswali akiwa amelala atapata nusu ya thawabu ya mwenye kuswali akiwa amekaa kitako”, Hadithi hii inahusu mwenye kuswali Swala ya Sunna vile vile ingawa anaweza kuswali akiwa amesimama au amekikaa” (Asna Al-Matalib Sharhu Rawdh Al-Talib 1/148, Dar Al-Kitab Al-Islami).
Ibn Qudaamah alisema katika kitabu cha Al-Mughni: “Suala moja: Al-Kharqiy alisema: “Na inaruhusiwa Kuswali Swala ya Sunna akiwa amekaa kitako” hatujui, tofauti katika suala hili, na kwamba kusimama ni bora zaidi, na Mtume S.A.W, anasema: “Mwenye kuswali hali ya kuwa amesimama ni bora zaidi, na mwenye kuswali hali ya kuwa amekaa kitako atapata nusu ya thawabu ya mwenye kuswali akiwa amesimama)), Hadithi hii imekubaliwa, na katika Sahihi Muslim: “Swala ya mtu aliyeswali huku akiwa amekaa kitako ni nusu ya thawabu ya Swala”, vile vile Aisha amesema: “Mtume, S.A.W hakufa isipokuwa Swala zake nyingi zilikuwa katika hali ya kukaa”, na imepokelewa Hadithi kama hii kutoka kwa Hafsah, Abdullah Ibn Amr, na Jabir Ibn Samra, kutoka kwa Imma Muslim, na kwa sababu watu wengi wanachoka kutokana na kusimama kwa muda mrefu, kama kusimama ni lazima katika Swala ya Sunna, basi watu wengi wangeliziacha Swala ya Sunna, kwa hivyo Mwenyezi Mungu amesamehe mwenye kuacha kusimama katika Swala ya Sunna, kwa ajili ya kuhimiza watu kuswali Swala hizo kwa wingi zaidi. Pia ameiruhusu na kuikubali swala ya juu ya kipando cha safari, na ameiruhusu na kuikubali nia ya funga ya Saumu ya Sunna inayonuiwa mchana” (Al-Mughni kwa Ibn Qudaamah 1/442, Ch. Dar Ihyaa Al-Turath Al-Arabiy).
Al-Nawawiy amesema katika kitabu cha [Al-Majmuu]: “Inaruhusiwa bila kupingwa kuswali Swala za Sunna katika hali ya kukaa ingawa kuna uwezo wa kusimama, na dalili yake inatoka katika Hadithi sahihi tulizotaja na nyinginezo, ambazo ni maarufu katika sahihi, lakini thawabu za Swala hii zitakuwa nusu ya thawabu za mwenye kusali hali ya kuwa amesimama, kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imran ibn Husein R.A., alisema: Mtume wa Mwenyezi Mungu – S.A.W. alisema: “Mwenye kuswali akiwa amesimama ni bora zaidi, na mwenye kuswali akiwa amekaa kitako atapata nusu ya thawabu za mwenye kuswali akiwa amesimama, na mwenye kuswali akiwa amelala atapata nusu ya thawabu za mwenye kuswali akiwa amekaa kitako” Hadithi hii imepokewa kutoka kwa Al-Bukhari, na maana ya kauli yake “akiwa amelala” yaani amejinyoosha kitandani, kama akiwa anaswali Swala za Sunna katika hali yake hii na ana uwezo wa kuswali akiwa amesimama na akiwa amekaa, basi kuna maoni mawili” [Al-Majmuu Sharhul Muhadhab 3/239, Uchapishaji nyumba ya Al-Miniriyah].
Kama ikisemekana kuwa imepokelewa katika sahihi kutoka kwa Anas kuwa: “Imam yupo kwa ajili ya kufuatwa, basi kama ataswali hali ya kuwa amesimama, basi swalini mkiwa mmesimama, kama akirukuu, rukuuni, na kama akisimama, simameni, na kama akisema: Samia Allah Liman Hamidah (Mwenyezi Mungu amemsikia mwenye kumhimidi), basi semeni: Rabana Wa Laka Al-Hamd (Mola wetu hakika unastahiki kuhimidiwa), kama akiswali akiwa amesimama, nanyi swalini mkiwa mmesimama, na akiswali akiwa amekaa kitako, basi nanyi nyote swalini katika hali ya kuwa mmekaa kitako”, yaani: Je wajibu kusimama kama Imamu ataswalisha hali ya kuwa amesimama? jibu ni:
Kwanza: hali hii inahusu swala ya faradhi tu, kwa sababu kusimama katika swala ya faradhi ni lazima.
Pili: baadhi ya Wanavyuoni wanaona kuwa suala hili limefutwa, kwani Mtume S.A.W. aliswali baada ya hapo akiwa amekaa kitako na watu nyuma yake wakaswali maamuma wakiwa wamesimama, kwa mujibu wa Sahihi mbili, lakini ikiwa uwajibikaji umefutwa, basi ruhusa imeendelea kuwepo, na ruhusa haikuzuia kupendekeza, yaani inawezekana kufahamu hali hii kuwa inapendekezwa kuswali kwao wakiwa wamekaa kitako; kwa sababu uwajibikaji umeondolewa kwani Mtume S.A.W. amekubali hali yao hii na hakuwaamuru kuswali swala hii tena. [Rejea: Fath Al-Bari, 2/177].
Tatu: sababu ya hukumu hii ilikuwa wazi katika Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Imamu Muslim: “Mmekaribia kufanya kama walivyofanya Waajemi na Warumi, walikuwa wanasimama kwa wafalme wao, na wafalme wao hao wakiwa wamekaa, msifanye hivyo”, basi sababu ni kutofanya hivyo pamoja na Imamu. Kufuatana na hali hii katazo halihusiki kinyume na suala hili. Na kuna mfano mwingine katika sharia, ambapo Imamu amekatazwa kuswali katika mahali pa juu kama ilivyopokelewa kutoka kwa Abu Dawud, kinyume na katazo hilo kwa Imamu, Maamuma hawakukatazwa kufanya hivyo. Hivyo ilikuwa Abu Hurayrah na wengine miongoni mwa Wanavyuoni waliotangulia wanaswali nyuma ya Imamu lakini juu ya msikiti, na Imamu anaswali ndani ya msikiti chini, kwa mujibu wa Hadithi iliyopokelewa kutoka kwa Abdurraziq na Ibn Abi Shaybah. Na hakukuwa na dalili ya kupinga yoyote na wengine.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyotangulia hapo juu, inaruhusiwa kwa maamuma kuswali swala za Sunna akiwa amekaa ingawa ana uwezo wa kusimama hata ikiwa Imamu wake anaswali akiwa amesimama.
Na Mwenyezi Mungu Mtukufu ni Mjuzi zaidi.
 

Share this:

Related Fatwas